Najaribu kuangalia nguvu kubwa inayotumiwa na Kamati ya Mazishi, kuonyesha ni jinsi gani Rais John Joseph Magufuli alivyokuwa akipendwa na wananchi. Ameagwa Dar es Salaam kwa siku mbili, akapelekwa Dodoma kwa siku moja kwa kigezo cha kutimiza ndoto za Nyerere kuifanya kuwa Makao Makuu. Akarushwa tena hadi Zanzibar kwa kigezo cha sehemu ya Muungano, akapelekwa Mwanza na hatimaye Chato.
Mtu mmoja mkubwa tu nchini hapa amesikika akiudanganya umma kuwa zaidi ya nusu ya watu duniani walitazama tukio la kuagwa kwake lililofanyika pale Dodoma. Sasa najiuliza, hivi kama shujaa halisi wa Afrika, Mwalimu Julius Nyerere angekuwa ni mpenda promo namna hii, mwili wake si ungekaa mwezi mzima ukizungushwa bara zima la Afrika ili aagwe? Maana licha ya kufikishwa katika mikoa yote Bara na Visiwani, angepelekwa Addis Ababa, Makao Makuu ya AU, maana yeye ndiye muasisi wa umoja ule.
Angepelekwa Maputo, Windhoek, Lusaka, Harare, Gaborone maana huko kote alizisaidia nchi hizo kupata Uhuru wakiwa na Base yao Tanzania. Wana Kamati ya mazishi yake wangempeleka pia Johannesburg kwa sapoti kubwa iliyopewa Afrika Kusini.
Lazima wangempeleka Kampala ambako aliwasaidia Waganda kumng'oa Idd Amin. Na bila shaka angepelekwa pia Tripoli, ambako Nyerere aliwarejesha mateka wa vita waliokuja kumsaidia Idd Amin vitani.
Ni lazima pia angepelekwa Burundi, Rwanda na DRC maana kwa miaka mingi tumewahifadhi wakimbizi wao katika ardhi yetu na baadhi yao walipewa hadi Uraia.
Sasa huyu wa kwetu tunamuita shujaa wa Afrika kwa lipi? Mbona tunajiongopea wenyewe?
Tupunguze promo, uacheni uhalisia uchukue nafasi yake, hata ndani ya CCM kuna watu wanafurahia kifo chake, sembuse wananchi wa kawaida?