Yule mwimbaji wa CCM sijamsikia kipindi hiki .Kulikoni? Yu wapi?
Komba huyu hapa:
Komba alia bei ya
sukari kwa Kikwete
*Asema Mbambabay inauzwa 3000/- hadi 3500/-
Na Suleiman Abeid, Mbambabay
MGOMBEA ubunge katika jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kapteni John Komba amemuomba Rais Kikwete awasaidie kuwatatulia kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jimbo lake ikiwemo ukosefu wa sukari ambayo sasa wanalazimika kuinunua kati ya sh. 3,000 na 3,500.
Kapteni Komba alitoa ombi hilo jana alipokuwa akielezea mafanikio ya utekelezaji wake Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete uliofanyika mjini Mbamba Bay.
Kapteni Komba alisema mbali ya tatizo la ukosefu wa sukari kwa wakazi wa Jimbo la Mbinga Magharibi hata huduma za afya hivi sasa hazipatikani kwa uhakika.
Alisema hali hiyo inasababishwa na hospitali teule katika mji huo inayomilikiwa na Kanisa la Anglican kusimamisha kutoa huduma zake kwa wananchi ambapo hata
wafanyakazi wake hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi 11 sasa.
Alisema baada ya serikali kuunda wilaya mpya ya Nyasa ingekuwa vyema hivi sasa pakajengwa Hospitali ya wilaya ili kuondoa tatizo la ukosefu wa huduma za
matibabu kwa wakazi wa wilaya hiyo mpya.
Mheshimiwa Rais pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita katika sekta za elimu, kilimo na huduma za kijamii, lakini hapa kwetu tuna matatizo kadhaa makubwa ambayo kwa kweli tunaomba utusaidie kuyapatia
ufumbuzi, alieleza Kapteni Komba na kuongeza,
La kwanza ni tatizo la ukosefu wa sukari, hatuna sukari hapa, na hata pale inapopatikana tunalazimika kuinunua kati ya sh. 3,000 na 3,500 ni bei kubwa
sana, hata ile ya kutoka nchi jirani ya Malawi ni sh. 1,500, sasa hili tusaidiwe, tunafikiri tukiruhusiwe kufanya biashara na wenzetu wa Malawi itasaidia
kutupunguzia tatizo, alieleza.
Aidha Kapteni Komba aliomba serikali iboreshe bandari iliyopo Mbamba Bay ili iweze kufanya kazi zake vizuri kuliko hali ilivyo hivi sasa, ambapo alisema ikilinganishwa na ile ya nchi jirani ya Ngata Bay, havilingani kabisa.
Pia aliomba serikali iwasaidie wakazi wa Mbamba Bay wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi kwa kuwapa elimu ya kutosha kwa kuwapatia nyavu zinazoruhusiwa kisheria ili waweze kuendesha shughuli zao na kuweza kuinua vipato vyao.
Akijibu maombi hayo Rais Kikwete alisema serikali inafanya utaratibu wa kuijenga upya bandari ya Mbamba Bay na kwamba suala la sukari atafanya utaratibu wa
kuzungumza na watu wa serikali ya Malawi ili kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa sukari.
Kuhusu suala la hospitali alisema serikali inafanya utaratibu wa kukipandisha hadhi kituo cha afya kilichopo ili kiwe na hadhi ya wilaya baada ya kuundwa kwa wilaya mpya ya Nyasa.
Pia Rais aliwaahidi wakazi wa Mbamba Bay kuwa katika kukabiliana na tatizo la usafiri katika Ziwa Nyasa, serikali itanunua meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani
400 na kwamba mipango ya ununuzi wa meli hiyo ipo mbioni kukamilika.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amewaahidi wakazi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma iwapo atachaguliwa tena kuongoza nchi atahakikisha anasaidia kukifufua Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima Mbinga (MBICU).
Alisema iwapo wananchi watampa tena ridhaa ya kuendelea kuwa Rais wa Tanzania kwa mara ya pili moja ya mambo atakayoyashughulikia baada ya kuunda serikali yake
itakuwa ni kulipa deni la sh. milioni 400 ambazo chama hicho cha ushirika kinadaiwa na benki.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka wanachama wa ushirika huo kuhakikisha wanajipanga vizuri kwa kutorudia makosa yaliyosababisha ushirika wao ufilisike kama ilivyotokea huko nyuma kwa kutowachagua tena viongozi wabadhirifu wa mali za ushirika.
Ndugu zangu nakuhakikishieni iwapo mtanipa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, moja ya mambo nitakayofanyia kazi ni kusaidia kukifufua chama chenu cha ushirika, tutawasaidia kulipa deni mnalodaiwa la sh. milioni 400, hizi tutazilipa, lakini hakikisheni hakiyumbi tena, alieleza Rais Kikwete. Source
Majira