SEHEMU YA 21
Machozi hayakutaka kusubiri, hapohapo yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake, akaanza kusikia maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, alihisi kwamba alikuwa ndotoni akiota kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Hiyo ilimaanisha kwamba Cassian hakutaka kuwa naye, ilimaanisha kwamba hakukuwa na ndoa tena, yaani alichwa siku ya harusi. Lilimuumiza moyoni, alitamba sana kwamba alikuwa akienda kuolewa, mitandaoni, gumzo lilikuwa ndoa hiyo, kila kona ilizungumziwa harusi hiyo.
Akarudi ndani ya gari, kabla ya kuondoka akalalia usukani, mbele yake akayaona maisha yake yakiwa yamejaa giza, hakujua sababu iliyomfanya Cassian kuchukua uamuzi ule na wakati mpaka mara ya mwisho mwanaume huyo alipokuwa akiagana naye alionyesha sura ya tabasamu, penzi zito lilionekana kupitia macho yake, sasa iweje abadilike ghafla hivyo?
Akaanza kuifikiria mitandao ya kijamii, alitumia kiasi kikubwa cha pesa kutamba huko, kama kila mtu alikuwa akijua kwamba alikaribia kufunga ndoa na mwanaume huyo siku hiyo ilimaanisha kwamba hata hapo alipoachwa kwenye mataa basi kila mmoja angejua kwamba ameachwa solemba.
Alilia sana, hakutaka kumpigia simu Mwajuma na kumwambia, alichokifanya ni kuwasha gari na kumfuata huko. Mawazo juu ya Cassian yalikuwa makubwa mno, hakuamini kama kweli mwanaume huyo alimuacha katika kipindi kigumu kama hicho.
Aliendesha gari huku akiwa na mawazo hayo ya kuachwa yakimsumbua kichwani mwake. Kila alipokuwa akipita na kupishana na watu, aliona kama wote hao tayari walijua kama aliachika.
Alipofika Sinza Makaburini, akakata kulia ambapo aliendesha mpaka katika nyumba moja iliyokuwa na wanawake wengi kwa nje, akasimamisha gari na kuwafuata wanawake hao, akawasalimia na kuingia ndani.
Alikijua chumba alichokuwa akikaa Mwajuma, moja kwa moja akaelekea mpaka katika chumba hicho na kugonga, mlango ukafunguliwa na msichana huyo ambapo baada ya kumuona tu, akaanza kulia.