Umepiga ‘Kenchi’ kweli, au Umepigwa? Hivi ndivyo Wateja wa Mbao wanavyotapeliwa Mitaani

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Natembea kuelekea Buguruni, eneo linaloitwa Binti Madenge. Mahala hapa kuna utitiri wa wafanyabiashara wanaouza mbao, huku wengine wakifanya kazi ya kuingiza mbao kwenye mapipa.

Ninavutiwa na hao wanaoingiza mbao kweye mapipa marefu yenye maji maji ya rangi ya kijani. Najiuliza kwa nini wanafanya hivyo? Hayo maji ya rangi ya kijani yana kazi gani?

Ninaposogea jirani, namwona kijana mmoja eneo hilo akitazama kazi inavyoenda. “Habari yako,” namsalimia. “Samahani naomba kuuliza, kwa nini mbao zinatumbukizwa kwenye hayo mapipa yenye maji?”

Ananisogelea huku naye akinihoji: “Kwa nini unaniuliza maswali?”

Ninamuelewesha kuwa mimi ni mteja, natafuta mbao za kenchi. Nataka tu kujua nauziwa nini. Kijana yule ananitazama, kisha ananivuta pembeni, ananinong’oneza: “Unamuona yule pale anachofanya? Anachukua hizo mbao maalum kwa kenchi, anazitumbukiza kwenye maji yaliyochanganywa na rangi ya ukindu ya kijani.

Ukindu ni jani linalotokana na mmea uitwao mkindu, kutoka katika jamii ya mitende. Jani hili hutumika kusukia kili za kushonea mikeka, vikapu, kawa na bidhaa nyingine kama hizo.

Watengengezaji hutumia rangi mbalimbali, ikiwemo rangi ya kijani, kutia nakshi kili zao ili bidhaa wanazoshona zivutie wateja.
Sasa katika mazingira haya ya mbao za kenchi, najiuliza, hivi rangi ya ukindu inahusikaje?

Kama vile ameusoma mshangao kichwani mwangu, mwenyeji wangu, ambaye jina limesitiriwa kwa usalama wake, ananifafanulia: “Rangi ya ukindu ya kijani inafanana na Tanalith C (ambayo) ni dawa inayotumika kupika mbao kuzuia zisipekechwe na wadudu, wakiwemo mchwa.”

Kumbe nilichokutana nacho hapa kwa Binti Madenge ni utapeli.

Mwenyeji wangu ananiambia wafanyabiashara wengi wa mbao siku hizi huwahadai wateja kuwa wanawauzia mbao zenye dawa, kumbe hazina chochote: zimewekwa tu rangi ya ukindu.

Wateja, haswa wanaofanya ujenzi, wanaaminishwa mbao hizo zimekidhi viwango, pasipo kujua kuna uwezekano zikapekechwa ama kuoza, zikihatarisha makazi yao na kuwatia hasara kubwa.
Mwenyeji wangu naye pia yumo katika biashara hiyo hiyo, akiuza mbao zilizopikwa kwenye banda jirani tu.

Huenda ndiyo maana anakataa kabisa nisitumie jina lake. “Usinitaje jina, sitaki kuingia kwenye mgogoro na wanaofanya vitendo hivi hapa Buguruni,” anasisitiza.
Tumefikaje Hapa?

Ili kuelewa tumefikaje hapa, ambapo wateja wanatapeliwa kwa kubambikwa mbao zisizo na dawa hadharani, Mwananchi inazungumza na Abbas. Naye amejikita katika biashara hiyo hiyo ya mbao.

Abbas ananieleza matumizi ya rangi ya ukindu kuchakachua mbao za ujenzi yalipamba moto kuanzia mwaka 2020 kutokana na kuadimika kwa dawa ya Tanalith C kufuatia mlipuko wa Uviko-19.

Baada ya nchi mbalimbali kufunga mipaka yake ili kudhibiti Uviko-19, upatikanaji wa Tanalith C inayotengenezwa nchini Uingereza ulikuwa mgumu.

Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wafanyabiashara kubuni njia mbadala ya kuwaaminisha wateja kuwa mbao wanazonunua zimewekewa dawa. Hapo ndipo wakaona rangi ya ukindu ya kijani inafaa.

