Waziri Gwajima: Hatuwezi kufikia Dira ya Maendeleo 2030 ikiwa mamilioni ya Wasichana wataendelea kukeketwa

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,988
Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima akizungumza kwenye Mkutano wa Kimataifa wa kupinga ukeketaji amesema mpango Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, hauwezi kufikiwa kwa mafanikio kama vitendo vya ukeketaji wa Wanawake havitokoma.
F8AKlBpXgAAiOJG.jpeg
Akizungumza kwenye katika mkutano huo ambao unafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambao umeanza Oktoba 9, 2023 ukitarajiwa kufanyika kwa siku tatu ukienda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo ufanyika Oktoba 11 kila Mwaka, amesema ukeketaji unaondoa utu wa Wanawake na Watoto wakike pamoja na kuhatarisha Afya zao.

"Ukeketaji unaondoa utu wa Wanawake na Watoto kike hivyo ikiwa ni pamoja na kuhatarisha afya zao na maisha yao ya baadaye. Ni imani yangu kuwa leo kwenye ukumbi huu uliojaa Watetezi wenye shahuku Wataalamu na watunga sera nayaona matumaini na dhamira ya kuwa na ulimwengu ambapo kila msichana anaweza kukupa bila kivuli cha ukeketaji."

Amesisitiza "Hatuwezi kufikia Dira ya Maendeleo ya 2030 ikiwa mamilioni ya Wasichana wataendelea kukeketwa kutokana na mila zenye madhara. Hatuwezi kujenga uwezo kamili wa rasilimali watu ikiwa wasichana wengi zaidi hawawezi kupewa fursa ya elimu na kufikia malengo."
F8AKqFyWEAA7Jja.jpeg
Pia, Waziri Gwajima ametumia nafasi hiyo kuwaomba Wadau mbalimbali kwenye jamii kuungana pamoja kuleta suluhu la changamoto hiyo, ambapo amedai kwa kuungana inawezekana kupata suluhisho.

"Kama Waziri mwenye dhamana nawaomba tuungane kutafuta suluhisho la kudumu kule kwenye jamii kwa kushirikiana na viongozi wa kimila, kidini vikundi vya kijamii, vijana asasi za kiraia viongozi wa Serikali na wadau wote inawezekana," amesema Waziri Gwajima.

Ameongeza "Tanzania inatoa wito kwa jamii zote wadau wetu wa ndani na nje ya Nchi pamoja na Nchi nyingine zote kuungana na sisi katika kuharakisha mabadiliko yanayohitajika ili kubadilisha maisha ya Wanawake na Watoto wetu."
F8AKrauXIAAIJrU.jpeg
Aidha, katika kuonesha ukubwa wa suala hilo amesema takwimu zinaonesha zaidi ya Wanawake milioni 200 Duniani wamefanyiwa ukeketaji ambapo amedai kuwa kati ya hao Wahanga milioni 20 wamefanyiwa vitendo hivyo na Wataalamu wa Afya.

"Kwahiyo lazima tuseme inatosha, inatosha, inatosha. Mabadiliko yanahitajika ili kulinda zaidi ya Wanawake na wasichana milioni 68 walio katika hatari ya kukeketwa kote Duniani ambapo Afrika inachukua zaidi ya milioni 50," amesema Waziri Gwajima.

Akifungua mkutano huo amesema mara baada mapendekezo ya wadau hao watakayoyatoa kupitia mijadala na kuyawasilisha kwake atayawasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mmoja kati ya washiriki wa mkutano huo ambaye ni mdau wa kupinga masuala ya ukeketaji nchini Kenya, Caroline Lahoi ambaye ni Mwandishi wa Kitabu cha 'Memoir of an FGM Survivor', amesema ukeketaji una athari kubwa huku akijitolea mfano alivyoathiriwa na kitendo hicho hali ambayo amedai imekuwa ikimsukuma kupinga ukeketaji kuendelea.

"Mimi nilifanyiwa ukeketaji kwa bahati mbaya zaidi yule Mama aliyenifanyia kitendo hicho alikuwa mlevi akanikata kwenye mfupa wa damu nikapelekwa hospitali nikaenda kushonwa, sasa huko hospitalini ndipo walinifanyia aina ya tatu ya ukeketaji ili kusaidia damu ziache kutoka lakini nilipata maumivu makubwa ambayo yamenifanya nipinge vitendo hivi visiendelee kwenye jamii," amesema Caroline.

Aliendelea kueleza "Katika mahusiano imekuwa ngumu ni kama nimeshonwa kabisa lakini pia wakati wa kujifungua nilihitaji usaidizi kutoka kwa madaktari lakini kwa sababu madaktari hawakujua vile kama mimi nilikatwa wakati huo najifungua ilipidi atoke mwenyewe lakini hali hiyo iliacha mikwaruzo na kupelekea kushonwa tena."

Amedai ukeketaji umeathiri maisha yake hasa katika hali ya kujifungua sambamba na mazingira mengine ambayo amedai yamekuwa yakimpa maumivu makubwa.

"Ukeketaji umeathiri maisha yangu kwa sababu kila wakati nikifikiria kujifungua nahisi kama nakeketwa tena kwa sababu nitakatwa tena. Niseme ukeketaji unaathiri sana Mwanamke wengine wanafikiri ni kawaida lakini mwanamke ambaye ajakeketwa kujifungua kwake ni rahisi lakini aliyekeketwa anapata shida sana na anachukua muda kupona," anasema Caroline.

Katika mkutano huo zaidi ya mataifa 20 wanashiriki kupitia wawakilishi mbalimbali ikiwemo mawaziri, ambapo kwa siku ya kwanza ya ufunguzi mawaziri nane kutoka Nchi mbalimbali ikiwemo Kenya na Gambia wameshiriki mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri Gwajima.

Mada mbalimbali zimeanza kujadiliwa ikiwa ni pamoja na Wadau kutoa maoni yao ambayo yanalenga kumulika vitendo hivyo na kuleta suluhisho la pamoja.

Itakumbukuwa Kwa mujibu wa Utafiti wa Kidemografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa Mwaka 2015/16 ulibaini Mwanamke 1 kati ya 10 hapa nchini Tanzania amekeketwa.

Aidha, utafiti huo pia ulibaini kiwango cha ukeketaji kwa wanawake na watoto kinaongezeka kulingana na umri. Asilimia 19 ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 45 hadi 49 walikuwa wamekeketwa ukilinganisha na 5% ya Wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19.

Takwimu za Mwaka 2022 Mikoa yenye viwango vikubwa vya ukeketaji ni Manyara (58%), Dodoma (47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (31%); hii ni kwa mujibu wa Utafiti wa Kidemografia na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa Mwaka 2015/16.

Pia Soma - Tanzania: Mikoa inayoongoza kwa Ukeketaji ni Manyara, Dodoma, Arusha, Mara na Singida
 
Hapo suala ni serikali kuongeza bajeti kwenye wizara husika ili ipambane na wote wanaochagiza na kushikilia misimamo ya kuendeleza huo ujinga.

Sheria kali ipitishwe kwa wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine.

Pia wasisahau kuangazia ndoa za utotoni na mila kandamizi kwa mabinti.
 
Back
Top Bottom