Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,997
Na. M. M. Mwanakijiji
Naomba niandikie kutoka kwenye hisia kidogo; Naomba niandike toka kwenye vionjo vyangu vilivyojeruhiwa; Naomba niandikie kutoka kwenye moyo uliojawa na hasira, kero na ambao unajihisi kinyaa!; Naomba niandike kama mtu ambaye akili zake hazijakaa sawasawa na ambaye anaweza kuitwa "fyatu"! Naomba niandike kuhusu haya ya Shirika letu la ndege la ATCL ambalo limekuwa kituko cha taifa na aibu ya nchi yetu!
Watawala wetu mmerogwa? Tumefikaje hapa, je hili limefika kama kwa ghafla na kwamba hakukuwa na dalili zozote? Kwamba leo bila haya mnaitisha vikao vya dharura na kutoa "siku saba" za kupata maelezo toka kwa wazembe na waliofuja mali za shirika hili kana kwamba hamkuliona hili? Ati leo mnathubutu kuelezea kilichofanyika ATCL kuwa ni uzembe wakati kwa mwaka mzima vumbi lake mlishaliona toka mbali? Mmerogwa nyinyi?
Nauliza kama mmerogwa kwa sababu hakuna maelezo yoyote ya kiakili ambayo yana ushawishi wa kimantiki na yenye uzito wa ushahidi wa kisayansi yanaweza kuelezea ubutu wa matendo yenu na ukimya wa maneno yenu kwa mwaka mzima tangu king'ora cha tahadhari tulipokipuliza mwezi Disemba mwaka jana! Ni watu waliopumbazwa na dawa za mitishamba au waliorogwa 'kisayansi' ndio pekee wanaweza kufafanua ni kitu gani kiliwakumba. Mmepitiwa na jini gani lililowafanya mduwae na kuangusha midomo yenu ya chini na denda zikidondoka kama wale wasemwao "washangaao feri"?
Tuliimba na kupaza sauti, makoo yetu yakakauka. Tukawaambia tena bila kuuma uma maneno kuwa ATCL kuna uozo; tena uozo mkubwa wa kiuongozi. Tukaweza mipango yao ya kukodisha dege lenye matatizo ya kiufundi zaidi ya 100 tena kwa bei mbaya; tukawawekea na mikataba yao waliyoingia kuhusu dege hilo hilo, lakini muda wote huo nyinyi mkaendelea kukaa kimya na kuacha ATCL ijiendeshe kama kikaragosi kinachoenda kwa kupiga ufunguo!
Tukawawekea na ushahidi jinsi gani watendaji wa ATCL wamefuja mali zetu huku wakikinga mikono yao kuyupa zaidi; tukawaonesha jinsi mikakati yao ilivyokuwa mibaya na mibovu; tukawaonesha ni jinsi gani David Mattaka na genge lake la makuwadi wa ufisadi wameshindwa kuliongoza shirika hilo. Kwa mwaka mzima tumefanya hivyo pasipo mafanikio.
Tumefanya kama kile tulichokifanya kwenye suala la Ukraine miaka miwili iliyopita ambapo tulionesha upungufu na uozo wa bodi ya mikopo. Mkasimama mkatubeza, mkatucheka kwa sababu ati tunawaonea wivu; kwamba hatupendi maendeleo yenu; kwamba tunajifanya tunajua sana; kwamba ati kama tuna uchungu basi turudi nyumbani kusaidia nchi yetu; kwamba tukae kimya kwa sababu sisi ni wakimbizi! Hivi nyinyi mmerogwa?
Mkadharau sauti za tahadhari zilizopigwa kama kengele kwenye Jamiiforums; mkanyamaza tulipoandika kwenye magazeti yetu; mkawa mnatafuta kujua ni nani anavujisha "siri za serikali". Mkawatimua watu kazi ATCL mkidhania kuwa mmeziba uozo wenu! Sasa leo mnashtuka kana kwamba mmegutushwa na mpiga mbiu!? Mnabeba shuka kupeleka hospitali wakati mgonjwa keshakufa? Mmerogwa nyinyi?
Leo ati kwa ujasiri mnasimama; macho meupe tena makavu, mnasema ati mnataka maelezo ya kina kuwa nini kimetokea ATCL! Ati mnaomba maelezo kutoka kwa watu wale wale ambao wanatakiwa wawe Keko wakiwa na pingu katika miguu na mikono yao. Leo mnakaa meza moja na mafisadi mliowaweka hapo, mkitumaini watawaambia kitu kingine zaidi ya kutaka fedha zaidi! Ati mmewapa siku saba za kujieleza! Maelezo gani zaidi ya kuangalia ndege zenu zisizoruka kama tai aliyekatwa mbawa!
