Wapaka mbao rangi kuhadaa wateja

Azniv Protingas

JF-Expert Member
Oct 29, 2020
264
405
lumber.shortage.stock_-1.jpg

Natembea kuelekea Buguruni eneo la Binti Madenge. Hapa nakutana na wafanyabiashara wanaouza mbao na wengine wakifanya kazi ya kuingiza mbao ndani ya mapipa. Navutiwa na kazi ile, nikitaka kujua ni kwa nini wanatumbukiza mbao ndani ya yale mapipa marefu yenye maji ya rangi ya kijani.

Nikasogea zaidi, nikaamua kumuuliza kijana aliyekuwa eneo hilo naye akishuhudia kazi ile inavyoendelea. “Habari yako, samahani naomba kuuliza, kwa nini mbao zinatumbukizwa kwenye hayo mapipa yenye maji? Ni swali nililomuuliza yule kijana.” Akanisogelea naye akaniuliza swali, kwa nini umeuliza? Nikamjibu nataka kujua tu, maana natafuta mbao za kenchi, ninunue. Yule kijana alinivuta pembeni akaanza kunisimulia kwa nini anatumbukiza mbao kwenye yale maji yaliyowekwa kwenye mapipa.

“Unamuona yule mtu pale anachofanya? Anachukua mbao ambazo ni maalumu kwa kenchi, anaingiza kwenye maji yaliyochanganywa na rangi ya ukindu ya rangi ya kijani inayofanana na dawa ya Tanalith c, inayotumika kupika mbao, ili zisiliwe na wadudu wakiwamo mchwa,” alisema.

Kijana huyo anayefanya kazi kwenye banda moja eneo hilo linalouza mbao zilizopikwa na ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini kwa usalama wake, alisema wafanyabiashara wengi wa mbao hivi sasa wanawadanganya wateja wao kuwa wanauza mbao zenye dawa, lakini kweli ni kuwa huziweka rangi ya ukindu. “Usinitaje jina, sitaki kuingia kwenye mgogoro na wanaofanya vitendo hivi hapa Buguruni,” alisisitiza kijana huyo.

Ili kupata undani zaidi wa hilo, Mwananchi ilizungumza na mfanyabiashara mwingine eneo hilo la Buguruni aliyejitambulisha kwa jina moja la Abbas, aliyesema mtindo wa kuweka rangi ya ukindu kwenye mbao ulianzishwa mwaka 2020.

Alisema hiyo ni baada ya mipaka ya nchi mbalimbali kufungwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19.Amesema kutokana na janga hilo, dawa aina ya Tanalith C inayotengenezwa nchini Uingereza maalumu kwa kutibu mbao, iliadimika, ndipo baadhi ya wafanyabiasha wakabuni njia ya kuweka rangi ya ukindu kwa lengo la kuwaaminisha wateja kuwa mbao zao zina dawa.

Abbas aliyataja maeneo ambayo mchezo huo umekithiri kuwa ni pamoja na Mwenge, Buguruni, Manzese, Tandale, Jijini Dar es Salaam na Mafinga mkoani Njombe. “Mbao hizi dadangu hawauziwi wananchi tu, hata Serikali imeshaingia mkenge. Kwa mfano mwaka 2021, ilinunua mbao za kenchi (2x6) zaidi ya 4,000 hapa Buguruni, zote zimewekewa rangi hiyo. Halafu mbao hizi zimeshatumika kupaua madarasa ya shule mbalimbali hapa Dar es Salaamu kupitia hela zile za Uviko – 19,” alieleza.

Abbas alisema ni wazi Serikali imeshaingia hasara kubwa kwa kuwa mbao hizo hazitadumu zaidi ya miaka mitano, kwani zitakuwa zimeshashambuliwa na wadudu kama mchwa, hivyo itawalazimu waezue mapaa na wapaue upya.

Aliziomba mamlaka husika na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wafike maeneo husika wafuatilie uwekaji wa dawa kwenye mbao hasa zile zinazopelekwa kwenye miradi ya huduma za kijamii kama zahanati na shule.

