USIFE KWANZA MPENZI WANGU....EPISODE.16-17
Penzi linachipuka kutoka ndani mwa Levina kwenda kwa Deo, kijana anayefanya kazi nyumbani kwao kwa kasi ya ajabu sana. Anashindwa kufanya kazi vyema kutoka na hisia hizo kali za mapenzi. Anajaribu kumweleza Deo, ambaye alimkubalia kwa shangwe!
Hili lilimfanya afunge duka lake haraka na kurejea nyumbani ili aweze kupata wasaa wa kuzungumza na Deo, lakini jambo la ajabu, alipofika akakuta Deo akiwa na maamuzi mengine mapya! Hakuwa tayari kuwa naye kimapenzi, kiasi cha kumsukuma mbali!
Baadaye wakiwa kwenye meza ya chakula, Levina alionesha alama zote kuwa anampenda Deo au walikuwa katika uhusiano, jambo ambalo baba yake, aliligundua! Akahisi kuwepo kwa jambo linaloendelea kimya kimya! Je, nini kitatokea? Endelea kufuatilia...
MZEE Masamu aligundua kitu kupitia macho ya mwanaye aliyekuwa akimwangalia Deo kwa macho yaliyojaa ubembe wa mahaba. Ni kitu ambacho hakukipenda hakika, hakutaka kabisa mwanaye awe na uhusiano na kijana yule. Hakuwa na hadhi ya familia yao.
Mara ghafla, akasogeza pembeni sahani yake ya chakula na kunawa mikono yake, jambo hilo lilimshangaza sana mke wake.
Vipi baba Levina?!
Im okay!
No dady, you are not okay, vipi chakula hujakipenda? Mama Levina akasema kwa sauti ya taratibu sana.
Nimeshiba mama Levina, akasema mzee Masamu akimwangalia Levina kwa macho yenye kiashiria kibaya.
Mama Levina aliweza kugundua kwamba kuna jambo ambalo si la kawaida lilikuwa likiendelea. Anamfahamu vizuri sana mume wake, hakuwa na kawaida ya kushiba haraka kiasi kile, lazima kulikuwa na kitu. Naye akasogeza sahani yake pembeni na kunawa mikono.
Mom, kwanini mnasusa chakula? Levina akauliza kwa mashaka kidogo.
Shiiiiii... mama Levina akamnyamazisha mwanaye.
Deo akagundua kwamba mchezo wa Levina ulikuwa umegundulika, mara moja akanawa mikono na kukimbilia chumbani kwake. Bwana na Bibi Masamu wote kwa pamoja wakaongozana kwenda chumbani kwako kulala.
Mume wangu mpenzi, nini tatizo? Nini kimetokea mpenzi wangu, maana naona haupo sawa kabisa! Mama Deo akamwuliza mumewe walipoingia chumbani kwao.
Unataka kusema hujaona chochote? Mzee Masamu akasema kwa hasira.
Nini tena dear?
Hivi unakumbuka kwanini tulimwondoa Rashid hapa nyumbani?
Ndiyo!
Unaona anayofanya mwanao?
Nani Levina?
Kwani nani mwingine?
Kivipi basi mume wangu?
Hujaona anavyomwangalia yule kijana?
Kwakweli sijawa makini kuwaangalia mume wangu!
Sasa wewe kuwa makini au usiwe makini, lakini nataka kukuambia kwamba, sitaki matatizo katika familia yangu! Deo hana hadhi ya kuwa na mwanangu!
Kwani amesema anataka hivyo?
Hapana, lakini dalili zipo wazi.
Nitazungumza na Levina!
Siyo utazungumza naye, nenda ukaongee naye sasa hivi, sihitaji matatizo katika familia yangu. Narudia tena sihitaji matatizo katika familia yangu, nenda kazungumze naye tafadhali.
Nimekuelewa mume wangu, ngoja niende nikaongee naye.
