Hata hivyo hili linanipeleka kwenye point nyingine kuwa kuna wakati ambapo bondia hata asiye na rekodi ya kutisha anaweza kujijengea jina inapotokea nafasi ya kupambana na bingwa wa dunia! Douglas Douglas hakuwa anajulikana na hakupewa nafasi ya kufanya vizuri hadi pale alipombumunda (notthe same as mabumunda) Mike "Iron" Tyson! Kuna wakati ambapo mpigani uoneshe kuwa unasimama kwa nguvu zako mwenyewe na siyo ahadi, sifa, au majina ya kujipachika au kupachikwa.
Mzee Mwanakijiji, heshima mbele mkuu!
kwanza nakubaliana na maneno machache ya Mzee Kitila Mkumbo kuwa kwa Kikwete "Urais ilikuwa ni accomplishment. Mzee Kitila made my day. Hakika, ukimuondoa Salim miongoni mwa waliokuwa wanautaka Urais mwaka 2005, ni Kikwete peke yake aliyekuwa ameranda randa dunia nzima na kukutana na viongozi wa mataifa yote duniani kuzidi mgombea mwingine yeyote. Binafsi, nilidhani kitendo cha kumchagua Kikwete kuwa Rais kingejenga imani miongoni mwa watanzania kuwa kiti chetu cha henzi kimekaliwa na Rais ambaye si limbukeni wa safari za nje ya nchi zinazowagharimu watanzania mamilioni ya fedha.
Rais wa Tanzania sio mtu binafsi bali ni Taasisi. Tungekuwa na ahueni tena mara dufu kama mtu binafsi aliyekalia taasisi ya Urais angekuwa na nia ya dhati kuwa kitendo cha kukalia hiyo taasisi in it and itself is an accomplishment. Basi tungemwombea ili amalize kipindi chake haraka sana so that we can move on. Lakini sheria ya asili inatutahadharisha. Wahenga walisema kuwa "nature abhors vacuum"-hulka huchukia hombwe. Hofu yangu kubwa sio kwa Kikwete anayefikirika kuiona Taasisi ya Urais as an accomplishment, and therefore a dead end. Hofu yangu ni wale wanaomtumia mtu aliyekalia Taasisi ya Urais wa nchi yetu in order to achieve something, ikizingatiwa kwamba mtu mwenyewe yupo kama hayupo.
Anyway, Mzee mwanakijiji unasema kuwa Douglas alikuwa hajulikani na hakupewa nafasi ya kufanya vizuri. Well, nadhani kujulikana sio sifa ya ubora bali ni sifa ya kutang'aa. Mara nyingi bidhaa inajulikana kwasababu ya matangazo. Kumbuka mapambano ya ngumi za uzito wa juu duniani ni miradi mikubwa kwa makampuni mengi ya kibepari. Mabondia wanauzwa kama bidhaa kabla ya mapambano. Biashara inayosifika kwa matangazo inahitaji umakini wa hali ya juu kutoka kwa wanunuzi. Bahati mbaya siasa za nchi yetu zimegeuka kuwa miradi mikubwa kwa makampuni ya kibeberu. Wanasiasa wanauzwa kama bidhaa.
Ni mkosi, ni nuksi, ni balaa, na ni bahati mbaya kuona biashara ya namna hii inafanyika katika nchi yetu. Nasema hivyo kwasababu watanzania baada ya uhuru hatukupewa nafasi ya kufanya mijadala ya wazi wazi kuhusu mambo ya siasa. Baada ya kukabwa kabali kwenye medani ya kisiasa, tulipumulia katika michezo. Mijadala ya michezo hasa mpira wa miguu ilishamiri mijini na vijijini katika virabu vya pombe, Migahawani, vituo vya mabasi, majumbani, mashuleni na vyuoni. Bahati mbaya tukazaa Mashabiki wengi wa mpira kuliko tulivyozaa wapenzi wa mpira.
Mshabiki ni yule anayependa kitu bila sababu. Mpenzi ni yule anayependa kitu akiwa na sababu za msingi. Wapenzi wanajadiliana kabla ya usajili wa wachezaji wa timu yao. Wanakosoana na kukubali makosa kabla ya mpira kuanza. Hata wakishindwa, wanakubali kwa dhati ya moyo wao kwasababu wanatambua udhaifu wa timu yao. Kwa wapenzi, kushindwa ni changamoto na wala sio nafasi ya kupigana mieleka. Ni fursa ya kuchanga bongo kwa lengo la kuondoa udhaifu na kujenga timu yenye kuleta ushindi.