Utapeli huo umekithiri sana katika maeneo ya Mwenge, Buguruni, Manzese na Tandale jijini Dar es Salaam, na Mafinga mkoani Njombe, anasema Abbas.

“Mbao hizi dadangu hawauziwi wananchi tu, hata serikali imeshaingia mkenge,” anasemba Abbas.

“Kwa mfano mwaka 2021, ilinunua mbao za kenchi (2 kwa 6) zaidi ya 4,000 hapa Buguruni, zote zimewekewa rangi hiyo. Halafu mbao hizi zimeshatumika kupaua madarasa ya shule mbalimbali hapa Dar es Salaamu kupitia hela zile za Uviko – 19.”

Mwananchi haijaweza kuthibitisha madai ya Abbas kuhusu serikali nayo ‘kupigwa’ na wauza mbao, ingawa anasisitiza italazimika kuezua mapaa na kupaua upya majengo yaliyotumia mbao hizo kwani hazitadumu “zaidi ya miaka mitano” bila kupekechwa na wadudu.

Wito wake kwa mamlaka husika na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali? Wafike maeneo husika na wafuatilie uwekaji wa dawa kwenye mbao hasa zile zinazopelekwa kwenye miradi ya huduma za kijamii kama zahanati na shule.

Mamlaka Ziko Wapi?

Mwananchi imezungumza na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga, aliyetuambia kuwa suala hilo wanalifuatilia, ingawa hawezi kusema lipo bila ya kulifanyia uhakiki.

Dawa za kutibu mbao zinafahamika na wafanyabiashara wa mbao wanajua usipotumia dawa husika mbao zinaoza, amekumbusha Msasalaga, akisisitiza kama kuna malalamiko, utaratibu wa kuyatoa ufuatwe.

“Si kwamba mtu akishasema basi iwe kweli, kuna watu wanasema lakini hawana uhakika na hilo jambo, hivyo mtu mwenye malalamiko anashauriwa aje hapa ofisini kuna kitengo cha malalamiko. Suala hili ni la kulifuatilia huwezi ukalizungumza bila ya kulifanyia kazi.”

Msasalaga anasema ikibainika ni kweli, sheria zipo, na zinaelekeza hatua gani zichukuliwe dhidi ya wale ambao wanakwenda tofauti na utaratibu uliowekwa.

Anaongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi na kuvifuatilia viwanda vinavyotumika kutibu mbao, hivyo mtu anaweza akawa analalamika kuna shida, lakini anatakiwa aelekeze tatizo lipo wapi na maeneo gani.

“Kama kuna mtu anafanya tofauti tunapokwenda eneo husika, tunaangalia jinsi gani wanavyofanya, wanatumia kitu gani kuweka kwenye mbao hizo na kinatakiwa kitumike kitu gani, lakini kwa sasa siwezi kutoa majibu ya moja kwa moja hadi tuthibitishe,” amesisitiza.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko ameiambia Mwananchi kuwa ofisi yake itafanya uchunguzi wa kina wa changamoto hii ili wanapotoa majibu, yawe ya uhakika.
Kwa Nini Ulaghai Unaendelea?

Hali ya upatikanaji wa Tanalith C hivi sasa si mbaya kama ilivyokuwa katika kilele cha mlipuko wa Uviko-19 mnamo mwaka 2020/21, wakati minyororo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ilipovurugika.

Fursa zimefunguka, huku biashara zikiaanza kurejea katika mfumo wa kawaida. Hata hivyo, Tanalith C, kama bidhaa nyingine nyingi, nayo imeathiriwa na mfumuko wa bei.

Innocent Halfan, anayeuza mbao Buguruni, ameiambia Mwananchi kuwa Tanalith C imekuwa ghali, hivyo kupelekea wafanyabiashara waendelee kutumia rangi ya ukindu ya kijani kuhadaa wanunuzi wa mbao za ujenzi.

Dumu moja la lita 20 la dawa ya Tanalith C linauzwa Sh750,000 na mbao moja inapoingizwa kiwandani, inalipiwa kulingana na urefu au unene kuanzia Sh600 hadi Sh1,000, anasema Halfan.

