Annael,
Pole sana kwa matusi yanayozidi kuwa utamaduni wa kawaida wa hapa JF (lakini ni baadhi ya mashabiki wa chama fulani), itabidi uyazoee.
Laiti JF tungejitahidi kuujadili ukweli kama ulivyo, pengine tungekuwa na mchango wa kulielekeza taifa letu katika suluhu. Huko kutofautiana kwa Mwalimu na Mzee Mtei ni kweli kulitokea (Soma kitabu cha Mtei mwenyewe; From Goatherd to Governor). Katika kitabu hicho Mtei anaeleza hilo suala la masharti ya IMF. Hao jamaa walitaka fedha ya Tanzania ishushwe thamani, viwanda na mashirika ya umma tuuze, tupunguze pesa tunazotumia katika sekta ya elimu, n.k. Mtei akakubaliana nao, maana wakati huo uchumi wa nchi ulikuwa unayumba si pole pole, na ili IMF watupe msaada wa kifedha 'kutuokoa' (bailout) ndio wakaja na masharti hayo. Mtei akayakubali, ila yeye alikuwa waziri tu wa fedha, ikabidi aende kwa mkuu wa kaya, ambaye aliwatolea nje, na akamwambia Mtei, 'Tanzania haitatawaliwa kutokea Washington, na hela yetu hatushushi ... over my deadbody' Kesho yake Mtei akajiuzulu.
Lakini hali ya uchumi ikaendelea kuwa ovyo, hatimaye Mwalimu akang'atuka. Akaja Mzee ruksa, asijue afanye nini na hiyo hali, ndipo ikabidi awakubalie IMF, tena kwa namna fulani akamtumia huyo huyo mzee Mtei kwa kumtuma awe mwakilishi wa Tanzania katika makao ya IMF Marekani. Kwa hiyo sera za kubinafsisha zilianzia hapo, Mkapa alikuja kuintensify tu. (Hapa utaelewa kwa nini watu wanasema CCM halisi, ile ya kijamaa iliondoka na Mwalimu)
Hatimaye Mzee Mtei akiwa amekwishashiba mambo ya IMF na Benki ya Dunia, na akiwa anajua fika matatizo yetu kiuchumi yalikoanzia, uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi nchini, ndipo yeye na wenzake wakaanzisha chama chenye mtazamo huo uliousema.
Turejee nyuma kidogo, kwa nini uchumi uliyumba hadi ikabidi IMF waje kutuwekea 'dhamana'? Sababu ni nyingi; 1. Vita vya Kagera (tumlaumu Mwalimu?) 2. Kupanda kwa bei ya mafuta ulimwenguni (tulaumu mfumo wa uchumi wa dunia?) 3. Ufisadi wa waliopewa dhamana ya kuendesha mashirika ya umma (hapa tujilaumu sisi wenyewe watanzania kwa tabia ya kutafuna kama mchwa, na kutothamini bidhaa zetu wenyewe).
Jambo jingine tujiulize; je, dhamana ya IMF imesaidia? Hata kidogo, tena ndio imefanya mambo yakawa mabaya zaidi.
Ndio maana nikasema, kama JF yaweza kuwa jukwaa la msaada kwa Tanzania, inabidi iwe sehemu ya kutafuta njia ya tunachomokaje katika udhaifu wa nchi kiuchumi ambao wahuni wa magharibi wameutumia kwa kutulaghai kwamba wanatusaidia kumbe ndio wanatuharibia zaidi.