Mama Levina akatoka haraka na kumuacha mumewe chumbani akiwa amefura kwa hasira. Alipofika sebuleni, alimkuta Levina akiwa anamalizia kuondoa vyombo mezani.
Levina nahitaji kuongea na wewe!
Natoa vyombo mama!
Achana navyo isitoshe si kazi yako, kwani Helena yupo wapi? Hiyo ni kazi yake, haikuhusu wewe hata kidogo.
Najua mama, lakini... Levina akaendelea kujitetea.
Wewe tusikilizane!
Im coming mom!
Hurry up!
Ok mom!
Levina akaacha kila kitu na kujisogeza kwa mama yake, aliyekuwa amekaa kwenye sofa kubwa pale sebuleni.
Hebu niambie, nini kinaendelea kati yako na Deo?! Mama yake akamwuliza mara baada ya kukaa sofani.
Unamaanisha nini mama?
Macho yako yanaonesha jinsi unavyofahamu ninachomaanisha!
Sijui kitu mama, kwani vipi?
Sasa mimi sina kitu cha kuzungumza zaidi au kubembelezana na wewe, lakini nataka kukuambia kwa kifupi sana, kama una wazo la kuanzisha uhusiano na Deo, futa kabisa wazo hilo!
Uhusiano?
Ndiyo nimekuambia sasa, ondoa wazo hilo kichwani mwako na kama mmeshaanza tafadhali acha mara moja!
Maamaaa...mimi na Deo wapi na wapi mama?
Hili agizo limetoka kwa baba yako! Mama Deo akaongeza kusema.
Mungu wangu, kweli mama? Levina akashtuka sana.
Nadhani unamfahamu vizuri sana mzee Masamu, unajua hasira zake, sasa endelea na upuuzi wako ndiyo utajua kitakachotokea! Mama yake akasema na kusimama kisha akaondoka zake.
Levina akabaki pale subuleni akiwa mwenye mawazo mengi sana kichwani mwake. Alimfahamu vizuri sana baba yake, kama ni kweli yeye ndiye alikuwa ameagiza aachane na Deo, basi hali ilikuwa mbaya kuliko alivyofikiria.
Jambo hilo lilimtisha sana, lakini halikusababisha penzi lake dhidi ya Deo lishuke, bado alihisi penzi zito sana moyoni mwake, alimpenda sana Deo na hakuwa tayari kumpoteza.
Je, Levina atatii kauli ya mama yake?
USIFE KWANZA MPENZI WANGU....EPISODE.18-19-20
Tayari mambo yamekuwa mabaya kwa upande wa Deo, ambaye Levina anaonekana kumpenda sana, lakini kitu cha ajabu ni kwamba, Levina anashindwa kuficha hisia zake na hivyo kusababisha baba mzazi wa Levina mzee Massamu kuhisi kitu!
Jambo hilo lilimtisha sana Deo, ambaye aliingia chumbani kwake akiwa na mawazo tele akianza kuhofia kupoteza ajira yake. Akiwa bado ana mawazo, usingizi ukiwa umekataa kabisa kumchukua, akasikia mtu akigonga mlango. Akashtuka sana.
Alipouliza aliyekuwa akigonga ni nani, hakujibu! Je, nini kitatokea? Endelea kuisoma...
DEO alishtuka kuliko kawaida, mawazo tele kichwani mwake yakamuandama, kitu kilichoingia kwa kasi sana akilini mwake ni kwamba aliyekuwa akigonga mlango ule alikuwa ni mzee Massamu.
Hapo hakika ungekuwa mwisho wa ajira yake. Jambo ambalo hakutaka kabisa litokee. Akasogea mpaka kwenye kitasa cha mlango wa chumbani kwake, akasogeza mdomo wake kwenye tundu la funguo, akauliza kwa sauti ya chini kabisa...
Nani?
Fungua! Sasa akajibiwa na sauti ya kike, ambayo haikuwa ngeni sana masikioni mwake.
Alikuwa ni Levina.
We Levina, acha ujinga bwana, rudi chumbani kwako.
