VIPEPEO WEUSI
SEASON 1 – FROM ZURICH WITH RULES
EPISODE 11
Kiza kinene. Hicho ndicho kitu pekee ambacho nilikuwa nakikumbuka. Kiza kinene. Kiza kinene na baridi kali hasa maeneo ya tumboni pamoja na woga wa aina ambao ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuusikia ndani ya nafsi yangu. Maumivu ambayo nilikuwa nayasikia sikuwa nayaogopa kama ambavyo nilikuwa naogopa kila nikitazama damu mkononi mwangu. Sikuwahi kujua hapo kabla ni namna gani mtu anajisikia au anaona pale ambapo anakaribia kifo. Sikiwahi kujua namna ambavyo macho yanaanza kupoteza nuru na kitu pekee ambacho unakiona mbele yako ni kiza. Sikuwahi kujua ni namna gani mwili wako unaweza kuwa na siha njema lakini ukashindwa kuinua hata kidole na kukisogeza.
Nikarejesha tena mkono tumboni kuzuia damu zisiendelee kutoka. Nikalaza tena kichwa changu sakafuni na kutazama juu angani.
“Huu hauwezi kuwa mwisho wangu.!!”
Nilitamka tena kauli ile ile ambayo nilikuwa nairudia tena na tena tangu nimedondoka. Nikainua tena mkono kutoka tumboni na kuutazama namna ambavyo ulikuwa umeloa damu. Macho yalikuwa yameanza kulegea tena kuashiria kuwa naweza kupoteza tena fahamu au labda ndio ikawa safari yangu ya mwisho nisiyafumbue tena.
Sikuwahi kudhania kabla ni namna gani mtu anajisikia akikaribia kifo. Kwa miaka yangu yote duniani kila nikifikiria kifo kitu pekee ambacho kilikuwa kikinijia akilini ni maumivu. Maumivu makali. Lakini ukweli ni kwamba ukikikaribia kifo hakuna maumivu yoyote ambayo unayasikia. Uhalisia ni kwamba nilikuwa sisikii hisia yoyoye ndani yangu zaidi ya woga. Ndio, woga sio maumivu. Woga wa kufumba macho kwa mara ya mwisho nisiweze kuyafumbua tena. Woga wa kulala usingizi ambao sitaweza kuamka tena. Woga wa kutohisi chochote tena, woga wa kutosikia chochote tena. Licha ya risasi ambayo ilikuwa tumboni mwangu lakini sikusikia maumivu yoyote kadiri mwili wangu ulivyoishiwa nguvu, kadiri macho yangu yalivyozidi kupoteza nuru, hakuna cuembe ya maumivu ambayo nilikuwa naisikia. Kitu pekee ambacho nilikuwa nakihisi kwenye nafsi kilikuwa ni woga.
Niliangalia mkono wangu namna ulivyojaa damu kisha nikaurejesha tena tumboni.
Nikajikuta natabasamu. Japokuwa nilikuwa natabasamu lakini kona za macho yangu machozi yalikuwa yanatiririka. Kwa kuwa nilikuwa nimejilaza chali sakafuni, niliyasikia machozi yakitiririka na kuingia masikioni.
Nilikuwa naogopa kufumba macho kwa mara ya mwisho, lakini nilichokuwa nakiogopa zaidi ilikuwa ni kuondoa kwa namna hii, mahali hapa ambapo naweza kuoza kama mzoga kwa wiki kadhaa bila mtu yeyote kujua.
Nikajikuta naanza kutathimini na kujitathimini mimi mwenyewe na chaguzi zote nilizozifanya katika maisha yangu. Nikajikuta natamani kama ningepata nafasi nyingine nirekebishe baadhi ya mambo au labda nipate fursa ya kuyafanya tofauti.
