Uhondo wote ni huu hapa chini kutoka nipashe la leo: -
Waziri Masha aibua matata
2009-01-29 10:14:05
Na Waandishi Wetu
Mchakato wa kupata mzabuni wa kutekeleza Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, umezua mambo, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kudaiwa kuingilia mchakato huo, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Habari za uhakika ambazo Nipashe imezipata, zinaeleza kuwa Masha anadaiwa kufanya hivyo akidai kutoridhishwa na hali halisi ya mchakato huo kabla hata matokeo ya kupatikana kwa mzabuni hayajatangazwa.
Vyanzo mbalimbali vya habari serikalini vimepasha kuwa Masha alifikia hatua hiyo, baada ya Bodi ya Zabuni ya Wizara kuiengua Kampuni ya Sagem Securite ya Uhispania katika mchujo wa kumpata mzabuni atakayetekeleza mradi huo ambao ni nyeti na muhimu kwa usalama wa nchi.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, kampuni hiyo ni kati ya makampuni 54 yaliyoomba kupewa zabuni hiyo, lakini ilienguliwa katika mchujo wa tatu, baada ya mchujo wa kwanza kuyaengua makampuni 33 na kubaki 21 na mchujo wa pili, kuyaengua makampuni 13 na kubaki manane tu.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba wajumbe wanaounda Bodi ya Zabuni ya Wizara hiyo, ni pamoja na Kamishna wa Magereza, Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na mchakato wa zabuni hiyo uliwahusisha pia maofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) na Usalama wa Taifa.
Haijafahamika sababu hasa iliyomsukuma Masha hadi kuamua kuitetea kampuni hiyo kwa nguvu zake zote.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Masha anadaiwa kuingilia mchakato huo akidai kupokea malalamiko kutoka kwa kampuni hiyo, kwa madai kwamba wameonewa kwa kuenguliwa kwenye mchakato kwa vigezo ambavyo havikuwapo katika nyaraka za awali za kuingia kwenye zabuni.
Taarifa zinasema kuwa Masha baada ya kupata malalamiko hayo, Novemba 4, 2008, alimwita Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni na Mratibu wa Vitambulisho vya Taifa ofisini kwake, mjini Dodoma.
Katika kikao hicho, vyanzo vyetu vinasema Masha anadaiwa kumfahamisha Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Zabuni ya Wizara kwamba, amepokea malalamiko kutoka kwa kampuni hiyo na kumhoji pamoja na mambo mengine, uhalali wa kuenguliwa kwa kigezo cha kutoambatanisha nakala ya mapatano (Joint Adventure Agreement).
Ofisa mmoja mwandamizi serikalini akielezea kukerwa na kujitosa kwa Waziri Masha katika mchakato huo alisema kuwa ilifika mahali akadai waziwazi kuwa kampuni ya Sagem Securite ilikuwa imesukiwa makakati wa kung\'olewa kwenye mchakato wa zabuni kwa sababu ilionekana ni tishio kwa kampuni nyingine.
Kutokana na hali hiyo, chanzo hicho kimesema kuwa Masha aliitaka bodi hiyo itoe nafasi kwa waombaji wote wa zabuni waliotimiza vigezo vilivyopo kwenye Nyaraka za Awali za Kuingia kwenye Zabuni (PD) wapewe nafasi ya kuendelea na hatua ya pili ya mchakato huo.
Kutokana na shinikizo la Masha, vyanzo vyetu vinasema Katibu Mkuu wa Wizara alimwandikia barua Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni na kumpa maelekezo ya kutaka kurejewa upya kwa mchakato ili kuiingiza kampuni hiyo na nyingine zilizokuwa zimeenguliwa awali.
Vyanzo vyetu vinasema kwamba Bodi ya Zabuni baada ya kupitia maelekezo ya Katibu Mkuu, ilitoa ufafanuzi, ambapo pamoja na mambo mengine, ilieleza kuwa imeridhika kwamba, hakukuwa na upungufu wowote katika kazi ya uchambuzi waliyoifanya na waombaji wote walioenguliwa, ikiwamo Sagem Securite walienguliwa kihalali.
Taarifa mbalimbali kutoka serikalini zimearifu Nipashe kuwa Katibu Mkuu aliridhika na majibu ya Bodi ya Zabuni, hali ambayo ilimfanya Waziri Masha awasiliane naye tena na kumtaka apate ushauri kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa kile alichodai kuwa ni kuepuka hisia na malalamiko kutoka kwa waombaji.
Wakati hayo yakiendelea, habari za uhakika zinasema kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupeleka taarifa ya utekelezaji kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri baada ya Katibu Mkuu huyo kumpelekea taarifa ya utekelezaji.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa hatua hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi, haikumridhisha Waziri Masha kwa madai kwamba, hakumhusisha kwa vile yeye ndiye atakayeiwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na ndiye atakayewajibika kwa maamuzi yoyote yatakayofanyika wizarani kwake bila kujali kwamba maamuzi hayo yalipata baraka za Katibu Mkuu Kiongozi au la.
Kutokana na hali hiyo, vyanzo vyetu vinasema kwamba Masha alimwandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, barua akimlalamikia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwa madai ya kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri bila kumhusisha yeye kama Waziri.
Waziri Masha alipoulizwa na Nipashe kwa njia ya simu jana kutoka mjini Dodoma kuhusu tuhuma dhidi yake za kuingilia mchakato wa kupata mzabuni wa mradi huo, hakukiri wala kukanusha.
``Aliyekwambia nimeingilia mchakato, muulize huyo. Mimi ninafanya kazi yangu kama waziri,`` alisema Waziri Masha.
Pia, alipoulizwa kama amemwandikia barua Waziri Mkuu `kumshtaki` Luhanjo, Waziri Masha alimweleza mwandishi kuwa: ``Kama barua nimemwandikia Waziri Mkuu, ni confidential (siri), sihitaji kukueleza hilo wewe.``
Wakati hayo yakijiri, PPRA imeeleza utaratibu wa zabuni na jinsi ya kulalamika kama mwombaji hakuridhishwa na matokeo.
Ofisa mwandamizi wa PPRA aliiambia Nipashe kuwa mzabuni anayeona ameonewa kwenye utoaji wa zabuni anapaswa kutoa malalamiko yake kwa Katibu Mkuu wa Wizara husika, wakati Masha anaonekana kufanya kwa niaba ya mzabuni, kampuni ya Sagem Securite.
Akizungumza na Nipashe kwenye ofisi hizo jana, ofisa huyo aliyekataa kutajwa gazetini kwa sababu si msemaji wa mamlaka hiyo, alisema endapo mzabuni huyo hataridhika na maamuzi yatakayotolewa na Katibu Mkuu anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake PPRA.
Ofisa huyo alisema kwa mujibu wa Sheria, mlalamikaji huyo anapaswa kuwasilisha malalamiko yake ndani ya siku 28 za kazi mara baada ya majibu ya mchakato wa zabuni kutoka.
Alisema endapo mzabuni huyo hataridhika na maamuzi ya PPRA anatakiwa kwenda Mahakama ya Rufani za Zabuni, Public Procurement Appeals Authority (PPAA), ambayo ndiyo ngazi ya juu kabisa.
Alisema kama zabuni imeshatangazwa na mkataba kusainiwa na pande husika, basi mlalamikaji hana haja ya kupitia kwanza PPRA na badala yake anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake moja kwa moja PPAA.
Mradi wa vitambulisho vya taifa ni kati ya miradi mikubwa ya serikali ukikadiriwa kuwa utagharimu Sh bilioni 200.
* SOURCE: Nipashe