Barrick Gold matatani tena
na Mwandishi Wetu
MISUKOSUKO inayoikabili kampuni inayomiliki migodi kadhaa ya dhahabu nchini, Barrick Gold Corporation, inaongezeka huku wafanyakazi wake wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga wakigoma, na mfanyakzi mwingi wa mgodi wa North Mara mkoani Mara akidai kufukuzwa kazi kwa mizengwe.
Habari zilizopatikana jana zilieleza kuwa wafanyakazi wa Bulyanhulu waligoma jana baada ya kutoa notisi juzi usiku kwa uongozi wa mgodi huo.
Notisi hiyo kutoka katika tawi la Chama cha Wachimba Madini na Ujenzi (TAMICO), ilitolewa kuufahamisha uongozi wa mgodi huo kuwa, wanachama wa chama hicho mgodini hapo, wamepanga kufanya mgomo Oktoba 25.
Hata hivyo, mara baada ya kuipata notisi hiyo, uongozi wa mgodi wa Bulyanhulu ulijibu na kukishauri chama hicho na wafanyakazi kuwa mgomo wao utakuwa batili na kinyume cha sheria.
Aidha, uongozi uliwaeleza wafanyakazi hao kuwa, iwapo wangegoma, uongozi ungechukua hatua zinazofaa kulingana na hali hiyo, kwa masilahi ya kampuni.
Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka mgodini hapo zilieleza kuwa, baadhi ya wafanyakazi hawakuujali ushauri huo na jana waligoma kufanya kazi.
Kampuni hiyo jana ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuwa Oktoba 17 mwaka huu, TAMICO na uongozi wa mgodi walikaa pamoja kuzungumza na kufikia makubaliano kuhusiana na masuala kadhaa.
Mazungumzo yalikuwa yamepangwa kuendelea asubuhi ya Oktoka 25, ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kubainisha kuwa, uongozi wa mgodi bado una dhamira ya kuendelea na mazungumzo hayo kama ambavyo ilikubaliwa awali.
Hata hivyo, kampuni hiyo ilisema kuwa, mazungumzo hayo hayawezi kuendelea wakati baadhi ya wafanyakazi wapo katika mgomo ambao umeuita kuwa ni batili.
Makubaliano katika mazungumzo ya awali yalikuwa wazi kuwa kila upande uendelee na mazungumzo ili kufikia muafaka wa masuala yote, ilisema taarifa hiyo.
Katika notisi iliyopelekwa kwa uongozi, Katibu wa kamati ya TAMICO anaelezea baadhi ya sababu zilizowafanya wafanyakazi wagome kuwa ni kushindwa kwa mwajiri kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 17 na hofu dhidi ya usalama wa wafanyakazi baada ya kumwagwa kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mgodini hapo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, Meneja Mkuu wa Bulyanhulu, aliwataka wafanyakazi wote waliogoma kurejea kazini, hasa wale waliopo katika shifti inayofuata.
Uongozi huo pia ulitoa taarifa kwa wafanyakazi hao kuwakumbusha kuwa uongozi una haki ya kuwafukuza kazi wafanyakazi wote watakaogoma.
Wakati huo hio, Edward Ibabila, anaripoti kutoka Tarime kuwa ofisa wa Kampuni ya Barrick, inayomiliki mgodi wa dhahabu wa North Mara, Terry Brown, raia wa Canada, anadaiwa kutoa lugha chafu za matusi na kutishia kumuua Bahati Ndimanya, aliyekuwa mhandisi wa kampuni hiyo, ambaye alifukuzwa kazi baada ya kuripoti tukio hilo polisi.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa masikitiko makubwa, Ndimanya alisema tukio hilo lilitokea Septemba 6 mwaka huu, majira ya saa 11 jioni wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wenzake wawili ofisini kwake.
Alisema Mzungu huyo aliwafuata na kumuuliza mmoja kati ya wafanyakazi aliokuwa akizungumza nao walikuwa wanafanya nini mahali hapo na Ndimanya alimfahamisha Mzungu huyo kuwa yeye ndiye aliyewaita.
Alidai kuwa baada ya kumjibu hivyo, Mzungu huyo alianza kumtolea lugha chafu kwa lugha ya Kiingereza.
Alisema baada ya kumtolea lugha hiyo chafu, aliondoka na kurejea tena baada ya muda mfupi na kuendelea kutoa lugha chafu, huku akimnyoshea kidole na kutishia kumuua iwapo ataendelea na tabia hiyo.
Aliporudi alikuwa amekasirika zaidi na aliendelea kunitukana huku akininyoshea kidole na kuniambia ataniua kama nitaendelea na tabia hiyo. Kwa kweli kauli hii ilinitisha na kunishangaza kwani sikuona kosa langu. Hata kama ningekuwa na kosa hakupaswa kutishia kuniua, alitakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi yangu, alisema.
Alisema alitoa taarifa kuhusiana na tukio hilo kwa mkuu wa idara, aliyemtaja kwa jina la Adam Wilson, ambaye ni Afisa Utumishi na Mwanasheria wa Kampuni, ambaye aliahidi kushughulikia suala hilo baada ya wiki moja kwa madai kuwa wakati huo alikuwa anajiandaa kusafiri.
Alisema kuwa pamoja na kutoa taarifa kwa maofisa hao, alichukua fomu maalum na kujaza akieleza jinsi tukio zima lilivyokuwa na kuzipeleka kwenye uongozi wa kampuni hiyo, lakini alidai hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema baada ya malalamiko yake kupuuzwa na uongozi wa kampuni hiyo, alimfuata meneja wa kampuni hiyo na mkuu wa idara na kuwaeleza dhamira yake ya kumchukulia Mzungu huyo, hatua za kisheria, ambapo maofisa hao walimruhusu kufanya hivyo.
Alisema ndipo aliporipoti katika kituo kidogo cha Polisi Nyamongo na kufungua kesi yenye namba RB/1153/2007 na kuelekezwa na Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi, kuwa kuna tararibu za kuwakamata Wazungu wanaofanya kazi nchini, hivyo isingewezekana mtuhumiwa huyo kukamatwa hadi taratibu hizo zitakapokamilika.
Kauli aliyotoa OCS kwamba eti Wazungu hawakamatwi hivi hivi mpaka hatua fulani zifuatwe, ilinishangaza. Huyu ni mfanyakazi wa kawaida na si mwanadiplomasia anayewakilisha nchi yake. Huu si unyanyasaji wa wazi kabisa tunaofanyiwa ndani ya nchi yetu? alisema na kuhoji.
Alisema alirudi kituoni hapo Septemba 11 mwaka huu, na kumweleza mkuu huyo wa kituo kuwa, Mzungu aliyetishia kumuua alikuwa akijiandaa kutoroka nchini na kurudi kwao Canada, lakini alisema mkuu huyo wa kituo hakuonekana kujali na hakukuchukua hatua yoyote.
Alisema Septemba 12 mwaka huu, Mzungu huyo aliondoka Nyamongo kwa ndege hadi Dar es Salaam akiwa katika safari kwenda kwao Canada. Alisema alipoona hali hiyo alitoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, ambaye hata hivyo alikuwa nje ya mkoa kikazi hivyo akamtaka kuwasiliana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
Alisema mara baada ya kuwasiliana naye, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara alipokea taarifa hiyo na kuahidi kuifanyia kazi.
Alisema alituma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya kiganjani kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema akimweleza juu ya kutoroka kwa Mzungu huyo.
Alisema alipata taarifa baadaye kuwa Mzungu huyo alikamatwa na polisi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam ambapo alihojiwa kwa zaidi ya saa moja na kuachiwa huru baada ya kuthibitisha kuwa angerudi nchini Oktoba 3 mwaka huu, lakini hadi sasa bado hajarudi.
Aidha, Ndimanya alisema baada ya kuonekana akifuatilia ili Mzungu huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma dhidi yake, uongozi wa kampuni hiyo ulianza mikakati ya kumfukuza kazi.
Akielezea kuhusu mikakati hiyo, Ndimanya alisema Septemba 20 mwaka huu aliitwa na meneja wa kampuni hiyo, Bill MacNevin na kutakiwa aeleze kile kilichosababisha aondoke katika eneo la kazi bila taarifa, ambapo alimweleza kuwa kabla ya kwenda kituo cha polisi alimjulisha msimamizi mkuu wa idara yake.
Alisema meneja huyo kwa dharau alikejeli hatua aliyoichukua ya kuripoti tukio hilo kituo cha Polisi na kwa IGP na kusema kuwa hata kama angeripoti kwa rais, hakuna hatua yoyote inayoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Alisema Septemba 14 mwaka huu, aliitwa na jopo la uongozi wa kampuni hiyo na kupewa onyo la mwisho kwa maandishi kutokana na madai ya kuondoka katika eneo la kazi bila ruhusa, madai ambayo aliyakana.
Alisema wakati kikao cha kumjadili kinafanyika, Meneja wa kampuni hiyo hakuwapo na aliporejea Septemba 19 mwaka huu, alishangaa kuona kikao hicho hakikumfukuza kazi ndipo mipango ya kuhakikisha anafukuzwa kazi iliendelea.
Alisema Septemba 20 mwaka huu, aliomba ruhusa ili kwenda hospitali kungolewa jino na siku iliyofuata alianza likizo ya wiki mbili. Alisema aliporipoti kazini baada ya likizo hiyo, Oktoba 5 mwaka huu, walinzi walimzuia kuingia wakidai walipewa maelekezo hayo na mwajiri.
Alisema baadaye aliongozwa na walinzi hao hadi ofisini kwa mwajiri ambapo alipewa barua ya kuzuiliwa kutoka kambini na kuwekwa kizuizini hadi Oktoba 8 mwaka huu ambapo alijadiliwa, bila ya yeye kuwapo kwenye kikao na baadaye kupewa barua ya kufukuzwa kazi (nakala tunayo), ambayo haielezi bayana sababu za kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
Alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya madai hayo, Meneja wa Kampuni hiyo, Bill MacNevin alijibu kupitia kwa Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo Makao Makuu Dar es Salaam, Teweli Teweli, akikiri kuwapo kwa ushahidi wa mfanyakazi huyo kutishiwa na ndiyo maana kampuni iliamua kumfukuza kazi Mzungu huyo aliyemtishia.
Akielezea kitendo cha kufukuzwa kwa Ndimanya, meneja huyo alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kitendo cha utovu wa nidhamu alichoonyesha Ndimanya kwa kuripoti tukio hilo polisi, wakati uongozi wa kampuni ulikuwa unalishughulikia.
Aidha, Teweli alishindwa kueleza chochote juu ya kitendo cha kumzuilia Ndimanya katika mgodi huo kinyume cha sheria.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, David Saibul, alikiri kupata taarifa za tukio hilo na akaongeza kuwa, yeye aliambiwa na uongozi wa kampuni hiyo kuwa, Mzungu anayelalamikiwa kwa kutishia kuua alienda likizo kwao.
Hata hivyo, alikanusha madai yaliyotolewa na mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Nyamongo kuwa Wazungu hawawezi kukamatwa hadi baadhi ya taratibu zifuatwe.
Aidha, Kamanda huyo wa Polisi alisema ni kinyume cha sheria kwa kampuni au mtu binafsi kumzuilia mtu mwingine mahali kwani ni kuingilia utu na uhuru wa mtu huyo na kuongeza kuwa aliyefanyiwa hivyo ana haki ya kuripoti polisi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mhusika.
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/10/26/habari2.php