Fungua kwanza, kuna kitu nataka kukuambia.
Nini?
Fungua.
Deo akatumia muda wa dakika mbili tatu kuwaza, kisha akaamua kwenda kufungua ili kuepuka kelele za levina ambazo zingeweza kusababisha matatizo zaidi.
Haya unasemaje? Akamwuliza baada ya kufungua mlango.
Kabla hata sijakaa? Akauliza Levina kwa sauti ya chini, ambayo Deo alishtuka sana kuisikia, akihisi kama ni kubwa.
Ongea taratibu bwana... Deo akasema kwa woga.
Niongee taratibu nini? Unamuogopa nani?
Wazazi wako.
Wameshalala bwana.
Kwani unasemaje?
Acha utoto, inamaana hujui kwamba mimi nakupenda?
Najua.
Sasa?
Sitaki tena.
Unasemaje?
Sitaki tena.
Utataka Deo, lazima utake, hujui ni kwa kiasi gani nimehangaika kukupata. Hujui nimefanya mambo mangapi na wakati mwingine kuwakosea watu kwa sababu yako.
Lakini Levina ukumbuke kwamba ulisema unanileta kazini.
Ndiyo nakumbuka.
Sasa?
Lakini si nilikuambia kwamba nakupenda? Unadhani ningeweza kufanya mambo yote hayo hivi hivi tu!
Hivi unajua kwamba haya mambo ni ya hatari sana? Kwanza baba yako anaonekana ameshaanza kuhisi kwamba kuna kitu kinaendelea, huoni kwamba ni tatizo kwangu? Hivi nikipoteza kazi, unadhani nitakuwa mgeni wa nani mimi?
Acha kuwaza mambo ya kijinga... akasema Levina akivua gauni lake jepesi la kulalia.
Acha kufanya hivyo Levina.
Levina hakusikia kitu, akalitupa mbali baada ya kumaliza kulivua na kumsogelea Deo, kisha akamsukuma kitandani. Kama mzigo Deo akaanguka kitandani na mara Levina akamzidi ujanja, dakika chache baadaye wakajikuta wakiwa kwenye kiota cha huba ya mapenzi, wakiwa wamesahau shida zote za ulimwengu.
***
Umeongea naye? Mzee Massamu akamwuliza mkewe.
Ndiyo.
Anasemaje?
Aseme nini?
Kwahiyo hajasema chochote?
Simaanishi hivyo...kifupi amekataa.
Amekataa?
Ndiyo amekataa.
Sasa kuanzia leo anza kuwafuatilia utapata majibu, tena nahisi huenda huwa wanalala pamoja usiku. Ngoja muda uende kidogo, nataka kwenda kuhakikisha mwenyewe leo.
Sawa mume wangu, unajua kama itakuwa ni kweli, utakuwa mchezo mbaya sana.
Siyo mchezo mbaya tu, sitaki mwanangu ajiingize kwenye matatizo. Unajua kuolewa na lofa, ni sawa na kukaribisha ulofa katika familia. Hilo siwezi kuliruhusu likatokea katika familia yangu. Siwezi kabisa.
Ni kweli kabisa baba Levina...itakuwa aibu kwa familia, akasema mama Levina akiunga mkono kauli ya mumewe.
***
Saa nane na dakika zake za usiku, Mzee Massamu aliamka kitandani na kutoka nje taratibu kabisa. Akaenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa chumba cha Levina. Akatega sikio kusikia kama Levina alikuwa akihema ndani, lakini hakusikia kitu. Kwakuwa taa ilikuwa haijazimwa, akaamua kuchungulia kupitia kwenye tundu la ufunguo kuangalia kama alikuwemo mle ndani.
Hakuwepo!
Akashtuka sana.
Akashika kitasa cha mlango na kukizungusha taratibu, mlango ukafunguka wenyewe. Mzee Massamu akaingia mpaka ndani na kuangalia kila kona, hakuona mtu! Ni kweli Levina hakuwemo ndani.
