Hoja ya kutokuwa na imani na serikali yasukwa
*Utabiri wa CCM kufuata nyayo za Kanu watolewa
*Vijana CCM waendelea kuasi K'njaro na Moro
Kuna kila dalili kuwa suala la fidia ya Sh. bilioni 94 kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans ambayo ilishinda kesi dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), litailipua nchi hasa baada ya chama tawala kuafiki uamuzi huo.
Mlipuko huo umeongezewa nguvu na uamuzi uliopitishwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wiki iliyopita kuwa fidia hiyo ni lazima ilipwe kwa kuwa mkataba wa Tanesco na Dowans ulivunjwa kinyume cha sheria.
Kutokana na tamko hilo, kundi la wabunge wa upinzani ambao si sehemu ya upinzani rasmi, limeibuka na kuazimia kwamba sasa wanakusudia kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Serikali kama kweli fedha hizo zitalipwa.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema kwamba ataliomba Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani na Serikali iwapo kampuni hiyo italipwa fedha hizo kabla ya Mkutano ujao wa Bunge, unaotarajiwa kuanza Februari 8, mwaka huu.
Alitaka hoja ya Dowans iruhusiwe kwenda bungeni kabla malipo hayo hayajafanyika ili wabunge wakaihoji Serikali juu ya suala hilo.
Kafulila akitoa msimamo huo huku akiungwa mkono na wenzake. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kinaunda upinzani rasmi bungeni tayari kimetahadharisha juu ya fidia hiyo, huku Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, akiwa amekwisha kuuibebesha serikali na CCM mzigo wa fidia hiyo kutokana na uzembe.
Akiwasha moto huu mpya, Kafulila alisema anataka Serikali iwaeleze Watanzania imekuwaje hadi kulazimishwa kuilipa kampuni ambayo mkataba wake una utata.
Kafulila, ambaye pia ni Katibu wa kamati ya kambi isiyo rasmi ya upinzani bungeni, alitoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari, ulioitishwa na kamati hiyo, katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, pamoja na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Teule ya Bunge la Tisa iliyochunguza mchakato wa zabuni iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond Development LLC, Mohammed Habib Mnyaa, waliunga mkono kauli ya Kafulila.
Uamuzi wa serikali wa kuilipa Dowans fedha hizo, ulitangazwa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Januari 6, mwaka huu akisema imekubaliana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) iliyoliamuru Tanesco kuilipa kampuni hiyo Sh. Bilioni 94.
Kafulila alisema amefikia hatua hiyo kwa vile uamuzi wa kuilipa Dowans ni mbaya na kwamba, endapo Serikali itautekeleza itakuwa inajitia kitanzi.
Alisema Desemba 10, mwaka jana aliwasilisha ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam barua ya kusudio la kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhoji kwanini Serikali isiwajibike kwa kuliingiza taifa hasara kwenye sekta ya umeme.
Pia, kuliomba Bunge kuazimia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa sera ya nishati na madini na mpango kabambe wa usambazaji umeme na hivyo kusimamia migawo mitatu ya umeme ndani ya miaka miwili ya uongozi wake.
Hata hivyo, alisema Desemba 14, mwaka huo, barua hiyo ilijibiwa kwa kuelezwa kwamba, maombi yake yanafanyiwa kazi.
Alisema wakati akisubiri kufanyiwa kazi maombi ya barua yake, Waziri wa Ngeleja akalitangazia taifa kuhusu uamuzi wa serikali wa kukubali kuilipa Dowans.
CCM ITAFUATA KANU
Kafulila alisema ubaya wa kuilipa Dowans, unatokana na kashfa ya kampuni hiyo kufanana na ile iliyoikumba Serikali ya Kenya, ya Goldenberg, ambayo ilipata kuuangusha utawala wa serikali ya nchi hiyo iliyokuwa chini ya Kanu mwaka 2007.
Kashfa ya Goldenberg ilijitokeza katika miaka ya 1990 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi, ambayo ilisababisha serikali kupoteza dola milioni 600 kwa njia ya biashara ya kughushi ya kusafirisha almasi na dhahabu nje ya nchi.