Mashabiki wanafanya mambo kinyume na wapenzi. Hata timu yao ikimsajili golikipa ambaye ni kipofu, mashabiki watatetea huo uozo hata kwa ncha ya upanga. Wakifungwa watavulumushiana matusi, masumbwi, na kubwatabwata kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu. Eti wameshindwa kwasababu uwanja ulikuwa na maji, kana kwamba timu iliyowafunga ilichezesha Samaki. Vitendo hivi vya kiushabiki ni mojawapo ya sababu zilizoigalgaza michezo yetu nchini. Sasa tunashabikia timu za Ulaya ambazo zina wapenzi wengi kuliko Mashabiki.
Nimeongelea suala la ushabiki na upenzi kwasababu baada ya kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, ushabiki uliokuwa mpirani ulihamia kwenye duru za siasa. Ndio maana siku hizi ukichanganya mpira na siasa watu wanapata kiwewe. Lakini ukweli ni kwamba nchi yetu inakabiliwa na tatizo la kuwa na idadi kubwa ya mashabiki wa vyama vya siasa kuzidi idadi ya wapenzi wa hivyo vyama. Wengi wanavishabikia vyama bila sababu, na vikifanya usajili wakati wa kinyanganyiro cha kugombea nafasi za uongozi, ushabiki unatawala kuliko upenzi. Kumwaga tindikali kwenye kidonda, makampuni ya kibeberu yanakuja na mfumo wa matangazo ya kuwauza wanasiasa wetu kama bidhaa sokoni. Wananchi wanaishia kuchagua hizo bidhaa (wanasiasa) kutokana na hayo matangazo ambayo nyuma yake wamejificha mabeberu.
Ni kweli, Tyson alikuwa ni moto wa kuotea mbali wakati anapigana na Douglas. Alikuwa na wapenzi pamoja na Mashabiki wengi. Tyson alijijengea sifa kwa kuwakwida mabondia luluki. Umaarufu wake haukuwa na doa. Kwa mtu aliyejijengea jina kama Tyson, ni rahisi kwa kila kampuni ya kibepari kutaka kuwekeza kwenye jina lake. Mantiki ni kuwekeza mtaji wa fedha kidogo kwa faida kubwa. Lakini hiyo haimaanishi kuwa Tyson hakuwa na kasoro za msingi. Pia, si kweli kwamba Douglas hakuwa bondia bora kabla ya lile pambano. Ni kwamba hakuna kampuni iliyokuwa tayari kuwekeza fedha kwa utangaza ubora wa Douglas.
Kumbuka "wapenzi" wa kambi ya Tyson, kabla ya lile pambano walianza kuingiwa na wasiwasi kuwa hakuna bondia yeyote aliyewahi kumfikisha Tyson katika raundi ya kumi. Yalikuwepo majadiliano kuwa pamoja na ubora wa Tyson, hajawahi kupigwa ngumi nyingi na akaanguka chini alafu akainuka na kumtwanga mpinzani wake mpaka akashinda. Uso wake ulikuwa haujapigika na walikuwa hawajuhi uvumilivu wake wa masubwi ni wa kiasi gani kama angepata bondia wa kumfikisha katika hali hiyo. "Mashabiki" wa Tyson hawakulifikiria suala hilo kwasababu walijua kuwa konde moja la Tyson likimpata bondia yeyote anazilai na hawezi kuamka. Kama ilivyo adha, "Mashabiki" huwa hawana utamaduni wa kufikiri zaidi ya hapo.
Douglas aliigia kambini kwa muda mrefu akijiandaa kupigana raundi nyingi. Aliongea bayana kabla ya pambano kuwa Tyson hajawahi kupigana raundi nyingi hivyo yeye alijiandaa na hilo na hakuona sababu ya kushindwa lile pambano. Kuingia ulingoni na kupambana na Tyson halikuwa lengo la Douglas na wala isingekuwa accomplishment kwake. Alidhamiria muda mrefu kumtwanga Tyson. Kwa "wapenzi" wa ndondi, pambano la Tyson vs Douglas lilimalizika katika raundi ya sita/saba wakati Tyson alipomtwanga Douglas sumbwi moja la nguvu na Douglas akaanguka chini.
Lakini Mashabiki wa Tyson walijua Dougla hasingeamka tena, hivyo huo ndio ulikuwa mwisho wa mchezo. Ndio maana "Mashabiki" wa Tyson hawakuamini kilichotokea baada ya mechi kumalizika. Waliishia kulalama kuwa refa alikosea kwa kuhesabu mpaka 11 badala ya kuishia 10, hivyo kumpa Douglas nafasi ya kuamka. Kitendo cha Douglas kuamka kilikuwa ni pigo kubwa la kisaikolojia kwa Tyson. Naam! alitambua kuwa aliyokuwa akiyasema Douglas yametimia. Na "wapenzi" wa Tyson, walitambua kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa Tyson.
Kumbuka Mama yake kipenzi wa Douglas alikuwa amefariki muda mfupi kabla ya pambano. Douglas alishauriwa akubali kuhailisha pambano ili akamzike Mama yake lakini yeye alikataa ombi hilo. Aliwaambia washauri wake kuwa haitakuja kutokea siku katika maisha yake akajiandaa kupigana raundi nyingi kama alivyokuwa amejiandaa. Alisema Mama yake alikuwa shahidi mzuri wa jinsi alivyojiandaa na kama angekuwa hai angetaka ashinde lile pambano. Muda mchache kabla ya pambano, Douglas alisema anataka pambano lile liwe la kumhenzi Mama yake. Ni kweli, baada ya ushindi ule akaenda kutumia fedha yote kwenye matanuzi. Akawa na matatizo ya uzito mkubwa na huo ndio ulikuwa mwanzo na mwisho wa Douglas na Tyson pia. Lakini dhamiri ya douglas ya kumtwanga Tyson ilitimia.
Mzee Mwanakijiji ni vema umetoa mfano wa Douglas kwani tunaweza kujifunza mengi katika siasa zetu za bongo. Kitu cha kwanza ni kuwa kujulikana sio sifa ya ubora bali ni sifa ya matangazo. Kujulikana kisiwe kipimo cha kuwapima wagombea uongozi katika nchi yetu. Tuweke machujio ambapo kila mtu, anayejulikana na asiyejulikana atatakiwa kuchujwa. Hivyo basi, yatupasa tuache ushabiki katika masuala ya msingi, hasa tunapotakiwa kumchagua mtu wa kukalia Taasisi ya Urais wa nchi yetu ambayo ina madaraka makubwa kuzidi Taasisi zote. Rais wa nchi yetu ni kama Mungu mtu aliye juu ya sheria zote. Tuvipende vyama vya siasa badala ya kuvishabikia.
Tuwe wapenzi wa nchi yetu kwa kukubali makosa tuliyoyafanya badala ya kujipa matumaini ya kufikirika. Tukubali kwamba mwaka 2005 nchi yetu ilikuwa imekabwa kabali na mikataba mibovu. Tulikuwa na chaguo la kuiondoa nchi yetu kutoka katika hilo janga ili iweze kupumua lakini hatukufanya hivyo. Hatukuwauliza au kuwapigia makelele wagombea Urais ili watueleze jinsi gani wangeiondoa nchi yetu katika koromeo la mikataba mibovu. Bahati nzuri, mmoja wa wagombea ambaye alitokea kushinda uchaguzi alikuwa kiongozi wa Wizara ya Nishati na Madini. Tulitakiwa kumkaba koo ili atueleze alichoona na anachojua. Kwasababu alikuwa anautaka Urais kama accomplishment, na laiti angejua kuwa ndoto zake zisingetimia bila kutupatia majibu ya uhakika, basi angesalimu amri kwa wananchi kwa kutueleza ukweli. Leo hii tungekuwa tunaongelea mengine.
Lazima tujue kuwa Kikwete hakuwa na utajiri unaoonekana machoni mwa watanzania. Hata angekuwa nao, usingefua dafu kwa kiasi cha fedha kilichotumika wakati wa kampeni za kumuingiza madarakani. Hatukujiuliza wakati ule kuwa zile fedha ni za nani na zingerudishwa vipi? Hata hivyo, hilo halitukatazi kukubali ukweli sasa hivi kuwa zile fedha zilikuwa na wenyewe na lazima zirudishwe. Tukisha kubali huu ukweli, basi tuachane na ndoto za kutegemea hotuba yenye kuleta matumaini kutoka kwa Kikwete. Binafsi naona tutafakari jinsi ya kujinasua kutoka katika hiki kitanzi tulichojiwekea wenyewe. Kilichoko mezani kwetu ni nchi yetu ya Tanzania na wala sio wale waliotoa fedha za matangazo na hongo na wala Kikwete mwenyewe. Kwetu sisi, iwe ama zake ama zao. Tudai nchi yetu irudishwe mikononi mwa watanzania. Na ole wao watakao ingilia kati kwani watakiona cha mtema kuni.
Mwisho tukubali ukweli kuwa sio watanzania waliomuingiza Kikwete madarakani. Waliomuingiza Kikwete madarakani wametulia kama maji ya mtungi. Wanalia kivulini huku wakiwa wamekunja nne. Kama Urais ni accomplishment, basi hotuba zake zote zitawahenzi waliofanikisha hilo na sio wale walioenda kutumbukiza karatasi kwenye masanduku ya kura.