NI mwanasiasa ambaye maisha yake yamegubikwa na usiri mkubwa. Wapinzani zake wamejaribu kuchokonoa ili kupata chochote watakachokitumia kama silaha katika kampeni zao za uchaguzi wa urais nchini Urusi, bila mafanikio.
Hata watu wake wa karibu, wameishia kumfahamu kijuu juu, ingawa wanakiri upole wake, kutokuwa na majivuno, mchukiaji wa rushwa na sifa nyinginezo nzuri tu, achilia mbali ile moja hasi inayotawala hivi sasa wakati akielekea kuikwaa nafasi ya juu zaidi ya Taifa linalojaribu kurudisha heshima na ubabe wake kama ilivyokuwa wakati wa Vita Baridi, lilipokuwa likishindana na Marekani.
Aidha, kwa watu hao wanaomjua Dmitry Medvedev wanamwelezea kuwa mtu mwenye akili na mchapakazi makini katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa.
Lakini je; anayo sifa ya kisiasa ya kuweza kuwa Rais mpya ajaye wa Urusi? Ni swali linalosumbua vichwa vya wengi, huku wadadisi wengi wa mambo wakitabiri chini yake, Urusi itaongozwa kwa ‘remote control' ya Rais wa sasa, Vladimir Putin.
Anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa urais utakaofanyika Jumapili wiki hii, ubashiri uliotolewa tangu mshirika wake wa karibu na wa muda mrefu wanayetoka eneo moja, Rais Vladimir Putin, alipompitisha awanie kuchukua nafasi yake mwaka jana.
Akiwa ameibuliwa na Putin kutoka kusikojulikana, haiba na sifa binafsi za Medvedev zinaelezwa kuendana na malengo ya Putin, anayehitaji mshirika mtiifu na wa uhakika katika kutimiza dhamira yake ya kuendalea kuiweka Kremlin (Ikulu ya Urusi), katika kiganja chake hata baada ya kumaliza muhula wake wa urais.
Rais Putin pamoja na kuchukiwa na nchi za magharibi, lakini zinakiri kwamba anao umaarufu mkubwa nchini mwake kutokana na sababu kadhaa, zikiwamo kurudisha heshima ya nchi kimataifa, kufanikiwa kufufua uchumi wa nchi hiyo uliokufa baada ya kumeguka kwa uliokuwa Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR) mapema miaka ya 1990 na kadhalika.
Kwa kutumia umaarufu huo, ambao imefikia kiasi cha baadhi ya Warusi kutaka awanie tena urais ili aweze kutimiza azma zake, hususan heshima na ushawishi wake wa huko nyuma, Rais Putin badala ya kuwania mwenyewe, ameamua kuheshimu Katiba ya nchi yake, akitegemea kutumia mlango wa nyuma kuliongoza Taifa hilo, ikiwamo kutarajia cheo cha uwaziri mkuu.
Aidha, Putin anaelezwa kulenga kurudia urais baada ya muhula wa Medvedev utakapoisha miaka minne ijayo kutokana na Katiba ya Urusi kuruhusu.
Baadhi ya washirika wa zamani wa Medvedev waliohojiwa na kuomba kutotajwa majina yao, pamoja na kukiri juu ya uwezo, umahiri, uadilifu na ujanja alionao Medvedev, uwezo wa kujijengea mamlaka yake mwenyewe, bado una utata.
"Dima ni mjanja. Mjanja vya kutosha kuwa Rais, na ni imara, imara vya kutosha kuwa Rais," anasema mmoja wa washirika wake wa enzi za miaka ya 1990, wakati akiliambia Reuters kwa masharti ya kutotajwa.
Anaendelea: "Lakini uwezo, hisia za kikachero, uwezo wa kutoa maamuzi pale Kremlin, Rais Putin alibarikiwa nayo, kama ilivyokuwa kwa Rais wa zamani, Boris Yeltsin. Je; Dima? Hilo sijui lakini wacha tuone." Dima ni kifupi cha jina Dmitry Medvedev.
Iwapo atashinda uchaguzi huo, Medvedev mwenye umri wa miaka 42, atakuwa kiongozi kijana zaidi wa Urusi tangu mtawala wa mwisho wa nchi hiyo, Tsar Nikolai II.
Aidha, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Urusi anayetoka katika sekta binafsi ya biashara.
Kulinganisha na Rais Putin, kachero wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Urusi (KGB), ambaye anatuhumiwa kurudisha nyuma demokrasia, Medvedev, mwanasheria wa zamani wa nchi hiyo, anasisitiza umuhimu wa uhuru na sheria.
Aidha, ameifurahisha sekta ya masoko wakati aliposema anataka kuweka ukomo kwa Kremlin kujishughulisha katika makampuni makubwa.
Lakini zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya uchaguzi wa urais, maisha binafsi ya Medvedev yamebakia kuwa siri.
Mtu ambaye mwenyewe binafsi husema anajiweka wazi kwa umma, ndiye huyo ambaye upande wa pili wa kampeni hauna kitu chochote cha kumhusisha juu ya tabia na historia yake.
