SoC02 Uwajibikaji sio ushamba ni heshima

Stories of Change - 2022 Competition

Ras Zimba

New Member
Jul 26, 2022
4
3
(ANDIKO) KUWAJIBIKA SIO USHAMBA, NI HESHIMA.

Kutokana na mfumo wetu wa siasa tumeaminishwa lazima mwanasiasa awe msemaji na kiongozi wako, marehemu Mtikila aliona mbali hasa katika kupambania kuwa na mgombea/kiongozi binafsi asiyefungamana na chama cha siasa.

Leo tupo katika nchi ambayo maisha ya kila mtanzania wa chini yamekuwa magumu, leo tupo Tanzania ambayo mwananchi akiamka na elfu 1 na kugundua sabuni imeisha na sukari imeisha pia ana kuwa na chaguo moja ikiwa vyote ni muhimu kwahiyo anachagua kati ya kuoga nyumbani au kunywa chai (kumbuka kipande cha sabuni ya kawaida ni 700) biashara nyingi zimekufa za mama/dada zetu!

Mfumuko wa bei wa bidhaa umedidimiza mapambano ya wengi. Kwanini? Mfano mdogo; Sukari, mafuta, ngano, gesi/mkaa vyote vimepanda na soko bado linakutaka uuze andazi 200/100 ukipandisha na kuuza 300/400 unapoteza soko, dawa ni kuacha tuu kuliko kupata hasara huku tukiendelea kuishi kwa matumani kwa kujifariji na kauli "Mungu yupo, ipo siku tuu" ndivyo hali ilivyo sasa huku chini.

Tupo Tanzania ambayo huoni takwimu zikiwekwa hadharani ni kwa namna gani mfumuko wa bei umeturudisha nyuma, ukosefu wa umeme wa uhakika umedidimiza taifa katika uzalishaji kwa kiwango gani, sio kwamba taasisi za kufanya tafiti hazipo ila zinaweza kufanya tafiti nyeti kwa uhuru? hilo baki na jibu lako ila hayo yote tunasubiri kusemewa na viongozi ambao hawana uwajibikaji. Natamani kuona Tanzania yenye viongozi wakiwajibika vile inatakiwa.

Viongozi ambao hawa wajibiki ni sumu katika maendeleo ya taifa, leo tulitegemea kuwaona mawaziri kadhaa wakiachia ngazi kwa kushindwa kuthibiti mfumuko wa bei, kushindwa kuthibiti mgao wa umeme n.k..

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi UWAJIBIKAJI ni ile hali ya kiongozi kujitambua yeye ni nani katika jamii, anatakiwa kufanya nini katika jamii na ofisi yake. Ukisha jitambua kutakufanya utii mda wa kazi na majukumu yote ya kazi, na kwakuwa wewe ni binadamu si mkamilifu kuwa mwepesi kujifunza na ukishindwa kabisa achia ngazi waje wengine. Huo ndio UWAJIBIKAJI.

Kutokuwepo kwa uwajibikaji ndani ya viongozi kuna zalisha zaidi madudu na kuficha njia kwa watu wenye dira na maarifa mapya mazuri ya kuendeleza taifa, viongozi wengi wamejisahau na kujimilikisha ofisi wakisubiri mda sahihi wa kustaafu.

Na wengi wanakwepa kung'atuka wakihofia NJAA ambazo sisi wananchi wa chini tunaishi nazo kila kukicha. Niwakumbushe tuu kutokana na wao kutowajibika wanasahau kuwa njaa wanayoikimbia huku ni kwasababu hawawajibiki katika majukumu yao.

Tukumbuke uwajibikaji unatokana na malezi pia kwahiyo ukiona mtu anakosea na hajioni katika fungu la kukosea ujue hakuwa katika malezi mazuri. Ukiona mtu hazingatii katika majukumu yake ujue hata udogoni alipokuwa akiambiwa hii kazi imalize kabla ya chakula cha usiku na ikatokea hajamaliza bila sababu za msingi na wazazi wakanyamaza bila kuonya ni kosa.

