NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WEMYE UCHUNGU
Sehemu ya Thelathini na Nne.
Kwa jinsi alivyokuwa, haikuwa rahisi kumkubalia, alionekana kuwa na hasira sana hivyo kuona kwamba kama wangemruhusu kuingia ndani basi angeweza kuanzisha timbwili huko ndani.
Wakati hayo yote yakiendelea, Dk. Fabian alikuwa katika chumba kingine na dereva, walikuwa wakizungumza lakini muda mwingi daktari huyo alionekana kuwa na mawazo tele.
Kitu kilichompa mawazo ni kuhusu Mike ambaye aliibuka tena na kuhitaji watoto wake. Alimfahamu kama bilionea lakini alisahau kwamba huyo mwanaume ndiye yule aliyemfuata kipindi cha nyuma na kumtoa mbegu zake za kiume.
Hakujua ni kitu gani alitakiwa kumwambia Dylan na mkewe, mwanamke hakujua kitu chochote kile kwani mchezo mzima ulipangwa na wao watatu tu. Alijua kwamba mwanaume huyo angeumia sana lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima amwambie ukweli kilichokuwa kimetokea.
Maofisa wa FBI walisubiri kwa dakika arobaini na tano, wakamchukua Dylan na kumpeleka katika chumba walichokuwa mwanaume yule, walitaka kuzungumza nao na kuwauliza kuhusu mahali watoto walipolekwa, walisema walichukuliwa na kupelekwa kwa baba yao, mbona baba mwenyewe alisema kwamba hakuwa amewapata watoto hao?
“Ulisema kwamba watoto walipelekwa kwa baba yao, si ndiyo?” aliuliza afisa wa FBI, pembeni yake akiwepo Dylan na mkewe, Katty.
“Ndiyo!”
“Wazazi wao ndiyo hawa hapa, mbona wanasema hawakuwapata watoto wao?’ aliuliza afisa yule huku akiwaangalia.
“Mkuu! Ila sisi tuliambiwa kwamba wanapelekwa kwa baba yao!”
“Sasa mbona hajawapata? Baba yupi?”
“Baba yao!”
“Si ndiye huyu! Mbona hajawapata?”
“Hata sisi hatujui!”
Walichokifanya FBI ni kumchukua Dk. Fabian na kisha kuwapeleka katika chumba kingine cha mahojiano, huko walitaka kufahamu sababu za wao kutekwa kwa kuhisi kwamba kupitia wao wangeweza kupata kitu fulani.
Alipoulizwa dereva, alisema tu kwamba alikwenda kuwachukua watoto hao, ghafla akatekwa yeye na watoto na kupelekwa gereji, watoto wakachukuliwa na kupelekwa kwa baba yao, kitu ambacho aliona si kweli.
“Na wewe dokta?” aliuliza afisa, Dk. Fabian akakaa kimya, maofisa wote waliokuwa humo ndani wakabaki wakimwangalia, hawakujua sababu ya kukaa kimya, alipomaliza kuwa katika hali hiyo, akauinua uso wake na kuwaangalia.
“Naomba nionane na BwanaDylan!” aliwaambia maofisa wale.
Hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa alimhitaji huyo, afisa mmoja akatoka na kwenda kumuita, baada ya dakika moja tu, akarudi akiwa na Bwana Dylan ambaye alikuwa akiongozana na mkewe.
“Naomba tupewe chumba cha siri, tuna mazungumzo binafsi...” alisema Dk. Fabian, hata Bwana Dylan akabaki akishangaa, kwanza kitendo cha kumuona daktari huyo hapo polisi, kilimchanganya.
Wakapelekwa katika chumba kimoja cha siri, hakukuwa na kamera za CCTV wala hakukuwa na vinasa sauti. Huko wakatulia, muda wote Bwana Dylan alikuwa akimwangalia daktari yule, alihisi kulikuwa na kitu.
“Kuna nini?” aliuliza.