Nikakumbuka namna ambavyo wiki yangu ya mwisho nilivyokuwa nyumbani Tanzania kabla ya kusafiri kuja Zurich namna ambavyo tuligombana na mkewangu Cheupe. Nikakumbuka hasira ambayo nilikuwa nayo kutokana na kumuona kama vile anaondoka kutoka mikononi mwangu kwa kung’ang’ana kwenda Nairobi kufanya kazi.
Japokuwa uamuzi wangu wa kuja Zurich ulikuwa ni kutokana na kiu ambayo ilikuwa ndani yangu kutamani kujua na kung’amua fumbo ambalo baba yangu alikuwa amenipa kutokana na ile bahasha ambayo aliniachia, lakini pia safari yangu hii ya Zurich pia ilichangiwa na kutamani kupata walau wiki chache kuwa mbali na Cheupe. Uhusiano wetu, ndoa yetu haiko sawa kabisa. Nilijua bila shaka kabisa kwamba ndoa yangu na Cheupe inapitia katika kipindi kigumu na labda Cheupe inawezekana kuna mambo amebadilika tofauti kabisa na Cheupe ambaye nilimpenda kutoka utotoni, tofauti kabisa na Cheupe tuliyepambana kuidondosha jumuiya ya The Bold, lakini kitu kimoja ambacho kamwe hakikubadilika ni kiwango changu cha kumpenda.
Hakuna jambo linaloumiza moyo kama kushuhudia ukiwa unampoteza mtu unayempenda kutoka mikononi mwako. Akilini mwangu wiki kadhaa zilizopita nilijiapiza kuwa ni vyema niende Zurich kukonga kiu ya kung’amua fumbo nililoachiwa na marehemu baba yangu kuliko kuendelea kukaa nyumbani nikishuhidia mapenzi yangu na Cheupe yakizama siku baada ya siku.
Lakini muda huu ambao nilikuwa sina hakika kama nitaweza kufikisha hata masaa matatu mbele, hakuna kitu ambacho nilikuwa nakitamani kama kumuona Cheupe akiwa pembeni yangu. Hakuna ambacho nilikuwa natamani muda huu kama nitafumba macho kwa mara yangu ya mwisho basi niyafumbe nikiwa mikononi mwa Cheupe, nipate fursa tena kumueleza jambo moja tu. Moja tu… kwamba nampenda kuliko kitu chochote kile.
Nilitabasamu tena na kuinua mkono kutoka tumboni na kuungalia jinsi ulivyofunikwa na damu. Nikatabasamu. Kila ambavyo nilitabasamu ndivyo ambavyo mchozi nao ulitiririka kutoka kwenye kona za macho na kudondokea masikioni. Ilikuwa kana kwamba najifariji na hiki kitendo cha kuutoa mkono tumboni na kuungalia mara kwa mara labda kungeweza kusaidia kufanya damu tumboni isiendelee kutoka. Lakini kila ambapo niliinua mkono kutoka tumboni na kuungalia ndivyo woga ndani yangu ulizidi maradufu. Woga wa kufumba macho kwa mara ya mwisho na nisipate nafasi ya kuyafumbua tena.
Nikaanza kufikiria siku mbili zilizopita. Siku ambayo nilipelekwa mtaa wa Wipkingen hapa hapa Zurich. Siku ambayo nilizibwa sura kwa tambara jeusi la kitambaa ili nisione. Siku ambayo nilipitishwa kwenye korido yenye kunuka harufu ya damu mbichi na kisha kuingizwa kwenye chumba cha kufanana na hoteli ya hadhi, chumba ambacho nilikutana na mzee ambaye nilikuwa namfahamu kama Hudini kutokana na sauti yake. Mzee ambaye tulianza maongezi kwa kunikabidhi picha mbili zenye utata. Moja ikionyeaha watu wanne mmoja nikimtambua kama Rais wa Tanzania Albert Kafumu na walinzi wake wawili wakiwa na mwanaume mmoja wa kizungu wa umri wa makamo kwenye eneo la kufanana na bandari. Picha ya pili ambayo ilinishangaza sana ilimuonyesha mtu huyo miaka mingi iliyopita akiwa kwenye picha ya pamoja na Cheupe akiwa mtoto na baba yake.
Katika maongezi yetu Hudini alionekana hakuwa anajua zaidi yangu kuhusu fumbo ambalo baba yangu alikuwa anataka niling’amue au labda alikuwa anafanya kusudi kutoniambia… kitu pekee ambacho alinieleza ni kwamba ananikabidhi maagizo kama ambavyo alielekezwa na hana la zaidi ambalo atanieleza. Alinikabidhi tu bahasha yenye nyaraka nyingi ndani yake na kisha kunieleza kuwa atanitafuta baada ya wiki mbili kunikabidhi bahasha nyingine. Nilipomuuliza natakiwa kufanya nini ndani ya wiki mbili hizobili, alinijibu huku anatabasamu kifedhuli… “I don’t know… I am just following my orders!” Na nilipomuuliza hizo “orders” zinatoka kwa nani alinijibu, “its none of your business.!”
Kwa mtindo ule ule wa walionichukua kutoka mtaa wa Hardstrasse, ndivyo ambavyo walinirudisha… lakini hawakunirudisha pale mtaa wa Hardstrasse bali walinirudisha hotelini nilipofikia karibu na uwanja wa ndege wa Zurich.
Kutokana na purukushani hizi za kunichukua na kunipeleka kule mtaa wa Wipkingen kutokea usiku wa manane, waliponirudisha hotelini tayari kulikuwa kunapambazuka. Ilikuwa ni asubuhi alafajiri. Kabla ya kuifungua ile bahasha niliyopewa na Hudini kwamba ilinipasa kulala ili kuweka akili yangu sawa. Nilikuwa najihisi kama nina karibia siku tatu sijapata usingizi. Na hakika ilikuwa ni zaidi ya siku tatu. Kuanzia safari yangu ya zaidi ya masaa kumi na sita kutoka Tanzania mpaka hapa Uswisi. Jumlisha usiku nilioenda kwenye mgahawa wa kichina na kufanyiwa mambo niliyopoteza fahamu na baadae kuamka kwenye jengo ambalo silifahamu mtaani Hardstrasse. Na baadae kupelekwa Wipkingen kuonana na Hudini. Kichwa kilikuwa kizito na kilikuwa kinauma haswa nilihitaji kupumzika kwa masaa kadhaa.
Nakumbuka nililala kwa siku nzima. Kuna muda nilihisi nilikuwa nalala tu sitamani kuamka kwa kuwa sikuwa nataka kukabiliana na uhalisia uliokuwa unanisubiri pindi nikiamka. Lakini hakuna marefu yasiyo na ncha na siwezi kulala milele. Hatimaye jioni yake niliamka na kufungua ile bahasha ambayo nilipewa na Hudini. Nilipoifungua na kusoma zile nyaraka zilizomo ndani nilielewa kwanini roho yangu ilikuwa nzito na kulala siku nzima bila kutamani kuamka. Nilielewa roho rangu ilikuwa inaogopa kukutana na uhalisia wa aina gani. Uamuzi ambao nilichukua baada ya kusoma zile nyaraka ndizo ambazo zimenifanya kuingia kwenye dhahama kubwa kwenye nchi hii ya ugenini niliyopo.
Lakini hayo yote yalikuwa ni siku mbili zilizopita. Leo hii nilikuwa nakabiliana na uhalisia mkubwa zaidi. Uhalisia wa kama nitathubutu kufumba macho basi kuna uwezekano mkubwa sitayafumbua tena. Uhalisia wa kiza kinene mbele yangu. Uhalisia wa kifo.