Muajiri anatakiwa kwenda kusimamia mfumo wa uwajibikaji kwa viongozi na anaweza, mtu akikosea mpe onyo na zaidi ya mara 3 kakosea kwanini ashikilie ajira ya mtu? weka mtu mpya na sio kumuamishia kitengo kingine /kumuacha na hii itaenda kutibu tatizo la hawa ambao hawakuwa na malezi mazuri wakagundua hapa nimekosea natakiwa kukiri na kung'atuka ili kuwapa wengine nafasi.

Tanzania ni nchi imekuwa na wasomi wengi mno kila mwaka wanahitimu toka kwenye vyuo vikuu na kwa mifumo yetu ya elimu haiendi kumjenga mwanafunzi kujitegemea ila inaenda kumuaminisha bila ajira hawezi kuishi. Ajira zenyewe ndio hizo hizo watu wanafanya madudu maofisini ila bado wapo hakuna UWAJIBIKAJI.

Athari ya kutokuwa na uwajibikaji ni kama;

1. Utoro makazini,
kuna mda una mtafuta afisa flani kama unatafuta shilingi chooni, na sio kwamba ni mara moja kila ukienda ofisini kwake humkuti na ukifuatilia kwanini kuna sababu ambazo hazina msingi ila huna la kumfanya, pole kwako.

2. Ufanisi kushuka, umeshajihakikishia nafasi ni yako, unajua hata ukikosea utapewa nafasi kwingine na hili linaenda kushusha sana ufanisi ila mtu mwenye hofu akajua hii nafasi mda wowote natolewa haraka lazima kila kukicha anaongeza ufanisi ili kumpa changamoto muajiri katika kufanya maamuzi ya kumtupia virago na ndio uwajibikaji tunaotaka!

3. Wizi/Ufisadi; Na ndio kilio cha wengi wa chini, ni sehemu ambayo haitaki maelezo mengi ila yote yanatokana kwa kukosa uwajibikaji.

Nini kifanyike katika kuhakikisha/kuboresha mfumo wa uwajibikaji Tanzania?

1. Kuundwa kwa vyombo huru vya kusimamia mienendo ya waajiriwa hasa wa serikalini; Ndio, kukiwa na vyombo huru vitakavyo husika na kuchambua malalamiko ya watu kuhusu kiongozi flani na kufikishwa sehemu husika itasaidia. Tumezoea kuona ofisi kadhaa zina masanduku ya maoni, unaamini ukipeleka malalamiko kiongozi flani wa ofisi husika ni mtoro/ufisadi kazini atawajibishwa? Na ikiwa wenzake/yeye mwenyewe ndio anakusanya hayo maoni.

Tukiunda vyombo huru vitawajibika kukusanya maoni katika ofisi zote na kutokana na wingi wa watu watatakiwa kubuni mfumo wa kimtandao ambao utampa mtu yotote uhuru wa kuwasilisha maoni kwa uhuru bila woga pia vyombo hivi vitawajibika kufanya tafiti kwa usiri juu ya malalamiko hasa ya utoro, nidhamu mbovu makazini. Malalamiko mengine kama ya ufisadi/rushwa basi yafikwishe sehemu husika kama TAKUKURU n.k na wahakikishe waliyo ripoti yanapatiwa ufumbuzi.

2. Kuundwa kwa miradi midogo midogo itayoenda kufundisha kwa mapana kuhusu uongozi na swala la UWAJIBIKAJI likiwa kiini; Miradi hii ikilenga kuanzia ngazi ya shule za msingi itaenda kuzalisha viongozi wazuri watakaoishi katika mfumo wa uwajibikaji na watakuwa mabalozi wazuri kwa wale waliowatangulia maofisini.

Hayo ni yangu machache kuhusu UWAJIBIKAJI, asante sana kwa mda wako ndugu msomaji. Andiko hili limeandikwa na Ras Zimba. Uwajibikaji ni silaha katika kuongeza maendeleo katika taifa nikiri tena napenda kuona Tanzania yenye viongozi wanaowajibika.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom