JKCI kutibu wenye mishipa ya moyo iliyopasuka

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Unaweza kuiita ni habari njema kwa watu wenye matatizo ya moyo, baada ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuanza kutibu wagonjwa wenye mishipa ya moyo iliyopasuka.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge ameeleza hayo leo, Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo maalumu kwa wataalamu wa taasisi hiyo yatakayotolewa na wataalamu kutoka Hospitali ya Open Heart International ya nchini Australia.

Dk Kisenge amesema sababu kubwa ya ugonjwa huo ni shinikizo la juu la damu ambalo husababisha kupasuka kwa mishipa ya moyo inayopeleka damu sehemu nyingine za mwili.

Amesema madaktari wa taasisi hiyo sasa wataanza kutoa huduma ya tiba baada ya kujengewa uwezo na madaktari kutoka Open Heart International ya nchini Australia.

"Wiki moja iliyopita tuliwapata wageni kutoka Australia, ni madaktari 23 wamekuja kufanya upasuaji mkubwa wa kuziba mshipa wa moyo uliopasuka kwa juu kutoka kwa mgonjwa aliyekuwa na tatizo hilo ambalo hatukuwa tunatibu.

“Kwa mgonjwa huyo kumpeleka nje, tiba yake ni Sh60 milioni na sasa tunawatibu wagonjwa wa aina hiyo hapa kwa Sh20 milioni," amesema.

Mgonjwa huyo ni miongoni kwa wagonjwa 11 waliopatiwa matibabu kwenye kambi ya madaktari hao na hadi Novemba 25, 2023 jumla ya wagonjwa 16 watakuwa wamefanyiwa upasuaji.

Kwa mujibu wa Kisenge, matibabu hayo yanayofanyika nchini, yataokoa zaidi ya Sh500 milioni ikiwa ni gharama ambazo zingetumika kuwawezesha wagonjwa hao kupata matibabu nje ya nchi.

Sababu ya ugonjwa huo wa kupasuka kwa mshipa wa moyo ni shinikizo la damu ambalo kwa takwimu za JKCI asilimia 10 ya watu wanaofika kwenye taasisi hiyo wana shinikizo la damu.

Shinikizo la juu la damu ni miongoni mwa magonjwa yaliyotajwa na Wizara ya Afya kuongezeka kwa kasi ambapo kwenye maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu duniani Mei mwaka huu, Serikali ilieleza kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaougua ugonjwa huo nchini.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika, inakadiriwa watu watatu mpaka wanne kati ya 10 wana tatizo hilo katika mikoa minane nchini ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Iringa, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Pwani, Geita na Pwani.

Ongezeko la ugonjwa huo kwa takwimu za Wizara ya Afya ni kutoka watu 688,901 mwaka 2017 hadi watu 1,345,847 mwaka 2021.

Chanzo cha shinikizo la juu la damu ni ulaji wa chumvi isiyopikwa, kutofanya mazoezi, matumizi ya sigara, pombe, unene kupitiliza na msongo wa mawazo na namna ya kukabili ugonjwa huo ni kuepuka vihatarishi vyake.

Katika hatua nyingine, Dk Kisenge amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuanzia Oktoba, taasisi hiyo imepokea wagonjwa 60 kutoka mataifa mbalimbali iliwemo Kongo, Malawi, Comoro na Zimbabwe.

"Tulishangazwa kupokea wagonjwa kutoka Ujerumani na Ufaransa ambao wamekuja kutalii ndani ya hospitali yetu, miaka ya nyuma walikuwa wakifika Kenya na mataifa mengine, lakini sasa wanakuja kwetu. Hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika kwenye taasisi yetu," amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi Hospitali ya Open Heart International ya nchini Australia, Dk Darren Wolfers amesema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya JKCI tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.

Amesema jambo kubwa linalowavutia kufika mara kwa mara JKCI kutoa mafunzo na kuendesha kambi za upasuaji ni upatikanaji wa vifaa vya kisasa vinavyowawezesha kufanyika kwa upasuaji huo.

MWANANCHI
 
Kwa mujibu wa Kisenge, matibabu hayo yanayofanyika nchini, yataokoa zaidi ya Sh500 milioni ikiwa ni gharama ambazo zingetumika kuwawezesha wagonjwa hao kupata matibabu nje ya nchi.
haya majina mengine bwana, mke wa Kisenge, gari la Kisenge, ushauri wa Kisenge ulifanyiwa kazi kwenye kikao walichokaa ukoo wa Kisenge n.k.
 
Back
Top Bottom