Ajali za Barabarani ziliua wastani Mtu mmoja kila baada ya saa 5 mwaka 2022

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Mtu mmoja alifariki dunia kila baada ya saa tano na dakika 40 mwaka 2022 kutokana na ajali za barabarani, ikilinganishwa na kifo kimoja kila baada ya saa 6 na dakika 24 mwaka mmoja kabla.

Takwimu za Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani zilizochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwenye ripoti ya Tanzania in Figure 2022 jumla ya watu 1,545 walikufa kutokana na ajali 1,720 za barabarani.

Kati ya ajali hizo, mbaya zimeongezeka kutoka 1,038 mwaka 2021 hadi 1,064 mwaka jana hii ikiashiria kwa nini vifo viliongezeka.

Mfano wa ajali hizo mbaya ni ya hivi karibuni iliyogharimu maisha ya watu wanne wa familia moja, iliyotokea katika eneo la Mbwewe, Chalinze mkoani Pwani.

Wakati makosa ya barabarani yakiongezeka kwa asilimia 46 mwaka jana ikilinganishwa na mwaka juzi, ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 7 ikiwa ni idadi ndogo zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 2018.

Takriban makosa makubwa ya barabarani 1,720 yameripotiwa mwaka jana huku makosa madogo yakiwa 2,545,202.

Licha ya ajali kupungua, idadi ya vifo imeongezeka kwa asilimia 13 mwaka jana ikilinganishwa na mwaka juzi, huku idadi ya majeruhi ikipungua kutoka 2,452 mwaka juzi hadi 2,278 mwaka jana.

Jumla ya vifo 1,545 viliripotiwa mwaka jana ikiwa ni sawa na vifo 128.7 kwa mwezi, 32 kwa wiki, vitano kwa siku na kifo kimoja kila baada ya saa tano.

Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vifo 1,368 vilivyotokea mwaka juzi sawa na vifo 114 kwa mwezi, 28.5 kwa wiki, vinne kwa siku na kifo kimoja kila baada ya saa sita.

Akizungumzia sababu za kupungua kwa ajali, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Ramadhani Ng’anzi alisema ni kutokana na kuweka mikakati mbalimbali kukaniliana na hali hiyo.

Ng’anzi alisema elimu kwa umma ni miongoni mwa mikakati hiyo ikihusisha sheria na kanuni kwa watumiaji wa barabara.

“Tumekuwa tukitoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali kama vile vyombo habari, mitandao pamoja na kuwafikia watu ana kwa ana kama mashuleni, kwenye vituo vya mabasi na vijiwe vya bodaboda,” alisema Ng’anzi.

Pia alisema mkakati mwingine ni oparesheni ambazo Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani limekuwa likizifanya katika maeneo mbalimbali nchini, ili kudhibiti makosa.

Kamanda huyo aliongeza kuwa mkakati mwingine ni pamoja na ukaguzi wa magari, kufanya vipimo vya pombe kwa madereva kabla ya safari na kukagua mwendo kasi kupitia vidhibiti mwendo vilivyofungwa kwenye mabasi.

“Tumekuwa tukishirikiana na wenzetu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kufunga vidhibiti mwendo kwenye mabasi ya abiria pamoja na magari ya abiria yanayokodishwa,” alisema.

Kuhusu ajali kupungua huku idadi ya vifo ikiongezeka, Ng’anzi alisema ni kutokana na ajali moja kuua idadi kubwa ya watu.

Ng’anzi alitolea mfano ajali ya basi iliyotokea Machi mwaka huu wilayani Korogwe na kuua watu 20.

Ng’anzi alieleza sababu ya kuongezeka kwa makosa madogo akisema hiyo imesababishwa na usimamizi mkubwa unaofanywa na jeshi hilo, na ndio chanzo cha ajali kupungua.

“Tunakamata makosa madogo ili kuzuia ajali,” alisema.

Aidha alisema jeshi linaendelea na jitihada mbalimbali katika kukabiliana na ajali za barabarani zikiwemo kufuta leseni zilizotolewa kinyume na utaratibu na kuwafutia leseni madereva wasio na vigezo.

“Hatuna mzaha katika hili, kwa sababu tumebaini wengi wanatumia leseni aina hii na hawana sifa, hivyo tukiwakamata tunawafungia,”alisema Ng’anzi.

Kwa upande wake Michael Kingazi wa jijini hapa ambaye anafanya shughuli za udereva, alisema usimamizi mkubwa unaofanywa na askari wa usalama ni miongoni mwa sababu za ajali kupungua.

“Zamani ilikuwa ni rahisi mtu kuendesha mwendo kasi popote na asionekane lakini leo kuna vifaa vya kudhibiti mwendo wengi tunaogopa kupigwa faini,” alisema Kingazi.

Naye Ramadhani Mzava kutoka Mara alisema kuwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara imechangia kwa kiasi kikubwa kusaidia kupunguza ajali.

“Sasa hivi kila mahali utakutana na polisi wa usalama wakitoa elimu ya usalama, kuanzia mitaani, kwenye redio, tv mpaka kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Mzava.

Hata hivyo takwimu mpya zinaonyesha ajali zimeendelea kupungua katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo wa mwaka huu ,ikilinganishwa na miezi hiyo mwaka jana.

Takwimu hizo zilizotolewa na Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Deus Sokoni zinaonyesha ajali zimepungua kwa asilimia 17, vifo asilimia 0.4 na Majeruhi asilimia 1.
 
Yeah. Inasikitisha sana!
Baada ya Mwigulu 'kuleta' trilioni moja, nimeiomba serikali ikate apo bilioni mia moja, wawape Estim construction waendelee na upanuzi wa Morogoro rd kipande cha Dar - Moro kwa kuongeza lane moja.

Mwakani tena tukipata fursa tutaongeza lane nyingine upande wa kulia Dar - Moro.

Tukifanya hivi, baada ya miaka minne tutakuwa na bara bara ya njia nne kutoka Dar hadi Dodoma.

Tatizo watendaji wengi wa serikali wana spidi ya kono kono. Jambo moja dogo linawachukua miaka kulitekeleza.

Kwa kweli viongozi na watendaji wanatakiwa wajue kuwa tuko nyuma ya muda ukilinganisha na 'vijana wenzetu (peers) wa Kenya, Ghana, etc hivyo yatupasa kufukua mbio (ku accelerate) ili tuweze ku catch up na 'vijana wenzetu'...
 
Barabara tu ndio chanzo cha yote,
Mbovu, nyembamba, parking humo humo, service road zisio na mwelekeo na si ajabu kukuta gari la mizigo au hata mkaa kati kati ya barabara likiwa limezimwa tena usiku bila hata reflector au triangle sign, pili boda boda na bajaji kwa mjini ni hatari kuliko na kisababishi cha ulemavu na vifo vingi kwa watanzania
 
Back
Top Bottom