Shiiiti, huyu mtoto amekwenda wapi? Akawaza.
Papo hapo likaja wazo lingine, akahisi huenda alikuwa ameingia msalani, kwa bahati nzuri choo kilikuwa mle mle ndani. Kwahiyo akaamua kuita kwa sauti ya chini...
Levina...Levina...we Levina... lakini Levina hakuitika.
Hapo akaamua kuusogelea mlango wa chooni, akajaribu kuusukuma kwa nguvu! Ukafunguka!
Levina hakuwepo!
Lazima atakuwa chumbani kwa Deo, akawaza na kutoka chumbani kwa Levina haraka.
Akapiga hatua za taratibu hadi kufikia mlango wa Deo. Korido nzima ilikuwa kimya kabisa. Alipoufikia mlango wa Deo alitarajia kusikia kelele za mahaba chumbani, lakini hakusikia.
Chumba kilikuwa kimya kabisa. Hakujiuliza mara mbili, akajaribu kuusukuma ule mlango ambapo ulifunguka mara moja kwakuwa haukufungwa!
Alihisi kuchangikiwa!
Akahisi kuzimia!
Alichokiona mle chumbani, ilikuwa vigumu sana kuamini. Macho yake yaliona gauni la kulalia la mwanaye likiwa chini, huku nguo yake ya ndani ikiwa juu ya kiti! Deo alikuwa amelala na mwanaye wakiwa kama walivyozaliwa!
Alihisia harufu ya damu!
Akatamani kuua!
Lakini akajipa moyo!
Deo unamfanya mwanangu hivi? akajisemea moyoni mwake.
Haikuwa na maana kwao maana wote walikuwa wameishilia kwenye usingizi mzito, wakiwa kama walivyozaliwa. Busara ya Mzee Massamu ikatumika, akaamua kutoka mle chumbani taratibu na kurudi chumbani kwake. Akamkuta mkewe akiwa macho. Kwa hali aliyoingia nayo, mkewe akajua lazima kulikuwa na kitu kibaya kimetokea.
Vipi mume wangu?
Nenda mwenyewe chumbani kwa Deo ukajionee.
Kuna nini?
Nenda mke wangu, akasema Mzee Massamu akitoka jasho mwili mzima.
Je, nini kitatokea?
USIFE KWANZA MPENZI WANGU ....EPISODE.21.
Mzee Massamu ametoka chumbani kwa Deo na kushuhudia akiwa amelala na mwanaye Levina, akamwamsha mkewe na kumwambia aende akajionee mwenyewe chumbani kwa Deo. Nini kitatokea? Endelea...
MAMA Levina ni kama alikuwa haelewi kabisa anachoambiwa na mumewe. Alimwangalia bila kupata majibu ya moja kwa moja. Kwanini anamwambia aende akajionee mwenyewe chumbani kwa Deo.
Mume wangu, niambie tafadhali, kuna nini?
Nenda mama, nenda ukaoane mwenyewe!
Mama Levina hakutaka kuuliza swali lingine zaidi, akatoka na kunyata hadi kwenye mlango wa Deo, kwa haraka za mzee Massamu, hakuufunga ule mlango, kwa hiyo mama Levina alivyotokeza tu akaona kila kitu!
Nusu azimie!
Akajikaza sana, lakini akashindwa, macho yake yakaanza kumwaga machozi. Hakutaka haraka, akaufunga ule mlango na kuwaacha waendelee na usingizi wao. akatoka haraka hadi chumbani kwao.
Huko akamkuta mumewe akiwa amejiinamia kwa mawazo tele. Mama Levina naye akaungana naye, yeye akaenda kujitupa kwenye sofa kubwa na kuyatupa macho yake juu ya dari.
Akawaza alichowaza!
Majibu hayakupatikana!
