Kiranga hapa hauko sahihi; utaona kuwa wale ambao tunawaandama CCM ufisadi hatuwaandami kwa ufisadi wa chumbani mwao au wa ndoa zao. Tunawaandama kwa ufisadi wanaofanya katika ofisi zao za umma na wenye kuhusu walipa kodi wa Tanzania. Wale ambao wanataka kuandama kwa ufisadi wa chumbani wana haki yao ya kufanya hivyo. Wengine hayo mambo ya nani amelala na nani, vipi, na wapi hayainuki kufikia wizi wa mabilioni ya fedha za Watanzania na kwa hakika hayafikii hata katika njozi kiwango cha wizi wa EPA, Meremeta au Dowans.
Kumbe, sisi wengine tunatofautisha tu kuwa mambo haya ya chumbani ni mambo ambayo yanatakiwa kujadiliwa katika ngazi ya familia na pale ambapo yanapoinuka na kuwa katika kiwango cha uhalifu basi tutayajadili katika kiwango hicho. Hivyo, Dr. Slaa kwa mfano angetajwa kuwa amechukua underage girl na kuwa na mahusiano naye ya kimapenzi basi hapo tungeona SOSPA ikiingia kufanya kazi na tungezungumzia hayo mengine. Lakini uamuzi wa mtu mzima ambaye anajua kuwa ameolewa na akaamua kutoka kwa mume wake na kuwakimbiza watoto wake toka baba yao ninaamini huyo mtu ana akili timamu.
Siyo mimi wala wewe wenye haki ya kumtaka abakie hapo. Lakini la pili ambalo ni more personal ni kuwa kama mtu huyo anataka furaha ya kitendo cha mapenzi ambayo ni haki yake kama binadamu siyo mimi wala wewe ambao tuna haki ya kulazimisha kuwa aende kwa mumewe ambaye hapatani naye ili apate furaha hiyo. Kwamba, ameamua kupata furaha hiyo nje ya ndoa yumkini halitamaniki na kuonekana vizuri; lakini kwamba amefanya hivyo akifuata dhamira yake baada ya kupima uwezekano wote uliokuwepo, ni suala la nafsi na dhamira yake na lapaswa kuheshimiwa.
Lakini kulivusha hilo kiasi cha kusema kuwa kwa hilo mtu hafai kuwa kiongozi wa umma ni kuweka chumvi isiyo ya lazima kwani hakuna ushahidi wowote wa kisayansi wenye kuonesha kuwa kuna uhusiano kati ya uaminifu katika ndoa na uaminifu katika utumishi wa umma. Niko tayari kusahihishwa.