Kama vile wasio na akili timamu wanakuja mbele yenu na suti zao za bei mbaya na kuomba fedha zaidi kuwa kinachohitajika ni fedha zaidi! Katika hali yenu ya kurogwa (bewitched state) mnakaa na kufikiria kuwapa fedha zaidi ili kulinasua shirika. Tutawapeleka hospitali gani nyinyi maana hata walioko Mirembe wanaweza wakawakimbia baada ya kuwauliza "ukichaa wenu umeanza lini"?
Badala ya kuamua kuchukua hatua za kushughulikia tatizo hili mnafanya kile ambacho ni kitendo cha woga kabisa; kwamba mnataka wachina waingie mkataba wa kuliendesha! kwamba ya Afrika ya Kusini hayakuwa funzo, ya Tanesco hayakuwa funzo, mnataka na ATCL mjaribu tena! Hivi katika taifa letu hakuna watu wenye uwezo kweli wa kuliendesha shirika hilo? Kweli mmekuwa waoga kushughulikia matatizo hadi tatizo likija mnakimbilia kwa "mjomba" Uchina, mmerogwa nyinyi?
Mnataka kutuambia kuwa mmeshindwa kukaa chini na kugonganisha vichwa vyenu kutafuta suluhisho la kitanzania kwenye tatizo la kitanzania? Hivi mnaogopa nini kufanya maamuzi magumu na kutoa nafasi kwa WAtanzania wazalendo wa kweli kuliendesha? NI ninyi wenyewe mlimrudisha David Mattaka licha ya kuwekwa nje ya utumishi, mlikuwa mnafikiria nini? Kwamba ATCL ni mahali pa mafunzo?
Katika wazimu wangu, nina uhakika tukitafuta watu wawili wa watatu wenye akili za biashara wanaweza kulitengeneza shirika hili na wenyewe wakatengeneza pesa vile vile. Tumeshindwa kuwaita wafanyabiashara wa Kitanzania, wasomi, na watalaamu wa mambo ya anga na kusema "tunaomba msaada tufanye nini"?
Kama mlivyokuwa goigoi kwenye wizi wa Benki Kuu, kama mlivyo goi goi kwenye suala la Elimu ya Juu (mmeunda kamati kuchunguza matatizo ya vyuo vikuu wakati mwaka mmoja mliopita mliunda kamati kama hiyo hiyo au hamkumbuki mlifanya hivyo?), kama mlivyo goi goi kwenye Jeshi la Polisi; kama mlivyo goi goi kwenye Usalama wa Taifa, mmekaa na kusubiri hadi vinuke kabisa ndiyo mnyanyuke! Mmerogwa na nani? Na ni kitu gani tunaweza kuwapa kikawazimua toka katika hali yenu ya bumbuwazi la ulozi?
Mnataka tuombe Bunge liunde Kamati Teule ichunguze ATCL? Msituambie kuwa sasa nchi yetu ianze kuongozwa na Kamati za Bunge maana hata la Dowans nusura mliingize Taifa mkenge licha ya kuwaambia tangu mwaka jana kuwa Dowans haikustahili kuchukua mkataba wa Richmond lakini katika kiburi chenu mkafanya hivyo.
Sasa hili la ATCL limedhihirisha tatizo liliopo. Mmezoea kubebana sana, mmezoea kuoneana haya sana, mmezoea kukenuliana meno kama fisi wanapoona mifupa!! Mmebakia kupigiana makofi!
Zindukeni katika usingizi wenu! Amkeni kutoka katika dimbwi la mshangao wenu, kwani hakuna hirizi itakayowazindua, hakuna ramli itakayowaamsha, hakuna mganga atakayeinua zindiko mlilojipigia wenyewe katika ufisadi wa matendo yenu. Na msitegemee kuchanjwa chale za kinga ya pingu zilizopo mbele zenu!
ATCL haihitaji kubinafsishwa, ATCL haina sababu ya kuitiwa wajomba zetu wachina kuja kuiokoa; ATCL haitaji wataalamu kutoka mbinguni na mabingwa wa utawala kutoka mbingu ya saba. Wamarekani wana msemo "you messed it up, you clean it up" kwamba "mmechafua wenyewe, safisheni wenyewe!". Hili mmelivundisha wenyewe, sasa linanuka mnauliza "kwanini linanuka"?
Labda mnahitaji kuombewa nyinyi; mnahitaji kupepewa; au kufukizwa kwa harufu ya maji yaliyochemshwa ya mwarobaini! au tumwombe Kakobe awawekee mikono! au Shehe aliyebobea katika mambo ya roho awasomee!
Au mwataka tuite mashehe waje wawasomee dua ya kuondoa majini mliyoyakumbatia, na tukawaombe wachungaji waje wakemee mapepo yenu ya ufisadi yaliyowapanda katika vichwa vyenu, labda...... labda... mtarudi kwenye akili timamu!
au mnatuonaje sisi Watanzania, tumerogwa?
labda nyinyi na sisi sote tumerogwa na hakuna wa kutusaidia!