Lakini akiwa katikati ya mawazo hayo, kumbukumbu za zamani zikaanza kurejea kama sinema ya kusisimua! Akakumbuka jinsi Levina alivyomweleza kuhusu kijana wao wa kazi aliyepita, ambaye alifukuzwa baada ya kumuonesha meseji za mapenzi akimtongoza!
Ni Levina yule yule!
Iweje leo alale na kijana wa aina ile ile? Mama wa watu akawaza lakini hakupata majibu.
Hii ni laana, huu ni upuuzi mtupu, akajisemea moyoni mwake.
Lakini ghafla kuna kitu kilianza kuingia kichwani mwake kwa kasi ya ajabu, kwamba kuna uwezekano mkubwa Levina alimsingizia yule kijana wa mwanzoni ili aweze kupata nafasi ya kumuingiza yule kijana nyumbani kwao.
Hilo lilikuja kichwani mwake hasa kutokana na kukumbuka tukio la kumweleza Levina kwamba alikuwa amepata kijana mwingine kutoka Bagamoyo, akalipokea bila furaha. Lakini baadaye aliposikia kwamba kijana huyo amefiwa na alitakiwa kusafiri kwenda kwenye msiba, zikawa taarifa njema kwake na kumleta Deo!
Kila kitu kikafunguka kama sinema ya kusisimua. Akagundua uchafu wote alioufanya Levina.
Shiiit! Kumbe ndiyo maana alikuwa anafanya yote yale ili aweze kuja kufanya uchafu wake na huyu mpuuzi siyo? akawaza kichwani mwake mama Levina.
Baba Levina alikuwa kimya kabisa, hakuelewa kilichokuwa kikiendelea. Alimpenda sana mwanaye, siku zote aliamini bado alikuwa kigori, lakini kitendo cha kushuhudia uchafu wake, tena mbele ya macho yake kabisa kilimchoma sana moyo wake.
Mama Levina... baba Levina akaita.
Abee mume wangu!
Umeona?
Acha tu!
Sasa?
Sasa nini tena, zaidi ya kumtimua huyo mpumbavu hapa nyumbani?
Sawa, tulale, hili nitalimaliza mwenyewe asubuhi!
Sawa mume wangu, lakini ukweli ni kwamba sijaamini kabisa kama Levina angeweza kutuabisha kiasi hiki!
Hata mimi pia, sina amani kabisa. Nahisi kama dunia nzima inaniangalia mimi. Huyu mtoto ametuvua nguo kabisa!
Wakaamua kulala, lakini wakiwa na majonzi tele mioyoni mwao.
***
Mzee Massamu aliamka mapema sana siku hiyo, lakini kila alipokuwa akitaka kutoka nje, alijikuta miguu yake ikikataa kabisa. Alihisi alikuwa na hasira kali ambayo ingeweza kusababisha madhara makubwa.
Baada ya kujishauri kwa muda mrefu, akatoka hadi sebuleni huku akiendelea kufunga tai yake shingoni.
Akiwa sebuleni, akafungua pazia kuangalia nje, akamuona Deo akikatia majani ya fensi, akahisi moyo wake kwenda mbio sana.
Akaketi kwenye kiti, akachukua viatu vyake, akafunga kamba na kutoka nje. Alipofika mlangoni, akajikuta anasita kuinua mguu wake kupiga hatua nyingine.
Deo, akajikuta ameita.
Naam baba, Deo akaitika haraka na kukimbia alipokuwa amesimama mzee Massamu.
Shikamoo baba! akasalimia Deo.
Mar-haba bwana, mzima?
Sijambo!
Hata mimi naona hujambo! Mzee Massamu akamjibu.
Kwa mara ya kwanza alimuona mzee huyo akiongea naye kwa muda mrefu, tena maneno ambayo yalionekana kuwa na mafumbo ndani yake. Moyo wake ukapiga kambi!...Puuu!
Mchezo umeshtukiwa nini? akawaza.
Hivi hapa ndani una mke? swali hili likazidisha utata kichwani mwake.
Mke?
Kwani umekuja kuoa au kufanya kazi? Lilikuwa swali gumu kidogo kujibu. Akabaki anababaika akikosa cha kuongea.
Hivi, unajua huyu Levina nimeteseka naye kwa kiasi gani? akamwuliza tena.
Deo akanyamaza kimya.
Im talking to you! akasema kwa Kiingereza, hapo ndipo Deo hakuelewa chochote kabisa.
Deo bado aliendelea kubaki kimya.
Sikia kijana...huwa nina roho nzuri sana, lakini pia nina roho mbaya sana. Naweza kukutwanga risasi kufumba na kufumbua...naomba ndani ya dakika tano, uwe umeshaondoka hapa kwangu...haraka sana naomba ufutike!
Sawa mzee.
Ingia ndani uchukue kila kilicho chako, uondoe nuksi nyumbani kwangu! akasema Mzee Massamu akionekana kuzidiwa na hasira.
Deo akabaki anatetemeka, hakuwa na neno lolote la kuongea, kwa hali aliyoonekana kuwa nayo Mzee Massamu, kama angeongea neno lolote, angeweza kuishia kupigwa risasi na kufa pale pale. Mzee Massamu akaondoka na kuingia kwenye gari lake, hapo Deo akaingia ndani na kuchukua nguo zake, akaondoka.
Hakumuaga Levina wala mama yake. Alijua ni kiasi gani angepata matatizo kama angefanya hivyo! Akatokomea mitaani akiwa anajuta. Usiku mmoja tu, ndiyo chanzo cha matatizo yale. Alikuwa anarudi kwenye dhiki ambayo tayari alishaisahau. Anarudi kwenye maisha yake ya mitaani!
Akaikumbuka Singida!
Alitakiwa kurudi kwao Singida!
***
Alikuwa amezama kwenye kumbukumbu ambazo zilibaki kuwa historia, Deo anaumwa, risasi zimepenyeza kwenye bega lake. Hana matumaini tena ya kufunga ndoa na mpenzi wake Cleopatra. Akiwa ameyatoa macho yake pale kitandani, sasa ameweza kumkumbuka vizuri mwanamke yule mrembo aliyekuwa amesimama.
Yes, alikuwa ni Levina!
Levina Massamu!
Pole na kuumwa! Levina akatamka akimkazia macho.
Deo hakujibu!
Pole sana mwaya, kwahiyo ndoa itaahirishwa? akauliza tena Levina.
Uso wa mwanamke huyu, ulikuwa wa upole, lakini aliachia tabasamu mwanana wakati wote alipokuwa akizungumza. Tabasamu ni kitu cha ajabu sana kwa wakati huu ambao Deo anaugulia maumivu kitandani.
Anatabasamu na wakati yeye yupo kitandani? Tena na tundu la risasi begani! Moyo wa Deo ukaingiwa ubaridi, mara akajihisi kuumia sana, machozi kama maji yakaanza kumiminika machoni mwake. Punde, akamuona mpenzi wake akija uelekeo ule. Mpenzi wake mpya ambaye alikuwa bibi harusi mtarajiwa!
Cleopatra!!!
Msomaji wangu mpenzi, kama kuna mahali nimekuacha kidogo, piga simu namba 0656 819552 nikuelekeze. Hii ni simulizi tamu ambayo itakuacha na mafunzo makubwa. Usikose kuendelea nayo
USIFE KWANZA MPENZI WANGU....EPISODE.22.
Deo amefukuzwa nyumbani kwa mzee Massamu alipokuwa anafanya kazi, haijulikani alipoelekea, lakini upande wa pili anaonekana akiwa amelezwa hospitalini Muhimbili. Mbele yake amesimama mwanamke ambaye sasa amemkumbuka vizuri, ni Levina aliyekutana naye sokoni Tandale akiwa anauza mchele.
Je, baada ya Deo kufukuzwa nyumbani kwa mzee Massamu alikwenda wapi? Ilikuwaje akakutana na Cleopatra na kuamua kuachana na Levina? Kwanini waliachana na nani aliyempiga Deo risasi? Endelea kufuatilia...
DEOGRATIUS aliyakodoa macho yake akiwa hajui la kufanya, akamwangalia Levina kwa umakani, lakini akiwa na maswali mengi sana kichwani mwake. Mosi, Levina alijuaje kwamba yeye anaumwa? Nani alimpa taarifa hizo?
Hata hivyo, hayo hayakuwa maswali magumu sana, swali gumu zaidi ambalo lilimchanganya kichwa chake ni akina nani wale waliompiga risasi na kwanini walifanya hivyo?
Akiwa katika maswali hayo, anamuona mwanamke mwingine akija uelekeo wa kitanda chake akitokea mlango mkubwa wa kuingilia pale wodini. Alimfahamu vizuri sana.
Ni Cleopatra!
Macho ya Cleopatra yalikuwa na wasiwasi mwingi, lakini alipokaribia yakaonesha ukali kidogo. Ukali uliosababishwa na kiumbe kilichokuwa mbele ya kitanda cha Deo.
Levina!!!
We malaya unafanya nini hapa? Cleopatra akauliza kwa sauti ya chini lakini iliyojaa ukali.
Umeniita nani?
Malaya!
Nani?
Malaya!!! Kwani hujasikia au hutaki? Au hufahamu kwamba wewe ni malaya?
Cleopatra mimi ni malaya?
Tena mchafu!
Ok! Ahsante sana, ahsante sana mama, sikuja kwa ugomvi, nilikuja kwa ajili ya kumsalimia mgonjwa!
Mgonjwa?
Ndiyo Deo!
Anakuhusu nini Deo?
Ni boyfriend wangu wa zamani, kwahiyo sina tatizo kuja kumsalimia akipata matatizo!
Kwanza aliyekupa taarifa za Deo kuumwa ni nani? Tena haraka kiasi hicho?
Unataka kumjua?
Ndiyo!
Ipo siku utamjua, lakini kwa leo hupaswi kumjua...kwaheri...kwa mara nyingine tena Deo pole sana mwaya, najua unaumia na una maumivu mawili! Ya kuugua, lakini pia una maumivu ya kusogeza ndoa yako mbele, pole sana... akasema Levina na kuanza kupiga hatua kuondoka pale kwenye kitanda cha Deo.
Deo hakuzungumza chochote, Cleopatra naye hakuwa na la kuzungumza zaidi ya kumsindikiza kwa macho mpaka alipopotea mbele ya macho yake. Akamgeukia Deo aliyekuwa ameyatoa macho yake kwa kukata tamaa kabisa. Akapiga magoti pale na kumbusu usoni mwake.
Pole mwaya Deo wangu!
Ahsante... akaitikia Deo kwa taabu kidogo.
Unajisikiaje sasa?
Nina nafuu!
Utapona mpenzi wangu, naamini hadi siku ya ndoa yetu utakuwa umeshapona kabisa na utaweza kwenda kanisani kutimiza ahadi yetu ya muda mrefu!
Siamini Cleopatra!
Kwanini?
Nakufa Patra, nakufa mpenzi wangu!
Hapana baby, usife kwanza mpenzi wangu kabla hatujafunga ndoa yetu...subiri kidogo mpenzi wangu, unioe kwanza... akasema Cleopatra akilengwa na machozi machoni mwake.
Siamini kama nitapona mpenzi, moyo wangu una maumivu makali sana, lakini hata mwili wangu naona unauma, sioni tumaini kabisa, nakufa mpenzi wangu!
Hufi baba!
Nakufa!
Usife kwanza mpenzi wangu, nakupenda Deo!
Deo hakujibu kitu, alikuwa na mambo mengi sana kichwani mwake. Alikuwa na maumivu ya kupigwa risasi, lakini pia alikuwa na maumivu na ndoa yake na Cleopatra!
Alimkumbuka sana Levina, kila alipojaribu kukumbuka sababu ya kuachana kwao, hakuona kama alistahili!
Akazidi kulia.
Unalia nini mpenzi wangu? Cleopatra akauliza.
Maumivu mpenzi!
Pole sana!
Ahsante!
Hivi dokta ameshakuja kukuona?
Sijajua!
Namaanisha baada ya kuzinduka!
Hapana.
Ngoja niende kumwita mara moja, Cleopatra akasema na kusimama mara moja kisha kwenda ofisini kwa daktari.
Muda mfupi baadaye daktari alikuwa ameshafika kitandani kwa Deo na kuanza kumpima na kumjulia hali yake.
Pole sana Deo, unajisikiaje sasa? Dokta akamwuliza.
Kidogo nina nafuu.
Usijali, kilichotokea ni mshtuko tu, hujaumia sana, utakuwa sawa wala usiwe na hofu!
Lakini dokta kama nilivyokuambia, wiki tatu zijazo tunafunga ndoa, anaweza kuwa ameshapona kabisa?
Bila shaka, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu, maadamu yupo chini yetu, kila kitu kitakuwa sawa, kikubwa ni kumuomba Mungu tu!
Ahsante sana, naweza kumpa chakula kwa sasa?
Umemletea nini?
Ndizi nyama!
Sawa, lakini hakikisha anakula chakula laini na chenye kumpa hamu ya kula. Unaweza kumpa.
Ahsante Dokta.
Dokta Pallangyo akaondoka zake na kumuacha Cleopatra akiwa na mgonjwa wake. Akatayarisha chakula na kuanza kumlisha kwa upendo.
Nakupenda sana Deo wangu, sipo tayari kukupoteza katika maisha yangu, usijali utapona!
Ahsante mpenzi wangu kwa kunipa moyo!
Muda wa kuwaona wagonjwa ulipoisha, Cleopatra alitakiwa kuondoka na kumuacha Deo peke yake, jambo ambalo lilimuhuzunisha sana. Moyo wake uliumizwa sana na jambo hilo, lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kuondoka!
Nitakuja kukuona mpenzi wangu, ugua pole na ulale salama.
Ahsante, msalimie mama!
Sawa, nitamsalimia.
Akaondoka.
***
Macho yake yalikuwa yanagoma kufumbuka kabisa, alihisi kama yanauma kwa mbali, hata hivyo hakuwa na tatizo la macho, alikuwa na tatizo la bega, lakini macho yake yalikuwa yakipambana na nuru ya asubuhi baada ya kuzoea giza kwa usiku mzima.
Akajilazimisha kuyafumbua, akayafumbua kwa tabu kidogo. Alipofumbua tu, akakutanisha macho yake na sura ambayo haikuwa ngeni kwake hata kidogo. Alimfahamu vizuri sana msichana aliyekuwa amesimama mbele yake.
Alikuwa ni Levina!
Habari za asubuhi Deo? Samahani nimekuja kukusalimia, nimefika mapema sana hapa, lakini sikuona sababu ya kukusumbua katika usingizi, ndipo nikaamua kukusubiri uamke mwenyewe...pole sana, akasema Levina akiweka uaridi jekundu mezani kwa Deo.
Ahsante Levina!
Unajua kwanini nimekuja mapema yote hii?
Deo hakujibu kitu, alitingisha kichwa kuashiria kwamba hakujua sababu.
Nilitaka kuwa wa kwanza kuijua hali yako baada ya kuamka leo, lakini pia nilitaka kukuthibitishia kwamba huyo Cleopatra wako hakupendi kama anavyokudanganya, kama angekuwa anakupenda asingeweza kulala usingizi ukiwa wewe unaumwa, alipaswa awahi kukuona...upo hapo? Akasema Levina akimwangalia Deo usoni.
Deo hakujibu kitu!
Akabaki anashangaa, akiwa katika hali ya mshangao huo, akamuona Cleopatra akiwa anaingia wodini. Sekunde chache baadaye alikuwa amesimama mbele yake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia