Wadau wa habari wahimiza kukamilika sheria mpya ya habari Zanzibar

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99

KAMATI ya Wadau wa Habari Zanzibar (ZAMECO) imekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya sekta ya habari, changamoto na hatua zilizofikiwa katika kuendeleza sekta hiyo muhimu katika ujenzi wa jamii inayozingatia usawa, maendeleo, haki za binadamu na inayojali misingi ya kidemokrasia.

Kikao hicho maalum kilijadili kwa kina changamoto za sheria za habari Zanzibar na hatua mbali mbali zilizochukuliwa na wadau wa habari katika kutoa maoni hususan katika kufanya uchambuzi wa kina wa sheria hizo ambazo kwa kiasi zinawakwaza waandishi wa habari katika kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Tunachukua fursa hii kuwapongeza wadau mbalimbali walioshirikiana na vyombo vya habari ikiwemo serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata haki ya kupata na kutoa taarifa kwa kuzingatia mamlaka yanayotolewa na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Kifungu cha 18, pamoja na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda inayosimamia uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Wakati tunaingia mwaka huu wa 2024, waandishi na vyombo vya habari wana matumaini makubwa ya kuongezwa ushirikiano pamoja na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, vyombo vya habari, waandishi wa habari na wadau wa sekta hiyo pamoja na watetezi wa haki za binaadamu na utawala bora, wamekuwa wakipigia kelele kuwepo kwa mazingira mazuri/rafiki ya utendaji kazi.

Mazingira haya huletwa na sheria iliyo rafiki ambayo hutoa hakikisho la kutumika kwa uhuru mpana wa kutoa maoni, na uhuru wa vyombo vyenyewe vya habari katika kutafuta, kuchakata na kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii ikiwa ni jukumu mahsusi la vyombo vya habari kwa umma na taifa.

Sheria kuu ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya magazeti namba 5 ya mwaka 1988 iliofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 1997 pamoja na Sheria ya utangazaji namba 7 ya mwaka 1997 iliofanyiwa marekebisho na sheria namba 1 ya mwaka 2010.

Aidha, tunapongeza na kuishukuru wadau na Serikali kwa jinsi ilivyobeba ajenda hii muhimu na kwa ahadi yake kupitia kauli na matamshi ya viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiongozwa na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye alieleza wakati wa kutimiza siku 100 za Uraisi wake.

Kwa bahati mbaya hadi sasa sheria hizo hazijarekebishwa. Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita pia amekuwa akieleza hamu hiyo ya Serikali ya kuwa na sheria mpya na nzuri.

Kutokana na mtazamo huo wa kiuongozi, tumekuwa na matumaini ya kuona utekelezaji wa ahadi hiyo unafanywa kwa mtitiriko mzuri katika namna ambayo unafikia tamati kwa kupatikana sheria mpya ya habari badala ya sheria iliyopo sasa ambayo sio sisi wadau wala serikali yenyewe isiyotambua ukweli kwamba ni sheria ya muda mrefu na ambayo haiendani tena na ile dhamira njema ya kiongozi wa nchi yetu, na kadhalika, ikiwa isiyokidhi mazingira mapya yaliyochagizwa na kasi ya ukuaji wa teknolojia, uwazi na uwajibikaji.

Kwa kuwa yamekuwepo maoni na mapendekezo mengi ya Waandishi wa Habari pamoja na Wadau wa Haki za Binaadamu, mapendekezo ambayo yapo mikononi mwa mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunaamini wakati umefika sasa wa kuendelea kufanyiwa kazi ili kuhakikisha lile lengo lililokusudiwa, linafikiwa kwa wakati muafaka.

Ni matamanio yetu kwamba mwaka huu wa 2024 ndio muda sahihi wa kuona lengo la kupatikana kwa sheria mpya iliyo rafiki kwa kila upande, linafikiwa.

Aidha wadau wa habari wataendelea kuwa tayari kutoa ushirikiano wa aina yoyote inapohitajika kwa ajili ya kutimiza lengo hilo.
 

Attachments

  • ZAMECO STATEMENT JANUARY 17, 2024.pdf
    321.8 KB · Views: 2
Back
Top Bottom