Mimi nadhani kila kitu kinawezekana, japokuwa kama wengi wanavyosema, si rahisi sana kwa Dr. Salim kutoka CCM. Dr. Salim si mtu anaeonekana kama anaweza kufanya maamuzi magumu kama hayo. Ni mtu ambae anaridhika na kuridhia matokeo hata kama yana maumivu kwake.
Kama ingewezekana hisia hizi zikamfikia, nae akaona anaweza kuzifanyia kazi, nadhani ingekuwa jambo jema sana kwake na kwa Taifa kuchukua hatua ya kuungana na Dr. Slaa kama mgombea mwenza. Ila kwa hali ilivyo, nahisi ni vigumu hiyo kutokea kwa sababu zifuatazo;
1. Inawezekana sana kuwa Dr. Salim bado anaimani kuwa mambo yanayotokea kwenye CCM sasa ni ya mpito tu. Kitu ambacho si kweli. Huko tuendako mambo yatakuwa mabaya zaidi, na wenye nia njema na nchi watajilaumu kwa kutochukua hatua za mabadiliko mapema zaidi.
2. Dr. Salim bado anajisikia na kuamini kuwa ni sehemu ya uongozi wa CCM. Hii inaweza kuwa kweli, lakini itabaki hivyo kwa muda mfupi sana.
3. Dr. Salim anaweza kutokuwa na uhakika na sera, nia, imani na madhumuni ya vyama vya upinzani kiasi cha kutoweza kuchukua hatua za haraka kuhama na kujiunga na CHADEMA ili kuweza kushirikiana na Dr. Slaa kupata ushindi wa kishindo. Hii inaweza kuwa sababu kubwa zaidi ya yeye kuona ni afadhali zimwi likujualo ambalo halikuli likakwisha.
Kwa mtazamo wangu, Dr. Slaa ni mgombea mwenye nguvu sana kutoka upinzani. Anatosha kuweza kusababisha upungufu mkubwa wa kura za CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ila akipata watu kama Dr. SAS, atakuwa na uhakika mkubwa sana wa kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sina uhakika kama CHADEMA wanataka kufanya hivyo (kwasababu nao ni sehemu ya mafanikio ya hili) na wala sina uhakika kama Dr. Salim anaweza kuchukua hatua kama hiyo kwa muda huu (maana yeye ni sehemu kubwa zaidi ya mafanikio hayo).