Wadau Zaidi ya 3,000 Kunufaika na Mikopo ya Ufugaji Samaki

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,897
941

WADAU ZAIDI YA 3,000 KUNUFAIKA NA MIKOPO YA UFUGAJI SAMAKI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 inatekeleza mradi wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba ya pembejeo za ufugaji samaki ambayo itawanufaisha wafugaji samaki 3,154.

Mhe. Silinde aliyasema hayo Mei 25, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mhe. Bryceson Tumaini aliyetaka kujua kuwa Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wavuvi ambao wameunda vikundi na kuanza ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Jimbo la Busanda, mkoani Geita.

“Jumla ya wanufaika 3,154 wameainishwa kunufaika na mradi huo ikijumuishwa vikundi 93, kampuni 10, na watu binafsi 32. Kwa upande wa Geita DC vikundi vitatu (3) vinatarajiwa kunufaika na program hiyo ikiwemo kikundi cha Tumaini chenye wanachama 10 kutoka Jimbo la Busanda. Vikundi hivi vitapatiwa mikopo ya pembejeo za ufugaji samaki kwenye vizimba yenye thamani ya shilingi milioni 69.4 kwa kila kikundi”, alisema

Aliongeza kuwa, katika mwaka 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza mradi huo ambapo utawezesha ufugaji samaki kwenye vizimba 893 huku akitoa wito kwa wafugaji samaki nchini wakiwemo wale wa Jimbo la Busanda kuendelea kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika wa ufugaji samaki.

Alisema kuwa mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu wamepokea fedha jumla ya Shilingi Bilioni 24 kwa ajili ya kuwezesha miradi ya ufugaji samaki na hatua ilyofikia kwa sasa ni utolewaji wa mikataba ya mikopo husika kwa wanufaika ambao ni wavuvi, wafugaji samaki kwenye vizimba na wakulima wa mwani.

“Serikali kupitia TADB inatoa mikopo kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wakuzaji viumbe maji ili kuboresha shughuli zao za uzalishaji. Aidha, Serikali inawahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi,” alifafanua.

WhatsApp Image 2023-05-27 at 20.34.24.jpeg
 
Back
Top Bottom