Vipepeo weusi season 2: From Zurich with rules

Habibu B. Anga

JF-Expert Member
May 7, 2013
6,557
25,716
VPWS2.jpg


VIPEPEO WEUSI

SEASON 2 - FROM ZURICH WITH RULES

EPISODE 01

BARABARA INAYOELEKEA KWENYE MAKAZI YA WAZIRI MKUU – MLIMWA, DODOMA

“Ili kuweka kumbukumbu kwa usahihi zaidi naomba urudie tena kujitambulisha..!” yule binti mrefu mwenye suti nyeusi akaongea tena kwa mara nyinine.

“..hivi tutarudia hii kwa mara ngapi ili uridhike.!” Nikajitahidi kumuuliza kwa kujifanya kukereka haswa, lakini ukweli ni kwamba akili yangu na macho yangu vyote vilikua kwenye mlango wa gari ulio wazi kama mita tano kutoka pale tulikosimama.

Giza nene na mwanga wa taa ya kurekodia video uliokuwa unanimulika usoni ulinifanya nisiweze kuona sawia kile ambacho nilitaka kukiona ndani ya gari. Japokuwa sikuweza kuona kwa usahihi niliotamani lakini katika pua zangu niliweza kabisa kusikia harufu ya damu mbichi ya binadamu, na haikuwa damu mbichi tu bali ilionyesha kabisa ilikuwa ni damu mbichi inayoendelea kutiririka kutoka kwenye mwili wa binadamu aliye hai.

“…tutarudia mara nyingi kadiri ambavyo utaendelea kunizungusha.!” Yule dada naye akaongea kwa ukali kiasi na safari hii kunifanya nihisi hisia ya kukereka kwenye sauti yake.

Sikumjibu chochote moja kwa moja, akili yangu na macho yangu bado vilikuwa kwenye ule mlango wa gari mbele yetu. Nikaanza kuhisi labda huyu binti hajui mwenzake yuko katika hali tete kiasi gani. Lakini kwa kadiri nilivyomsoma juu ya weledi wake wa matumizi ya silaha ilinifanya niondoe hisia za kudhania kuwa labda binti huyu alikuwa hajui hali tete aliyonayo mwenzake pale kwenye gari. Silaha ambayo nilitumia kufyatua risasi aliiona na ilikuwa pale ndani ya gari, bastola aina ya glock 19 na nilikuwa na uhakika kabisa alikuwa anajua madhara ambayo bastola hii inafanya kwenye mwili wa binadamu ikifyatuliwa umbali wa karibu kaka ambavyo mimi niliifyatua.

“…mwenzako kama hatutampatia huduma ya kwanza ndani ya dakika chache zijazo tutampoteza.!” Nikaongea tena kwa mara nyingine huku bado macho yangu nimekaza kuelekea kule ambapo mlango wa gari ulikuwa umefunguliwa.

Nadhani safari hii alikuwa amegundua jinsi ambavyo nilikuwa nahangaika na kujitahidi kukaza macho kuelekea lilipo gari. Hakunisemesha chochote kile, akageza ile taa ya kurekodia video na kumulika pale mlangoni kwenye gari. Hisia zangu na harufu ya damu niliyokuwa naisikia puani kwangu sikuwa nimekosea, Yule dada wa kizungu bado alikuwa anaendelea kuvuja damu. Lakini jambo ambalo lilinishangaza ni kwamba, alikuwa amejishika maeneo ya karibu na kifua huku damu zikibubujika na pale pajani ambapo nilimlenga kulikuwa nako kunatoka damu lakini haikuwa damu nyingi kama ile niliyoiona inatoka pale juu karibu na kifua ambakoa alikuwa amejishika. Nilipofyatua risasi nilikuwa nimemlenga pajani kwa makusudi kabisa nikiwa na lengo la kumsababishia jeraha kubw lakini asipoteze uhai. Kabla ya huyu mwenzake kugeuza taa na kunimulikia pale kwenye gari niweze kuona, nilipo kuwa awali bado nahisi tu kwa kusikiliza harufu ya damu puani kwangu na nilipong’amua kwamba damu ilikuwa bado inaendelea kutiririka kwa binti huyu wa kizungu, kichwani mwangu nilikuwa nimehisi labda nilipomlenga pale pajani nilikosea na kupasua mshipa mkuu wa ateri na ndio maana nilisikia harufu ya damu mbichi inayobubujika kutoka kweny mwili, lakini kumbe hisia zangu hazikuwa sahihi, binti wa kizungu alikuwa pia anabubujikwa na damu kutoka kwenye kifua.



Lakini nilikuwa nakumbuka kwa usahihi kabisa kuwa nilifyatua risasi moja tu na nililenga pajani. Kama kumbu kumbu yangu ikomsahihi, kwa nini huyu binti wa kizungu ameshikilia mikono kifuani huku anavuja damu?

Nikainua kichwa kumuangalia tena Yule mwenzake, binti mrefu, mweusi ambaye alikuwa ananirekeodi video muda wote huu na akinikera kwa kutaka niongee kitu kile kile tena na tena akidai kwamba bado sijaeleza kwa ufasaha vile anataka. Ilikuwa ni kana kwamba muda wote huu alikuwa ananisoma kile ambacho nilikuwa nakiwaza kichwani mwangu, kwa sababu nilipogeuza shingo tu na kumuangalia nilimkuta ameganda ananikodolea macho akionyesha dalili kuwa aklikuwa ananiangalia hivyo kwa muda mrefu sana. Akageuza tena ile taa ya kurekodi video na kuwasha tena camera ya vieo ili tuendelee kurekodi .

“…je ne…peux…pas…respirer..!” (siwezi kupumua)

Sauti ya Yule binti wa kizungu ililalamika kwa taabu sana kutoka pale kwenye mlango wa gari uliofunguliwa.

“…etre fort Ilana..” (vumilia Ilana)

Huyu binti mwingine akamjibu mwenzake kwa kifarasa chenye lafudhi ya Rwanda bila kugeuka kumtazama mwenzake, bado alikuwa ananiangalia mimi kwa kunikazia macho.

