SoC03 Uwajibikaji na Utawala Bora ni muhimu ili kuzuia mikataba inayonyonya damu

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Nimevutiwa kuandika Makala hii kutokana na mjadala unaoendelea hivi sasa, kuhusu mchakato wa bandari ya Dar-es-Salaam kuingia mkataba wa uendeshaji na kampuni ya DP World ya Dubai. Ni habari ambayo imetawala vyombo vingi vya habari!

Kielezo Na. 1: Bandari ya Dar-es-Salaam
Bandari Salama Dar.png

Chanzo: KWELI - Bandari ni Suala la Muungano

Mjadala huu umenifanya nifuatilie kwa makini maswala yanayohusu uwekezaji hapa nchini toka enzi tunapata uhuru hadi sasa. Mjadala huu, pia umenikumbusha programu maalum ya serikali ya kubinafsisha mashirika ya Umma, kuanzia miaka ya 90.

Nitatoa mfano wa vitega Uchumi viwili; ambavyo ni Hoteli ya Kilimanjaro na Hoteli ya Sheraton. Hoteli ya Kilimanjaro iliuzwa kwa mwekezaji, akaiita “Kempinski Hotel”, na hii hoteli nyingine ilijengwa na mwekezaji ikaitwa “Sheraton Hotel”, zote za Dar-es-Salaam. Baada ya miaka kadhaa, majina ya hoteli hizi yalibadilikabadilika. Hivi leo, hoteli ya Kilimanjaro inaitwa “Hyatt Regency Dar-es-Salaam” na ile ya Sheraton, inaitwa “Dar-es-Salaam Serena Hotel”. Kwa mtizamo wangu, kubadilishwa majina ya makampuni ya uwekezaji ni moja ya mbinu za kukwepa malipo ya serikali.

Wakati Tanzania inasherehekea miaka takriban sitini na mbili sasa tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Waingereza, bado kuna mashirika na makampuni mengi yenye wawekezaji wa nje ambapo serikali na watanzania wanafaidika kidogo sana kama siyo kutonufaika kabisa. Hii inatokana na mikataba inayoandaliwa na wawekezaji kwa manufaa yao na kuridhiwa na serikali.
Ndio maana Andrew Coulson (1976) aliita mikataba ya namna hii “Mikataba inayonyonya Damu”.

Nitaeleza kwa ufupi hali ilivyokuwa miaka ya sitini. Kuna mashirika kadhaa yaliyoanzishwa na serikali aidha kwa ubia na makampuni ya nje na/au kuendeshwa na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Nitazungumzia zaidi Hoteli ya Kilimanjaro. Huu ni mradi huru wa kwanza wa kifahari kwa Tanzania (Andrew Coulson, 1976).
Ilikuwa ni kati ya miradi ya kwanza iliyotekelezwa kwa gharama zilizozidi makadirio, kwani ilikadiriwa shilingi za kitanzania milioni kumi na mbili (12,000,000/=), lakini ilijengwa kwa shilingi za kitanzania milioni thelathini na mbili (32,000,000/=).

Pamoja na ukweli kwamba hoteli ingemilikiwa na Tanzania (Tanganyika kwa wakati huo) kwa asilimia mia moja (100%), karibu nusu ya gharama za ujenzi ilikuwa inatolewa kama mkopo na taasisi ya fedha kutoka Israel.

Wakala wa usimamizi ilikuwa ni kampuni inayoitwa Mlonot, uchoraji ni Zevel na ujenzi ni Solol Boneh. Kampuni zote hizi tatu ni za Israel zilizotumia fursa ya nchi yenye uhuru mchanga kujinufaisha zenyewe.

Bidhaa ambazo zilikuwa hazipatikani Tanzania, ziliagizwa moja kwa moja kutoka Israel hata kama zingepatikana nchi nyingine zinazoendelea.Unyonyaji Tanzania ulianza hata kabla hoteli haijafunguliwa. Hoteli ilifunguliwa tarehe 9 Disemba 1965.

Marekebisho ya mkataba kuwezesha uendeshaji wa hoteli ulisainiwa mwezi Oktoba 1965. Mpangilio ulikuwa kwamba Mlonot alipe serikali theluthi mbili ya faida halisi ya hoteli, salio la faida lingebaki kwa Mlonot. Andrew Coulson (1976) anasema, kwa miezi mitatu ya mwanzo, hotel ilipata faida, na serikali ilipata gawio lake; lakini vipindi vingine kama hivyo, mahesabu yalionyesha kuwa hoteli inapata hasara. Kwa kifupi, mradi huu ulizinufaisha zaidi kampuni za Israel kuliko Tanzania.

Kipindi hiki cha miaka ya sitini tukiwa na uhuru mchanga tulikuwa na wasomi wachache sana katika sekta zote, hivyo hii inaweza kuwa sababu ya kuridhisha kwa makampuni ya nje kutunyonya!
Cha ajabu, unyonyaji kama huo, umeshamiri zaidi wakati huu, pamoja na nchi kuwa na mafuriko ya wasomi na wabobevu katika kila idara. Tatizo kubwa hapa ni NAKISI ya UADILIFU na UZALENDO!