Nikatabasamu tena. Machozi yalitiririka tena kwenye kona za macho. Nikainua tena mkono kutoka tumboni na kuangalia namna ulivyoloa damu. Nikaurudisha tena tumboni kujishika damu isitoke kwa kasi zaidi. Macho yalikuwa yanazidi kulegea na nuru kupotea. Maumivu yote yalikuwa yamepotea. Sio kwamba hayakuwepo lakini mwili wangu ulikuwa unakufa ganzi na nilikuwa siyasikii kabisa. Uhalisia ni kwamba nilikuwa hata sihisi mwili wangu mwenyewe. Kitu pekee ambacho nilikihisi, kitu pekee ambacho kilikuwa ni halisi kwa sasa ni woga. Woga wa uhalisia kwamba nikifumba macho tu sasa hivi hakika sitafumbua tena.
Nikaanza kufikiria hatua kwa hatua mpaka mahali hapa nilipo muda huu. Sikuwa hotelini, na nina zaidi ya masaa ishirini na nne sijui kitanda cha hoteli yangu. Kwa uzuri zaidi niseme sijakiona kitanda cha hoteli yangu tangu juzi niliporejeshwa hotelini alfajiri na vijana wa Hudini na kisha kulala siku nzima mpaka jioni. Nipo koridoni mwa jengo ambalo visanga na vitimbi vyote vilikoanzia, jengo la HARDSTARASSE 201, 1985. Jengo ambalo siku kadhaa zilizopita nilijikita nimeamka ndani yake. Jengo ambalo nilisikiliza kipande cha video cha ujumbe ambao uliachwa na marehemu baba yangu. Jengo ambalo nilikuta nyaraka kwenye vault ndogo zikionyesha kwamba ninalimiliki. Hapa ndipo nilipo muda huu. Kwenye korido nje ya mlango wa kuingia kwenye kile chumba ambacho siku kadhaa niliamka ndani yake.
Nilikuwa nimelala hapa koridoni nikihesabu sekunde zilizobakia za uhai wangu. Nilikuwa nimelala nikiwa na jeraha la risasi tumboni linalovuja damu.
Japokuwa mwili ulikuwa umeishiwa nguvu na hata akili yangu kushindwa kufikiria sawa sawa nikiona maluweluwe tu, lakini nilijitahidi kuwaza. Kuwaza ni nini hasa kilikuwa nyuma ya pazia. Kuwaza nimewezaje kutegeka kirahisi hivi?
Niliwaza kweli kweli, ni nani hasa alikuwa nyuma ya pazia ya hiki kilichofanyika? Hudini? Lakini akili yangu ilikataa… Hudini alikuwa na uwezo wa kuniua Kyle Wipkingen kama angekuwa na nia hiyo. Lakini kila nilipotaka kumsafisha kichwani mwangu Hudini, akili ilikataa…. Hudini ndiye pekee anayejua uwepo wangu hapa Zurich. Au labda kuna mwingine? Ndio… nilijijibu mwenyewe… yule mzee wa kichina na vijana wake? Inawezekana wao ndio walikuwa nyuma ya pazia? Hapana… akili yangu ilikataa… nao walikuwa na uwezo wa kuniua siku ile ambayo walinipotezesha fahamu kwa kunichoma sindano ya kemikali.! Au kuna mwingine anayefahamu uwepo wangu hapa Zurich bila mimi kujua?
Ghafla nikasikia mlango wa komeo wa kule nje wa kutoka kwenye uchochoro, nikasikia unafunguliwa kwa staili ile ile niliyoisikia mara ya kwanza kabla ya kupigwa risasi. Macho yangu yaliyokuwa yanasinzia kwa kuchoka kutokana na mwili kuishiwa nguvu, niliyatoa kama vile nimekabwa. Woga ambao niliusikia ulikwa halisi mpaka niliweza kuuhisi kwenye ngozi yangu ya mwili. Kifo kilikuwa halisi mbele yangu kuliko hata nilivyohisi mwili wangu.
“Huu hauwezi kuwa mwisho wangu.!”
Nikajifariji japo nilikuwa siwezi hata kuinuka kupiga hatua moja.
Itaendelea…
THE BOLD