Kwa hakika kabisa nikaelewa huyu binti ni mtu wa weledi na likuwa anajua anachokifanya na alikuwa tayari kuhatarisha kila kitu kama sitataka kukubaliana na kile anachonieleza. Nikapiga hesabu ya haraka haraka kichwani. Hapa tulipokuwa tumesimama ni umbali wa kama mita mia moja tu kutoka katika barabara binafsi inayoelekea kwenye makazi ya Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungani wa Tanzania na tulikuwa tumebakiza kama kilo mita mbili tu kutoka hapa tulipo mpaka kufika kwenye makazi ya Waziri Mkuu. Kama tutaendelea kuzozana hapa nilikuwa naona hatari mbili mbele yetu. Hatari ya kwanza ni huu mwanga wa taa ya kurekodia video aliouwasha huyu binti unaweza kugundulika na Wanausalama wanaomlinda Waziri Mkuu kule walipo jee sehemu ya mwinuko wanayoiita Mlimwa. Lakini pia hatari ya pili niliyokuwa naiogopa zaidi ni Yule binti wa kizungu anayevuja damu, akiendelea kuvuja damu vile kwa dakika kadhaa zijazo basi hakuna shaka kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumpoteza.

“Ok! Unatakaje?” nikamuuliza yule binti.

“nataka utambulisho ulio sahihi zaidi ndio uingie kwenye kumbukumbu.!” Akanijibu kwa hasira kwa Kiswahili kilichojaa lafudhi ya kinyrwanda.

“sawa!” nikmuitikia tu kwa kifupi.

Sijui ni muda gani alizima tena kamera, lakini nikamuona kwa mara nyingine tena anaiwasha kamera na kasha kuniangalia kuashiria kuwa yuko tayari niendelee na ninachopaswa kukifanya.

“Jina langu naitwa Rweyemamu Charles Kajuna, watu wa karibu wanapendelea kuniita Ray na marafiki zangu wanapendelea kuniita jina la utani ‘Kichwa’… hii ni recording namba 004W22 kuthibitisha kuwa ninayo mkononi mwangu password ya sanduku 7712/LH lililopo Union Bank Of India, jijini Mumbay nchini India. Narudia hii isomeke kama recording namba 004W22.!”

Nikamaliza na kumuangalia usoni yule binti huku nimeamkazia macho, “Umeridhika?” nikamuuliza nikiwa nimekereka haswa.

“Angalau inaridhisha kwa utambulisho.!” Akanijibu huku kwa mara ya kwanza nikimuona akitabasamu.

“…jene.. peux… pas… respirer..!!” (siwezi kupumua)

Sauti yenye kugugumia kwa maumivu ya yule binti wa kizungu ililalamika tena.

“..ca va! Je suis ici Ilana.!” (Usijali.! Niko nawe hapa Ilana) Yule binti mweusi mrefu akamjibu mwenzake akikiongea kifaransa kwa lafudhi ya Kinyarwanda.

Akaanza kukusanya kusanya vifaa vyake vya kurekodia, yaani kamera, taa, stendi ya kamera na vitu vingine na kisha nikamuona ameviweka kwenye mfuko wa plastiki, kisha akaweka kwenye mfuko mwingine tena wa pastiki lililoonekana kuwa gumu zaidi na kisha kuviweka vitu vyote kwenye begi la mgongoni ambalo lilikuwa kando yake. Alikuwa anafanya zoezi hili haraka haraka kana kwamba anafanya kitu hiki kila siku. Muda wote huu ambao alikuwa anakusanya vifaa vyake nilikuwa nimesimama tu pale pale ambako nilikuwa nikimuangalia yeye lakini akili yangu yote ilikuwa kwa yule binti wa kizungu anayegugumia kwa maumivu.

Baada ya kumaliza kuweka kila kitu chake kwenye begi, kwa haraka sana akageuka na moja kwa moja kwenda pale kwenye mlango wa gari uliofunguliwa. Akarusha begi ndani ya gari na kisha kumuinua mwenzake kutoka kwenye gari na kumlaza chini kwenye ardhi. Alikuwa anafanya kila kitu kwa haraka haraka sana kana kwamba mwenzake huyu ndio kwanza amemuona muda huu majerajha yake. Nikavuta picha dakika chache tu zilizopita jinsi ambavyo nilikuwa nikimsisitiza kuhusu mwenzake na alivyokuwa anajikaza kutoonyesha hisia kana kwamba alikuwa hamuoni mwenzake.

Sasa hivi ndio nilikuwa nimepata wasaa mzuri zaidi wa kuisogelea ile gari yao na kuichunguza kwa makini zaidi. Ilikuwa ni Range Rover nyeusi ambayo kwa kuiangalia kwa haraka haraka nilihisi kwamba ilikuwa ni toleo la zamani kidogo japo sikuweza kujua ni toleo la mwaka gani hasa. Nikatupa jicho kwenye namba za gari na haraka haraka nikazikariri kichwani, “T338 CNL”. Kila ambapo nilijaribu kutupa jicho ndani ya gari ili kujaribu ufahamu labda kama kuna chochote kile cha muhimu ili nikifahamu lakini kutokana na giza kubwa na taa za ndani ya gari kuzimwa sikuweza kuona chochote kile. Lakini japokuwa sikuweza kuona kitu chochote ila kutokana na mlundikano wa ile sehemu ambayo yule binti alirusha begi ndani ya gari, nilikuwa na uhakika kabisa ndani ya gari kulikwa na zaidi ya begi lile moja lililowekwa muda huu.

“..jene…peux… pas…repsirer..!”

Nikamsikia tena yule binti wa kizungu analalamika pale chini ambako amelazwa na mwenzake. Bado alikuwa analalamika kwamba hawezi kupumua. Mwenzake nikamuona ameongeza juhudi ya kujitahidi kufuta damu kifuani huku anajitahidi kuzuia damu isiendelee kutoka.

Ilibidi niiname pale chini alipolazwa yule binti wa kizungu ili niweze kuona kwa usahihi zaidi ni kiasi gani alikuwa ameumia. Kilichokuwa kinanishangaza zaidi ni kwamba nakumbuka nilimpiga risasi pajani kwa makusudi kabisa ili nisimuue, lakini sasa namshuhudia akiwa anavuja damu kifuani.

“kwa nini anatokwa na damu kifuani?” nilimuuliza yule binti wa kinyarwanda baada ya kuinama pale chini na kujiridhisha kuwa ni sahihi kabisa macho yangu yalikuwa haayanidanganyi. Alikuwa anavuja damu kifuani.

“Swali gani hilo… Idiot! Si umempiga risasi.!!” Yule binti wa kinyarwanda alifoka huku anaendelea kumfuta damu mwenzake.

“Yeah.!! Najua nimempiga risasi, lakini haikuwa kifuani… nilimpiga pajanii.!” Na mimi nikafoka.

“alidondoka kwenye kisiki cha mti kikamchoma kifuani baada ya kumpiga risasi pajani.!” Alinijibu bila kuniangalia akiendelea kufuta damu mwenzake.

Niakelewa sasa kwa nini yule binti wa kizungu alikuwa analalamika kuwa alikuwa anshindwa kupumua. Ila kilichonishangaza zaidi ni kwanini huyu binti wa kinyarwanda alikuwa hajaelewa kile ambacho mimi nimekigundua. Huyu binti alikuwa anaonekana dhahiri kabisa kwamba alikuwa na uzoefu wa mikiki mikiki ya matukio ya namna hii, lakini ajabu ni kwamba alikuwa haoni kile ambacho nilikuwa nakiona. Kichwani nikanza kupata shaka kidogo kama huyu binti ndiye yeye haswa ninaye mfikiria ndiye na anavyojitahidi kunionyesha kuwa ndiye.

“Nadhani hicho kisiki cha mti kilichomchoma kilifika mpaka kwenye pafu na naamini kuna damu imeingia pafuni ndio maana anashindwa kuhema.!’ Nikamueleza huku namsukuma taratibu kwa mkono ili asogee pembeni nijaribu kusaidia kuokoa uhai wa yule binti wa kizungu.

“Una kisanduku cha huduma ya kwanza?” Nikamuuliza huku napapasa pale kifuani kwa yule binti wa kizungu ambapo amejeruhiwa.

Yule binti wa Kinyarwanda akainuka bila kunijibu chochote na kuelekea kwenye gari. Niliendelea kupapasa pale juu ya kifua cha yule binti kwenye kidonda mpaka nikagusa nilipo pataka. Kati kati ya kidonda pale kifuani kilikuwa na kipande cha mti kimekatikia.

“hii hapa.!” Yule binti wa Kinyarwanda alikuwa amerejea na briefcase ambayo alipoifungua ilikuwa imesheheni vifaa mbali mbali vya kidaktari na madawa.

Nikapekua pekua na kuchukua bomba la sindano. Nikachana kifungashio chake cha plastiki na kisha nikaondoa ile sindano ya mbele inayotumika kuchoma kwenye nyama. Pia nikaondoa mshikio wake wa nyuma ambao unatumika kuvuta dawa kutoka kwenye chupa ya dawa na kisha kubonyezwa ili kusukuma dawa kwenda kwa mtu anayechomwa. Mshikio huu nao niliuondoa pia. Kwa hiyo lilikuwa limebaki bomba tupu liko wazi pasipo sindano yake ya mbele na pasipo mshikio wake wa nyuma.

Nilichokuwa nataka kufanya ni kuondoa ile damu ambayo nilikuwa naamini kabisa imeingia ndani ya pafu na kulijaza na ndio maana binti huyu wa kizungu alikuwa analalamika kuwa anashindwa kupumua. Mapafu yenyewe yana asili ya kuwa na “presha” innayosukuma kitu kutoka nje yake. Kwa hiyo nilikuwa nataka kutumia nadharia hiyo kuingizia bomba hili tupu la sindano ili kulipa pafu uwezo wa kusukuma damu hiyo iliyoingia kutoka nje na nilikuwa nataka kutumia bomba la sindano kwa kuwa japo nimeondoa sindano pale mbele lakini bado kuna mdomo mwembaba unaoshikilia sindano pale mbele, ambao mdomo huu ndio hasa nilikuwa nataka kuutumia kuuzamisha ndani ya pafu.

“Mshikilie mikono.!” Nikamueleza yule binti wa kiinyarwanda.

“Unataka kufanya nini?” Yule binti akaniuliza kwa mshangao mkubwa huku ametumbua macho.

“Nimekwambia mshike mikono.!” Nikamfokea.

Safari hii hakunishia tena, akamshika mwenzake mikono na kwa kuigandamiza chini kwenye ardhi kama vile tulikuwa tunataka kumchinja. Na mimi nikakaa upande wa miguu katika namna amabyo nilikuwa nimetumia miguu yangu kugandamiza chini ardhini miguu ya yule binti wa kizungu.

Japokuwa hapa tulipo kuliwa na giza totoro lakini macho yetu tayari yalikuwa yamezoea hali ile ya giza kwa hiyo kwa kiasi fulani tulikuwa tunaonana kwa ufasaha kabisa. Nilikuwa namuona yule binti wa kizungu jinsi alivyo nikodolea macho kwa uoga bila kujua ni nini nilichokuwa nataka kukifanya.

“Ilana… this is going to hurt!” nikamueleza kwa kingereza yule binti huku namuangalia machoni.

Akaniitikia kwa kutikisa kichwa akimaanisha kuwa ananiruhus kufanya kile ambacho nilikuwa nataka kufanya. Moja ya udahifu wa asili wa binadamu, tumaini lolote linaokuwa mbele yetu linakuwa ni tumaini bora kuliko kutokuwa na tumaini kabisa.

Nikapapasa tena pale kwenye kidonda chake mpaka niliposhika sawia kile kipande cha mti kilichokatikia kifuani na kwa haraka nikakichomoa na kwa kasi ya ajabu nikachomeka lile bomba la sindano pale pale nilipochomoa kipande cha mti.

“Aaaaaaaaaaaaaaaaaaa..!!!”

Yule binti wa kizungu alilia kwa nguvu kwa sauti ya maumivu ya hali ya juu. Damu ilikuwa inaruka kutoka kwenye lile bomba la sindano nililochomeka katika nmana ya kufanana kabisa na mtu anapojaza maji mdomoni na kisha kuyapuliza nje kwa nguvu. Hali hii ilidumu kwa muda wa kama sekunde ishirini hivi kisha damu ikaacha kuruka.

Mwenzake yule binti wa Kinyarwanda alikuwa ametumbua macho kwa woga huku jasho linamtoka. Alionekana dhahri kabisa hakuwa amezoea kuona damu ikimwagika hivi au kumuona mtu kwenye maumivu makali kiasi hiki. Nilijikuta nazidi kupata shaka kama binti huyu ndiye ninayemfikiria kuwa ndiye.

Yule binti wa kizungu alikuwa anahema juu juu kama alikuwa anakimbia kupandisha mlima kwa masaa kadhaa. Taratibu akaanza kurejea kwenye hali ya kawaida na hata kuhema nako akawa anahema kawaida.

“..merci beaucoup…merci … merci.!!” (Asante sana…asante… asante.!!)

Yule binti alikuwa anashukuru huku ana hema akionekana kupata haueni sasa.

Nikamsafisha kidonda chake na kisha kukifunga vizuri kwa bandeji, na pia nikafanya vivyo pale pajani ambapo nilimpiga risasi. Baada ya hapo mwenzake akambadili nguo na kisha wote tukaelekea kwenye gari.

Yule binti wa Kinyarwanda likuwa ameketi kwenye usukani, mimi nimeketi kwenye siti ya mbele ya abiria na yule mwenzake ameketi peke yake siti ya nyuma.

Tulikuwa tumeketi kwenye hali ya ukimya kwa takribani dakika tano nzima kila mmoja akitakari namna ya kuanza kwa maongezi haya baada ya mwanzo mbaya wa awali.

“Jina langu naitwa Giselle Pie….”

“Nakufahamu wewe ni nani… Giselle Jean Pierre… uko hapa kwa niaba ya LE BLOC..!!” nilimkatiza yule binti wa Kinyarwanda kabla hajamaiza senetesi yake.

“lakini huyu mwenzako ndiye mgeni machoni mwangu japo naamini yeye ndiye mwenye namba ya sanduku la Zurich.” Niliongea huku nageuka nyuma kumuangalia yule binti wa kizungu.

“..je m’appelle Ilana Dario… suis ici au nom du president de Citibank.!” (jina langu naitwa Ilana Dario niko hapa kwa niaba ya rais wa Citibank). Yule binti wa kizungu naye akajitambulisha.

“I’m sorry I shot you.!” (samahani nimekupiga risasi) nikamuomba msamaha kwa sauti ya kinafiki kabisa.

“Baise toi.!” Yule binti wa kizungu kwa hasira akanitukana tusi la nguoni, ‘f*ck you.’

Binti wa Kinyarwanda, Giselle nikamuona anatazama saa kwenye kiganja cha mkono. Japokuwa kulikuwa na giza ndani ya gari lakini kwa namna fulani alionekana kuona alichokuwa anatazama mkononi.

“tumebakiwa na dakika kumi na tano pekee… una kila kitu tunachohitaji?” Giselle aliniuliza.

“Kila kitu kiko sawa upande wangu.. sijui nyinyi.?”

Hakunijibu chochote kile. Akawasha gari na tukaanza kutoka porini kukamata barabara inayoelekea kwenye makazi ya Waziri Mkuu.

Alipoawasha gari ndipo nilipopata wasaa mzuri zaidi wa kupepesa macho mule ndani ya gari. Kwenye siti ya nyuma pembeni kwa Ilana ambako aliweka lile begi lenye vifaa vya kurekodi video kulikuwa na mabegi mengine mawili ya mkononi yakiwa yamejaa vitu fulani ambavyo sikuweza kuvitambua kwa haraka. Lakini juu ya mabegi haya mawili zilikuwa zimewekwa bastola mbili ambazo kwa kuziangalia kwa haraka niling’amua kuwa zote mbili zilikuwa ni “9mm” huku moja ikiwa ni Berette na nyingine ikiwa aina ya Heckler.

Nilikuwa nakumbuka dhahiri kabisa tangu mara ya kwanza nawaona mabinti hawa wananifuatilia hawakuwa na silaha mikononi na kwa kuzingatia kuwa walikuwa wamenifuatilia kwa zaidi ya dakika arobaini na atano au zaidi ni lazima walikuwa wanafahamu kuwa nilikuwa na silaha. Swali ambalo lilikuwa linajirudia rudia kichwani mwangu ni kwanini walicha silaha zao na kuamua kukabiliana nami bila silaha ilhali wakijua fika kuwa nilikuwa na silaha.

Kichwani nilizidi kuwa na sintofahamu nikihisi kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kitu fulani nyuma ya pazia kinaendelea tofauti kabisa na nilivyokuwa nafikiri. Maana mwanzoni tayari Giselle alikuwa amenitia shaka baada ya kushindwa kung’amua kuwa mwenzake alikuwa na damu imejaa kwenye pafu hivyo kumfanya ashindwe kuhema sawa sawa. Lakini pia uoga wake alioonyesha kipindi ambapo nilikuwa namtoa mdamu mwenzake Ilana kwa kutumia bomba la sindano. Na sintofahamu ya tatu ilikuwa ni hizi silaha mbili zilizowekwa siti ya nyuma. Kwa nini waliziacha kabla ya kukabiliana na mimi. Hisia yangu hii ya kwamba kuna jambo la zaidi linaendelea hapa tofauti na ninavyodhani ilizidi kupata nguvu zaidi kichwani mwangu.

Tulikuwa tumeendesha kama mwendo wa dakika tano nzima kuelekea kwenye makazi ya waziri mkuu ndipo ambapo tulisimamishwa na gari ya kwanza ya maaskari wanaolinda maeneo yanayozunguka makazi ya Waziri Mkuu.

Ilikuwa ni gari aina ya ‘Difenda’ iliyo wazi nyuma, ambayo ilipakia nyuma maaskari wanne huku mbele kukiwa na askari wawili.

Mara tu baada ya kutusimamisha walishuka maaskari wawili waliovalia makoti marefu ya doria, na moja kwa moja wakaja mpaka kwenye gari letu. Hawakutuuliza kitu chochote kile wala kutusalimu, walitumulika tu tochi usoni kila mmoja wetu na kisha wakaturuhusu kuendelea na safari yetu kuelekea kwenye makazi ya Waziri Mkuu. Kitendo chao kile cha kutotuhoji chochote na kuturuhusu tuende kiliashiria kwamba walikuwa wamepewa taarifa kuhusu ujio wetu na walikuwa wanatutegemea.

Tuliendesha gari kwa takribani dakika tano nyingine ndipo tulipoingia hasa kwenye mandhari ya eneo hili la Mlimwa. Eneo hili liko katika mwinuko mkubwa kiasi kwamba ukifika hapa naa kutazama nyuma yako unaweza kuuona mji wote wa Dodoma mjini kwenye upeo wa mcho. Kwa kaisi fulani lilikuwa ni eneo ambalo limejitenga mno na hakukuwa na nyumba yoyote nyingine ndani ya kipenyo cha kilomita tatu.

Tulikuwa hatimaye tumefika mbele ya geti kuu la kuingia kwenye makazi haya adhimu kabisa. Makazi haya yalikuwa yamezumgukwa na ukuta mkubwa wa urefu wa kama mita tano hivi ukiwa na senyenge za umeme juu yake pamoja na taa kubwa juu ya ukuta kila mahali. Pia upande wan nje wa ukuta nako kulikuwa na maaskari kila baada ya hatua kadhaa ambao walikuwa wanafanya doria.

Ajabu ni kwamba hata askari hawa wa doria nao hakuna yeyote kati yao ambaye alijishughulisha nasi. Nao dhahri kwamba walikuwa na taarifa juu ya ujio wetu.

Baada ya kufika tu getini, geti likafunguliwa na gari yetu kuingia. Ndani ya geti upande wa kushoto kuna kijichumba kikubwa cha ulinzi ambacho kwa haraka niliona maafisa usalama watatu ndani yake ambao wote walikuwa wamevalia sare za kijeshi lakini zenyewe vikiwa na rangi fulani kama kijivu.

“Passcode?” Afisa mmoja ambaye alikuwa nje ya kile kijichumba aliuliza huku anatazama ndani ya gari yetu.

“December 19”Nikamjibu kwa kifupi.

Akatuonyesha kwa mkono muelekeo ambao tulikuwa tunapaswa kuufuata kwa ajili ya kupaki gari yetu.

Ndani ya makazi haya ya Wziri Mkuu, ukiingia tu getini upande wa kulia kuna jengo la ghororofa moja ambalo ni ofisi rasmi ya Waziri Mkuu na Idara zake za usaidizi wa majukumu yake. Alafu katikati kuna eneo kubwa la wazi lenye bustani murua kabisa. Upande wa kulia ndiko ambako kuna makazi ya waziri Mkuu ambayo anaishi yeye na familia yake.

Sehemu ambayo tulionyeshwa kupaki gari ilikuwa ni mahali fulani nyuma ya kijichumba kile cha ulinzi.

Mpaka muda huu nilikuwa sikujua ni kwanini lakini hisia zangu zilikuwa zinaniambia kuwa hali ya ulinzi ndani ya makazi haya ilikuwa ni ulinzi mwepesi tofauti na nilivyokuwa natarajia. Nilibaki kujiuliza maswali kichwani kama hali hii iko hivi kila siku au ni leo tu, na jibu lilikuwa linanijia kichwani kwamba ni leo tu hali hii iko hivi. Kila jibu hili liliponijia kichwani kwamba ni leo tu hali hii iko hivi, nilijikuta napata swali lingine la kwanini ulinzi uwekwe mwepesi siku ya leo.

Tofauti na desturi ya sehemu za makazi za viongozi wakuu wote ambazo nimewahi kufika, hapa kwa Waziri Mkuu hatukusachiwa sisi wala gari yetu kupekuliwa kabla ya kuingia na hata baada ya kuingia. Nilijua pia kuwa huu ni “upendeleo” fulani tu kwa ajili yetu sisi. Kwa mtu mwingine angeweza kuhisi labda hii ni heshima kubwa tulikuwa tunapewa lakini binafsi nilihisi kuna swala ambalo linaendelea nyuma ya pazia.

Tulishuka kwenye gari na afisa mmoja wa usalama alikuja kutuongoza kuelekea kwenye jengo ambalo Waziri Mkuu anaishi na familia yake. Tulifunguliwa mlango mkubwa wa mbele uliotengenezwa kwa mbao adimu na nakshi za kimanga, mlango ulifungukia ndani ambako moja kwa moja tulikutana na sebule kubwa sana yenye viti vya masofa ya gharama ya hali ya juu. Hakika yalikuwa na mnadhari hasa ya kuishi Waziri Mkuu wa nchi. Hapa sebuleni nako nilishangaa hakukuwa na hata mtu mmoja wa usalama kama ambavyo nafahamu inapaswa kuwa. Kichwani ile hisia yangu kwamba kuna kitu hakiko sawa ilizidi kukua.

Yule afisa usalama aliyetusindikiza kutuleta hapa sebuleni kutoka kwenye gari alikuwa ameshaondoka na hapa kwa sasa tulikuwa tunakarimiwa na Bibie Sarah Shomari, msaidizi maalumu wa Waziri Mkuu ambaye tulimkuta ameketi kwenye sofa na aliinuka mara tu alipotuona tunaingia. Huu ni mwaka wa pili tangu nimfahamu Sarah lakini leo hii uso wake nilikuwa nauona wenye uchangamfu kuliko siku yoyote ile. Mara zote ambazo nimewahi kukutana naye uso wake huwa unamuonekano wa kikazi. Sio mtu wa utani wa reja reja au maongezi madogo, unapokutana na Sarah Shomari unakuwa umekutana na mtu mwenyekuzingatia weledi wa kazi yake na kila sentensi ambayo itatoka kinywani mwake ni kuhusu kazi na jambo husika lililo mezani. Lakini siku ya leo Sarah alikuwa anatabasamu kana kwamba ni muhudumu wa mapokezi ya hoteli na sisi tulikuwa ni wateja wake.



“Welcome guys… Sarah Shomari, Personal Assistant to te Prime Minister.!” Sarah alijitambulisha kirafiki kabisa huku anampa mkono Giselle akitumia neno la reja reja “guys” kuonyesha ukarimu wake.

“Giselle Jean Pierre… LE BLOC.” Giselle alijitambulisha huku naye akimpa mkono Sarah.

“Ilana Doria… Citibank” Ilana naye akajitambulisha huku anampa mkono kwa taabu Sarah kutokana na maumivu ya kidonda chake pale kifuani.

“Ilana?? Are you ok?” Sarah akamuuliza kirafiki Ilana baada ya kumuona ananyoosha mkono kwa taabu sana.

“She had a small ‘accident’ few minutes ago.!” Giselle alidakika kueleza hali ya Ilana huku akitumia vidole kuonyesha hewani alama za kufungua na kufungua usemi, “…….” Alipotaja neon ‘accident’.

“oooohh so sorry Ilana.!” Sarah akongea akionyesha kuelewa maana ya Giselee kutumia zile alama za funga na fungua usemi hewani.

Kabla sijajitambulisha, Sarah alinigeuka na kuniangalia huku anatabasamu, “and ofcourse Ray, The Kichwa.!” Aliongea kirafiki huku anatabasamu na kunipa mkono.

“hello Sarah.!” Nikampa mkono.

Kwa namana ambavyo tulisalimiana mtu asiyetufahamu angeliweza kuhisi labda mimi na Sarah ni marafiki tulioshibana na labda hata siku nzima leo tulishinda wote kutokana na ureja reja wa namna ambavyo tulisalimiana. Lakini kwa mimi ambaye nilikuwa namfahamu Sarah vizuri nilikuwa bado najiuliza kichwani lengo la maigizo yote haya ya Sarah ilikuwa ni nini.

