Mifumo ni watu. Taasisi ni watu. Na vyote hivyo ni kwa ajili ya watu.
Hakuna mfumo uliojiumba wenyewe tu na unaojiendesha wenyewe. Hakuna taasisi iliyojitengeneza yenyewe. Hakuna taasisi inayojiendesha yenyewe. Kumekuwepo na manung’uniko mengi sana kuhusu ukosekanaji wa mifumo bora na taasisi bora hapa Tanzania.
Muundo wa serikali yetu kwa sasa ni ‘top heavy’. Rais wetu ana madaraka makubwa sana na mengi mno. Sawa, hiyo ni kweli kabisa. Lakini, kilicho cha muhimu kabisa kabla hatujaanza kubadili namna tunavyojiongoza, ni lazima kuwepo na mabadiliko ya kifikra.
Ni lazima tubadilike kifikra na ndipo tutaweza kujenga mifumo imara na taasisi zilizo bora. Fikra kama za ‘ameula’, pale mtu anapoteuliwa kwenda kuutumikia umma, hazijengi chochote kile kilicho bora na imara.
Fikra za kwamba ‘Rais hakosei’, hazijengi chochote kilicho bora na imara. Fikra za kumuona Rais ni kama mungu mtu flani hivi, ni lazima zikome.
Fikra za kinafiki nazo lazima zikome. Kama mtu upo serikalini na hukubaliani na mwelekeo wa serikali unayoifanyia kazi, achana nayo. Jiuzulu. Siyo kujifanya unaunga mkono ili mradi tu uendelee kuitwa waziri lakini kumbe moyoni huamini katika chochote serikali hiyo inachokisimamia!
Mabadiliko ya kifikra hayakwepeki endapo kweli tunataka kuliendesha taifa letu kiutofauti na tunavyoliendesha sasa. Hata tukija kupata katiba bora kabisa duniani, endapo fikra zetu hazitobadilika, katiba hiyo itakuwa ni kazi bure tu. Our collective national ethos has to change. No two ways about it!
Peace ✌️. I’m outta here like last year.