Wafanyabiashara wauza Vifaranga wasiofaa kuliwa baada ya Kuku kuadimika Dar

SemperFI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
1,762
3,565
Afisa Mifugo Mkoa wa Dar es Salaam Odetha Mchunguzi, amethibitisha kukosekana kwa kuku na kueleza kuwa hali hiyo imetokana na kupanda kwa bei ya vyakula vya kuku na zuio la Serikali la uingizaji wa vifaranga kutoka nje.

Uhaba huo kwenye masoko makubwa ya kuku ya Shekilango na Mwananyamala umesababisha baadhi ya Wafanyabiashara kuuza kuku wenye muda wa wiki mbili ambao sio sahihi kwa kuliwa.

Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala, Bertha Shekalaghe mtu anapokula nyama ya kuku wa kisasa ambaye hajafikisha siku 30 anajiweka katika hatari ya kupata magonjwa mengi ikiwemo presha ya damu, maradhi ya moyo, kuongeza sumu mwilini, kuongezeka uzito bila mpangilio na upungufu wa nguvu za kiume.

=======================

Nipashe ilibaini kuwapo kwa uhaba huo baada ya kutembelea masoko mbalimbali ambayo wafanyabiashara walikuwa wanauza kuku wadogo wanaokadiriwa kuwa chini ya miezi sita.

Katika soko la Shekilango, walionekana wafanyabiashara wengi wakisubiri magari yanayoleta kuku bila mafanikio. Hata waliobahatika, walipata kuku wadogo.

Aidha, Nipashe iliwaona wafanyabiashara wa chipsi na mama lishe katika masoko ya Mwananyamala na Shekilango wakiondoka sokoni bila kitoweo hicho.

Jabiri Omari, mfanyabiashara wa chipsi alisema amefikisha siku tatu hajapata kuku sokoni hivyo imemlazimu kuuza chips tu.

“Sokoni siku hizi kuku hawashikiki kabisa. Kila wanaokuja kwenye matenga tayari wana oda kwa hiyo unakaa unasubiri. Hata ukiwapata bei inakuwa kubwa tofauti na awali maana tulikuwa tunanunua Sh. 5,500 lakini sasa ni Sh. 8,000 kuku mmoja na mdogo,” alisema.

Irene Mfyate, anayejishughulisha na mama lishe, naye alisema: “Kwa kweli kuku hawashikiki kabisa na hali hii imeanza kama wiki tatu hivi, sijui shida nini? Mimi nauza wali na nilikuwa nauza wali kuku, lakini kuku sina na siuzi wali kuku tena mpaka pale watakapoanza kupatikana kwa wingi,”alisema.

Mmoja wa wauzaji wa kitowewo hicho katika soko la Mwananyamala, Stephano Balama, alisema uhaba wa bidhaa hiyo unatokana na uzalishaji mdogo tofauti na ilivyokuwa awali.

“Sisi tunanunua kwa bei ya juu kutoka kwa walanguzi, hivyo lazima tutawauzia wateja bei kubwa. Hii yote kwa sababu serikali imepiga marufuku vifaranga kutoka nje bila kujua uwezo wa kuzalisha hapa kwetu ni mdogo, kuku wetu pia ni wadogo sio kama wale wa kutoka nje ya nchi,”alisema.

“Wafugaji wanalalamika bei za vyakula vya kuku ziko juu kwa hiyo hata gharama za utunzaji wake tofauti na awali, hivyo lazima bei itapanda kuanzia kwa mteja mdogo hadi mkubwa,” aliongeza.

Kutokana na hali hiyo, mfanyabiashara wa kuku, Amiri Ali, alisema anafikiria kuachana na biashara hiyo kwa kuwa anapata faida ndogo na malighafi haipatikani.

“Hawapatikani hata ukiwapata unawapata wadogo halafu kwa bei kubwa kwa hiyo inakulazimu na wewe uuze kwa bei kubwa ukiwauza kwa bei ndogo faida hupati,”alisema.

Nipashe pia ilishuhudia kuku wadogo tena wachache wakiwa katika matenga tayari kwa kuwauziwa wateja waliokuwa wamefurika maeneo hayo.

Simoni Tarimo, ambaye ni mbobezi katika biashara akijihusisha na kununua kwa wafugaji na kuwauza sokoni anasimulia hali ilivyo alisema: “Unaenda kwa mfugaji kufuata kuku unakuta naye hana kwa sababu vifaranga havipatikani kwa urahisi kutoka kwa wazalishaji. Kingine, bei ya vyakula vya kuku iko juu kiasi kwamba mfugaji anaona hapati faida kutokana gharama za matunzo.”