Giselle alikuwa ametukata jicho fulani hivi mimi na Sarah tulipokuwa tunasalimiana. Tungekuwa katika mazingira mengine, siku nyingine toauti na hii siku ya leo ningeweza kuhisi lilikuwa ni jicho la wivu. Tulipokutanisha macho, Giselle aligeukia pembeni kuna kitu fulani ambacho sikukisikia akamueleza mwenzake Ilana.

Japokuwa hii ilikuwa ni mara yangu ya nne kumuona Ilana, lakini hii ndio ilikuwa kama mara ya kwanza kumuona kutokana na mazingira yote ya awali nilipokuwa namuona kila mmoja wetu alikuwa anajitahidi kujifanya kuonyesha hamuoni mwenzake.

Kwa hiyo leo ndio nilikuwa nimepata fursa nzuri zaidi ya kumtazama tena na kuzingatia mwanga angavu wa hii sebule ya kifahari tofauti na kule gizani ambako tulikuwa dakika chache zilizopita. Alikuwa ni binti mrembo haswa mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde na uso mwembamba wa kitusi. Mrefu wa wastani na mwenye umbile zuri la saizi ya kati ambalo si kubwa sana na wala halikuwa dogo. Suruali yake ya suti na shati lake alilovalia vilimkaa sawa sawa na kuongeza uzuri zaidi ambao alikuwa nao.

Kuna kitu ambacho tulipokuwa gizani nilishindwa kuking’amua kutokana na giza lakini hapa kwenye mwanga wa kutosha nikiwa naendelea kumuangalia moja kwa moja macho yangu yalitua mikononi mwa Giselle. Hakuwa na pete ya ndoa tofauti na ambavyo inapaswa kuwa. Wasi wasi wangu juu ya Giselle ulizi kuongezeka. Kwanza kushindwa kutambua tatizo lililosababisha mwenzake kushindwa kupumua, kisha kuogopa damu na sasa hana pete ya ndoa.

Nilijikaza kiume ili yeyote kati yetu tuliopo pale asiweze kuhisi kilichokuwa kinaendelea kichwani mwangu.



“The Prime Minister is going to be with you guys in a few minutes.!” Sarah aliongea kwa tabasamu huku anaondoka pale sebuleni.



Moyo ulianza kunienda mbio kila ambavyo dakika zilivyokuwa zinakaribia kabla ya Waziri Mkuu kuja kuonana nasi. Sikuwa namuhofia Waziri Mkuu bali nilikuwa napatwa na wasi wasi kwamba kuna kitu hapa hakiko sawa na mbaya zaidi sikujua ni kitu gani. Si tu kwamba moyo ulikuwa unanienda mbio bali pia ulikuwa unauma, unauma kwa uchungu wa kila nilipofikiria kwamba kuna kitu hakiko sawa. Nikikumbuka kwa namna ambavyo kwa miaka miwili iliyopita nimepigana kufa na kupona, nimeishi maisha ambayo ni kama nillipita jehanum, yote hii ili kufanikisha kikao hiki, kikao cha siku hii ya leo, kikao kati yangu, Citibank na LE BLOC. Hii ni siku ambayo nahitaji kila kitu kiende sawa, ni siku ambayo hakutakiwi kuwa hata na chembe ya kukosea, ni siku ambayo itaamua sio hatma yangu tu, bali pia familia yangu kwa maana ya mke wangu Cheupe, mwanangu na mama yangu mzazi.



Tukasikia ule mlango wa mbele unafunguliwa na na msafara wa watu ukaingia. Ulikuwa ni msafara wa Waziri Mkuu na walinzi wake karibia nane. Jambo ambalo mra moja lilinishitua ni kitendo cha Waziri Mkuu kuongozanana na walinzi wengi hivi. Wakati tunaingia hapa kichwani mwangu nilikuwa na uhakika kuwa Waziri Mkuu alikuwa kwenye lile jengo lingine la ofisi akimalizia shughuli zake. Na sio tu kwamba nilihisi, bali siku nzima ya leo nilikuwa nafuatilia mwenendo wa kila mahala ambapo Waziri mkuu alikuwepo na saa moja iliyopita nilikuwa nimehakikisha bila shaka yoyote kuwa Waziri Mkuu alikuwa ndani ya haya makazi yake.



Lakini kitendo cha kuongozana na walinzi wengi hivi hii ilimaanisha kuwa alikuwa nje na haya makazi na muda huu ndio alikuwa narejea. Na hii ilikuwa inafafanua kwanini wakati tulipoingia mara moja niling’amua kuwa mahala hapa ulinzi ulikuwa ni mwepesi tofauti na ambavyo niilitarajia iwe. Sasa nilielewa kumbe sababu ilikuwa ni kutokuwepo kwa Waziri Mkuu muda huo tunawasili. Akili ilizidi kuvurugika, hii inawezekana vipi? Muda mchache uliopita kama saa moja tu iliyopita nilikuwa nimehaikisha kwa asilimia mia moja kwamba Waziri Mkuu alikuwa ndani ya Makazi yake hapa Mlimwa.



Nikatupa jicho ukutani kwenye saa, ilikuwa ni saa tano na dakika kumi usiku. Ghafla moyo ulinipasuka na nikaanza kuhisi kijasho kwa mbali kinaanza kunitioka, nilianza kuelewa kwa mbali ni nini kilikuwa kinaendelea nyuma ya paza hapa. Nikaelewa kwa nini muda ule porini kabla hatujaondoka Giselle alitazama muda kwenye saa ya mkononi.



“Habari yako kichwa.!” Waziri Mkuu Zephania Zuberi, ambaye mpaka siku tatu tu zilizopita alikuwa labda ndiye adui yangu namba moja juu ya uso wa dunia alinisalimia kwa bashasha huku anaketi kwenye sofa mbele yetu.





WIKI MOJA ILIYOPITA – DODOMA HOTEL




Imepita miaka mitatu, miezi minne, wiki mbili, siku sita, masaa kumi na nne na dakika ishirini na tano tangu siku ambayo nilimshuhudia baba yangu mzazi akielekeza bunduki kichwani mwake na kujipiga risasi mbele ya macho yangu. Siku hii sio tu kwamba ilikuwa ya ajabu kutokana na kitu ambacho baba yangu alikifanya mbele yangu, bali pia ilikuwa siku ya ajabu Kutokana na kuwa ndio siku yangu ya kwanza na siku ya mwisho kuwahi kumuona baba yangu mzazi. Sikuwahi kumpenda baba yangu wala kumchukia lakini kwa namna moja au nyingine tukio lile lilinifanya nikose ujasiri wa kuweza kukanyaga tena mji wa Dodoma kwa mika mitatu iliyopita mpaka siku hii ya leo.