Kashfa ya Goldenburg, iliangusha utawala wa Kanu na kusababisha (Rais wa sasa wa Kenya, Mwai) Kibaki, aingie madarakani kupitia chama cha NARC. Sasa serikali ya Tanzania ikicheza na Dowans/Richmond mpaka 2015 wajue historia ya Kanu itatimia kwao, alionya Kafulila.
Aliongeza kuwa: " Ni miaka tisa tu, 1993-2002 Goldenberg ikaondoa Kanu Kenya, 2006-2015 Dowans/Richmond itaondoa CCM Tanzania. Kwa hiyo miaka tisa (1993-2002) ya Goldenberg iliangusha Kanu mwaka 2002. Na miaka tisa (2006-2015) itaangusha utawala wa CCM uchaguzi wa 2015.
Kafulila alisema ushahidi mwingine wa ubaya wa uamuzi wa kuilipa Dowans, ni namna ilivyozua mtafaruku hadi ndani ya serikali yenyewe, ambako mawaziri wa serikali moja wamekuwa wakitoa matamshi ya kupingana.
Alisema mbali na hayo, uamuzi wa kuilipa Dowans, unaipunguzia serikali uhalali wake wa kisiasa, ambapo inakuwa vigumu kuwahamasisha watu kuisikiliza, kuiamini na kuiunga mkono.
Alisema pia, kashfa ya Dowans, hadi sasa ukweli wake haujulikani, umefichwa.
"CCM wameshaiba na kufanya ufisadi mkubwa. Wizi huu wa Dowans hauna muafaka. Unakwenda kuiondoa CCM madarakani, alisema Kafulila.
Aliitaka serikali kutocheza na Dowans, badala yake akataka suala hilo lifikishwe bungeni ili serikali ikalitolee ufafanuzi kwa kueleza kwanini ilishindwa kesi iliyofunguliwa na kampuni hiyo na kuwafikisha Watanzania hapa walipo.
"Hoja ya Dowans iruhusiwe, iende bungeni kabla malipo hayajafanyika. Huko ndiko ambako tutaulizana tumefikishanaje hapa? Wakilipa kabla haijapelekwa bungeni, hoja itapanuka.
Sasa sitaliomba Bunge kama nilivyokusudia awali limwajibishe Waziri wa Nishati na Madini tu, bali nitaliomba liazimie kutokuwa na imani na serikali yote. Kwa sababu hakuna haraka ya kulipa 'fasta fasta'," alisema na kuongeza kuwa:
"Watu wengi wanahitaji sheria, lakini mbona ilishafikia hadi walimu wanavua nguo katika kudai haki zao? Wazee wetu wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki karibu miaka 20 wanadai haki zao hadi wanalala barabarani.
Mbona haraka ya kuwalipa haikuwapo? Hivyo, nitamwomba Mheshimiwa Spika, hili jambo (la Dowans) lifikishwe mwisho na kuwawajibisha wote waliohusika."
Hamad Rashid Mohamed akiunga mkono kauli ya Kafulila, alisema wanataka hoja ya Dowans ipelekwe bungeni ili ifikie tamati.
Alisema hata mtu aliyefungwa gerezani, hukumu yake inaweza kurudishwa mahakamani ikapitiwa upya.
" Hata kama ni wabunge ndio walioamua kuhusu Richmond/Dowans nao ni binadamu vilevile," alisema Hamad akitilia msisitizo wa kutaka hoja ya Dowans ipelekwe bungeni kujadiliwa.
Alisema kwa sasa kanuni za Bunge haziruhusu suala lililokwishaamuliwa na Bunge kujadiliwa upya, lakini akasema kanuni ya 150 ya Bunge inawaruhusu wabunge kutengua kanuni hiyo iwapo jambo linalotaka kujadiliwa ni kwa maslahi ya taifa.
Naye Mnyaa, alisema wabunge wako tayari kuijadili upya hoja ya Richmond/Dowans iwapo itaruhusiwa kurejeshwa bungeni na kwamba, hilo haliwapi hofu yoyote.
SITTA, MWAKYEMBE NI MASHUJAA
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameunga mkono tamko la Umoja wa Vijana wa CCM(UVCCM), kwa ujasiri na uzalendo wao wa kupinga Kampuni ya Dowans kulipwa Sh. bilioni 94 ambazo ni jasho la Watanzania wote.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam, Mtikila alisema kitendo cha UVCCM, kutoa tamko lenye uzalendo inadhihirisha kwamba wao ni daraja muhimu la kuunganisha na wananchi katika vita ya ukombozi wa nchi.
"Naunga mkono tamko la UVCCM la kupinga Dowans kulipwa mabilioni hayo ambayo awali zilitakiwa kukombwa Sh. bilioni 186, lakini baada ya wazalendo kupiga mayowe dhidi ya majambazi, hesabu ikapungua na kuwa Sh. bilioni 94," alisema Mchungaji Mtikila na kuongeza kuwa:
"Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ni viongozi pekee wanaotetea maslahi ya nchi dhidi ya majambazi wanaotegemea jasho la walalahoi."
Alisema Watanzania wakisimama kwa pamoja kuhusu Dowans haitatolewa hata senti moja na kwamba anaungana na wote wenye mawazo kama yaliyotolewa na UVCCM.
VIJANA MORO NAO WALIPUKA
UVCCM Morogoro wameunga mkono tamko la kamati ya utekelezaji Umoja huo taifa uliotolewa wiki iliyopita kuhusu sakata la Dowans kurejeshwa bungeni na kujadiliwa upya.
Umoja huo umeitaka Serikali na uongozi wa taifa wa CCM kuchukua hatua za haraka za kuwaweka kando baadhi ya mawaziri wanaopingana na misimamo ya Serikali kuhusiana na sakata hilobila kufuata taratibu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wake, Jonas Nkya baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilichoshirikisha pia viongozi wa matawi ya umoja huo kutoka vyuo vikuu.
" Tunaomba chama chetu kuwachukulia hatua haraka ili kuwaweka kando watu hao ili kukinusuru chama na serikali, lazima kuwe na msemaji mmoja. Iweje leo maelekezo na misimamo yake ipingane," alisema Nkya.
Aliiomba Serikali na CCM kutoa msimamo wa msemaji kwenye masuala nyeti na muhimu ili kutowapa nafasi viongozi waropokaji na wanaokurupuka.
Akitoa msimamo wa UVCCM kuhusu Dowans, Mjumbe wa Baraza hilo kutoka Chuo cha Ualimu (Motco), Said Sambala, alitaka Serikali itafakari kwa umakini kuhusu Dowans kwa kuwa linawagusa wananchi.
" Tunataka hoja ya Dowans irudishwe bungeni ili wahusika wajulikane na kama wapo walioishauri Serikali na wale wote wenye makosa wachukuliwe hatua za kisheria, alisema Sambala.
KILIMANJARO NAKO MOTO
Nao UVCCM mkoani Kilimanjaro umeunga mkono tamko la Kamati ya Utekelezaji la Umoja huo Taifa na kueleza kuwa mabishano ya baadhi ya mawaziri hadharani juu ya Dowans kulipwa kulipwa fedha hizo kuwa ni ishara mbaya kwa Taifa.
Mwenyekiti wake, Godliving Moshi,alisema mabishano hayo yanahitaji utatuzi wa haraka kwani ni aibu kwa mawaziri kubishana hadharani wakati kauli zaozinapaswa kuwa moja.
Alisema sakata hilo limesababisha mawaziri kuwa na kauli tofauti, jambo ambalo alisema linashangaza na kutoa mfano mbaya.
Wiki iliyopita, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM pamoja na mambo mengine, ilipinga mpango wa serikali kuilipa Dowans kiasi hicho cha fedha kama hukumu ya ICC ilivyoagiza.
Baraza hilo lilitoa tamko kwamba hoja hiyo irudishwe bungeni ili wananchi wajue ni nani aliyeifikisha hapo ilipo.
CHANZO: NIPASHE