Wafanyabiashara wengi hushindwa kumudu gharama hizo.

“Ndiyo maana wakabuni utapeli huu, japokuwa upo tangu zamani, lakini sasa hivi baada ya janga la Uviko 19 ndiyo umezidi.”

Pakiti moja ya rangi ya ukindu huuzwa Sh2,000, huku mchuuzi wa mbao akitakiwa kulipia kati ya Sh300 mpaka Sh400 kwa ubao mmoja kulingana na ukubwa, ili ulowekwe katika maji ya rangi ya ukindu ya kijani.

Anaeleza Halfan: “Pakiti moja ya rangi ya ukindu ya Sh2,000 unaweka mbao 2,000 – ukiwa na pakiti mbili unaweka mbao 4,000 – (wakati) kwa upande wa dawa ya kuzuia wadudu (ya) Tanalith C dumu la lita 20 unaweka mbao zisizozidi 4,000.”

“Mbao zilizowekwa dawa zenye urefu wa 2 kwa 4 zinauzwa Sh7,000, na mbao ya 2 kwa 2 inauzwa Sh3,500 na 2 kwa 6 inauzwa Sh9,000. Lakini zilizopakwa rangi ya ukindu 2 kwa 4 inauzwa Sh4,800 huku ya 2 kwa 2 ikiuzwa Sh2,700 na 2 kwa 6 Sh6,000,” anasema.

“Mteja anayekuja kununua mbao zilizowekwa rangi ya ukindu akija kichwa kichwa, mbao ya 2 kwa 4 atauziwa Sh7,000 ambayo ni bei ya mbao zilizowekwa dawa, lakini akiomba kupunguziwa anapunguziwa hadi Sh5,000 au Sh4,800,” anafafanua.

Mfanyabiashara huyo amesema wateja wengi wanapenda bei nafuu, hivyo hawako tayari kununua mbao ya 2 kwa 6 yenye dawa kwa Sh9,000 kama wanaamini kuna sehemu wataipata kwa Sh 4,800.

Mfanyabiashara mwingine wa Manzese, Andrew Sichawa ameieleza Mwananchi kuwa mbao zinatakiwa zipelekwe kiwandani ili ziwekwe dawa ya Tanalith C ambayo inaingia hadi ndani.

Dawa hiyo hairuhusiwi kuchanganya kwenye maji kwa kutumia mikono kwani inababua ngozi, na muandaaji anapaswa kuvaa barakoa anapoichanganya ili kuzuia kuvuta sumu kwa kupitia pua na mdomo.

“Hii dawa kwa ajili ya kuzuia mbao zisishambuliwe na wadudu inatakiwa ichanganywe kwenye viwanda maalumu, huwezi ukachukua dawa ya Tanalith C, unaiweka kwenye pipa la maji kisha unaloweka mbao na kuzitoa, lazima ikuletee madhara,” anasema Sichawa.

Mmiliki kiwanda kilichopo Mwenge aliyeomba jina lake lihifadhiwe ameiambia Mwananchi idadi ya wauza mbao wanaopeleka bidhaa hiyo kiwandani kwake kuwekewa dawa inapungua kila kukicha.

“Hii biashara imeshaingiliwa, siku hizi wanaloweka mbao kwenye maji ya rangi ya mkeka, ikitoka pale kama huna uelewa, utadhani imetiwa dawa lakini siyo.”

“Mbao tunazoweka dawa tunachaji moja Sh600 hadi Sh1,000 kulingana na urefu na unene, lakini ile ya rangi (muuzaji) analipia Sh300 hadi 400,” anasema. “Tamaa yao inawaingiza wateja wao kwenye hasara kubwa.”

Manase Isaya, anayefanya biashara ya mbao eneo la Mwenge, anadai kuna tatizo la wao kuuziwa mbao ambazo miti yake haikukomaa hasa zitokanazo na mti wa “saplasi” ambazo pia hutumika kutengenezea kenchi.

Alisema mbao hizo ndizo haswa zinazolowekwa kwenye maji ya ukindu ili zisitambulike. “Unajua mti wa saplasi mpaka uvunwe unatakiwa ufikishe miaka 18, lakini wakulima wengi siku hizi wanavuna ikiwa na miaka mitano au sita, jambo linalochangia kuliwa haraka na wadudu,” alisema Isaya.