Kuna msemo ambao wanasema kwamba huwezi kamwe kuikimbia hatma yako, na hiki ndicho ambacho nilikuwa nahisi kilikuwa kimenitokea mpaka leo hii kujikuta niko tena kwenye mji ule ule ambao nilijiapiza kwamba sitakuja kukanyaga tena mguu wangu kwa maisha yangu yote yaliyobaki.



Muda huu nilikuw nimekaa mahala fulani ndani ya hotel sehemu yenye mgahawa pembeni ya bwawa la kuogelea nakunywa kinywaji changu huku naangalia ile picha kwenye simu ambayo Issack alikuwa amenitumia ikiwa na maelezo yake.



Wale mabinti wawili, mmoja wa Kiswahili japo nilihisi kabisa kwa muonekano wake lazima atakuwa Mnyarwanda na mwenzake wa kizungu walikuwa wanaendelea kufurahi pale kwenye bwawa la kuogelea huku wanajipiga ‘selfie’ kwa simu zao. Hii ilikuwa ni mara ya tatu naonana na mabinti hawa kwa ‘bahati mbaya’ na kila nikonana nao walikuwa wako na furaha hii hii huku wanapiga ‘selfie’. Lakini kutokana na maisha niliyopitia kwa miaka mitatu iliyopita nilikuwa na uwezo mzuri sana wa kung’amua kusudi la mtu hata kama alikuwa anajitahidi sana kulificha. Hii ilinifanya nijue kwa mara zote mbili mabinti hawa nilizokutana nao wakipiga ‘selfie’ uhalisia ni kwamba walikuwa wananipiga mimi picha. Hii ndio sababu ya kunifanya na mimi nitumie ‘uhuni’ wangu niliojifunza miaka yote hii mitatu kumpiga picha kwa siri yule binti wa Kinyarwanda na kumtumia Issack ili aone kama anaweza kufanya utundu wake wa TEHAMA na kujua yule binti ni nani.



Muda huu ndio alikuwa amenitumia picha kadhaa za binti huyu ikiwa na maelezo machache tu ya msingi.

“Giselle Jean Pierre

27 years old

Rwandan

LE BLOC Agent”


Maelezo haya machache yalinitosha kufahamu ni nini kilikuwa kinaendelea. Na niling’amua wazi kwamba kama huyu binti wa Kinyarwanda ni wakala wa LE BLOC basi lazima huyu binti wa kizungu atakuwa ni mtu wa Citibank.

Kilichokuwa kinanichanganya ilikuwa ni kwanini walikuwa wananifuatilia kwa siri na walikuwa hawajitambulishi kwangu ?



Nikapiga tena funda lingine la kinywaji changu na kisha kupiga simu kwenda kwa swahiba wangu Eric Kaburu ambaye mara ya mwisho tuliongea asubuhi ya siku ya leo.



“Kichwa… habari yako?” Kaburu alinisalimia baada ya kupokea simu.



“Nataka uandae kile kikao na Waziri Mkuu” nikaongea moja kwa moja hoja yangu bila kujibu salamu yake.



Ukapita kama ukimya wa dakika moja nzima bila yeyote kuzungumza.



“Ray.! Are you sure about this?”



“I don’t know! Ila andaa kikao, kiwe wiki ijayo.!”



“Citibank na LE BLOC wameshafika?”



“Still not sure about that too!”



“Una maana gani?”



“Inawezekana wameshafika na niko nao hapa na inawezekana bado hawajafika”



“Ray hivi hauwezagi kuongea vitu kwa lugha nyepesi bila mafumbo?” kaburu akafoka kwa kukereka.



“Eric! Andaa kikao.!”



“Ok boss.!” Akanijbu kwa kifupi.



Nikakata simu.



Nilijua fika kwanini Kaburu alikuwa anahofia kikao hikli nilichokipigania kwa zaidi ya miaka miwili sasa kati yangu, Waziri Mkuu, LE BLOC na Citibank.

Alikuwa hawahofii Citibank au LE BLOC bali alikuwa anamuhofia Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye mpaka sasa alikuwa ndiye adui yangu namba moja chini ya uso wa jua.



Labda ni ville tu sababu watu wengine akiwemo Kaburu pia, hajaishi maisha mabayo nimeyaishi kwa miaka mitatu iliypita. Safari hiyo ya maisha yangu mapya ambayo ilianza baada ya kwenda Zurich kwenye bank ambayo nilielekezwa na nayaraka nilizokabidhiwa na marehemu babab yangu. Safari ambayo ilinifanya nione upande wa pili wa siri wa maisha ya watawala na mifumo yake. Safari ambayo ilinifanya niielewe dunia katika namna ambayo wengi walikuwa hawaifahamu.



Ni katika safari yangu hii ya Zurich na kutokana na mambo na vitu nilivyo viona na kukutana navyo huko ndio ilinifanya nijiapie na kujiwekea kanuni TATU za kuongoza maisha yangu tangu siku hiyo. Three Rules.

Na kanuni ya kwanza, Rule number one; nilijiapia siku hiyo, tofauti na wengi wananvyo amini na kuaminishwa ila mimi niliamini kwamba… katika maisha hakuna rafiki wa kudumu, hakuna adui wa kudumu, na wala hakuna maslahi ya kudumu. There is only survival.



Na hii ndio sababu iliyokuwa inanifanya intake kikao na adui yangu Waziri Mkuu wa Jamuhuri, Zephania Zuberi.



Nikapiga fundo la mwisho la kinywaji changu, na kisha nikainuka kuelekea juu ghorofani pale hotelini kilipo chumba changu nilichofikia.




