Wilfred Lwakatare
Member
- Dec 10, 2015
- 22
- 70
Ndugu zangu wana JF, si desturi yangu kutumia mitandao ya kijamii na media kueleza mambo yote ninayofanya wala yanayonipata kila mara.
Naamini leo ukienda katika hospitali zetu wapo watu wengi wanaopata huduma za matibabu, wengine wakitibiwa na kuondoka, wengine hulazwa na wengine huzidiwa na hata wengine kupoteza maisha.
Mimi Lwakatare, kama binadamu ninayeishi na kupumua sio ajabu na wala si mara ya kwanza kuumwa na kwenda hospitali na hata kulazwa. Na ndivyo ilivyotokea nikiwa katika bunge la bajeti na nikahudumiwa ipasavyo na mamlaka ya Bunge.
Ninaloshangaa ni kuona baadhi ya watu wachache kuachia fikra zao kuingiliwa na mitazamo ya kutaka kutumia kuumwa kwangu kutengeneza sintofahamu zisizo na sababu na sijui kwa lengo gani
Kwa mtu yeyote aliyekwazika na taarifa hizo zilizotolewa kuhusu kuumwa kwangu ni kwamba; ni kweli niliumwa na kupelekwa hospitali za General - Dodoma na Shree Hindu Mandal - Dar es Salaam ambako ndiko kuna daktari wangu kwa miaka ishirini iliyopita.
Nilitibiwa ipasavyo na kuruhusiwa na hivi sasa niko nyumbani kwangu Kimara Stop-Over, DSM.
Wakati wowote wiki ijayo nitatinga jimboni kwangu Bukoba Mjini kupiga kazi na wapiga kura wangu.
Mbali na viongozi wa Bunge na Prof. Tibaijuka, pia nimetembelewa na kutumiwa salamu na viongozi wangu wa chama, Wabunge, Marafiki kwa idadi kubwa sana kama ambavyo hufanyika hata kwa wabunge na viongozi wengine wanaokumbwa na tatizo la kuumwa.
Utaabani huo unaozungumzwa, namwomba Mungu usinifike. Niko Salama Salmin na NINADUNDA.
TUKUTANE BUKOBA MJINI.