Utoaji Fomu za PF3 bado una utata Nchini licha ya agizo la Serikali tangu miaka 7 iliyopita

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
1690799531269.png

Miaka saba tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipoagiza fomu ya Polisi namba tatu (PF3) kutolewa hospitalini na miaka miwili baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka mabadiliko ya utaratibu wa kudai fomu hiyo kabla ya tiba kutolewa, utekelezaji wa maagizo hayo umegubikwa na utata.

Agosti 22, 2016 aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliagiza PF3 kutolewa hospitalini, akisema vifo vya majeruhi wengi, hutokana na kucheleweshwa kwa ufuatiliaji wa fomu hizo vituo vya polisi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu hilo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Tiba wa wizara hiyo, Dk Magreth Mhando alisema kwa wagonjwa wote ambao wamepata matatizo ya kupigwa, kuumia na ajali wangepata matibabu pasipo usumbufu.

“Kuhusu fomu za PF3 tumeshakaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kujua kama tunatakiwa kuwarahisishia wagojwa, fomu hizo zitakuwa ndani ya hospitali. Hili tutaendelea kulifanyia kazi na kama zitapungua au zimeisha, basi mchakato wa kuziwasilisha utafanyika haraka iwezekanavyo ili kuzuia vifo vitokanavyo na ucheleweshwaji wa huduma,” alikaririwa Dk Mhando na gazeti hili.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan, miezi 26 iliyopita aliagiza mtu aliyeumia apatiwe tiba ndipo utaratibu wa kupata PF3 ufuate.

Mei 18, 2021 Rais Samia aliagiza kuangaliwa upya kwa sheria hiyo ili wanapofikishwa hospitali watibiwe kwanza ndipo yafuate masuala ya Polisi, akisema uwepo wake husababisha watu kupoteza maisha wakiwa wamefikishwa hospitali.

Alisema wanaopata ajali huumia kwa viwango tofauti, wengine wanapofika hospitali hutakiwa kushughulikiwa kwa haraka, lakini sheria ya nchi ni kuwa hawezi kuhudumiwa hadi aende na PF3.

Serikali iliweka utaratibu wa mtu anapokuwa ameumia apate PF3 kwa mujibu wa kifungu cha 170 cha Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi ili aweze kupokewa na kupewa matibabu katika hospitali.

Msingi wa PF3 ni kutaka kujua mazingira ya mtu huyo aliumia wapi na alikuwa anafanya nini. Fomu hiyo pia hutumika kama kielelezo mahakamani iwapo mtu ameshambuliwa au kupigwa ili Mahakama ijue ameumia kiasi gani ili kurahisisha utoaji wa adhabu stahiki.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika hospitali nne za mkoani Dar es Salaam na moja kwa kila mikoa ya Mwanza, Mara na Pwani unaonyesha kuwapo utata katika utekelezaji wa maagizo hayo.

Hospitali hizo hazitoi PF3 kwa majeruhi wa ajali, huku baadhi zikiwahudumia pasipo kuwa na fomu hizo na nyingine zikikataa kutoa tiba mpaka zinapowasilishwa.

Hali ilivyo hospitalini

Licha ya takwimu za Jeshi la Polisi kuonyesha asilimia 53 ambayo ni zaidi ya nusu ya ajali zilizotokea nchini kati ya Januari na Machi mwaka 2019, zilitokea jijini Dar es Salaam, bado hakuna utaratibu wa kutoa PF3 kwa majeruhi hospitali.

Mwandishi wa makala haya, juzi alitembelea hospitali za rufaa za mkoa za Amana na Temeke jijini Dar es Salaam kuangalia iwapo fomu hizo hutolewa hospitalini.

Katika hospitali ya Temeke mhudumu aliyekuwa mapokezi alibainisha kuwa hakuna utaratibu wa kutoa PF3.

Kwa upande wa Amana, licha ya kutokuwepo utaratibu wa utoaji fomu hizo, muuguzi alisema kuna uwezekano wa kutibiwa pasipo kuwa na PF3.

"Ukiwa majeruhi unatakiwa kuwa na PF3, lakini kama huna hapa hatuachi kumhudumia mgonjwa kwa sababu hiyo, utatibiwa kisha taratibu nyingine zitaendelea," alisema muuguzi huyo, kauli sawa na iliyotolewa na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Bryceson Kiwelu.

Dk Kiwelu alisema: "Hapa hatuna kitengo cha kutoa PF3, ingawa ni jambo jema, acha tuone namna ya kuzungumza na wenzetu wa polisi kwenye hili tuone tutaendaje, ingawa hospitalini hapa cha kwanza ni kutoa huduma kwa majeruhi wakati PF3 inafuatiliwa, kwetu sisi ni uhai kwanza."

Dk Benela Zavery, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa ya Mwananyamala alisema PF3 zinazotolewa hospitalini ni kwa ajili ya manusura wa vitendo vya ukatili.

"Kwa majeruhi wa ajali zinatolewa polisi moja kwa moja, hapa tuna kitengo cha wale manusura wa vitendo vya ukatili ambao PF3 zao zinatolewa hapa hapa," alisema Dk Zavery.

Malalamiko ya wananchi

Chiando Masatu, mkazi wa Pugu jijini Dar es Salaam, akizungumza na gazeti hili alisema wiki tatu zilizopita alivamiwa na vibaka eneo la Majohe ambao walimtoboa kwa bisibisi kichwani na mkono wa kulia alipokuwa akijikinga asitobolewe macho.

Alisema alikwenda kupata matibabu kwenye hospitali moja ya Serikali iliyopo jirani, lakini kwa kuwa hakuwa na PF3 hakupewa huduma, hivyo alikwenda ya binafsi alikotibiwa na baada ya kupata nafuu hakufuatilia tena fomu hiyo.

Malalamiko kama hayo pia yalitolewa na Gaspar Robert, aliyesema baada ya kupata ajali ya gari eneo la Kiluvya Madukani, walikataliwa kupewa angalau huduma ya kwanza kwenye moja ya hospitali za Serikali mjini Kibaha mkoani Pwani.

"Hakuna aliyekubali japo kuandikisha taarifa zetu, tulijaribu kuwaeleza kwamba Polisi waliokuwa eneo la tukio hawakuwa na fomu hizo muda ajali inatokea na wamesema watazileta wenyewe, sisi tuwahi kupata matibabu lakini walikataa kutusaidia.

"Nilichanika mkono wa kushoto na kwenye sikio, nilijikata kwenye kioo cha mbele, mke wangu aliumia kichwani na jirani yetu mmoja alipasuka kichwani, huyu alikuwa akivuja damu nyingi, lakini bado manesi walikataa kutupokea na kutupa japo huduma ya kwanza kwa kuwa tu hatukuwa na PF3," alisema Robert, aliyekuwa dereva wa gari lililopata ajali miezi tisa iliyopita.

Alisema wauguzi walitaka mmoja wa majeruhi atafute bodaboda nje ya geti la hospitali ili wamtume akafuatilie PF3 polisi na zitakapofikishwa ndipo watibiwe.

"Huo ndio ulikuwa msimamo wao, nakumbuka walikuwa watatu asubuhi ile, saa moja kasoro, nilijaribu kuwaomba wanisaidie japo mimi tu nipate huduma ya kwanza, ili kuzuia nisiendelee kuvuja damu niweze kwenda polisi kufuatilia fomu hizo, bado walikataa," alisema.

Agripina John, ambaye ni mke wa Robert alisema waliendelea kuugulia maumivu, huku wakivuja damu kwa zaidi ya nusu saa hospitalini hapo, hadi askari wa usalama barabarani walipofika wakiwa na fomu hizo.

"Ilikuwa ni kama muujiza, hata manesi walishituka. Mwanzoni walisema itakuwa ni maajabu ya mwaka askari kupeleka PF3 hospitali, lakini kama walivyotuahidi kwenye eneo la ajali kwamba tutangulie hospitali watazileta walifanya hivyo,” alisema Agripina.

Mkazi wa jijini Mwanza, Fodia Gamba yeye anasimulia machungu ya kumpoteza kaka yake Juni mwaka huu akidai alichelewa kupata huduma baada ya kupata ajali kwa kuwa hakuwa na PF3.

"Alikuwa kwenye hali mbaya, alihitaji msaada wa haraka. Aligonga mti akiwa anaendesha gari, alisaidiwa na wasamaria wema waliompeleka hospitali, lakini alichelewa kupata huduma kwa kuwa tu hakuwa na PF3.

"Japokuwa tunaamini kifo ni mpango wa Mungu kwa mwanadamu, lakini wakati mwingine msaada wa matibabu unaweza kukusogezea siku za kuishi na kukuepusha na kifo kwa wakati huo," alisema.

Kauli ya Polisi

"Wanaokataa kuwatibu majeruhi kwa kigezo eti hadi wawe na PF3 huo ni ukosefu wa maadili. Hata awe jambazi, mwizi au mtu mwingine yeyote, anapopata ajali asinyimwe matibabu kwa sababu tu hana fomu hii. Ni kweli PF3 ni muhimu, lakini uhai ni muhimu zaidi."

Hii ni kauli ya Mkuu wa Usalama Barabarani nchini, Ramadhani Ng'anzi, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kutopatiwa huduma kwa kukosa fomu hiyo.

Alisema kitu cha kwanza kwa majeruhi ni kuokoa maisha yake bila kujali ana PF3 au la.

"Yule atakayekuwa karibu kutoa msaada kwa wakati huo amuwahishe kwanza hospitali, wakati akiendelea kupatiwa matibabu ndipo akafuatilie fomu hiyo. Atafikisha taarifa polisi ambao watakuja kuangalia kama ni kweli wakiwa na hiyo fomu. Wajibu wa raia aliyemsaidia majeruhi ni kutoa tu taarifa, kama majeruhi ana hali mbaya mpeleke kwanza hospitali, kama ana nafuu ndipo mnaweza kuanzia polisi. “Wengine sawa lazima wapitie polisi, lakini inategemea na hali yake, mfano unaanza kuzunguka naye kwenda polisi kufuatilia PF3 akikufia utakuwa umemsaidia?" alihoji.

Alisema wajibu wa kwanza wa daktari ni kuokoa maisha ya mtu awe jambazi, kibaka au mwananchi wa kawaida.

Mganga mkuu anena

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema mgonjwa yeyote anapokwenda hospitali hata awe wa ajali cha kwanza ni kumtibu.

"Hayo masuala ya PF3 kwa majeruhi ni ya kipolisi, utaratibu wa kujaza ni wao siwezi kuwasemea, lakini sisi kwenye afya maadili yetu kitu cha kwanza ni kutibu," alisema na kuongeza:

"Kama ni kweli wapo wauguzi wanaokataa kuwapokea majeruhi kwa kuwa hawana PF3, kwa upande wetu Dar es Salaam, tupewe tu taarifa na sisi tutaichunguza kabla ya hatua kuchukuliwa. Kikubwa hapa ni ushirikiano ili kumsaidia mgonjwa."

Muuguzi katika hospitali moja ya binafsi mkoani Mara, Zawadi Zaidi alisema wamekuwa wakiwapokea majeruhi na kuwatibu bila fomu hizo.

"Wengi hasa wale wanaoumia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, huwa wanakimbilia hapa kwa kukwepa kuulizwa PF3 kwa kuwa hospitali hii ni ya kulipia.

"Utakuta mwingine anakuja amekatwa mapanga ana majeraha makubwa, mwingine ukimuangalia anahitaji msaada wa haraka zaidi; wengi tunawatibu bila PF3 kisha mengine yatafuata," alisema.

Ambakisye Mwakifwange, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuelimisha na kupambania haki za abiria (Shikuhata), anasema PF3 kama zikianza kutolewa hospitali, itakuwa jambo rahisi kwa majeruhi kupata tiba.

"Fomu hii ni muhimu kwa sababu ya usalama, ingawa ni kama naona inatiliwa mkazo zaidi mijini. Vijijini hospitali nyingi majeruhi wanatibiwa tu," alisema.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom