VIPEPEO WEUSI
SEASON 1 – FROM ZURICH WITH RULES
EPISODE 05
Waziri mkuu Zephania Zuberi alikuwa ananitazama huku anatabasamu baada ya kuniomba nieleze kwa undani kuhusu dhamira yangu ya kufika hapa nyumbani kwake leo hii na nini hasa kilikuwa kimetokea mpaka kupata msukumo huu wa kunifanya nimfuate licha ya uadui wetu ulio wazi kabisa.
Nilielewa kuwa swali hili lilikuwa na mtego ndani yake na lingenifanya kueleza mambo ambayo katika namna ya kawaida nisingeliweza kuyaeleza. Lakini nilijua fika kwamba kama sitaeleza masuala haya kuna uwezekano mkubwa kwangu kushindwa kutimiza dhamira ambayo imenileta hapa.
“Sawa muheshimiwa… nitaeleza kila kitu ambacho kimetokea miaka miwili au mitatu iliyopita na kufanya tuwe hapa kwako elo hii.!”
Nikavuta pumzi ndefu ndani na kuishusha… nikakaa sawia pale kwenye kiti.
“Lets start from the beginning.!”
MIAKA MITATU ILIYOPITA
Nilikuwa nimewasili kwenye chumba changu cha Hotel hapa jijini Zurich kama dakika arobaini zilizopita kutokea uwanja wa ndege wa Zurich hapa nchini Uswisi. Safari hii ya masaa karibia nane na dakika hamsini kutoka Dar es Salaam mpaka hapa ilikuwa imenichosha haswa na nilikuwa nahitaji kupumzika vya kutosha kabla ya kuanza ratiba nyingine yeyote ile. Nilikuwa nimetumia dakika arobaini zote tangu nimefika nikiwa ndani ya bafu sio tu nikioga bali pia nikitafakari hatua kwa hatua vitu ninavyo takiwa kuvifanya nikiwa hapa. Kila kitu ambacho nilitakiwa kukifanya nilipaswa kukifanya kwa ukamilifu wa hali ya juu pasipo chembe ya hitilafu au kukosea.
Saa yangu mkononi ilikuwa inaniambia ilikuwa yapata saa kumi na moja jioni na nilikuwa katika dirisha langu la chumba cha hoteli maarufu niliyofikia hapa Zurichinayoitwa Radisson Blu Hotel ambayo iko mtaa wa Fracht Magharibi (freacht west) takribani kama kilomita kumi kutoka uwanja wa ndege wa Zurich. Japokuwa macho yangu pale dirishani yalikuwa yanafurahia kutazama uzuri wa muonekano wa jiji hili lenye kupendeza hasa, lakini akili yangu na fikira zangu zilikuwa mbali mno nikitafakari leo usiku nitakapo kutana na mtu ambaye nilimfahamu kwa jina moja tu la Hudini. Sikujua kama mtu huyu ni mwanamke au mwanaume, kijana au mzee. Nilichokuwa nakijua tu ni kwamba yeye ndiye mtu wa kwanza kabisa ambaye napaswa kuonana naye baada ya kufika hapa Zurich.
Nikatoka dirishani na kusogea tena mpaka kwenye meza iliyomo humu chumbani ambayo juu yake nilikuwa nimeweka bahasha ambayo miezi kadhaa iliyopita nilikabidhiwa na baba yangu Dodoma dakika chache kabla hajajiua kwa risasi mbele ya macho yangu. Ni bahasha hii ambayo siku ile aliponikabidhi alinieleza kuwa anataka nifuate maelezo ambayo yalikuwa ndani yake na nije hapa Zurich kwa ajili ya lengo ambalo alikuwa amelipanga.
Siku ile Dodoma sikudhani kama itakuja kutokea maishani mwangu siku moja nikafika hapa Zurich kutokana na kutimiza matakwa ya baba yangu kunitaka nifike hapa. Lakini binadamu wote tumeumbwa na laana kubwa kuliko zote, laana ambayyo muda mwingi huwa tunaihesabu kama Baraka au ubora wa binadamu… shauku… curiosity! Japokuwa shauku ndiyo imetufanya binadamu kuimiliki dunia na kuielewa kuliko viumbe vingine vyote, lakini pia shauku ni moja kati ya laana kubwa zaidi ambazo ziko ndani ya ubongo wetu. Unapopata wazo fulani, au kutaka kujua kitu fulani, shauku inayotengenezeka kwenye nafsi inakuwa kama vile muwasho wa upele ambao hautapoa mpaka ukiukuna.
Shauku ndiyo iliyonifanya licha ya kupita miezi takribani minne bila kuifungua bahasha hii niliyopewa na baba yangu, hatimaye nikaifungua na kusoma kilichomo ndani. Siku ambayo nilifungua bahasha ile, ndiyo siku ambayo nami laana hii ya shauku ilipanda mbegu ndani yangu ya kutaka kujua undani hasa wa suala nililoliona na kunifanya leo hii kuwa hapa Zurich.
Nakumbuka kwa ufasaha kabisa siku ile ya kufungua bahasha jinsi ilivyo kuwa. Ilikuwa imepita miezi mine tangu siku ile Dodoma porini kwenye kijumba cha mbao ambapo mzee wangu alinikabidhi bahasha. Siku hii niliyofungua bahasha ilikuwa muda wa usiku wa manane kama saa saba hivi. Siku hii nakumbuka kabla ya kulala nilikuwa nimezozana mno na Cheupe, Hasnat, mama mtarajiwa. . Mzozo wenyewe ulianza kama suala la kawaida tu… Cheupe alikuwa amenieleza kuhus ‘offer’ ya kazi ambayo alikuwa ameipta Nairobi na alikuwa anatakiwa kwenda kuripoti miezi mitatu kutoka sasa, siku hiyo ambayo alikuwa ananieleza. Nilimkatalia kata kata kwa kuzingatia uhalisia kwamba ulikuwa umebakia mwezi mmoja kabla ya kujifungua. Hii ilimaanisha kwamba ingempa miezi miwili tu ya kupimzika na kisha asafiri kwenda Nairobi kwa ajili ya kazi. Nakumbuka nilifoka haswa kuwa kama anataka kazi basi asubiri walau mtoto afikishe mwaka mmoja ndipo hapo aanze hizo harakati zake za kufanya kazi. Naye alifoka kweli kweli kwamba licha ya kumuhudumia kila kitu lakini kama msichana msomi hawezi kukaa bure nyumbani akisubiri kuzeeka, anataka atumie ‘potential’ aliyo nayo. Japokuwa nilimuelewa hoja yake hii ya kutaka kujishughulisha lakini bado nilishikilia msimamo wangu kuwa hawezi kuanza kazi mpaka mtoto atakapofikisha mwaka mmoja.
Mabishano yalipo pamba moto haswa nakumbuka Cheupe alitamka neno ambalo liliuchoma moyo wangu kuliko ambavyo alifikiria, aliniambia kukwa “Ray siku zote huwa hauelewi hisia za wengine… its always about you!” Mneno haya yalinichoma sio moyoni tu bali nilisikia maumivu yake mpaka kwenye mifupa ya mwili. Nilijikuta mwili wote umeniishia nguvu nikitafakari kauli hii… ati mimi sizingatii hisia za wengine? Ati mimi siku zote najali kuridhisha nafsi yangu tu? Mimi huyu? Mimi Ray au mtu mwingine?
Sikuamini kuwa Cheupe anaweza kutamka sentensi ya namna hii baada ya mambo yote tuliyopitia pamoja tangu utoto na leo ni watu wazima. Nikajikuta naingia katika msongo wa mawazo ya kuwaza na kuwazua kwanini Cheupe ametamka sentensi hii. Katika kuwaza kwangu huko na kuwazua ndipo ambapo ukafika muda nikaanza kuhisi labda kuna ukweli katika maneno aliyoyaongea, labda kuna ukweli kwamba najali hisia zangu tu bila kuzingatia hisia za wengine.
Katika kujilaumu kwangu huku kuhusu kotojali hisia za wengine, ndipo nikajikuta nawaza kuhusu bahasha ambayo nilipewa na baba yangu kule Dodoma. Nikajikuta Napata wazo kwamba yawezekana nilikuwa sitaki kuifungua bahasha hii kutokana na ubinafsi wangu kama ulivyosemwa na Cheupe kwamba najali hisia zangu tu. Kwa nini sijali hisia za baba yangu mzazi ambaye kauli yake ya mwisho kabla ya kufariki ilikuwa ni kuniomba niende Zurich kwa kufuata maelezo yaliyomo ndani ya bahasha?
Nakumbuka niliinuka kitandani na kumuacha Cheupe akiwa amelala fofofo usingizi wa hasira, nikaelekea kwenye chumba kidogo pembeni ya chumba chetu cha kulala ambacho nakitumia kama ofisi ya nyumbani na kufungua droo ya meza ambayo nilihifadhi ile bahasha niliyopewa na mzee wangu.
Nakumbuka ilinichukua kama dakika kumi na tano nzima nikitafakari kama niifungue ama la. Baada kusita sita sana, hatimaye nikaifungua.!!
Ndani ya ile bahasha kulikuwa na na ratasi tatu zenye maandishi ya kuchapwa. Pamoja na karatasi hizi tatu pia kulikuwa na picha mbili za mnato. Macho yangu kwanza moja kwa moja yalitua juu ya picha hizi mbili. Zilionekana kama vile ni picha ambazo zilipigwa kwa siri mno na mtu ambaye alikuwa amejificha mno kuogopa kugundulika. Juu ya picha hii kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa mkono kwa kalamu ya wino ambayo yalikuwa yanasomeka “STRIKE #1”.
Picha ilikuwa inaonekana imepigwa usiku kwenye eneo fulani ambalo kwa haraka haraka ningeweza kusema bandarini kutokana na makontena mengi yaliyokuwa yanaonekana pichani. Pia picha ilionyesha watu wanne ambao walionekana dhahiri kabisa walikuwa mahala hapo walipo kuwa kwa kificho mno kuepuka kuonekana. Kwa kutazama kwa haraka haraka nilihisi kabisa kutokana na namna walivyokuwa wamesimama watu hawa wanne… watu wawili walionekana walikuwa ni walinzi wa mmoja wapo wa watu wale wawili waliosalia.
Nikaitazama ile picha tena na tena… lakini kila ambavyo niliendelea kuitazama akili yangu ilikuwa inaniambia kuwa moja ya wale watu wawili alikuwa ni Rais Albert Kafumu. Nilikuwa najitahidi kuitazama ile picha kwa makini zaidi nikijifariji akilini mwangu kuwa labda macho yangu yalikuwa yananidanganya tu, laniki haikujalisha niliangalia picha ile mara ngapi… jibu moja tu lilikuwa linajijenga akilini tena na tena kuwa yule alikuwa ni Rais albert Kafumu, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Yule mwenzake ambaye alionekana kuongea naye, sura yake haikujificha lakini bahati mbaya kumbukumbu zangu zilikuwa zinaniambia kuwa sijawahi kumuona yule mtu, nilikuwa simfahamu.
Picha ya pili juu yake nayo ilikuwa imeandikwa kwa mkono kwa kalamu ya wino, “STRIKE #5”.
Nikajikuta napekua pekua tena ile bahasha na kuikumg’uta labda kuna picha ilikuwa imebakia ndani yake lakini hakukuwa na chochote. Nilikuwa najiuliza kwa nini picha hii nyingine iandikwe “STRIKE #5” badala ya kuandikwa ‘strike #2’?? Nikahisi labda kulikuwa na maana ambayo nitaielewa nikianza kusoma zile karatasi tatu ambazo nazo nimezikuta ndani ya bahasha.
Katika hii picha ambayo imeandikwa “STRIKE #5” nayo kama picha ya kwanza ilionekana kupigwa kwa siri kubwa na kwa kujificha ficha sana. Picha ilikuwa inawaonyesha watu wanne wakiwa wamesimama mahala fulani kwa umma, mtaani, pembezoni mwa barabara yenye msongamano wa watu wengi sana… lakini mandhari yalionyesha kabisa mta huu haukuwa Africa, ulikuwa ni mtaa mahala fulani Ulaya au Marekani.
Pich hii haikuwa na kitu chochote kile cha ajabu ambacho mtu kinaweza kukutia mashaka kama ile picha ya kwanza. Watu hawa wanne ambao wote walikuwa wamevalia suti, walikuwa wanaonekana wanaongea kwa kujiamini bila kificho hapa waliposimama kwenye msongamano wa watu wengi tena mchana wa jua kali kabisa. Baada ya kuiangalia tena picha hii kwa mara kadhaa ndipo nikagundua kuwa moja ya watu wale wanne ni yule mtu ambaye nilishindwa kumtambua katika picha ile ya kwanza na mtu ninaye amini ni Rais Albert Kafumu.
Nikaziweka zile picha pembeni na kuchukua zile karatasi tatu.
Karatasi ya kwanza ilionekana kama vile ilikuwa ni barua ambayo iliandikwa lakini haikutumwa kwenda kwa muhusika.
Barua ilikuwa na maneno machache sana. Upande wa kulia ilikuwa na anuani ya posta ambayo iliandikwa;
HUDINI
AFFOLTERNSTRASSE 44
CITYPORT
POSTFACH 8131
8050
ZURICH
SWITZERLAND.
Anuania hii ilikuwa imeandikwa upande wa kulia mwa karatasi kama ambavyo barua za kiofisi huandikwa.
Kama mistari miwili hivi chini, kati kati mwa karatasi kulikuwa kumeandikwa neno moja tu la kifaransa, “REMPLACEMENT” yaani ikimaanisha “Replacement” kwa umombo au “Mbadala” kwa Kiswahili. Kulikuwa na neno hilo tu basi bila neno linguine lolote lile baada ya hapo. Baada ya kuisoma ile karatasi tena na tena nikahisi labda huyo “Hudini” ilikuwa labda ni ofisi au kampuni fulani hivi.
Nikaiweka pembeni na kuchukua karatasi nyingine.
Karatasi hii ilikuwa na maneno machache zaidi, katikati ya karatasi kulikuwa kumeandikwa;
“DECEMBER 19
7712/LH. A+. A+.
CITIBANK. ZURICH”
Nilikodoa macho tu bila kujua ni kitu gani hasa ambacho maandishi haya mafupi yalikuwa yana maanisha.
Nikaweka pembeni pia hii karatasi na kuchukua karatasi ya mwisho ile ya tatu.
Karatasi hii yenyewe ilikuwa na orodha ya vitu vitano ambavyo sikuweza kuvielewa kwa muda huu na mpaka sasa leo hii nilikuwa bado sijavielewa. Kulikuwa kumeorodheshwa majina ya sehemu yakiwa na namba mbele yake.
1. UPANGA 3639
2. DODOMA 2488
3. MINESSOTA 126455
4. ZURICH 7712
5. MUMBAY 10033
Kwa hiyo kwa ujumla ile bahasha ambayo baba yangu alinikabidhi kabla ya kufariki, bahasha ambayo ilionekana aliitunza kwa moyo wake wote na ilikuwa na siri kubwa, hivi ndivyo vitu ambavyo vilikuwa ndani yake. Picha mbili za mnato na karatasi tatu zenye maandishi ya kuchapwa ambayo mpaka sasa hakuna hata moja ambayo niliweza kung’amua maana yake.
Nakumbuka nilikaa pale kwenye chumba changu cha ofisi ya nyumbani kuanzia muda huo wa saa saba mpaka karibia na saa tisa usiku nikitafakari ni nini hasa vitu hivi vilikuwa vinamaanisha. Nilijikuta akili yangu imejikita zaidi kwenye ile picha iliyopigwa kwa kificho sehemu yenye makontena ikimuonyesha Rais Albert Kafumu na mtu ambaye sikuweza kumtambua pamoja na wale wengine wawili ambao walionekana kama walinzi wa Rais. Roho yangu ilikuwa haitulii kabisa kila ambapo nilikuwa naiangalia hii picha. Kwa mazingira ya picha ile ilionekana dhahiri kuwa kulikuwa na suala nyeti sana ambalo lilikuwa likijadiliwa na kwa namna moja aua nyingine suala hili lilimfanya Rais ashindwe hata kuongea na mtu huyu ofisini kwake Ikulu.
Ilipotimia muda huu wa saa tisa usiku, nakumbuka nilirejesha zile picha na zile karatasi kama ambavyo vilikuwa mwanzoni kwenye bahasha na kisha nikaifunga bahasha na kuirejesha kwenye droo mezani. Nilirudi kitandani na kumkumbatia Cheupe wangu kwa kiasi fulani nikisahau hata kuhusu ugomvi wetu. Akili yangu ilikuwa imezama kwenye kutafakari kuhusu zile picha na karatasi ambazo nilizikuta kwenye bahasha. Nilijikuta akili yangu inapata kiu ya kutaka kujua ni nini haswa kilikuwa kinaongelewa kwenye zile karatasi na nini hasa kilikuwa nyuma ya pazia. Ndipo hapa ambapo nasema kuwa, shauku…. Curiosity… ni moja ya laana kubwa zaidi amabazo tumeumbwa nazo binadamu wote. Ilikuwa ni kana kwamba mbegu ilikuwa imepandwa kichwani mwangu na ilikuwa inamea. Haijalishi ni kwa kiasi gani kesho yake na wiki nzima baadae nilijitahidi kuilazimisha akili yangu iache kufikiri kuhusu nilichokiona kwenye bahasha ile, lakini kadiri nilivyojilazimisha kutokuwaza kuhusu ile bahasha na vilivyomo ndani yake ndivyo ambavyo shauku ya kutaka kujua iliongezeka maradufu.
Ndipo siku moja kama wiki moja na nusu baadae nakumbuka nilikata shauri la kufanyia kazi hiki nilichokiona kwenye ile bahasha. Nilijifungia ndani ofisini kwangu nyumbani kwa masaa kadhaa niitafakari naanzaje?
Kwa mujibu wa baba yangu siku ile Dodoma alinieleza kwamba natakiwa niende Zurich na kufuata maelezo ambayo nitayakuta ndani ya bahasha hiyo. Lakini changamoto ambayo nilikuwa nayo, nilikuwa sijaelewa chochote ambacho kilikuwa ndani ya ile bahasha aliyonipa. Kwa hiyo hata nikisema nifunge safari kuelekea Zurich nilikuwa sijui naenda kufanya nini nikifika huko. Ndipo hapa nikaamua nijaribu kitu fulani cha kijinga lakini kilikuja kuleta manufaa ya kunipa mwangu baadae kuhus suala hili.
Nilichukua ile karatasi yenye anuani ya posta na maneno “remplacement” alafu nikaidurufu. Baada ya kuidurufu, nikachukua nakala na kuiweka kwenye bahasha nyingine niliyonunua, bahasha ya kawaida kabisa ya kutumia barua. Juu ya bahasha hii niliandika anuani ambayo ilikuwa kwenye karatasi ile, yaani;
HUDINI
AFFOLTERNSTRASSE 44
CITYPORT
POSTFACH 8131
8050
ZURICH
SWITZERLAND.
Yaani kwa maneno mengine ni kwamba nilikuwa natuma barua kwenda kwa huyo mtu au kampuni au ofisi ambayo inaitwa Hudini, na atakapoipokea ndani yake atakuta nakala ya karatasi ambayo ina anauani yake ya posta na neno moja tu “REMPLACEMENT”.
Nikafunga bahasha hii vizuri na kwenda posta. Nikanuna stamp, nikabandika juu yake na kutuma barua yangu. Niliondoka pale posta huku natabasamu nikijicheka mimi mwenyewe huu ‘ujing’ ambao nilikuwa naufanya. Nilikuwa najicheka kwa sababu huyo mtu atakapoipokea hiyo barua hatojua imetoka kwa nani, kwa sabau sijaweka anuania yangu wala mawasiliano yotote yale. Nilituma ile nakala niliyo durufu kama ambavyo ilivyo.
Nakumbuka zilipita kama wiki tatu hivi hivi, siku hii ilikuwa ni kama wiki moja baada ya Cheupe kujifungua. Nilikuwa natokea mjini sokoni kununua mahitaji kadhaa ya kutengeneza chakula cha mama mzazi. nikiwa nakaribia kabisa nyumbani kwetu Forest simu yangu ya mkononi iliita. Niliendelea kuendesha gari bila kuipokea, lakini nilipotupa jicho juu ya kioo cha simu nilishituka mpaka kujikuta napaki gari pembeni. Simu ilikuwa inaita lakini hakukuwa na namba yoyote ambayo ilikuwa inaonekana juu ya kioo. Niliangalia simu kwa sekunde kadhaa na kwa haraka nikakata shauri ya kuipokea.
“do you have a pen?” sauti nzito ya kukoroma iliongea kwa lafudhi nzito ya kifaransa upande wa pili.
“hallo.!!” Nilijikuta naongea bila kujibu swali ambalo nililisikia kabisa.
“do you have a pen?” ile sauti nzito iliuliza tena vile vile.
“yes… yes.. I have it!” nilijibu haraka haraka kwa kitete.
“this is Hudini… write down… get to Zurich in twenty one days and call this number +41 44 256 56 56… call once and wait.!”
“Hudini… who are you… hallo.. hallo… hallo!” simu ilikuwa imekatwa tayari.
Nikatupa jicho kwenye kikaratasi nilichokuwa nimekiweka pajani huku naandika, sikumbuki haswa niliandika muda gani kwa jinsi ambavyo nilikuwa na hofu, lakini nilikuwa nimeandika kwa usahihi kabisa ile sentesi aliyokuwa ameiongea pamoja na namba za simu alizozitaja.
Kwa mazingira yalivyoonyesha hili lilikuwa ni jibu la barua yangu ile niliyotuma wiki tatu zilizopita. Lakini nilijiuliza huyu Hudini alipataje namba yangu ya simu au alijuaje kuwa mimi ndiye niliyetuma ile barua?
Swali hili lilinisumbua kichwani wiki nzima. Alinijuaje? Na je, nifanye nini? Nifanye uwendawazimu wa kwenda Zurich bila kujua nafauata nini aua naenda kukutana na nani?
Kama nilivyosema kuwa, shauku… curiosity… ni moja ya laana kubwa zaidi tulizoumbwa nazo binadamu. Nilijikuta nafsi yangu inakosa raha kila nilipojishawishi kuwa niache kufuatilia suala hili. Hatimaye nikajifariji moyoni kuwa “maji nimeyavulia nguo, sharti niyaoge!”.
Nikakamilisha taratibu zote za viza na hatimaye kusafiri mpaka hapa Zurich nilipo leo hii katika hoteli ya Radisson Blu Hotel mtaa wa Fracht West.
Niliangalia bahasha juu ya meza ya chumba changu cha hotel tena na tena. Niliichukia bahasha hii na kuipenda pia. Bahasha hii na vilivyomo ndani ndivyo vimenileta hapa kufanya kitu ambacho eidha kitaniingiza kwenye matatizo makubwa au kunifungulia mwanga mkubwa mbele yangu.
Nikavuta pumzi ndefu ndani na kuishusha. Huu ulikuwa ni muda sasa wa kukabiliana na ‘mashetani’ wangu. Ni muda wa kuonana na Hudini.
Nikachukua simu yangu ya mkononi na kufanmya kama ambavyo nilielekezwa wiki tatu zilizopita… “get to Zurich in twenty one days and call this number +41 44 256 56 56.. call once and wait”.
Sentensi hii ilinikaa kichwani na nilikuwa naikumbuka kwa ufasaha kama ambavyo nilikuwa nakumbuka siku yangu ya kuzaliwa.
Nikabofya zile namba na kubofya kitufe cha kupiga. Simu iliita kwa takribani dakika nzima bila kujibiwa mpaka ikakatika. Nilijua hii ndio sababu ya kuambiwa “call once and wait”. Nikaweka simu yangu juu ya kitanda na kusubiri kama ambavyo niliambiwa.
Sikujua nilikuwa nasubiri nini? Mtu aje? Simu ipigwe? Au kitugani? Nilichokifanya ni kusubiri tu kama ambavyo nilielezwa… “call once and wait!”
Itaendlea…
THE BOLD