EPISODE 2 POST # 65

EPIOSDE 3 POST # 82



THE BOLD
 
Nifah Divine... glory to yhwh BansenBurner Alisen Papushikashi Magazine Fire miss chagga SANCTUS ANACLETUS mngony Excel Mussolin5 Jimena Inferiority Complex gwijimimi wambura marwa Hoshea shareef conscious wambeke The Boss Deejay nasmile gkileo Juma chief Mangi flani hivi Ngongo makaveli10 KENZY kadada wa pili Root aretasludovick jonnie_vincy Clkey KAFA.cOm mbewe makedonia Afande Nyati peterchoka Leonard Robert Nchi Kavu STUNTER Chrizo jully Van persie Khalidoun Tetramelyz punje haradari Mazigazi @Alybaba babu na mjukuu platozoom jimmyfoxxgongo Nicodemas Tambo Mwikozi Ls man Heaven Sent sifongo Infantry Soldier haa mym 20acres MTS MarkHilary compos Tembo2 Erick the future nancy1983 Bulah binsaad Fazzaly the wolf everhurt Melvine Mgibeon kijana wa leo samsun Coolant Jagood pacesetter apologize payton George Betram kisengeli Kiranga Jiwe Linaloishi Madame B jay john Guasa Amboni Dinazarde Analyse Diva Beyonce snowhite Mmanu Expected Value onechromosome Missy rose Innocenthezron Immortal_MH Ficus sunola Robot la Matope mamaafacebook II JEKI likikima Compact scorpio me G'taxi YNWA adna yuzo ntamaholo Otorong'ong'o naan ngik-kundie kandukamo1 AFRICA101 mwalidebe Kobe Blaki Womani kalendi savius The Great Emanuel r2ga Ntaluke.N. Transcend Msemachochote Mchumiajuone mwampepec MTOTO WA KUKU Fukara proto cute kawombe zinginary MLALUKO JR Vupu barafu BlackPanther Ntuzu Matola impongo ntamaholo Mkoroshokigoli Deadbody KING easy mahoza Msolo kkenzki deborah1 KIDUDU buffalo44 winlicious riziki Allys MUHUNZI Moses2015 nacktary Liuumi dochivele Renzo @barbers hmjamii mbere TATIANA famicho LUCKDUBE mwanadome Straton memphis ghazar Graph Theory Honey Faith Shunie Slave ddcmanesto zinginary pacesetter Nkanaga KOMUGISHA mikatabafeki johnsonmgaya lee empire wigo MJINI CHAI Asprin mtzmweusi Erasto kalinga Chrizo kichakaa man LULU bike FORTALEZA poleni shibumi ZE DONE umande Edger Sr sir joshua sammoo Roram Password Bavaria hambiliki mwanangu Asili100 Evarist Massawe nice1 Jumong S Rogie 1babake nasreen uberito baest dustless Kilemachocho Tumosa mtembea kwa miguu Debbs Joe scorpnose musacha shibumi seeker of knowledge Simuchi Veni Vidi Vici TUJITEGEMEE abuu garcia Hon Nkundwe Festo Festo marion09 mike2k The dream bro kay vandelintz kirikou1 POINT LOAD lusaka city Dirham Rodcones bato MANCNOO multiphill90 GEORGE Dalali mwanamalundi90 MwaFreeca Roram Ta-kibombo troublemaker mambo KOMUGISHA calabocatz Papaa Azonto Msemachochote Mdomo bakuli tizo1 option dikembe iL Buono fakalava ABDUL KAREEM @Gobe Justine Marack Goodluck Mchika MR UNINFORMED darcity nkasoukumu nG'aMBu thatonegAl kabanga MPARE KIBOGOYO Edward Sambai Rassa mnonje srinavas last king of uscoch proto cute Kennedy krava Rais2020 kbosho Mzee wa BsN sam2000 fuma 999 Bableee dawa yenu The Certified DON SINYORI mij adden
bwii ONTARIO Kobe The Vein Mondray jaxonjaxon successor mzee wa liver sawariya Sitaki ukuda Domhome Mpatanishi MKANDAHARI mtugani wa wapi huyo wealthier cluecell Toyota escudo mgumu2 troublemaker Linamo shedede kamtu33 SteveMollel ngushi Donald stewart Mshuza2 Glycel mnonje Ochuanilove SingleFather Santi DEOD 360 ngushi anatory antony ukhuty chris van chicha auxillius Goma Son Hubeb pes KING DUBU VILLAIN mwayena donbeny Aleppo JipuKubwa shoo61 BOMBAY John mungo Nyakageni bato Dogo 1 sufra chamlungu painscott wegman Bravo Engliash MOSELBAY wa stendi FaizaFoxy bigmind cadabraa Internal Kelvin mwalukas mnonje Kelvin X Somoche Wgr30 Miiku Poise Jabman kalamuyamwalimu BOMBAY the say juxhb witnessj Gide MK Mmanyema mgogoone Mnongane Mandingo koncho77 afsa ngaboru Paradoxer Heavy Metal KIMBURU 06 Raaj kichekoh ngumba njeche kikale DullahTza Goodluck Mshana julius Darcy Denis Kasekenya mashonga kitalembwa Khaleed Shaban middle east SirChief jiwe jeusi Mkambarani mansakankanmusa gambada ynwa ney kush
 
Oyoooooooo ule msimu wa kupiga msuli umerudi tena maana vipepeo weusi ni zaidi ya somo hahahaaa.

Ni kama vile EPL imerudi,ni raaaaaaha.
Naipendaje simulizi ya vipepeo weusi sasa?
Chondechonde naomba Cheupe niendelee kukimbiza humu,nimemiss kujisoma hihiiiiiii.

Umekuja kuwashika tena as always bae,bring it on....
#MyHubbyBaeIsAGenius#
 
Oyoooooooo ule msimu wa kupiga msuli umerudi tena maana vipepeo weusi ni zaidi ya somo hahahaaa.

Ni kama vile EPL imerudi,ni raaaaaaha.
Naipendaje simulizi ya vipepeo weusi sasa?
Chondechonde naomba Cheupe niendelee kukimbiza humu,nimemiss kujisoma hihiiiiiii.

Umekuja kuwashika tena as always bae,bring it on....
#MyHubbyBaeIsAGenius#
Hahahah.!! Karibu mama...

And thank you for the support and comfort unanipa mpaka natoa madini hivi...

Unajua vile nakupenda soulmate!
 
Oyoooooooo ule msimu wa kupiga msuli umerudi tena maana vipepeo weusi ni zaidi ya somo hahahaaa.

Ni kama vile EPL imerudi,ni raaaaaaha.
Naipendaje simulizi ya vipepeo weusi sasa?
Chondechonde naomba Cheupe niendelee kukimbiza humu,nimemiss kujisoma hihiiiiiii.

Umekuja kuwashika tena as always bae,bring it on....
#MyHubbyBaeIsAGenius#
Ramadhan kareem bibie kwema huko?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom