BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,007
Dk. Slaa awindwa bungeni
Waziri Kombani, Ghasia waongoza mkakati
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
Waziri Kombani, Ghasia waongoza mkakati
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MWENENDO wa mambo katika mkutano wa 15 wa Bunge, unaoendelea mjini hapa, unazidi kuwa na utata mara baada ya kuwapo taarifa kuwa serikali imeanza mkakati maalumu wa kummaliza kisiasa na kumfungulia kesi ya jinai, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa.
Habari za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima Jumatano kutoka kwa baadhi ya wabunge, zimedai kuwa, kwa siku kadhaa sasa, mawaziri wawili wamekuwa wakipanga mkakati huo wakishirikiana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadhi wa kutoka kambi ya upinzani.
Mawaziri wanaotajwa kuendesha mkakati huo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani.
Habari hizo zinadai kuwa, mawaziri hao wamekuwa wakipita kwa wabunge wakiwaeleza kuwa serikali imetambua kuwa ni jambo la hatari kuendelea kuwa na mtu wa aina ya Dk. Slaa bungeni, akiwa na wadhifa wa unyekiti katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa.
Mbunge mmoja aliyefuatwa na mmoja wa mawaziri hao na kushawishiwa kushiriki katika mpango wa kumshughulikia Dk. Slaa na kufanikiwa kuzungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini, alieleza kuwa, Waziri Kombani anasimamia mpango wa kumuondoa Dk. Slaa katika wadhifa wake wa Uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, huku Waziri Ghasia akiwa ameweka watu maalumu wanaochunguza maofisa wa serikali anaozungumza nao, wanaodhaniwa kuwa ndio wanaompatia nyaraka za siri za serikali zinazohusu ufisadi.
Mimi nilifuatwa na Waziri Kombani mwenyewe, kwa mdomo wake akaanza kunishawishi niisaidie serikali kumshaghulikia Dk. Slaa, kwa sababu ni mtu hatari anayeinyima usingizi. Aliniambia kuwa ni vigumu kujua watu wanaompatia nyaraka za siri za serikali, hasa zile zinazohusu ufisadi, kwa sababu Waziri Ghasia ameweka watu maalumu wanaofuatilia maofisa wa serikali alio karibu nao, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio.
Waziri Kombani aliniambia kuwa, Waziri Ghasia alifikia uamuzi huo ili kujua maofisa wa serikali anaowasiliana nao kwa sababu hao ndio wanaompatia nyaraka za siri za serikali, na kwamba kama akikamatwa nazo safari hii, hatapona, alisema mbunge huyo.
Mmoja wa viongozi wa kambi ya upinzani aliyezungumza na gazeti hili na kutaka jina lake lihifadhiwe kwa sababu ameteuliwa kuongoza timu ya kuchunguza madai hayo dhidi ya Dk. Slaa, alisema kambi ya upinzani inazo taarifa hizo na inazifanyia kazi kwa siri, kwa sababu baadhi ya wabunge wa kambi hiyo wamenunuliwa ili kumuangamiza.
Alisema uchunguzi wa timu yake umebaini kuwa, Dk. Slaa alianza kuingia katika mgogoro na wabunge baada ya kuzuia posho ambazo wajumbe wa kamati walikuwa wakilipwa na halmashauri mara wanapokwenda kuzikagua.
Hali ni mbaya, lakini tunafanya kazi na tutalipua bomu ili wananchi wajue kuwa vita hii inapiganwa pia na mawaziri na si wabunge peke yao.
Uchunguzi wa timu yangu umebaini kuwa, Dk. Slaa alianza kuchukiwa na wabunge wenzake alionao katika kamati moja ambayo yeye ni mwenyekiti wake, baada ya kuzuia malipo ya posho kutoka halmashauri walizokuwa wakifika kuzikagua kwa sababu ni kinyume cha taratibu.
Lakini Dk. Slaa, alikuwa na sababu ya msingi ya kuzuia posho hizo, kwa sababu Bunge linawalipa wabunge kila wanapokuwa katika shughuli halali za Bunge. Kulipwa na halmashauri ni kinyume cha taratibu, kwa sababu wanakuwa wamelipwa posho mara mbili kwa kikao kimoja. Sasa alipozuia kwa sababu walikuwa wamezoea, chuki ikaanza, alisema kiongozi huyo wa upinzani ambaye pia ni mbunge.
Akizungumzia wabunge na mawaziri wanaoongoza mkakati huo wa kummaliza Dk. Slaa, alisema taarifa za uhakika alizonazo ni pamoja na Waziri Kombani na Mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene, ambao wamekuwa wakipita kwa wabunge wakiwataka kuungana kwa pamoja kupinga hatua za upotoshaji zinazofanywa na Dk. Slaa kwa lengo la kulichafua Bunge.
Alisema Waziri Kombani tayari amekwishakutana na Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kihwelu (CHADEMA) na kumshawishi akubali kuchukua wadhifa wa Dk. Slaa wa uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa mara tu atakapoondolewa, na kwamba alimuahidi kuwa serikali itakuwa pamoja naye katika shughuli zake zote zinazohusu ubunge.
Kuhusu Waziri Ghasia, alisema baadhi wa wabunge wameishasikika wakieleza kuwa wamepewa kazi maalumu na waziri huyo ya kuchunguza na kumpatia taarifa iwapo Dk. Slaa ana nyaraka mpya za serikali na mahali alikozihifadhi ili akamatwe na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri Kombani alilieleza gazeti hili kuwa, hana ugomvi na Dk. Slaa, hivyo hana sababu yoyote ya kushiriki katika mpango wa kumuangamiza kisiasa au kumfikisha katika vyombo vya dola.
Aliongeza kuwa, alichokisema Dk. Slaa hakihusiani na wizara yake na kwamba tangu alipoingia katika utumishi wa umma, hajawahi kuhusika katika tuhuma au kashfa yoyote na jambo hilo hataruhusu litokee.
Tanzania Daima Jumatano lilipowasiliana na Kihwelu na kumuuliza kuhusu madai hayo, alisema hana taarifa hizo, lakini lilipomueleza kuna ushahidi kuwa alikutana na Waziri Kombani na akashawishiwa kukubali kuchukua nafasi ya Dk. Slaa katika kamati yake atakapoondolewa, alinyamaza kwa muda kisha akasema ni jambo la kweli, lakini hapendi kulizungumzia.
Jamani hili jambo umelijuaje, sikiliza ndugu yangu, mimi Waziri Kombani alinifuata pale ofisi za benki bungeni, akaniambia jambo hilo, lakini nilikataa hapo hapo na nilimueleza wazi kuwa siwezi kumsaliti kiongozi wangu kwa sababu hana kosa na anachokitetea ni cha kweli. Sikuendelea kusikiliza maneno yake, nilimuacha hapo benki, alisema Kihwelu.
Baadaye gazeti hili liliwasiliana tena na Kombani na kumueleza kuwa kuna taarifa alikutana na Kihwelu na kumshawishi awe tayari kushika nafasi ya Dk. Slaa, waziri huyo alikana, na kueleza kuwa katika maisha yake yote bungeni hajawahi kufika katika ofisi hizo.
Naomba mniamini, simo katika mkakati huo, hapo benki ya Bunge mimi sijawahi kufika na hata leo nilikuwa sina hela kabisa, lakini nilimtuma mtoto wangu benki akaenda kunichukulia. Mimi ni msafi, simo katika kashfa hizo, alisisitiza Waziri Kombani.
Naye Simbachawene alipoulizwa kuhusu madai ya kushiriki kwake katika mpango huo alikana na kueleza kuwa, Dk. Slaa ni shemeji yake, hivyo hawezi kushiriki katika mpango wowote wa kumuumiza.
Simbachawene alieleza zaidi kuwa, ingawa hakubaliani na vitendo vya Dk. Slaa, hasa kutangaza maslahi ya wabunge, lakini hata kama yeye na wenzake wana nia hiyo, hawawezi kufanikiwa kwa sababu suala hilo halihusiani na kamati.
Dk. Slaa ni shemeji yangu, siwezi hata kidogo kushiriki mkakati wowote wa kumuumiza. Mimi sikubaliani naye anapotangaza maslahi ya wabunge, kwanza tunalipwa kidogo sana kulingana na wabunge wenzetu wa nchi nyingine. Lakini hata kama mimi na wenzangu tuna mpango wa kumshughulikia, naamini hatuwezi kufanikiwa kwa sababu suala hilo halipo katika kamati yake, alisema Simbachawene.
Tanzania Daima Jumatano ilipowasiliana na Dk. Slaa kuhusu madai hayo, alikiri kuwa anazo taarifa za kuwapo kwa mikakati hiyo, lakini haimtishi kwa sababu uenyekiti wa kamati si uhai wake, bali ni sehemu ya majukumu ya kuwashughulikia wananchi.
Alisema hashangazwi na hatua ya mawaziri hao kuandaa hujuma dhidi yake, kwa sababu anatambua kuwa mtu yoyote anapokuwa mwiba kwa serikali, lazima ifanye mkakati wa kumshughulikia.
Nina taarifa kuhusu mipango hiyo, lakini mimi ni mbunge ninayejua majukumu yangu, jambo hilo halinisumbui. Hawa mawaziri wamepoteza mwelekeo, hawamsaidii rais, wanamuumiza. Niwaambie kwamba nikiletewa nyaraka hizo wanazoita za siri lakini zinaeleza ufisadi, nitazichukua wanikamate. Wakinikamata nitafurahi sana kwa sababu tutakwenda mahakamani, tutapambana, huko kila kitu kitajulikana kuhusu siri za serikali, alisema.
Alipoulizwa anavyojisikia baada ya kuzomewa na wabunge na hata kubezwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta kutokana na hatua yake ya kutaja mishahara na posho za wabunge alisema kwa kujiamini: Hata Spika akiwa mkali ninapozungumzia mishahara na posho kubwa za wabunge, hanisumbui, kwani mara ngapi amenitaka nifute kauli zangu bungeni, kama sifuti au nafuta najua mimi. Mara ngapi ameniambia atanipeleka polisi? Muhimu afahamu kuwa jabali huwa halitikisiki.
Tangu kuanza kwa mkutano wa 15 wa Bunge, Dk. Slaa amekuwa katika wakati mgumu kutokana na wabunge kumshambulia kwa maneno na kumzomea anaposimama kuzungumza bungeni, wakimtuhumu kuwa amefanya kosa kutaja kiwango cha mishahara na posho wanazolipwa wabunge.