Moja ya matatizo yetu kama nchi na wananchi ni kuchukia watu wanaofikiri tofauti. Tumezoea mazoea; ukiona mtu anaenda tofauti na mazoea tunaanza kumpa majina kibao: kanunuliwa, msaliti, anajipendekeza, hana ushirikiano, n.k.. Lazima tubadilike na kujua kwamba binadamu tu tofauti kimwili, kiakili na kila kitu. Ili tutoke hapa tulipo lazima turuhusu akili zifikirii sawasawa na tena tuhangaike kufikiri kitofautitofauti. Kama tunataka kila mtu afikiri kama sisi ni kuendeleza utamaduni wa kutumia akili za kuazima. Zitto ni miongoni mwa watu wachache hapa nchi aliyeamua kujipambanua na kuamua kufikiri kitofautitofauti. "Kosa" lake ni kwamba ameamua kuacha kufanya mambo kwa mazoea na ameamua kuhangaika kufikiri kitofautitofauti. Zitto analaaniwa kwa kudiriki kwake kuhangaika kufikiri na kuachana na mazoea. Atabambikizwa majina yote ya ovyo kama usaliti, kujipendekeza, n.k. Tunamtia moyo aendelee kuhangaika kufikiri, wapo watakaomuelewa.
Sidhani kama kuna mtu anamchukia Zitto kwa mawazo anayotoa au juhudi anazozionesha katika sekta ya nishati na madini. Kitu kinachojitokeza kwa sasa ni yeye kujiendesha kama Taasisi huru nje ya chama chake.Amekuwa kama Mwanasiasa wa kujitegemea asiyeamini uwepo wa chama chake cha siasa. Ni wazi kuwa huko nyuma enzi za Zitto kuwa kwenye siasa za Majukwaani, kuibua kashfa dhidi ya Serikali (Mf.Buzwagi), kuwa mstari wa mbele kukijenga chama chake hakukuwa na hali hii ya Zitto kupingwa na idadi kubwa ya watu.
Binafsi siko kwenye Chama chochote cha Siasa lakini kila ninapowaona viongozi wa CDM wakimenyeka na maandamano, kufanya mikutano ya hadhara, kupigwa mabomu na Polisi na hata wengi wao kukumbwa na kesi kadhaa mahakamani kitu cha kwanza kinachonijia ni ukweli kuwa wako tayari kujitoa muhanga ili kuwaeleza wazi Watanzania juu ya uozo unaoendelea nchini, mfumo mbovu wa Utawala ikiwa ni pamoja na upuuzi ulioko kwenye sekta ya Gesi, mafuta, madini na nishati kwa ujumla wake ambao Zitto amekuwa akiushikia kidedea.
Sasa kinachomzuia Zitto kutumia platform ya CDM na movement zake (M4C, Vua gamba vaa gwanda nk.) katika kueleza uozo ulioko Serikalini hasa kwenye Sekta za nishati na madini ni nini hasa? Kwa nini amekuwa na personal platforms na mbaya zaidi haonekani kabisa kwenye mihenyeko inayowakumba viongozi wenzake ndani ya CDM? Kwa mtu yeyote makini lazima ahoji haya na kwa kweli Wananchi wanashindwa kumuelewa.
Sasa mambo kama haya yakiongezwa na taarifa (Binafsi sina hakika nazo) za Zitto kuwa na uhusiano wa karibu na watu wa aina ya Rostam Aziz,tetesi za yeye mwenyewe (Zitto) kumiliki mali zisizooana na kipato chake, kutetea wabadhirifu wa aina ya William Muhando ndani ya TANESCO na zaidi kutetea ununuzi wa mitambo ya Dowans nk. nk. yanawafanya watu wengi si tu wahoji Uhalali wa Zitto Kabwe katika hoja anazotoa bali pia uhalali wa hoja zenyewe.
Nakumbuka kipindi fulani kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru East zilikuwa zimepamba moto na CDM ilikuwa imepigwa kwelikweli na propaganda chafu za CCM (Rejea propaganda za Wassira dhidi ya CDM/Dkt. Slaa) ghafla Zitto akaibuka kuutaka urais. Watu wengi walishtuka, wakahoji inakuwaje Mheshimiwa huyu viongozi wenzake wako kwenye mapambano Arumeru yeye anaibuka kusikojulikana na kutangaza nia ya kugombea urais kupitia CDM? Hili pekee liliwafanya watu wengi kumuona Zitto katika jicho tofauti.
Dkt. Kitila Mkumbo unaweza ukasema huku ni kufikiria tofautitofauti lakini ni wazi hii ni aina ya kufikiri inayolenga kudhoofisha taasisi ya kisiasa uliyomo.