Pinda asitisha bomoabomoa
Monday, 07 March 2011 07:54 newsroom
*Asema kasi ya Magufuli inatisha
* Muafaka sasa kupatikana bungeni
NA Angela Sebastian,Chato
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk.John Magufuli, kusitisha mara moja operesheni bomoabomoa inayoendelea nchini hadi serikali itakapotafakari upya suala hilo. Alitoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Chato, mkoani Kagera.
Waziri Mkuu alisema uamuzi huo unatokana na malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi ikiwemo kutopewa elimu ya kutosha juu ya operesheni hiyo.
Kutokana na hilo, alisema iwapo operesheni itaendelea, ni wazi itaibua migogoro isiyokuwa ya lazima.
Operesheni hiyo imekuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya barabara.
Katika utekelezaji wa operesheni hiyo, nyumba na maendeleo mengine ikiwemo vibanda vya biashara ambavyo vimejengwa ndani ya hifadhi ya barabara vimekuwa vikibomolewa.
"Magufuli akishaagiza, meneja wa TANROADS jasho linamtoka na kuanza kubomoa... hatuendi hivyo. Ukitizama X wanalolibandika linakera," alisema Waziri Mkuu
Alisema kasi ya waziri Magufuli katika kutekeleza operesheni hiyo ni kali, na husababisha watendaji wa TANROADS wakilalamikiwa na wenyewe kushindwa kuweka bayana kwa waziri husika.
Kutokana na hilo, alisema suala hilo linarudishwa serikalini ili Baraza la Mawaziri likae na kulitafutia ufumbuzi na baadaye liwasilishwe bungeni kujadiliwa na muafaka kufikiwa.
Baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo, waliipokea kauli hiyo kwa furaha huku wakisema serikali imesikia kilio chao.
Ayoub Musa, ambaye ni mkazi wa Chato, alisema serikali imekuwa ikisemamaeneo fulani ni hifadhi ya barabara, lakini katika maeneo hayo hakuna alama inayoonyesha ni hifadhi, jambo ambalo limekuwa likiwachanganya.
Mbali na hilo, alisema wananchi wengi hawajawahi kupewa elimu juu ya hifadhi za barabara, bali husikia kwenye vyombo vya habari operesheni bomoabomoa inapofika eneo lao.
Mkazi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema serikali imesikia kilio chao na kwamba elimu itolewe kwa watendaji na wenyeviti wa mitaa na vijiji, ili waweze kuwaelimisha wananchi.
My take
Juzi juzi tulishuudia minyukano katika baraza la mawaziri, wateule wa jk wakitoa matamko kila moja kivyake na mbaya zaidi misimamo ikiwa imetofautiana. Mawaziri hawo ni Ngeleja (ufisadi), sitta na mwakyembe walitoa misimamo yao ambayo ilitikisa serikali juu ya hujuma za dowans kwa wananchi. Kabala ya hata miezi miwili kupita tunasikia mtoto wa mkulima aka Pinda akimvua nguo Makufuli kuwa ana spidi kali na anaweza kuwamwangia unga. Je hii ni serikali au kundi la wabaka uchumi?