Sehemu ya 111
“Kweli tena. Nilipokuona kwa mara ya kwanza, moyo wangu ulibabaika, nilishindwa kukuangalia mara mbili. U mzuri sana, unapokasirika, uzuri wako haupotei, unapokuwa kimya, bado u mzuri mno, unapokasirika, uzuri wako unazidi kuonekana maradufu.
Patricia, hivi ulizaliwa muda gani?” aliuliza Walker baada ya maneno mengi yalimfanya msichana huyo kutabasamu kila wakati.
“Hahah! Unanichekesha!”
“Sidhani kama ulizaliwa hospitalini! Nahisi ulizaliwa supamaketi, tena karibu kabisa na friji lililokuwa na chokolate.
U mrembo sana, sina mtu wa kukufananisha nawe,” aliendelea kusema Walker huku akichukua maneno mengi kutoka katika Kitabu cha Romeo And Juliet kilichoandikwa na mwandishi wa Kiingereza, William Shakespear.
“Walker! Hujakutana na wazuri!”
“Nimekutana nao, ila moyo wangu umekukubali zaidi wewe! Unajua kutabasamu, unajua kuringa, unajua kupetika, kwa kifupi wewe ni malkia wa nyuki, acha kidume niwe mtafuta maua.”
“Hahah! Nashukuru sana!”
“Hebu rudia tena! Nataka niisikie sauti hiyo tena!” alisema Walker huku akitoa kicheko cha mbali kabisa.
“Kwani sauti yangu ipoje?”
“Hebu rudi kwanza. Kidogo tu!”
“Niambie kwanza ikoje!”
“Jamaniiiii! Rudi basi mpenzi! Rudia basiiiii...”
“Nashukuru!”
“Patricia, nimekwambia una sauti nzuri sana, kwa sauti yako ina uwezo wa kulifungua daraja la London, kwa sauti yako ina uwezo wa kuufanya mnara wa Eifel jijini Paris ukapinda na hata kuanguka,” alisema Walker.
“Hahah! Utanifanya nisikie aibu!”
“Hakuna bwana! Unajua nashindwa kuvumilia, nashindwa kuongea lolote lile. Nahitaji nikuchore, picha moja matata sana,” alisema Walker.
“Kweli?”
“Haswaa! Nitakuchora. Haiwezekana nikutane na msichana mrembo kama wewe halafu niache kumchora. Patricia, ninakupenda mno!” alisema Walker huku simu ikiendelea kuwa sikioni mwake, Waltr alishindwa kuzungumza lolote lile kwani kwa jinsi ndugu yake alivyokuwa akiendeshwa kwa nguvu kubwa ya mapenzi, hata kwake ilikuwa hivyohivyo.
Walizungumza mengi, Patricia akajisikia raha moyoni mwake, alipenda kupendwa, alijihisi kuwa msichana aliyekuwa na bahati kubwa mno maishani mwake.