Masaibu ya Waathirika

John Konga ni mmoja wa wahanga wa ulaghai huo. Konga, mkazi wa Chanika, ameiambia Mwananchi kuwa Machi mwaka 2022 alinunua mbao zaidi ya 100 eneo la Buguruni na alifanikiwa kupaua, lakini mwanzoni mwa mwaka huu aliamua kuongeza ukubwa wa sebule.

Hivyo akakubaliana na fundi wake, Rashid Ngonyani, aliyemwelekeza mbao watakazotumia zikiwemo zilizopauliwa na alielezwa aongeze mbao za 2 kwa 4 nane na za 2 kwa 2 saba.

Hata hivyo, baada ya fundi Ngonyani kuezua bati ili kuanza kazi, akakuta mbao zote zimeliwa na wadudu. “Hapa nilipo nimechanganyikiwa,” anasema Konga.

“Nimenunua mbao zinazoonekana zina dawa lakini kinachonishangaza mbao zimeliwa na wadudu – na kila mbao ya 2 kwa 4 nimenunua Sh7,500 na 2 kwa 2 nilinunua Sh3,500 pale Buguruni.”

Mbao hizo hazina hata mwaka na zimeshaoza, anasema Konga. Hapo ndipo alipobaini amebambikiwa. “Fundi ameniambia ninunue tu mbao nyingine, nimejikuta naingia gharama zaidi.”

Ngonyani pia ameshauri kwa baadhi ya mbao, yatafutwe mafuta machafu yapakwe ili zisiendelee kupekechwa na wadudu.

Mkazi wa Zingiziwa, Isaya Robert naye yamemkuta. Ana nyumba ya vyumba vitatu aliyoiezeka bati mwaka 2021.

Mwaka jana (2022) alibaini baadhi ya mbao zimeshapekechwa na wadudu, akaamua kutafuta mtu apake mafuta machafu kwenye mbao zote ili zisiharibike zaidi.

“Utakuta mtu amenunua mbao zinazoonyesha zimewekwa dawa, lakini kabla hazijapigiliwa juu anaziweka mafuta machafu akihofia kupata hasara kama wengine ilivyowatokea,” alisema.

Robert aliziomba mamlaka husika kufuatilia suala hilo kwa kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiwaingiza hasara wakiwaaminisha kuwa wameweka dawa ya kutibu mbao, kumbe wameweka rangi ya ukindu.

Fundi wa kupaua nyumba kutoka Buguruni, Daud Mallya amesema amekutana na changamoto ya mbao ‘zilizopigwa’ maji ya rangi ya ukindu kwa wateja wake wanne ndani ya miaka mitatu iliyopita.

Hivi karibuni, mmoja kati yao alimpa kazi ya kuongeza ukubwa wa vyumba viwili vya nyumba iliyopo eneo la Gongolamboto. Wakati anatoa mabati alishuhudia mbao kumi za kenchi zimeshambuliwa na wadudu hao.

“(Na hiyo) ilikuwa (kwa vile) vyumba viwili tu – nilivyoangalia kwenye vyumba vingine kwa haraka niliona mbao kama sita zimeoza kutokana na kushambuliwa na wadudu,” anasema Mallya.

Anamalizia: “Kwa kweli tutegemee ndani ya miaka mitano kutakuwa na malalamiko mengi (zaidi) kutoka kwa wananchi.”

MWANANCHI
 
Baada ya kupigwa kwa kununua mbao za rangi ya ukindu na ukiwa ushaweka kenchi,kuna suluhisho lingine kuokoa hizo mbao au ni kubadilisha mbao zote?
Hapo kuna Muhanga mmoja kasema alipotaka kuongeza ukubwa wa sebule alipofumua bati alikuta mbao zimeanza kuliwa na wadudu ilibidi apake mafuta machafu kupunguza athari hiyo,nadhani ukiwahi kabla hazijaliwa sana unaweza kuokoa kwa kupaka mafuta machafu.
 
Back
Top Bottom