Wataalamu wa magonjwa ya moyo 100 wa JKCI wapigwa msasa wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,814
11,991
Wataalamu wa magonjwa ya moyo 100 kutoka Kurugenzi ya Upasuaji ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliipongeza Kurugenzi ya upasuaji kwa kuwa na wazo la kuikutanisha Kurugenzi nzima kupata mafunzo hayo kwani ni ya muhimu katika kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

“Kumuhudumia mgonjwa aliye mahututi sio kazi ya mtu mmoja inahitaji timu ya wataalamu wa afya mbalimbali walio na mafunzo ya kiwango cha juu cha kuokoa maisha kama ambavyo Kurugenzi yenu imekuwa ikifanya na kuongeza ujuzi mara kwa mara,” alisema Dkt. Kisenge.
Picha 3.JPG

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kurugenzi ya Upasuaji wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge alisema ni muhimu kwa mafunzo hayo ya siku mbili yakabadilishe muenendo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi na kupokea mawazo kwa kila mshiriki kwani huduma ya dharura inahitaji ushirikiano wa pamoja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema hii ni mara ya pili kurugenzi hiyo kuandaa mafunzo hayo yanayohusisha mafunzo kwa vitendo ili kila mtaalamu wa afya aweze kuona kwa uhalisia vifaa vinavyotumika na kufanya mazoezi kwa vitendo.

“Wakati wa upasuaji mgonjwa anaweza akabadilika na kuhitaji matibabu ya dharura hivyo kama wahusika wakuu wa huduma za upasuaji lazima kila mfanyakazi ajue ni kitu gani kinatakiwa kufanyika ili kuokoa maisha ya mgonjwa”, alisema Dkt. Angela.

Dkt. Angela alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kusaidia wataalamu wa Kurugenzi ya Upasuaji kuwa katika viwango vya kimataifa vya kutoa huduma inayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopo.
Picha 2 (1).JPG

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya akitoa neno na shukrani wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Kurugenzi hiyo leo jijini Dar es Salaam.

“Mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi ni ya muhimu kwetu sisi kwasababu tunaamini kama wataalam wa afya tunatakiwa tuweze kuwa na utayari wa kuwahudumia wagonjwa wakati wowote”, alisema Dkt. Angela.

Washiriki wa mafunzo hayo ni wataalamu kutoka Hospitali ya JKCI Dar Group, madaktari wa upasuaji, wataalam wa kuendesha mashine mbadala wakati wa upasuaji, wauguzi wanaofanya kazi katika chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na wauguzi wanaojifunza kuwahudumia wagonjwa wa dharura.
Picha 4.JPG

Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akichangia mada wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.​
 
Back
Top Bottom