Ushauri; Uwiano Wa 30:10:3:1 Ni Kanuni Inayotumika Kununua Nyumba Za Kupangisha Zenye Faida Mikoani

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Kununua nyumba ya uwekezaji linaweza kuwa jambo rahisi sana wakati ambapo una mtaji fedha wa kutosha kununua nyumba unayotaka. Lakini kuuza nyumba ambayo huitaki inachukua miezi mingi mpaka miaka kadhaa.

Kwa kutumia kanuni hii ya uwiano ninakuonyesha jinsi unavyoweza kununua nyumba ya uwekezaji ambayo inatengeneza kiasi kikubwa cha faida au kipato endelevu.

Hii ni kanuni ambayo inawatofautisha wawekezaji wa kawaida na wawekezaji makini wanaojenga mafanikio makubwa sana kupitia ardhi na majengo.

Kwa kanuni hii ya uwiano wa namba utaweza kufanikiwa kwenye mambo yafuatayo;-

✓ Kumiliki kiwanja chenye thamani na kinacho ongeza thamani kubwa kila mwaka.

✓ Kumiliki mashamba ya kukodisha yenye manufaa makubwa.

✓ Kumiliki ardhi inayopanda thamani kwa ajili ya kuuza miaka 10, 15, 20, 25 ijayo.

✓ Kumiliki nyumba za kupangisha zenye kipato kikubwa kila mwezi.

✓ Kupata uzoefu wa uwekezaji majengo ndani ya muda mfupi tu.

✓ Kuweka shabaha kwenye mambo ya msingi ya kuchagua nyuma ya uwekezaji.

✓ Kufahamu hali ya soko mahalia la ardhi na majengo ndani ya miezi michache tu.

✓ Kufahamu hali ya uchumi mahalia unavyoweza kuathiri uwekezaji wako.

Kanuni Ya Uwiano Ya Kwenye Majiji.

Kwenye majiji makubwa ambayo uwekezaji kwenye ardhi na majengo umekua kanuni hii haina ufanisi mkubwa. Kuna kanuni nyingine ambayo inaweza kukusaidia kumiliki nyumba au ardhi yenye faida kubwa kwa majiji kama Dar Es Salaam.

Siku nyingine nitakushirikisha kanuni hiyo na jinsi inavyoweza kukusaidia wewe rafiki yangu mpendwa. Tuendelee na uwiano wa kanuni ya kununua nyumba mikoani.

Programu Ya Siku 30.

Hii ni programu ya siku thelathini (30) tu. Ni programu ya kutokwa jasho haswa. Jasho linaweza kukutoka wewe au dalali wako wa ardhi na majengo. Hakuna mafanikio makubwa utakayopata kupitia kanuni hii ya uwiano pasipo kufanya kazi kwa bidii.

Maelezo Ya Uwiano Wa Kanuni Yenyewe Ya 30:10:3:1

Namba 30; Nyumba 30/Viwanja 30.

Hizi ni nyumba ambazo unatakiwa kupata na kuzitathmini juu juu tu. Hapa unafanya utathmini wa awali kuhusu ardhi au nyumba unayotaka kununua.

Pia, utakuwa unafanya ukaguzi wa awali wa ardhi au nyumba unayotaka kununua. Ukaguzi huu hauhusishi kutembea eneo la ardhi au nyumba moja kwa moja.

Namba 10; Nyumba 10/Viwanja 10.

Hapa unaandika muhtasari wa ukaguzi wa ardhi au nyumba unayotaka kununua kwa ajili ya uwekezaji. Nyumba hizi 10 zinatokana na nyumba zile 30 kutoka kwenye orodha ya hapo juu.

Ni muhimu sana kuorodhesha bei ya mauzo, tarehe ya kuanza kutangaza, ukubwa wa ardhi au nyumba kwa mita za mraba na taarifa nyingine za msingi.

Namba 3; Nyumba 3/Viwanja 3.

Hizi ni nyumba tatu ambazo zimekidhi vigezo vyako vyote vya uwekezaji kwenye ardhi na majengo. Kwa kutumia vigezo vyako unapata nyumba tatu tu kutoka kwenye nyumba 10 za hapo juu.

Unatakiwa kuandika ripoti nzuri ya ukaguzi na ripoti ya tathmini ya hali ya uwekezaji kwenye nyumba hizo 3. Hizi ndizo nyumba zinazofaa kwa ajili ya uwekezaji utakaokufanya ujenge mafanikio makubwa.

Namba 1; Nyumba 1/Kiwanja 1.

Hii ni nyumba unayoweza kuilipia sasa. Hii ni nyumba ambayo muuzaji wake amehamasika kuliko wauzaji wengine wa nyumba mbili (2) zinazobaki hapo juu.

Nyumba hii ni ile yenye kasoro zinazohitaji ukarabati na maboresho ili uiongezee thamani kubwa. Hii ndiyo nyumba inaweza kukupatia utajiri kwa kuingiza kipato endelevu cha kila mwezi.

Mahitaji Ya Uwiano Wa Kanuni Hii.

Moja.

Maarifa ya kutathmini ardhi au nyumba.

Hapa unatakiwa kuwa na maarifa ya kusoma hali ya masoko mahalia ya ardhi na majengo. Kwa kuwa uwekezaji huu huathiri na hali ya soko mahalia ni muhimu sana kufahamu jinsi ya kutathmini soko mahalia la ardhi na majengo.

Hapa unaweza kutumia mambo yafuatayo kufanya tathmini;-

✓ Taarifa kutoka kwenye idara za ardhi za halmashauri yako.

✓ Historia ya jumla ya gharama za ujenzi kwenye mtaa unaotaka kumiliki nyumba.

✓ Historia ya upandaji wa thamani wa ardhi au majengo kwenye kata au jimbo unalotaka kuwekeza.

✓ Uwepo wa miradi mikubwa ya biashara, kilimo na uwekezaji kwenye kata au mtaa unaotaka kuwekeza.

✓ Uanzishwaji wa miradi mipya inayobadili kabisa hali ya masoko ya ardhi na majengo. Kubadili kutoka hali mbaya kwenda hali nzuri ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

✓ Sera za zamani na za sasa za serikali za mitaa na serikali kuu kuhusu eneo unalotaka kununua ardhi au nyumba.

Mbili.

Muda wa kutathmini ardhi au nyumba.

Hapa unatakiwa kuandika ripoti ya makisio ya mapato na matumizi ya nyumba unayotaka kununua. Kwa nyumba zisizohamishika za kupangisha unatakiwa kutumia kanuni ya 2%.

Kwa nyumba zinazohamishika unatakiwa kutumia kanuni ya 4% kufanya tathmini itakayokuwa na tija kwako na kwa timu yako ya uwekezaji.

Tatu.

Maarifa sahihi na uzoefu wa kuandika ripoti za ukaguzi wa ardhi au nyumba.

Ripoti ya ukaguzi wa nyumba au kiwanja inatakiwa kuandika kwa mpangilio mzuri. Unaweza kutumia ripoti zilizoandaliwa mapema ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

Nne.

Maarifa sahihi na uzoefu wa kukagua ardhi au nyumba.

Ukaguzi wa ardhi au nyumba ndio jambo kubwa linalobebwa na mchakato wa kununua nyumba au kiwanja. Ukishindwa kukagua ardhi au nyumba ipasavyo hutaona manufaa ya uwiano wa kanuni hii nzuri.

Utatakiwa kukagua hati na mikataba yote inayohusiana na umiliki wa ardhi au nyumba unayotaka kununua. Utatakiwa kukagua usalama na ubora wa mazingira kuzunguka ardhi au nyumba unayotaka kununua.

Utatakiwa kukagua ubora wa ujenzi wa nyumba unayotaka kununua. Zoezi hili linaambatana na uandishi wa ripoti nzuri ya ukaguzi wa ardhi au nyumba.

Tano.

Chanzo cha uhakika cha mtaji fedha.

Hakikisha una mtaji fedha tayari ya ajili ya kukamilisha manunuzi ya kiwanja au nyumba yako. Kama huna mtaji fedha na upo kwenye mchakato wa kutumia kanuni hii itakuchosha na kutokuona manufaa yoyote.

Pia, unaweza kutumia kanuni hii kupata nyumba ya uwekezaji ambayo unataka kuiandikia MPANGO MKAKATI wa kuombea ubia au mkopo wa majengo.

Sita.

Timu yako ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Dalali wa ardhi na majengo, mshauri mbobezi kwenye ardhi na majengo na wakili ni wanatimu muhimu sana unaotakiwa kuwa nao wakati wa kununua ardhi au nyumba kwa kutumia uwiano wa kanuni hii.

Saba.

Vigezo vya uwekezaji wako.

Huu ni ufupisho wa mwongozo wa kumiliki ardhi au nyumba yenye manufaa kwako kulingana na malengo yako makubwa ya kiuwekezaji.

Mfano; ninanunua kiwanja kilichopimwa, kisiwe na hati ya hakimiliki, kiwe halmshauri ya Rungwe, kiwe mita 500 kutoka stendi kuu ya wilaya, kiwe kinauzwa na muuzaji aliyehamasika na kiwe kinauzwa kwa shilingi milioni mbili (2) au pungufu.

Huu ni mfano wa vigezo vyangu vya kununua kiwanja kwa ajili ya uwekezaji kwenye nyumba za kupangisha.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

Mbobezi wa ardhi na majengo.

Mawasiliano; +255 752 413 711

BLOG; UWEKEZAJI MAJENGO
 
Back
Top Bottom