A
Anonymous
Guest
JE ILIKUWA NI AHADI HEWA YA KUPITISHWA NA KUANZA UTEKELEZAJI WA MUUNDO WA UTUMISHI KWA SEKTA YA AFYA (KADA YA UUGUZI NA UKUNGA) KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026 ILIYOTOLEWA NA OFISI YA RAIS – MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA MWEZI MEI 2025?
- Habari,
- Kwa masikitiko makubwa napenda kuwasilisha kero yangu kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hasani kuwa, watumishi wa kada ya afya nchini wanataka majibu ya kwanini walidanganywa kuhusu utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi wa kada ya uuguzi na ukunga nchini kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambao kimsingi unagusa maslahi yao kama watumishi wa umma.
- Wauguzi na wakunga nchini ni kiuongo muhimu katika idara ya afya lakini wamekuwa hawatendewi haki ipasavyo kwani serikali kupitia watendaji wake imekuwa ikiwaahidi mara nyingi kuhusu utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi kwa kada ya uuguzi/ukunga pasipo mafanikio wakati wa mikutano ya kitaaluma ambayo hufanyika mwezi Mei kila mwaka kwa ajili ya kuadhimisha kilele cha siku ya wauguzi duniani.
- Upitishwaji na utekelezwaji wa muundo huu mpya utaondoa kero ya unyonyaji kwa muuguzi /mkunga mwenye shahada (Degree) anayeajiriwa kwenye utumishi wa umma ya kuanza na ngazi ya mshahara ya TGHS C ya muundo wa utumishi wa kada ya afya wa mwaka 2009 (https://hssrc.tamisemi.go.tz/storage/app/uploads/public/5ac/0df/f38/5ac0dff383516084704482.pdf) badala ya TGHS D iliyopo kwenye muundo mpya unaopendekezwa.
- Hii ni haki ya muuguzi/mkunga mwenye shahada kuanza na mshahara wa TGHS D kwani muuguzi huyo ili apate shahada anapaswa kusoma miaka minne darasani na mwaka mmoja wa mafunzo tarajali yaani internship, hivyo inapaswa aanze na mshahara wa TGHS D kwani mishahara yote ya watumishi wa kada nyingine za afya kwenye muundo wa mwaka 2009 imezingatia miaka ya masomo tofauti na ilivyo kwa wauguzi/ wakunga nchini. Mfano madaktari wenye shahada wanasoma miaka mitano darasani + mwaka mmoja wa internship mshahara wao unaanza na TGHS E, Wafamasia wenye shahada wanasoma miaka minne darasani + mwaka mmoja wa internship mshahara wao unaanza na TGHS D, Wataalamu wa maabara wenye shahada wanasoma miaka mitatu darasani + mwaka mmoja wa internship mshahara wao unaanza na TGHS C wakati huo Wauguzi/wakunga wenye shahada wanasoma miaka minne darasani + mwaka mmoja wa internship lakini mshahara wao unaanza na TGHS C ).
- Pia muundo huu mpya utatoa motisha kubwa kwa watumishi wa kada ya afya wakiwemo wauguzi/wakunga kujiiendeleza kielimu kwa ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi hivyo kuongeza tija katka utoaji wa huduma za afya nchini kwakuwa muundo huo mpya unatambua rasmi kiwango hicho cha elimu hivyo mtumishi atafaidika moja kwa moja kupitia ngazi ya mshahara bila kuangalia yupo kwenye ngazi ipi ya kituo cha kutolea huduma za afya hapa nchini.
- Vilevile muundo huu mpya utakuwa jawabu na mwarobaini wa watumishi wa umma wengi wa idara ya afya (ambao tayari ni mabingwa/bingwa bobezi) waliopo ngazi za chini za vituo vya kutolea huduma za afya hasa mikoani/wilayani (TAMISEMI) kuvihama vituo vyao na kwenda hospitali zilizopo mjini kama za rufaa za kanda au Taasisi kama vile MNH,BMH,JKCI,BMC,MOI etc na hospital kubwa za binafsi ambazo zina fursa nyingi ikiwa ni pamoja na miundo yao ya utumishi ambayo inawapa maslahi makubwa kupitia mshahara na motisha mbalimbali.
- Kipekee wauguzi/wakunga wa Tanzania wanatamani kupata majibu (kwa vitendo) ya ahadi iliyotolewa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani iliyofanyika mkoani Iringa Mei 2025 na kisha kutangazwa rasmi na Naibu Waziri wa afya kwenye tovuti ya wizara kwamba muundo umepitishwa na utekelezaji unaanza mwaka wa fedha 2025/2026 (ambapo hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika), Angalia ahadi hiyo hapa https://www.utumishi.go.tz/news/naibu-waziri-sangu-atangaza-muundo-mpya-wa-utumishi-wa-kada-ya-uuguzi-na-ukunga-kuanza-kutumika-mwaka-fedha-2025-2026?utm
- Tunaomba utekelezaji ufanyike mara moja kama ivyoahidiwa kwani ni fedheha kwa serikali kutoa ahadi ya uongo kwa watumishi wake kwasababu kufanya hivyo inatafsirika kama dharau na kejeli kwa watu wanaopambana na kujitoa usiku na mchana kwaajili ya watanzania huku hali zao zikibaki kuwa duni!. Je wategemee tena ahadi hewa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambayo imepangwa kufanyika mkoani Arusha mwezi Mei 2026?
- NB: NImekuwekea tangazo rasmi la muda wa mafunzo ya shahada ya uuguzi na ukunga lilitolewa na baraza la wauguzi na wakunga Tanzania na Muundo mpya unaopendekezwa kwaajili ya rejea, asante.