Tanzania na China zapigana jeki katika kukuza na kutangaza sekta zao za utalii

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
VCG111228224109.jpg


Utalii nchini Tanzania umekuwa ni moja ya sekta muhimu ambayo inaingiza mapato mengi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini. Ni jambo lisilopingika kwamba Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya asili zikiwemo mandhari za kuvutia, maeneo ya kihistoria na ya kiakiolojia, hifadhi za wanyamapori wengi na baionuai mbalimbali, fukwe safi na za kuvutia na utamaduni uliosheheni makabila 158.

Ili kuongeza hamasa ya watalii kutoka nje hasa kutoka nchini China kwenda kutalii kwa wingi zaidi Tanzania na kujionea kwa macho yao vivutio hivyo ambavyo ni tunu sana duniani, Tanzania inashirikiana na China kwa lengo la kuboresha soko la China, sambamba na kuangalia ni maeneo gani wanaweza kushirikiana ili kuweza kukuza na kutangaza soko la Utalii la Tanzania. Halikadhalika Tanzania pia imeamua kubadilisha mfumo wake ili Wachina waingie kwa wingi nchini humo.

Miaka kadhaa iliyopita Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika harakati zake za kutangaza utalii wa Tanzania kwa Wachina, iliamua kumtumia muigizaji maarufu wa China anayejulikana kwa jina maarufu la ‘Maododo’ pamoja na Dkt. Jane Godaal anayetunza sokwe mkoa wa kigoma kwa sababu walionekana kuwa na mvuto kwenye jamii.

Pia katika hatua nyingine, katikati ya mwaka huu mawakala 40 kutoka kampuni kubwa za Utalii za China walikwenda Zanzibar kutembelea vivutio vya Utalii Zanzibar na Tanzania Bara wakiwa kwenye programu maalumu ya kuongeza watalii. Safari ya mawakala hao, zikiwemo televisheni za kitaifa, wasanii na wataalamu wa mitandao ya kijamii imeandaliwa na ubalozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kwa lengo la kuhakikisha wanaifahamu vyema Tanzania na Zanzibar ili waanze kuingiza kwenye misafara yao ya Utalii nchini humo.

Mkakati mwingine wa kukuza utalii wa Tanzania ambao unatia nuru matumaini ya Watanzania ya kunufaika zaidi na fursa za kiuchumi katika sekta ya utalii na uwekezaji, ni kuanzishwa kwa uhusiano wa kirafiki kati ya jiji la Dar es Salaam na jiji la Hangzhou la nchini China. Alipohudhuria kwenye hafla fupi ya kutangaza jiji la Hangzhou iliyofanyika kwenye ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Angellah Kairuki alisema ukiachilia mbali Dar es Salaam, nchi bado ina vivutio vingi akitolea mfano Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Zanzibar, Pangani, na pia ina wanyama wa kila aina.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Oktoba idadi ya watalii wa China ilikuwa ni 11,929 huku idadi hii ikiongezeka hadi watalii 36,441 mwaka 2023 katika kipindi kama hicho sawa na ongezeko la mara tatu zaidi.

Kwa maana hiyo ushirikiano huu wa majiji ni mzuri hasa ukiwa unalenga zaidi katika maeneo ya kimkakati kama vile utalii na uwekezaji. Vilevile utakuwa na tija kubwa kwani Wachina ni watu wanaopenda sana kusafiri duniani, na pia China ni miongoni mwa masoko ya kimkakati ya utalii. Tovuti ya ‘world traveller’ inasema China ni nchi inayoongoza kwa kuwa na watalii wengi zaidi duniani, ambapo takribani Wachina milioni 150 husafiri kila mwaka katika maeneo mbalimbali duniani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Watu wa Jiji la Hangzhou, Dkt Li Huolin ambaye alikwenda Tanzania kwa ajili maalumu ya kutangaza mji wake kiutalii, anaamini kwamba ushirikiano na urafiki huu utaendelea zaidi kwasababu China na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu sana.

Kwa sasa China na Tanzania ni nchi zenye muingiliano mkubwa, na kufungua milango zaidi kupitia ushirikiano maalumu kama huu kutaongeza chachu zaidi. Faida hii haitakuwa kwa majiji husika tu bali hata kwa mataifa haya mawili kwa jumla kupitia miji mingine inayoguswa na biashara na utalii.

Wakati nchi hizi mbili mwaka 2024 zinaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, zimekubaliana kuwa mwaka huo utakuwa mwaka wa kukuza ushirikiano wa Utamaduni Na Utalii Kati ya Tanzania na China.
 
Back
Top Bottom