Mikataba ya Uwekezaji kati ya Nchi Mbili (MIUMBI) Iliyoingiwa Na Tanzania na Athari zake

Waandishi Sabatho Nyamsenda & Amani Mhinda (Julai, 2022), wanadadavua baadhi ya mikataba ya uwekezaji iliyosainiwa na Tanzania pamoja na athari zilizojitokeza mara baada ya kuanza utekelezaji.
Sabatho na menzake wanasema, taarifa zilizopo kwenye tovuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo Duniani (UNCTAD) zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2022 kulikuwa na MIUMBI kumi na tisa (19) kati ya Tanzania na nchi zingine. Nchi hizo ni pamoja na Afrika Kusini (2005), Canada (2013), China (2013), Denmark (1999), Italia (2001), Korea (1998), Kuwait (2013), Mauritius (2009), Misri (1997), Omani (2012), Uswidi (1999), Ufini (2001), Uholanzi (2001), Uingereza (1994), Ujerumani (1965), Uswisi (2004), Uturuki (2011), Yordani (2009), na Zimbabwe (2003).

Jedwali 1: Mashauri yaliyofunguliwa na Kampuni za Nje dhidi ya Tanzania katika Kituo cha ICSID
Kesi za Mikataba 1.png

Chanzo: Tovuti ya Benki ya Dunia Search Cases | ICSID

Jedwali 2: Mashauri yaliyofunguliwa na Kampuni za Nje dhidi ya Tanzania katika Kituo cha ICSID (inaendelea)

Kesi za Mikataba 2.png

Chanzo: Tovuti ya Benki ya Dunia Search Cases | ICSID

Athari za MIUMBI

Nchi inaposaini MIUMBI inapoteza uwezo wa kutunga sera na sheria za kulinda uchumi na rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi wake. Matokeo yake ni kuwa sera zinazotungwa ni zile zinazoongeza umaskini kwa wananchi huku zikinufaisha wageni.

Pale ambapo nchi hujaribu kuchukua hatua za kulinda rasilimali zake na kuratibu uwekezaji, wawekezaji huifungulia nchi hiyo mashitaka katika mahakama za kimataifa ambazo zimeundwa mahususi kwa ajili ya kulinda maslahi ya wawekezaji. Kuna gharama kubwa sana katika uendeshaji wa kesi hizi nje ya nchi, ambazo ni mzigo kwa walipa kodi. Pia, adhabu inayotolewa ni kubwa sana kiasi cha kuifanya nchi ikope ili iweze kulipa fidia kwa wawekezaji.

Tunaweza Kupokea Uwekezaji Mkubwa kutoka Nje ya Nchi bila MIUMBI
Watetezi wa MIUMBI husema kuwa inasaidia kuvutia wawekezaji lakini dhana hii siyo sahihi. Kwanza, ukitazama orodha ya nchi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania, utaziona nchi pia ambazo hazina MIUMBI na Tanzania, kama India, Kenya na Umoja wa Falme za Kiarabu. Hii inamaanisha kuwa MIUMBI sio kigezo kikuu cha kuvutia uwekezaji. Ipo mifano mingi ya nchi ambazo zimeamua kujiondoa katika MIUMBI na bado zinaendelea kupokea uwekezaji mkubwa tu kutoka nje ya nchi.

Hitimisho
Ni vyema serikali iweke wazi swala la Bandari ya Dar-es- Salaam na Kampuni ya DP World na isiharakishe kusaini mkataba bila kushirikisha wadau mbalimbali hasa wananchi, kwani subira yavuta heri! Na kila mmoja awajibike vyema katika nafasi yake na hivyo kuimarisha Utawala Bora katika kila sekta.
Naungana na Padri Privatus Karugendo ambaye amenukuliwa akisema: “Ipo siku itatimia. Ndiyo, itatimia, ile ndoto yako ya kuiona Afrika iliyo huru, inayojitegemea kiuchumi na yenye kuamua mustakabali wake na kutumia rasilimali zake kwa ustawi wa watu wake”.

Marejeo

Uwekezaji wa Umma – Jamhuri ya Muungano ya Tanzania


Sabatho Nyamsenda & Amani Mhinda (Julai, 2022), Mikataba ya Uwekezaji Kati ya Nchi Mbili (MIUnMBI) na Athari zake kwa Tanzania.
 

Attachments

  • Bandari ya Dar.png
    Bandari ya Dar.png
    36.5 KB · Views: 7
Mwaka 1884, Chifu Mangungo wa Sagara (Kilosa ya leo) aliingia mkataba na Ujerumani na hivyo kuachia himaya yake, watu wake na hadhi yake kwa sababu mkataba uiandikwa kwa kijerumani, na mkalimali wake hakujua kijerumani.
Lakini leo hii, zaidi ya miaka 130, katika karne ya 21, inashangaza kuona mikataba ya aina hiyo ikiendelea kusainiwa.
 
Bahati mbaya, ni watu wachache sana wanaojua umuhimu wa mikataba inayohusu matumizi ya rasilimali zetu kuwa wazi na kujadiliwa na watu wengi kadri inavyowezekana kabla ya kusainiwa na kuanza utekelezaji. Habari zinazochukuwa ufahamu wa watu wengi ni zile za Simba na Yanga, mipira ya Ulaya, Mambo ya Wasanii mbalimbali, na mambo mengine ya udaku!!
 
Nchi hii imeingia mikataba mbalimbali huko nyuma bila kushirikisha umma; Siku hizi, walau watu wengi wanajua nadhani kutokana na utandawazi uliopo sasa, ambapo inasaidia angalao kuwawezesha kupiga kelele.
 
Mikataba inayogusa maisha ya mwananchi ni budi iwekwe wazi, ijadiliwe na wadau wote, na ikibidi ipigiwe kura ya maoni.
 
Miaka ya sitini, wakati Tanganyika inapata uhuru, tulikuwa na wanasheria wawili (2) tu, leo tunao wanasheria maelfu, wengi wakizagaa mitaani. Haniingii akilini kusikia nchi inasaini mikataba yenye utata wa kisheria!!
 
Back
Top Bottom