Mfugaji wa kuku maeneo ya Tandale, Fred Amidu, alisema kukosekana kwa vifaranga kutoka kwa wazalishaji ndio sababu ya kushindwa kuwafuga pamoja na wimbi la utapeli lililopo katika kupatikana kwa mbegu nzuri ya vifaranga.

“Licha ya serikali kuzuia vifaranga kutoka nje ya nchi, bado kuna shida ya kupata mbegu nzuri ya kuku. Mbegu inayopatikana hapa vifaranga havikui, unakuta mwezi unaisha bado kuku mdogo yupo kwenye rika la kifaranga

“Vile vifaranga vya kutoka nje ya nchi yaani wiki mbili tu tokea ulipoanza kuvihudumia vinakuwa tayari unapata kuku mkubwa na anakuwa na nyama nyingi. Sasa hivi tunawalisha wahitaji vifaranga na si kuku kama ilivyokuwa awali. Kitaalamu kuku hao wasipotimiza muda wake huwa wanakuwa na madhara makubwa kwa afya,”alisema.

WAZALISHA WANENA

Mmoja wa wazalishaji wa vifaranga hivyo, Jeremia Jumanne, alisema: “Wakati wa kuzalisha vifaranga tunapata changamoto sana. Mbegu ya kuku wa ndani ni tofauti na wale kuku wa nje. Vifaranga vinakufa sana wakati wa kuzalisha katika vifaranga 100 lazima 30 vitapotea, havina uwezo wa kustahimili hali ya hewa sasa ukizingatia msimu huu kuna baridi kidogo.

“Hata huko tunakochukua mayai kwa ajili ya kuyatotolesha nako yanapatikana machache kimsingi mayai yanayokuja hayakidhi mahitaji ya kuzalisha kuku wengi.”

Mtaalamu wa Lishe Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mwananyamala, Bertha Shekalaghe, aliyataja madhara kwa mtu anapokula nyama ya kuku ambaye hajatimiza muda wake.

“Mtu anapokula nyama ya kuku wa kisasa ambaye bado hajafikisha siku 30 anajiweka katika hatari ya kupata magonjwa mengi sana ikiwamo presha ya damu, maradhi ya moyo, kuongeza sumu mwilini, pamoja na kuongezeka uzito bila mpangilio, upungufu wa nguvu za kiume,” alisema.

KAULI YA SERIKALI

Ofisa Mifugo Mkoa wa Dar es Salaam, Odetha Mchunguzi, alithibitisha kukosekana kwa kuku ambayo inachangiwa na kupanda kwa bei ya vyakula vya kuku na zuio la vifaranga kutoka nje.

“Ni kweli kuna uhaba wa kuku kwa sababu gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana, lakini uzalishaji huu unatokana na zuio la kuchukua vifaranga kutoka nje ya nchi, kama serikali itaruhusu tena vifaranga kutoka nje ya nchi basi uhaba utapungua kama ilivyokuwa awali,” alisema.

Alisema bei ya chakula cha kuku imeongezeka kutoka Sh. 50,000 hadi 80,000 kwa mfuko wa kilo 50, hali ambayo inakwamisha wafugaji wengi kuachana na biashara hiyo.

Kwa mujibu wa Mchunguzi, vifaranga vinavyozalishwa hapa ndani ya nchi vinaathiriwa na hali ya hewa ya kipindi hiki cha baridi kidogo vifaranga vinakufa sana hiyo nayo inapunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Julai 22, mwaka huu, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akiwa jijini Dodoma alipiga marufuku uingizaji vifaranga kutoka nje ya nchi kwa lengo la kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege na kulinda soko la ndani.

Chanzo: Nipashe
 

antimatter

JF-Expert Member
Feb 26, 2017
35,326
90,855
...mtu anapokula nyama ya kuku wa kisasa ambaye hajafikisha siku 30 anajiweka katika hatari ya kupata magonjwa mengi ikiwemo presha ya damu, maradhi ya moyo, kuongeza sumu mwilini, kuongezeka uzito bila mpangilio na upungufu wa nguvu za kiume.
Walaji wakubwa wa kuku wa kisasa ni wanawake na watoto, siyo wanaume 😁
 
2 Reactions
Reply
Top Bottom