VIPEPEO WEUSI
SEASON 2 – FROM ZURICH WITH RULES
EPISODE 06
Nilikaa kwenye kiti na kuiangalia simu pale juu ya kitanda kwa muda wa karibia dakika kumi nzima. Kichwani nilikuwa najaribu kujiuliza kama nijaribu kupiga tena au niendelee kusubiri. Hakuna kitu ambacho kinatesa akili kuzidi mshawasha wa kusubiria simu muhimu ipigwe. Kila dakika iliyokuwa inapita nilikuwa naona kama mwaka mzima kwa jinsi ambavyo muda nilikuwa nauona unaenda taratibu sana.
Nilisubiri kama dakika tano nyingine ndipo nikaona simu yangu inaita pale kitandani. Kama ambavyo ilikuwa siku ya kwanza, ndivyo hivyo pia ilikuwa siku hii ya nleo, simu iliita lakini hakukuwa na namba yoyote ambayo ilikuwa inaonekana juu ya kioo cha simu.
“hallooo.!!” Nilipokea simu haraka haraka.
“do you have a pen?” sauti nzito ya kukoroma kama ile kama ya siku ya kwanza iliongea kwa lafundhi nzito ya kifaransa.
“aaah.. wait a second! Let me get it..!” nilitembea haraka haraka mpaka kwenye moja ya mabegi yangi na kuingiza mkono kwenye mfuko wa pembeni na kupapasa papasa mpaka nikapata kalamu, “I have it now!”
“write down! Get out of your hotel… walk down the street for five minutes.. you will see a Chinese restaurant… the code is ‘Fox Wings’.!”
“code name for wha….hallo…halloo..hallo..!” simu ilikatwa kama siku ya kwanza ilivyokuwa.
Nikaikodolea simu macho kana kwamba nilikuwa namuangalia huyo aliyekuwa naongea nami. Uzuri nilikuwa na mkono mwepesi wa kuandika kwa hiyo kila ambacho alikuwa amenieleza nilikuwa nimekiandika kwenye kipande cha karatasi.
Sikutaka kupoteza muda zaidi, nikachukua sweta na kulitupia mwilini na kisha kushuka mpaka chini ya hotel na kutoka nje kabisa. Hali ya hewa nje ilikuwa ya ubaridi wa wastani na msongamano wa watu barabarani ulikuwa umepungua kadiri usiku ulivyokuwa unakaribia.
Nikiwa pale nje ya hotel nikajiuliza haswa ni upande gani ambao nilikuwa natakiwa kuelekea. Ile sauti kwenye simu ilinieleza tu “walk down the street”. Nikatafakari kama kwa muda wa kama sekunde ishirini hivi na hatimaye nikakata shauri kuwa niteremke kuelekea upande wa kushoto wa mtaa. Nilitembea mwendo wa dakika tano nzima kama ambavyo nilieklekezwa kwenye simu na hatimaye nikaona mgahawa wenye maandishi ya kichina upande wa pili wa barabara.
Nilivuka barabara na kuingia ndani ya mgahawa na kuketi kama mteja mwingine yeyote wa kawaida. Ndani ya mgahawa. Wahudumu wote walikuwa ni watu wenye asili ya china na hata asilimia kubwa ya wateja niliowakuta walikuwa ni wakichina vile vile pamoja na wazungu wachache sana. Nilikuwa ni mteja pekee mwenye ngozi nyeusi humu ndani.
Haukuwa mgahawa wa fahari sana au wa hadhi ya juu sana kama migahawa mingine ambayo nimeiona hapa Zurich. Ulikuwa ni mgahawa wa viwango vya kawaida tu japokuwa muonekano wake ulikuwa ni wa kuridhisha.
“welcome Sir.!” Kijana muhudumu alinikaribisha huku anatabasamu baada ya kuketi. “what can I get you sir?”
“just water please!” nilimjibu huku naangaza macho huku na huko kuangalia labda kuna dalili yoyote naweza kuiona kunisaidia hasa suala lililonileta hapa.
Muhudumu aliitikia tu kwa kutingisha kichwa na kuanza kuondoka. Alipogeuza kisogo tu na kuanza kuondoka nilipata wazo.
“excuse me.!” Nilimuita yule muhudumu.
“yes sir.!” Aliniitikia na kurudi pale nilpoketi.
“can I get some ‘fox wings’ please.!” Niliongea kwa kujiamini huku namuangalia usoni.
Wazo lilinijia haraka tu kichwani kwamba labda muda huu ndio nilipaswa kutumia ile ‘code name’ niliyopewa na mtu niliyeongea naye kwenye simu kama dakika kumi zilizopita.
Muhudumu mwanzoni alitabasamu na kuniangalia kama vile nimeongea neno la utani na alikuwa anasubri nisahihishe nilichokuwa nakisema. Lakini sikutabasamu, niliendelea tu kumkazia macho. Aliponiona niko ‘serious’ na naendelea kumtazama usoni bila kucheka wala kutabasamu, nikamuona uso wake unaanza kubadilika na kuwa na kiasi fulani hivi cha woga. Alinitumbulia macho kana kwamba alikuwa ameona jini.
“right away sir.!” Alinijibu kwa unyenyekevu mkubwa uliopitiliza mpaka nikashindwa kuzuia mshangao wangu.
Aliondoka huku anageuka nyuma mara kwa mara kuniangalia pale ambapo nimeketi. Akapinda kona kwenye mlango karibu na kaunta ya mgahawa na kuelekea nyuma ambako nilihisi ndiko jikoni.
Muda ukapita kama dakika tano hivi nikawaona watu watatu wameibuka kutoka kule alikoenda na wamekuja sehemu hii ya wateja.
“we are closed! Everyone get out please.!” Mzee mmoja wa makamo wa kichina aliongea kuwaambia wateja.
Watu wote waliacha kula na kumuangalia huyu mzee kwa mshangao. Alionekana kwamba alikuwa ni mmoja wa wapishi huko jikoni kutokana na ‘aproni’ na kofia ya upishi aliyokuwa amevaa. Wenzake wawili alioongozana nao walikuwa ni vijana wa kichina waliovalia suti nadhifu na kwa namna fulani walionekana kama vile ni walinzi wake.
Nilisikia wateja kadhaa wakining’unika kuwa hawajamaliza kula wengine wakionekana kuwa walikuwa hawajamaliza mazungumzo yao na manung’uniko mengine ya kila namna.
“I said everyone get out NOW.!!”
Yule mzee aliongea kwa sauti fulani ya ukali na ya kimamlaka zaidi kuonyesha kuwa alikuwa hatanii alichokuwa anakiongea na alikuwa anataka haswa kila mtu aliyepo hapa atoke nje sasa hivi. Nahisi wateja wote walisoma uzito wa sauti aliotumia na mara moja nikaona kila mtu anainuka haraka haraka na kuanza kuondoka.
Kwa namna fulani ambayo sikujua ni kwa nini nilijikuta akili yangu inanishawishi kuwa watu nisitoke nje. Kwa hiyo nikasubiri tu.
Wateja wote walikuwa wametoka nje ya mgahawa na kuondoka. Ajabu ni kwamba hata dada wa kichina ambaye nilimuona pale kwenye kaunta wakati naingia naye alikuwa ameondoka. Na sisi yeye tu, hata wahudumu wengine wote walikuwa wameondoka. Kwa hiyo pale tulibakia mimi, huyu mzee wa kichina na vijana wawili waliovalia suti ambao aliongozana nao.
“what are you waiting for young man?” yule mzee aliniuliza huku amenikazia macho akipiga hatua za taratibu kunifuata pale ambapo nilikuwa nimeketi.
Mapigo ya moyo yalikuwa yanaenda mbio kweli kweli na presha ilikuwa imepanda juu haswa lakini nilijitahidi kwa kila namna nisionyeshe hofu niliyokuwa naipata ndani yangu kwa muda huu.
“I’m waiting for my ‘fox wings’.!” Nilimjibu kwa sauti thabiti kabisa pasipo kuonyesha chembe ya hofu kwenye sauti yangu.
Yule mzee akatabasamu na kuja kukaa kwenye kiti cha upande wa pili kwenye ile meza ambayo nilikuwa nimeketi. Alipoketi alinitazama kwa takribani dakika nzima akiwa anatabasamu tu bila kuongea neno lolote lile.