“Mike amerudi!”
“Mike! Ndiye nani?”
“Yule bilionea!”
“Unamzungumza huyu Mike bilionea, amerudi kutoka wapi sasa?” aliuliza Bwana Dylan.
“Unakumbuka zile mbegu tulizozitoa, zilikuwa zake na ndiye yeye aliniteka na kuniuliza nilimuwekea nani mbegu zile, nilikataa kusema, akatishia kuniua..” alijibu Dk. Fabian na kuhadithia kila kitu kilichotokea.
Bwana Dylan alibaki kimya, mwili ulikuwa ukimtetemeka, japokuwa ndani ya chumba kile kulikuwa na kiyoyozi lakini alihisi kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini alichokisikia kwamba yule Mike ambaye alifanikisha zoezi zima la upatikanaji wa watoto wale eti alirudi na kuwataka watoto wake.
“Haiwezekani! Nilimalizana naye, wale ni watoto wangu na si wake ni wangu,” alisema Dylan huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hali ya hewa ilibadilika, wakatoka ndani ya kile chumba, kwa jinsi alivyokuwa Dylan kipindi kifupi kilichopita, alionekana kuwa tofauti kabisa na kipindi hiki. Alionekana kuwa mwingi wa hasira, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile.
“Kuna nini?” aliuliza afisa mkuu wa FBI, Bwana Pierre August.
“Nataka nizungumze na wewe...” alijibu Dk. Fabian.
“Kuhusu nini?”
“Aliyewateka watoto.”
“Unamjua?”
“Ndiyo!”
“Ni nani?”
“Bilionea Mike...”
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Ila kuna kitu....”
“Kitu gani?”
“Mtafuteni yeye kwanza...” alisema Dk. Fabian.
Maofisa wa FBI hawakutaka kusubiri, waliambiwa juu ya mtuu aliyekuwa amewateka watoto hao, alikuwwa bilionea mkubwa, hawakujua sababu ya kuwateka hivyo walichokifanya ni kuanza kwenda nyumbani kwake.
Huku nyuma, Dylan alikuwa amechanganyikiwa, akaona kama dunia ikiimgeuka, hakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna ile, alimwangalia mke wake, alionekana kuwa mtu mwenye maswali mengi lakini hakutaka kuzungumza kitu chochote kile.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa siri kubwa na muda huo ulionyesha kabisa kwamba ile siri iliyodumu kwa miaka yote ilikuwa ikienda kujulikana, angefanya nini? Hakujua.
Polisi na maofisa wa FBI wakaelekea mpaka nyumbani kwa Mike, wakaoba kuonana naye, wakaruhusiwa kuingia ndani. Walipofika sebuleni, macho yao yakatua kwa watoto waliokuwa wakiwatafuta, walionekana kuwa kawaida, hawakuwa na furaha wala hawakuwa na huzuni.
Mike alikuwa sebuleni hapo pamoja na mkewe, Aisha, walikuwa wakizungumza mambo mengi na watoto wale, kwa kutumia maneno mengi, bado Mike alikuwa akiwaambia kwamba yeye alikuwa baba yao.
“Na mama yetu ni nani?” aliuliza Patrick.
“Huyo aliyewazaa...”
“Nini kilitokea?” aliuliza Patricia.
“Ni stori ndefu sana, ila nataka mfahamu kwamba mimi ndiye baba yenu,” alisema Mike.
Maofisa hao waliposimama kwa muda, waliimwangalia Mike na mkewe, hawakuonekana kuhofia kitu chochote kile, walichokifanya, hapohapo wakamwambia juu ya kile kilichotokea kwamba alikuwa akishutumiwa kuwateka watoto.
“Sikuwateka watoto...” alijibu Mike.
“Kumbe wamefikaje hapa?”
“Nilikwenda kuwachukua, hivi kweli kuna mtu anaweza kuwateka watoto wake?” aliuliza Mike huku akiwaangalia maofisa hao.
“Watoto wako hawa?”
“Ndiyo!”
Kila mmoja alionekana kumshangaa, walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka katika kituo cha polisi huku akiongozana na mapacha wale. Mike hakuonekana kuogopa hata mara moja, njia nzima uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana.
Walipofika katika kituo hicho, wakaingizwa ndani ambapo huko wakakutana na Bwana Dylan akiwa na mkewe, Katty. Patrick na Patricia walipomuona mama yao, wakamfuata na kumkumbatia, walionekana kuwa na furaha mno.
“Mlikuwa wapi?” aliuliza mwanamke huyo.
“Tulikuwa kwa baba...”
“Baba gani?”
“Baba yetu....”
“Yupi?”
“Huyu hapa!” walijibu huku wakimnyooshea mkono Mike.
Hakukuwa na kitu kilichomuuma Dylan kama kuona watoto wake wakimtaja mwanaume mwingine kwamba ndiye baba yao. Aliyasikia maumivu makali moyoni mwake, yaani kitendo cha Mike kukaa na watoto hao kwa muda mfupi tu tayari aliwaambia maneno mengi, kuwashawishi kwa mifano mpaka watoto wote kuamini kwamba yeye alikuwa baba yao.
Dylan hakujibu kitu, alikwenda pembeni na kutulia kwenye kiti. Muda wote machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea mahali pale.
Katty alibaki na maswali mengi, alipomwangalia Mike, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana lakini alipoyapeleka macho kwa mumewe, alikuwa akilia kwa uchungu, hakujua kitu gani kilitokea, katika kumbukumbu zake, hakukumbuka kama alikwishawahi kuonana na Mike, sasa iweje hao watoto wawe wake? Kila alichojiuliza, akakosa jibu.
“Wewe unasema watoto hawa ni wako! Si ndiyo?” alisema Bwana August huku akimwangalia Mike.
“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Dylan anaelewa kila kitu! Watoto ni wangu! Hii ni damu yangu!” alijibu Mike huku akionekana kujiamini.
“Unanichanganya!”
“Angalia hata sura zetu, huoni kama nafanana nao sana...”
“Hilo si tatizo!”
“Basi muulize Dylan, hawa ni watoto wa nani!” alisema Mike.
Bwana August akamgeukia Dylan ambaye alikuwa pembeni akilia tu. Kila mmoja alimuonea huruma lakini ilikuwa ni lazima ukweli ujulikane kwamba hao watoto walikuwa wa nani.
Mke wake mwenyewe alibaki akimwangalia, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Bado alichanganyikiwa, kwa nini mumewe ajiumeume na wakati alijua fika kwamba watoto wale alizaa nao. Kila Dylan alipoulizwa, alibaki kimya.
“Hawa ni watoto wangu! Dk. Fabian, hebu eleza kila kitu kilivyokuwa!” alisema Mike huku bado tabasamu lake likionekana kuwa usoni mwake.
Ilikuwa ni lazima ukweli ujulikane, hata Catherine, mdogo wake Dylan alibaki kimya akiangalia kilichokuwa kikiendelea. Yeye mwenye alichanganyikiwa, kila alipowaangalia mapacha wale, walifanana mno na Mike ambaye alidai kwamba ndiye alikuwa baba wa watoto wale.
Hapo ndipo Dk. Fabian alipoanza kusimulia, alitakiwa kufanya hivyo, hakutakiwa kunyamaza au kuficha kitu chochote kile, alitakiwa kuzungumza ukweli juu ya kila kitu kilichotokea huko nyuma.
Kila mtu alibaki kimya akimsikiliza, muda wote huo, Dylan alijiinamia, machozi mfululizo yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake. Alikuwa tajiri mkubwa, aliyeheshimika, hapo ndipo akagundua kwamba utajiri haukuwa na maana yoyote ile.
Ulikuwa na uwezo wa kununua dawa ila si uhai, ulikuwa na uwezo wa kununua magari ila si furaha. Maneno aliyokuwa akizungumza Dk. Fabian yalimuumiza mno, kila alipoyasikiliza, alihisi kuna mtu alichukua mkuki wenye ncha kali iliyounguzwa na moto na kisha kuuchoma moyo wake.
Mpaka anamaliza kusimulia, Katty alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kimesimuliwa. Yaani kila siku alijua kwamba watoto wale walikuwa wake na mume wake kumbe nyuma ya pazia kulikuwa na kitu kingine, kumbe alipandikiziwa mbegu katika mfumo wake wa uzazi.
Kilio kilisikika kwa sauti ya juu, hakukubali hata mara moja, akamfuata mumewe na kuanza kumgombeza huku akilia, moyo wake ulijisikia uchungu, kama mumewe alikuwa na tatizo, kwa nini hakumwambia kabla. Kila siku alikuwa akifanya naye mapenzi, alikuwa akifanya na nini? Kila alipojiuliza, alichanganyikiwa.
Dylan hakuzungumza kitu, hakutaka kubaki mahali hapo, akatoka nje na kuanza kuondoka huku dada yake akiwa nyuma akimfuata.
“Dylan, unakwenda wapi?” aliuliza Catherine, tayari Dylan alikuwa ndani ya gari, naye akaingia.
“Catherine, nitaishi vipi? Nitaificha wapi sura yangu?” aliuliza Dylan, alikuwa akiendelea kulia tu.
“Unakwenda wapi? Nijibu!”
“Niache, sioni umuhimu wa kuishi, sioni umuhimu wa kuwa tajiri. Nimeumia, utajiri hauna maana, ni utajiri wenye uchungu, utaniliza kila siku. Kwa nini? Kwani imekuwa hivi? Kwa nini Catherine?” aliuliza Dylan, alikuwa akilia mno, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno.
Catherine mwenye hakujibu maswali hayo, alibaki akimwangalia kaka yake, kwa jinsi alivyoonekana tu, alikuwa na maumivu makali moyoni mwake, hakujua nini cha kumwambia na hakutaka kumuache kaka yake kwani alijua ni kitu gani kingetokea endapo angemuacha, ilikuwa ni lazima ajiue kwani alikata tamaa, hakuona umuhimu wa kuishi.
Akawapigia simu wazazi wake, akawaelezea kwamba anahitaji msaada mkubwa kutoka kwao kwani vinginevyo Dylan angejiua. Wazazi wao walichanganyikiwa kusikia hivyo, wakaahidiana waonane nyumbani kwa Dylan.
“Naomba niendeshe gari tafadhali,” alisema Catherine, Dylan akampisha, akashikilia usukani na kuanza kuondoka.
Huku ndani, Katty hakujua afanye nini, alibaki kimya huku akiwaangalia watoto wake, kila alichokisikia hakukiamini, alimchukua mumewe, Dylan kwa kile alichomfanyia, uamuzi wa kuondoka mahali hapo na watoto wake ndiyo uliomjia kichwani, hakutaka kurudi nyumbani, alipanga kuondoka haraka sana kuelekea Los Angeles.
“Katty...samahani sana kwa kilichotokea, hakikuwa dhumuni langu, najua umeumia sana lakini haina jinsi, naomba unisamehe kwa kila kitu,” alisema Mike huku akimwangalia mwanamke huyo.
“Usijali...”
“Sasa unakwenda wapi?”
“Ni lazima niende Los Angeles, siwezi kubaki hapa...”
“Na watoto wangu?”
“Ni watoto wangu pia...”
“Najua! Lakini ningependa kuwa nao karibu!”
“Najua!”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
Moyoni mwake aliumia, kila kitu alichokiacha nyumbani, hakutaka kukirudia, aliamua kuondoka kuelekea Los Angeles. Watoto hao hawakuwa wake peke yake, bali baba yao alikuwa Mike ambaye naye alikuwa bilionea mkubwa.
Wakapanga mikakati ni kwa namna gani wangewatunza watoto hao, hivyo siku hiyohiyo Mike kumsindikiza kuelekea Los Angeles kwa ndege yake binafsi. Huku nyuma, hata vijana ambao walifanya utekaji wakaachiwa huru kwani kesi yenyewe ikagundulika kwamba watoto hawakutekwa bali walichukuliwa na baba yao, mjadala ukaishia hapo.
Wakafika mpaka Los Angeles ambapo wakapanga apartment na kuishi huko. Kwa kuwa Mike aliwapenda sana watoto wake, akaamua kuwanunulia nyuma ya kifahari, kuwawekea kila kitu na kumtaka Katty aishia nao huko.
Kila siku Katty akawa mtu wa kupokea meseji na kupigiwa simu na Dylan na kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea, hakujibu meseji hizo kwani mwanaume huyo alimuumiza moyo wake kupita kawaida.
Siku zikaendelea, watoto wakakua, Dylan akaendelea na maisha yake yenye uchungu, ya kulia kila siku. Hakuwa na furaha hata siku moja, aliwakumbuka Patrick na Patricia lakini hakuwa na jinsi, hawakuwa watoto wake.
Hayo mambo yalimalizwa kimyakimya, hata maofisa wa FBI walipewa fedha nyingi kutunza siri, hakikutakiwa kujulikana kitu chochote kile. Kutokana na kuwa na msongo wa mawazo, afya ya Dylan ikaanza kuzorota, akaanza kukonda, akawa hali na baada ya kwenda hospitali kupimwa, akagundulika kuwa na shinikizo la damu ambalo lilimfanya kudhoofika kila siku mpaka kufikia hatua ya kupelekwa hospitali.
Afya yake haikubadilika, bado aliendelea kuumia kila siku, akakosa amani, furaha ikapotea, fedha hazikumsaidia, hazikuweza kuinunua afya na kurudi kama zamani.
Kuumwa kwake ukawa gumzo duniani kote, kila kona watu walimzungumzia yeye, kila mmoja alisema lake, kwa jinsi alivyokuwa amedhoofika kitandani pale kila mmoja aliamini kwamba Bwana Dylan asingeweza kupona, angekufa palepale kitandani.
Maneno ya watu hao yakawa kama sumu kwani tangu watu wawe na hofu namna hiyo na kutamka maneno mabaya, Dylan hakuchukua muda mrefu, akafariki kitandani hapo.
Ilikuwa ni huzuni mno, watu walisikitika kwani alikuwa mtu mwema, aliyewasaidia watu wengi ila mwisho wa siku, shinikizo la damu likamuua kitandani hapo.
Katika mazishi yake, Katty hakuacha kwenda, alikwenda ila hakwenda na watoto kwa kuwa huyo hakuwa baba yao, ndugu za Dylan walikuwa wakimwangalia kwa jicho baya lakini hakutaka kujali, alichojua alikwenda hapo kwa ajili ya kuonyesha ushirikiano na kwa kuwa alimpenda Dylan, hakukuwa na kingine.
Baada ya siku mbili, Dylan akazikwa katika makaburi ya Victoria Cementary yaliyokuwa New Orleans ambapo ndipo alipokuwa amezaliwa, sehemu ambayo wazazi wake walikuwa wakiishi hata kabla ya kupata utajiri.
Baada ya mazishi hayo, Katty akarudi zake Los Angeles ambapo aliendelea kuwalea watoto wake. Hakuhitaji urithi, hakuhitaji kitu chochote kutoka katika familia ya Bwana James, aliwaacha na utajiri wao, yeye aliendelea kufanya vitu vyake huku Mike akimtunza na kumfungulia biashara mbalimbali za kufanya ambazo zilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha.
MWISHO.