SoC03 Ajira Lukuki za Vijana Kupitia Sekta ya Utalii Nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Utangulizi
Wakati ninasoma, nilidhani kuwa watalii ni lazima wawe wazungu kutoka Ulaya, na pia nilidhani utalii unafanyika katika mbuga za Wanyama pekee. Nikiwa bado shuleni, nilibahatika kwenda pamoja na wanafunzi wenzangu kutembelea mbuga za Wanyama Manyara na Ngorongoro, tulipokuwa tunakutana na wazungu huko, tulikuwa tunasema, angalia watalii wale; mimi na wenzangu hatukujiona kama watalii, bali wazungu ndiyo walikuwa watalii. Pia tullikutana na Wamarekani wenye asili ya Afrika, hatukuwahesabu kama watalii kwa sababu sii wazungu.

Mtizamo niliokuwa nao wakati huo, upo mpaka leo kwa watu wengi, ndio maana nimesukumwa kuandika Makala hii, ili ukweli kuhusu utalii, pamoja na utajiri uliojificha ndani yake vijulikane.

Utalii ni nini? Kwa mujibu wa sw.wikipedia.org, Utalii ni kitendo cha kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa lengo la burudani, biashara, kujifunza au makusudi mengine.

Kuna makundi mawili ya utalii: Utalii wa nje, ni kundi linalohusisha watu wa nchi Fulani wanaotembelea maeneo ya nchi nyingine; wakati Utalii wa ndani ni kundi linalohusisha watu wanaotembelea maeneo mbalimbali katika nchi yao.

Kilelezo Na. 1: Vivutio vya Kitalii
Maeneo ya Kitalii.png

Chanzo: Google: Utalii

Vivutio vya Kitalii Nchini Tanzania

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia tovuti kuu ya serikali, sekta ya Utalii nchini Tanzania ni moja ya sekta muhimu inayotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi. Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya asili kama vile mandhari za kuvutia, maeneo ya kihistoria na ya akiolojia, hifadhi zenye wanyamapori wengi na baionuai mbalimbali, fukwe zisizochafuliwa na wingi wa utamaduni wa makabila 158.

Taarifa inaendelea kusema, Nyanda za Juu za Kusini na Kaskazini zina safu nyingi za milima ya kuvutia hasa yenye urefu wa kati ya mita 500 mpaka mita 1000 katika maeneo yaliyoizunguka. Mlima Kilimanjaro wenye urefu wa mita 5,895 na Meru mita 4,500 inayopatikana Kaskazini Mashariki mwa Tanzania ni milima iliyotokana na milipuko ya volkano miaka mingi iliyopita. Mwambao wa bahari una urefu wa zaidi ya kilomita 804 pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba (ambavyo kwa pamoja vinaunda Zanzibar) na kisiwa cha Mafia. Visiwa hivyo vina mkusanyiko wa vivutio vya asili, utamaduni, historia na akiolojia. Maliasili nyingine ni pamoja na Ziwa Viktoria, ziwa la pili kwa ukubwa duniani na chanzo cha mto Nile.

Aina za Utalii
Kuna aina mbalimbali za utalii; katika Makala haya nitataja na kuelezea aina sita za utalii. Kwa mujibu wa ukurasa wa recursosdeautoayuda.com, zifuatazo ni aina za utalii: Utalii wa Burudani, Utalii wa Utamaduni, Utalii wa Asili, Utalii wa Michezo, Utalii wa Kidini na Utalii wa Matibabu au Afya.

Utalii wa Burudani
Utalii wa aina hii huhusisha watu au kikundi cha watu wanaokwenda sehemu tofauti na makazi yao ambapo kuna vivutio na burudani mbalimbali. Sehemu hizi ni kama fukwe, Mahoteli, Bustani za maua, na kadhalika.

Utalii wa Utamaduni
Utalii huu unahusisha watu wanaotembelea sehemu za kihistoria na utamaduni. Hii ni pamoja na vitu au vifaa vya kale, mila na desturi za makabila mbalimbali.

Utalii wa Asili
Huu unahusisha watalii wanaotembelea maeneo ya asili, kama mbuga za Wanyama, misitu, milima, mabonde, maziwa, mito na kadhalika.

Utalii wa Michezo
Unahusisha watalii wanaosafiri kwenda sehemu nyingine kushiriki au kuangalia aina mbalimbali za michezo. Mfano, matamasha mbalimbali ya michezo, kama Olimpiki, Kombe la Dunia la FIFA, na mengine.

Utalii wa Kidini
Utalii wa kidini ni aina nyingine ya utalii ambapo watu huenda mahali pa kidini au mahali pa kufuata nyayo za mwanzilishi wake au kuhudhuria sherehe ya kidini. Wakristo Wakatoliki, kwa mfano, wanafanya hija katika maeneo ya Misri, na Ardhi Takatifu ya Israel kujionea sehemu mbalimbali walizoishi au walizopita watu mashuhuri katika kitabu cha biblia kama Ibrahim, Yakobo, Suleiman, Yusuph, Isaka, Yesu na wengine. Kwa upande wa Waislamu, hawa hutembelea Maka, Madina na kwingineko kujionea sehemu alikopita Mtume Muhamad na wengine. Yapo maeneo mengi ya utalii wa kidini ya dini na madhehebu mbalimbali, ambayo hutembelewa na wahusika kila mwaka.

Utalii wa Matibabu au Afya
Utalii wa kimatibabu au kiafya ni aina mpya ya shughuli za utalii ambapo lengo kuu la safari ni kuboresha afya, muonekano wa mwili au usawa wa mwili. Watu wanaweza kuvutiwa kwenda hospitali au kituo cha afya kujionea huduma za kiafya zinazotolewa hapo, ili kwenda kuwahabarisha watu wengine wanaohitaji huduma hiyo, au wao wenyewe wakiwa na shida inayohitaji huduma hiyo baadaye, wawe wamejua pa kwenda.

Kila Kata Inaweza Kuwa na Vivutio vya Kitalii
Kwa kuzingatia aina za utalii nilizotaja hapo juu, utagundua kwamba utalii sii tu kwenye mbuga za Wanyama, bali unaweza kufanyika mahali Popote, na kwamba watalii sii wazungu na/au watu kutoka nje ya nchi pekee, bali pia ni watu wa nchi husika (ambao ndio wanafanya utalii wa ndani). Waafrika, na hasa Watanzania hawana utamaduni wa kutembelea vivutio vya kitalii hata vile vilivyopo maeneo yao; hali hii imepelekea serikali kutegemea mapato kutokana na watalii wa nje ambao hawafiki milioni mbili kwa mwaka.

Kati ya Watanzania milioni zaidi ya 60, wangepatikana watalii wa ndani milioni 20 tu kwa mwaka, Uchumi wa Tanzania ungepaa.

Kwa mujibu wa tovuti ya ALAT (Statistics | ASSOCIATION OF LOCAL AUTHORITIES OF TANZANIA-ALAT), kuna kata 4,263 nchini Tanzania. Serikali pamoja na wadau wengine wanaweza kubuni na kuwezesha kila kata kuwa kivutio/vivutio vya kitalii tofautitofauti kulingana na jiografia, mila na desturi ya eneo husika.

Hii ina maana gani katika swala la ajira? Kama kila kata itakuwa na waajiriwa 100 (wa moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja), kwa ujumla kutakuwa na ajira mpya zaidi ya 400,000 nchini. Kwa kiasi kikubwa, watalii watakaohusika ni wale wa ndani.

Kilelezo Na. 2: Vijana Wakishiriki Utalii wa Ndani Tanzania
Utalii wa Ndani.png

Chanzo: Site Title

Hitimisho

Utalii ni dhana pana sana, unaweza kufanyika Popote, wananchi wapaswa kuhamasishwa kuwa watalii wa ndani, jambo litakaloongeza ajira kwa vijana na kuboresha Uchumi wa nchi.

Marejeo
Statistics | ASSOCIATION OF LOCAL AUTHORITIES OF TANZANIA-ALAT

Maana ya Utalii - Elezo - 2023

Utalii - Wikipedia, kamusi elezo huru

Aina za utalii ambazo zipo

Tovuti Kuu ya Serikali | Maliasili na Utalii
 
Nchi nyingi za kiarabu zipo jangwani; vyanzo vikuu vya mapato ni mafuta na utalii! Nyingi kati ya nchi hizi zipo katika uchumi wa kati.
 
Nchi nyingi, hasa zile tunaziita zimeendelea, zinamezea mate sana rasilimali tulizonazo, na baadhi yake zinafanya kila mbinu ya kuzitumia kwa manufaa yake; wakati sisi tukiwa watazamaji!
 
Back
Top Bottom