Amekataa kushiriki katika mijadala ya televisheni, na ni mara moja tu alifanya mahojiano ya moja kwa moja kama sehemu ya kampeni zake.
Waziri Mkuu wa zamani wa Urusi, Mikhail Kasyanov, enzi zile Medvedev akifanya kazi katika ofisi ya Putin, Kremlin, alijalibu kujitutumua kumshambulia Medvedev akisema:
"Hana lolote. Ni mmoja wa wale wafanyabiashara warasimu tulio nao." Kasyanov, ambaye ameondokea kuwa mkosoaji mkali wa Kremlin baada ya kufukuzwa uwaziri mkuu mwaka 2004, anajitutumua akisema hoja ambayo haina uzito wowote mbele ya wengi.
Hata wafuasi wa Medvedev, hawana mengi ya kumhusu. "Ni mtu mzuri, mtu mzuri tu," kilisema chanzo kimoja cha habari kilichopo karibu na Kremlin na kuongeza: "Hufanya kila anachoona chema kwa uangalifu."
"Ni mpenda utamaduni mno. Unaweza kumzungumzia kuhusu maonyesho ya sanaa za utamaduni na muziki," anasema Nataliya Rasskazova, ambaye alisoma na Medvedev katika kitivo cha sheria cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Petersburg, ambacho pia alisomea Putin.
"Hajabadilika. Nilimuona mwaka mmoja uliopita, na hana majivuno, hana ubwana mkubwa wala fahari," alimwagia sifa.
Medvedev alifundisha sheria baada ya kuhitimu masomo yake, kabla ya kwenda kufanya kazi kwa Putin, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya masuala ya Nje, chini ya Meya wa Mji wa Mtakatifu Petersburg.
Ni katika kipindi hicho pia Medvedev aliingia rasmi katika anga za biashara. Alifanya kazi kama mwanasheria muhimu wa Kampuni ya Ilim Pulp, akisaidia wakati wa mchakato wa uanzishaji wa kampuni hiyo, ingawa wafanyakazi wenzake wa wakati huo wanasema, hakuwahi kutendewa sawa sawa na wamiliki wa kampuni hiyo.
Kampuni hiyo ya mbao, kwa sasa imeibukia kuwa moja ya makampuni makubwa yanayoongoza katika sekta hiyo ya biashara nchini Urusi, ikiwa na imewekeza mabilioni ya dola za Kimarekani.
"Alipata mshahara na wakati huo, akawa mfanyabishara kamili katika miaka 1990," anasema mmoja wa wafanyakazi wenzake wa zamani.
Wafanyakazi wake wa zamani wanasema Medvedev, hakuwa mtu wa kawaida linapokuja suala la uadilifu. Aliepuka kutoa rushwa, na alikuwa tayari kuona kampuni yake inapoteza kesi mahamani hata kama itaigharimu kampuni, kwa sababu hakuwa tayari kumpatia hongo hakimu.
Maisha ya awali ya Medvedev. Dmitry Anatolyevich Medvedevlisten, alizaliwa Septemba 14, 1965 katika kitongoji cha Leningrad, akitoka katika familia ya walimu wa chuo kikuu, na alikulia katika kitongoji hicho hicho, kilichoko mjini Kupchino.
Alimaliza masomo yake ya sheria katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Leningrad mwaka 1987, akiwa na kina Ilya Yeliseyev, Anton Ivanov, Nikolay Vinnichenko na Konstantin Chuychenko, kabla ya kujipatia Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria mwaka 1990, katika chuo hicho hicho.
Anatoly Sobchak, aliyekuwa mmoja wa wanasiasa wana demokrasia wa mwanzo nchini humo, na hasa katika miaka ya 1980 na 1990, alikuwa mmoja wa maprofesa wake, kabla ya Medvedev baadaye kushiriki katika kampeni zilizofanikiwa, za Sobchak, kwa kuukwaa Umeya wa Mji wa Jiji la Saint Petersburg.
Mwaka 1990, alifanya kazi katika Manispaa ya Leningrad, kabla ya mwaka kati ya 1991 na 1999, kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Leningrad, sasa Chuo Kikuu cha Taifa cha Saint Petersburg kama mwalimu wa sheria.
Aidha, kati ya mwaka 1991 na 1996, alifanya kazi kama mtaalamu wa sheria katika Kamati ya Uhusiano wa Kigeni, katika Ofisi ya Meya wa Mji wa Saint Petersburg, iliyokuwa chini ya Putin.
Novemba 1993, Medvedev alifanywa kuwa Mkurugenzi wa masuala ya Sheria wa Kampuni ya Ilim Pulp Enterprise, kampuni inayojishughulisha na ununuzi na uuzaji wa mbao katika jiji la St. Petersburg.
Mwaka 1998, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda cha Karatasi cha Bratskiy LPK.
Kuiingia katika siasa Novemba 1999, Rais huyo mtarajiwa wa Urusi, alikuwa mmoja wa watu kutoka St. Petersburgers, walioletwa na Putin kushika nafasi za juu serikalini.
Desemba mwaka huo huo, aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Watumishi wa Rais, Ikulu, kabla ya kuwa mmoja wa wanasiasa walio karibu na Rais Putin, na hata wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000, alikuwa Mratibu Mkuu wa Kampeni za Rais, akiwa makao makuu.
Kuanzia mwaka 2000 hadi 2001, Medvedev alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Gazprom, kabla ya kufanywa Naibu Mwenyekiti, kati ya mwaka 2001 na 2002.
Juni 2002, Medvedev alifanywa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Gazprom kwa mara ya pili, kabla ya Oktoba 2003, kuchukua nafasi ya Alexander Voloshin, kuwa Mnadhimu Mkuu wa Watumishi Ikulu.
Novemba 2005, aliteuliwa na Rais Putin kuwa Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu, Naibu Mwenyejkiti wa Kwanza wa Kamati ya Utekelezaji wa Miradi ya Kipaumbele ya Taifa ya Shirikisho la Urusi, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utendaji.
Akiwa mtu mtaratibu, Medvedev anahesdabiwa kuwa Mliberali wa kisasa, mwenye nadharia ya vitendo, mtendaji mahiri na mfuasi mtiifu wa Putin.
Aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa Urusi, Novemba 14, 2005, kabla ya Desemba 10, mwaka jana, kupitishwa kuwa mgombea urais wa Chama Tawala cha Urusi, cha United Russian, na uteuzi wake rasmi ulifanywa wiki moja baadaye, Desemba 17.
Kugombea kwa Medvedev katika nafasi hiyo ya urais kunaungwa mkono na Putin mwenyewe pamoja na vyama vingine washirika.
Taasisi Huru ya Urusi, ya Levada Center, iliendesha kura ya maoni kati ya Desemba 21 na 24, mwaka jana, maoni ambayo yameonyesha kwamba asilimia 79 ya Warusia, wako tayari kumpigia kura Medvedev, iwapo uchaguzi ungefanyika wakati huo.
Zaidi ya kuwa mwanasiasa mteule, mfanyabiashara na mwanasheria, Medvedev hajawahi kushiriki na kuchaguliwa katika madaraka yanayohitaji uchaguzi.
Akiwa tayari kushiriki, anatarajia kuachia ngazi uenyekiti wa Gazprom, kwa sababu katika sheria ya sasa nchini humo, Rais haruhusiwi kushika wadhifa mwingine katika taasisi yoyote ile.
Vyanzo vilivyo karibu na kampuni ya Gazprom na Medvedev, vililiambia gazeti la Vedomosti kwamba nafasi ya Medvedev, huenda ikashikwa na Putin katika kampuni hiyo.
Aidha, Medvedev, alipitishwa rasmi kuwa mgombea halali wa urais na Tume ya Uchaguzi ya Urusi, Januari 21, mwaka huu.
Kama ilivyovumishwa kwa muda mrefu, mara baada ya kupitishwa kuwania urais, Medvedev alitangaza kwamba akiwa Rais wa Urusi, atamteua Putin katika wadhifa wa uwaziri mkuu.
Ingawa anazuiwa na Katiba kuwania urais kwa muhula wa tatu mfululizo, wadhifa kama huo wa uwaziri mkuu, utamruhusu Putin kuendelea kuwa Rais wa kitaifa, na Katiba pia itamruhusu kurudi katika urais iwapo atapenda hapo baadaye.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kwamba kauli ya Medvedev, ya kumteua Putin kuwa Waziri Mkuu, inaonyesha namna atakavyokuwa kama ‘Rais pambo tu.'
Ingawa Putin ameahidi kutobadilisha mamlaka kati ya Rais na Waziri Mkuu, wachambuzi wengi wanategemea madaraka mengi kuinuliwa kutoka urais kwenda uwaziri mkuu, iwapo Putin atapewa wadhifa huo chini ya urais wa Medvedev.
Jambo jingine muhimu kwa Medvedev, ni kwamba Desemba 2005, aliteuliwa na Expert Magazine, kuwa Mfanyabiashara Bora wa Mwaka. Hilo ni gazeti maarufu linaloheshimika kibiashara nchini humo, linalochapishwa kila mwezi.
Alitwaa Tuzo hiyo sambamba na Alexei Miller, Ofisa Mkuu Mtendaji wa Gazprom.
Medvedev ni baba wa familia yenye motto mmoja wa kiume, Ilya, aliyezaliwa mwaka 1996 kwa mkewe Svetlana Vladimirovna Medvedev. Kabla ya kuoana wawili hawa walikuwa marafiki wakati wa utotoni, wakiwa shuleni.
Walioana miaka kadhaa baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1982.
Medvedev ni mmoja wa waandishi wa kitabu kinachoelezea masuala ya sheria ya kiraia kwa vyuo vikuu, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1991, na ambacho kinaheshimika vyuoni na wanafunzi wengi wa kiraia.
Aidha, ni mwandishi wa kitabu cha vyuo vikuu kijulikanacho kama Questions of Russia's National Development, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka jana, kuhusiana na jukumu la Taifa la Urusi katika sera za maendeleo ya uchumi na jamii. Aidha, ameshiriki kuandika vitabu vingi vingine vya sheria.
Huyo ndiye Dmitry Medvedev