Responded Wizara ya Ujenzi: Wanaosafirisha mizigo mikubwa waache kutumia vishoka kuomba vibali, wanakwamisha kazi

Responded Wizara ya Ujenzi: Wanaosafirisha mizigo mikubwa waache kutumia vishoka kuomba vibali, wanakwamisha kazi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
4,783
Reaction score
14,975
Baada ya Mdau wa JamiiForums.com kuandika Wizara ya Ujenzi ishughulikie ucheleweshwaji wa vibali vya usafirishaji wa mizigo maalumu (Special Load Permits) katika Mfumo wa ePermit , Wizara ya Ujenzi imetoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Hoja ya Mdau ~ Wizara ya Ujenzi ishughulikie ucheleweshwaji wa vibali vya usafirishaji wa mizigo maalumu (Special Load Permits) katika Mfumo wa ePermit

Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Kashinde Musa amefafanua:

"Usafirishaji wa mizigo unatawaliwa na sheria ya Afrika Mashariki, inaitwa East African Community Vehicle Load Control Act 2016, pamoja na sheria hiyo, kuna Kanuni zake za Mwaka 2018.

Kanuni hizo zimegawanyika katika sehemu tatu: Kuna Kanuni za Special Load, kuna Kanuni za Enforcement, na kuna Kanuni za Dimensions and Axle Configuration.

Hayo yote yanafanyika kudhibiti matukio ya ajali, ikiwa ni sehemu ya tahadhari.

Kisheria, msafirishaji yeyote anayesafirisha mzigo ambao ni hatari (hazardous) au mzigo ambao haugawanyiki na unazidi vipimo vya kawaida (abnormal load), lazima aombe kibali maalum kutoka kwa Mamlaka ya Barabara (Road Authority), ambayo ni Wizara ya Ujenzi.

Sheria inasema ukiomba kibali, unaweza kujibiwa ndani ya siku 30, lengo ni kuipa mamlaka muda wa kufanya ukaguzi wa barabara na madaraja ili kuona kama mzigo huo unaweza kupita kwa usalama.

Hata hivyo, Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi imerahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kupitia mfumo wa kieletroniki wa Special Load Permit System ambapo msafirishaji akiomba kibali anauwezo wa kukipata ndani ya saa 24 endapo maombi yake hayatakuwa na changamoto yoyote.

Muda huo wa saa 24 unaipa nafasi Wizara kupitia wataalamu wake kuchakata maombi hayo na kuona sahihi wa vipimo ili kuepuka kuleta madhara ya ajali katika barabara na watumiaji wengine wa barabara.

Kumbuka kwamba kuna wakati tunapata maombi takribani 300 kwa siku moja, hivyo muda huo unahusisha kujiridhisha taratibu mbalimbali za usafirishaji mzigo husika na kukagua vibali kulingana na aina ya safari.

Tukikagua tukagundua kuna shida mhusika anapewa mrejesho kurekebisha, kusafirisha mizigo mikubwa mara nyingi sio suala la dharura, mara nyingi linajulikana.

Gharama ya kibali hiki ni Dola za Kimarekani 10 tu ($10). Malipo yanafanyika kwa shilingi ya Tanzania kupitia Control Number unayopewa kwenye mfumo, ambayo ni takriban shilingi 24,000 mpaka 25,000 kulingana na viwango vya kubadilishia fedha.

Changamoto kubwa tunayoiona ni kuwepo kwa mawakala au 'vishoka'. Hawa watu wanawaambia wasafirishaji kuwa kupata kibali ni vigumu au mfumo unasumbua, kisha wanawatoza fedha nyingi, hadi shilingi 100,000 au zaidi, wakati gharama halisi ni ile ya serikali ya dola 10. Vishoka hawa pia huchelewa kuomba vibali na kusingizia mfumo, jambo ambalo si kweli.

Ili kusaidia wasafirishaji, Wizara imeanzisha Kundi la WhatsApp la Mtandaoni linalojulikana kwa jina la E-Permit Transporters, humo ndani kuna maafisa wa Wizara ambao wanatoa msaada wa kiufundi na majibu ya papo hapo kwa msafirishaji yeyote anayepata changamoto kwenye mfumo.

Lengo la vibali hivi si kuzuia biashara, bali ni kulinda miundombinu yetu.

Barabara hizi zimejengwa kwa gharama kubwa na kodi za wananchi, kwa mfano, kama mzigo una upana wa mita tano kwenye barabara yenye upana wa mita sita, lazima kuwe na masharti ya usalama kama magari ya ulinzi (Escort Vehicles), bendera nyekundu, na wakati mwingine kutumia polisi ili kuzuia ajali kwa watumiaji wengine wa barabara.

Kwa mizigo ya mifugo, sasa hivi tumeweka mfumo wa automation zaidi kwa sababu haina changamoto kubwa ya uzito unaoharibu miundombinu kama ilivyo kwa mizigo mingine ya viwandani.

Vilevile, Wizara kwa sasa inafanya mapitio ya mfumo huo wa kieletroniki ili kuuboresha zaidi hivyo muda utakapofika wasafirishaji watapewa nafasi ya kutoa maoni yao ili yaweze kuzingatiwa wakati wa maboresho stahiki

Tunawasihi wasafirishaji watumie mfumo wenyewe ili kuepuka gharama zisizo za lazima na kucheleweshewa mizigo yao."
 
Back
Top Bottom