“I have been waiting for this moment my whole life… its nice to finally meet you Rweyemamu.!” Mzee aliongea kwa tabasamu la furaha huku ananipa mkono.
“Do I know you? Who are you?” nikauliza kwa mshangao baada ya kusikia huyu mzee wa kichina ambaye ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kumuona maishani lakini alikuwa analijua jina langu kwa ufasaha kabisa.
“aah don’t worry about me…. (anaongea kichina huku anamuangalia moja ya wale vijana aliokuja nao)..”
Katika maneno yale ya kichina ambayo aliongea sikuweza kung’amua chochote kile lakini nilifanikiwa kusikia maneno ‘fox wings’ yakitajwa.
Kijana mmoja kati ya wale wawili aliondoka kutoka pale ambapo tulikuwa na kwenda kule kwenye chumba cha jikoni ambako walitokea. Nikajikuta macho yangu yameganda kwenye zile suti nyeusi ambazo wale vijana walikuwa wamevaa. Kila nilipowaangalia, nilijikuta kichwani mwangu nakumbuka suti za jumuiya ya The Board namna ambavyo walipendelea wote kuvaa suti nyeusi kama hizi.
Yule mzee alikuwa ananiangalia kwa makini sana kila kitu ambacho nilikuwa nakiangalia. Nadhani alifahamu ni nini hasa kilikuwa kinaendelea kichwani mwangu nikiwa nawatazama wale vijana. Nilpogeuza macho na kumtazama alitabasamu tu pasipo kusema neno lolote lile.
Yule kijana aliyeondoka kwenda kwenye chumba cha jikoni alirejea akiwa na briefcase mkononi na akaliweka juu ya meza mbele ya mzee huyu wa kichina.
“These are your fox wings.!” Yule mzee aliongea huku anatabasamu.
Sikujibu chochote kile nikaendelea tu kumtazama.
Akafungua ile briefcase taratibu na kisha kuanza kutoa vitu kadhaa kutoka ndani yake. Macho yangu hayakuganda kwenye vile vitu ambavyo alikuwa anavitoa bali yaliganda kwenye upande mmoja wa ndani wa ile briefcase. Ulikuwa na rangi ya zambarau ya kukoza sana na kati kati yake kulikuwa kumechorwa kichwa cha samba kwa rangi ya dhahabu. Pembezoni mwa mchoro huu wa kichwa cha simba kulikuwa na nakshi za kufanana kabisa kama na kito cha sapphire zikiwa zimezunguka mchoro huu wa kichwa cha samba.
Mchoro huu ulinikumbusha kabisa zile pini za walizokuwa wanavaa wanachama wa The Board juu ya suti zao kwenye ukosi kukaribia usawa wa titi. Tofauti pekee ilikuwa ni zile nakshi za vito vya sapphire kuzunguka mchoro wa kichwa cha samba.
Yule mzee hakuonekana kujali mshangao wangu aliendelea tu kutoa vifaa kadhaa kutoka kwenye lile briefcase na kuviweka juu ya meza. Alitoa mabomba mawili ya sindano, chupa ndogo ambayo nilihisi ilikuwa na ‘spirit’, pamba, mpira wa kufunga mkono, na kichupa kingine kidogo chenye kimiminika ambacho sikukijua mara moja.
Alipomaliza kutoa ila kitu alichokihitaji alinitazama kwa mara ya kwanza uso ukiwa ‘serious’.
“Give me your left hand!” mzee aliongea huku anachukua mpira wa kufunga mkono kama ile itumiwayo na hospitalini wakati wa kutafuta mshipa wa damu.
Nikiangalia vile vifaa alivyoviweka pale mezani na kauli yake kwamba nimpe mkono wa kushoto, nilielewa fika kuwa alikuwa anataka kunichukua damu na lile bomba la sindano.
Kitendo hiki kilinikumbusha siku ile ya kwanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita nilipoenda gorofa la PPF HOUSE na kutolewa damu. Ilikuwa ni kana kwamba kitu hiki kilikuwa kinataka kujirudia tena. Tofauti tu kwa sasa nilikuwa nimeisambaratisha jumuiya yote ya The Board na nilikuwa Zurich sio posta Dar es salaam.
“what are you doing?” nilimuuliza yule mzee kwa sauti ya mshangao na mshituko.
“I need to verify you!” yule mzee alinijibu kwa kifupi tu.
“verify me about what?” niliuliza tena kwa mshangao mkubwa zaidi.
“Ray, if you are not ready for this you can go back home.! Its your choice...no one is forcing you to do anything.!” Mzee aliongea kwa upole mno na ustaarabu.
Kauli hii nayo ilinikumbusha siku ile pale PPF HOUSE nilipokuwa nasita sita kumpa mkono yule mama anitoe damu niliambiwa hivi hivi kuwa kama bado siko tayari naweza kwenda tu.
Kama ambavyo siku ile ‘nilijilipua’ na kumpa mkono yule mama ndivyo hivyo navyo nilifanya leo hii. Bila kufikiria mara mbili mbili nilinyoosha mkono na kumpa yule mzee.
Alinifunga mpira katikati ya mkono, kisha akapaka spirit sehemu fulani mkononi mbapo mishipa ilionekana vizuri kisha akaingiza sindano na kutoa damu ya kutosha kabisa kujaza bomba lote.
Akaichukua ile sindano na kuirudisha ndani ya briefcase.
Tofauti na siku ile PPF HOUSE ambayo nilitolewa damu tu lakini mzee huyu nilimuona anachukua bomba lingine la sindano na kunyonya kimiminika mabcho kilikuwa kwenye chupa ile ndogo. Nilielewa kabisa kwamba hiki kinachotokea leo ni tofauti kabisa na kile ambacho kilitokea siku ile pale PPF HOUSE na sikudhania tena kama kuna uhsuika wowote wa The Board ukizingatia kwamba jumuiya hii nilikuwa nimeisambaratisha tayari.
Akachukua tena mkono wangu na kunichoma sindano yenye ile kimiminika nisichokijua. Kuna upande fulani wa nafsi yangu ulikuwaunaniambia kuwa nilikuwa nafanya jambo la kipuuzi kuruhusu yote haya yafanyike, lakini kila nilipo fikiria nilivyosafiri umbali wote huu ili kufika wakati huu, nilijikuta natamka tu ‘liwalo na liwe’, maji nimeyavulia nguo sharti niyaoge.
Baada ya kunichoma sindano hii, nilimuona anakusanya kusanya vitu vyote pale mezani na kuvirudisha tena kwenye briefcase na kumpa yule kijana akaondoka nalo.
Mwili niliusikia unaishiwa nguvu kabisa na kama kizungu zungu kikali kilikuwa kinanijia kwa kasi ya ajabu.
“what is happening?” niliuliza kwa suati ya ulevi kama vile nimelewa pombe.
Yule mzee hakusema chochote kile. Alitabasamu. Lakini tabasamu lake lilikuwa la kifedhuli safari hii. Kwa namna nilivyoliona halikuwa tabasamu la kheri.
“sweet dreams Ray.!!” Mzee aliongea taratibu huku bado akiwa na lile tabasamu la kifedhuli usoni mwake.
Aliinuka na kuondoka pale tulipo akiwa na yule kijana aliyesalia. Nilibaki peke yangu pale mgahawani. Nilijaribu kuinua miguu lakini ilikuwa kama vile imekufa ganzi. Nilishindwa kuinua hata kidole cha mkono. Ilikuwa kana kwamba ghafla mwili wote umepooza.
Nikaanza kuona kiza mbele yangu. Macho yakawa kama vile yanapoteza nuru. Usingizi mkali wa ajabu ukaanza kuujaza ubongo wangu. Jasho lilikuwa linanitoka nikijua kuwa kuna jambo baya sana liko mbele yangu. Nilishindwa tena kuendelea kufumbua macho, taratibu yakajifunga. Na mara moja nilipoteza fahamu.
Itaendelea….
Usisahau kutembelea tovuti yangu jamiiforums.com
THE BOLD - 0718 096 811 (Namba kwa ajili ya wale ambao wanataka kujiunga na group langu la WhatsApp (kuna ada)... Usipige tafadhali