Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,815
- 11,992
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amewasili Maputo Nchini Msumbiji kwa ziara ya kikazi ya siku nne (4), ambapo amepokelewa na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Cristovao Chume kabla ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kiulinzi.
Lengo la ziara yake hiyo, ni pamoja na kuendeleza undugu na kuimarisha mahusiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Msumbiji kupitia nyanja za ulinzi na usalama.
Kulingana na Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo kwa Vyombo vya Habari, imesema kuwa akiwa nchini humo, mbali na kutembelea maeneo mbalimbali yanayoshughulika na masuala ya kiulinzi na kiusalama Dkt. Stergomena atapata pia, fursa ya kutembelea Kituo cha Uratibu cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Regional Coordination Centre) na Kamandi ya Ulinzi wa Amani chini ya Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SADC Mission in Mozambique - SAMIM).
Tanzania na Msumbiji zilisaini makubaliano ya ushirikiano kuhusu Masuala ya ulinzi na usalama. Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kuhusu Masuala ya Ulinzi na Usalama (JPCSD) uliofanyika kuanzia tarehe 03 – 05 Juni, 2021 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre, Dar es Salaam.