Viwango vya kubadilisha fedha vyakuza deni nchi za Afrika

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,991
12,343
Na. Eva Valerian na Peter Haule, WF, Victoria Falls, Zimbabwe

Madeni ya nchi nyingi za Afrika yanakua kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa viwango vya riba na kubadilisha fedha duniani na kusababisha kushuka kwa thamani ya fedha za ndani.

Hayo yamebainishwa Mjini Victoria Falls, Zimbabwe, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi kutoka nchi za Umoja wa Afrika unaoratibiwa na Kamisheni ya Uchumi chini ya Umoja wa Mataifa (UNECA)

Bw. Mwandumbya alisema kuwa awali ukuaji wa deni ulikuwa unaendana na ukopaji lakini kwa sasa imebainika kuwa kuna sababu zingine zinazochochea kuongezeka kwa deni hilo ikiwa ni pamoja na mabadiliko makubwa ya viwango vya kubadilisha fedha na riba hivyo kuzifanya nchi za Afrika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo.

Alisema kuwa katika kulihudumia deni “dept service” lililoongezeka, kumekuwa na changamoto kubwa kwa sababu nchi nyingi bado hazina uwezo wa kukusanya mapato ya kutosha kuweza kugharamia huduma mbalimbali.

“Sisi Tanzania tunashukuru kwa kuwa kupitia Taasisi za Kimataifa za Moody’s na Fitch zinazojihusisha na ufanyaji tathimini kwa nchi ili kujua uwezo wake wa kukopesheka katika masoko ya fedha ya Kimataifa, wamethibitisha kwamba nchi yetu ipo kwenye viwango vizuri vya kuweza kuendelea kukopesheshwa miongoni mwa nchi chache”, alisema Mwandumbya.

Bw. Mwandumbya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza vyema kwenye suala hilo na hatimae nchi kuweza kuwa na viwango vya deni ambavyo ni himilivu na vinavyokubalika kimataifa.

Aidha Bw. Mwandumbya alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa madeni hususani kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya tabianchi ni lazima nchi za Afrika kuwa na mkakati wa kuhakikisha zinapata rasilimali fedha ili mipango inayotekelezwa iweze kukidhi mategemeo ya wananchi.

“Changamoto kubwa ambayo tunaiona hapa kwa nchi zetu za Afrika ni ile haja ya kuendelea kukusanya mapato ya kutosha ili kujihakikishia kwamba tunaweza kupata rasilimali za kuweza kuhudumia deni lakini pia tunaweza kulipa mishahara pia kuhudumia gharama mbalimbali za kibajeti”, aliongeza Bw. Mwandumbya.

Alisema katika mkutano huo agenda kubwa inayojadiliwa ni kujaribu kupata suluhu ya namna gani nchi zitaboresha viwango vya ukusanyaji wa mapato ili kutoka kwenye viwango vya chini ya asilimia 11 na 12 ya Ukuaji wa Mapato ya Ndani (GDP) kwenda viwango ambavyo vinavyokubalika kuanzia asilimia 16.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, alisema kuwa dhumuni la mkutano huo wa 56 ni kubadilishana mawazo na hasa kwenye kauli mbiu inayosema Financing the Transition to Inclusive Green Economies in Afrika inayotoa hamasa na kutafakari njia ambazo zinaweza kutumika kufadhili Uchumi na kufanya uwekezaji ambao unazingatia mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaendesha Uchumi kwa njia ya kodi kwa hiyo tunapambanua ni jinsi gani tutaweza kuboresha masuala ya utawala wa kodi katika nchi za Afrika kuweza kuongeza wigo wa kodi lakini vilevile kuhakikisha kodi inayokusanywa inaenda kwenye malengo kusudiwa, alieleza Dkt. Kida.

Dkt. Kida, alisema kuwa kwenye mkutano huo wameweza kuona njia nyingi mpya zinazoibuka za kusaidia uchumi hususani mikopo nafuu kwenye uchumi wa kijani ambayo inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kufadhili mipango na miradi ya maendeleo.

Mkutano huo wa 56 unaoratibiwa na UNECA ni Jukwaa ambalo limeanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kuzisaidia nchi za Afrika kufanya mijadala na tafiti mbalimbali ili kuzalisha na kufanya ubunifu utakaokuza uchumi hivyo kutengeneza fursa ya kujadiliana na kuhakikisha ushauri unaotolewa unaendana na mazingira halisi.
1.jpg

Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi wa nchi za Afrika, wa tano kwa waliosimama kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (aliyemwakilisha Waziri wa Fedha) na wa pili kulia waliosimama ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, baada ya Rais kufungua mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi Afrika (UNECA) uliofanyika Victoria Falls, Zimbabwe.
2.jpg

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida wakielekea Ukumbi wa Elephant Victoria Falls Zimbabwe, wakati wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi (UNECA) uliojadili mikakati ya ukusanyaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, ambapo Bw. Mwandumbya alimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango.
3.jpg

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kulia), ambaye amemwakilisha Waziri wa Fedha katika Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na na Maendeleo ya Uchumi (UNECA) akiteta jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, nchini Zimbabwe.
4.jpg

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya akiteta jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro (kushoto) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi Afrika (UNECA) uliojadili mikakati ya ukusanyaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, uliofanyika nchini Zimbabwe.
5.jpg

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi (UNECA), uliofanyika Zimbabwe.
6.jpg

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kulia) akisikiliza kwa makini maelezo ya Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. Simon Sirro, wakati wa Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi (UNECA), unaofanyika Victoria Falls, Zimbabwe.
7.jpg

Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi pamoja na maafisa wengine kutoka nchi za Afrika wakiwa katika Mkutano wa 56 wa Mawaziri hao unaofanyika Victoria Falls, Zimbabwe.
 
Back
Top Bottom