TBS Kufuatilia
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga alisema dawa za kutibu mbao zinafahamika na wafanyabiashara wa mbao wanajua usipotumia dawa husika mbao zinaoza, hivyo suala hilo wanalifuatilia ingawa hawezi kusema lipo bila ya kulifanyia uhakiki. Alisema kuna utaratibu wa kupokea malalamiko, ukishayapokea unakwenda kufuatilia, ili kuangalia kama ni kweli hizo rangi zinatumika kama inavyozungumzwa.

“Si kwamba mtu akishasema basi iwe kweli, kuna watu wanasema lakini hawana uhakika na hilo jambo, hivyo mtu mwenye malalamiko anashauriwa aje hapa ofisini kuna kitengo cha malalamiko. Suala hili ni la kulifuatilia huwezi ukalizungumza bila ya kulifanyia kazi,” alisema Msasalaga.Msasalaga alisema ikibainika ni kweli hatua za kisheria zipo, zinaelekeza wale ambao wanakwenda tofauti na utaratibu uliowekwa lazima wachukuliwe hatua.

Alisema ofisi hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi na kuvifuatilia viwanda vinavyotumika kutibu mbao hizo, hivyo mtu anaweza akawa analalamika kuna shida, lakini anatakiwa aelekeze tatizo lipo wapi na maeneo gani. “Kama kuna mtu anafanya tofauti tunapokwenda eneo husika, tunaangalia jinsi gani wanavyofanya, wanatumia kitu gani kuweka kwenye mbao hizo na kinatakiwa kitumike kitu gani, lakini kwa sasa siwezi kutoa majibu ya moja kwa moja hadi tuthibitishe,” alisisitiza Msasalaga.

Alipotafutwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko kuzungumzia hilo, alisema watafanya uchunguzi wa kina ili wanapotoa majibu, yawe ya uhakika.

Sababu ya kuweka rangi ya ukindu
Mfanyabiashara wa mbao eneo la Buguruni, Innocent Halfan alisema miongoni mwa sababu kwa sasa, wafanyabiashara wengi wanadai dawa aina ya Tanalith C ya inauzwa bei kubwa.

Halfan alisema dumu moja la lita 20 ya dawa ya kuulia wadudu inauzwa Sh750,000 na mbao moja inapoingizwa kiwandani, inalipiwa kulingana na urefu au unene kuanzia Sh600 hadi Sh1,000.

Hivyo, alisema wengi wao hushindwa kumudu gharama hiyo. “Ndiyo maana wafanyabiashara wakabuni utapeli huu, japo kuwa upo tangu zamani, lakini sasa hivi baada ya janga la Uviko 19 ndiyo umezidi.”

Kwa upande wa rangi ya ukindu, alisema pakiti moja inauzwa Sh2,000, muuza mbao ili mbao zake zilowekwe kwenye maji hayo, anatakiwa kulipa kulingana na urefu na unene wa mbao pia na hulipia kati ya Sh300 mpaka Sh400 kwa ubao mmoja.

“Mbao zilizowekwa dawa ya Tanalith C zenye urefu wa 2 kwa 4 zinauzwa Sh7,000, na mbao ya 2 kwa 2 inauzwa Sh3,500 na 2 kwa 6 inauzwa Sh9,000. Lakini zilizopakwa rangi ya ukindu 2 kwa 4 inauzwa Sh4,800 huku ya 2 kwa2 inauzwa Sh2,700 na 2 kwa 6 ni Sh6,000,” alisema Halfan.

“Mteja anayekuja kununua mbao zilizowekwa rangi ya ukindu akija kichwa kichwa, mbao ya 2 kwa 4 atauziwa Sh7,000 ambayo ni bei ya mbao zilizowekwa dawa, lakini akiomba kupunguziwa anapunguziwa hadi Sh5,000 au Sh4,800,” alifafanua.

Mfanyabiashara huyo alisema wateja wengi wanapenda kununua kwa bei nafuu, alitolea mfano bei ya mbao ya 2 kwa 6 iliyowekwa dawa inauzwa Sh9,000, lakini mfanyabiashara akiwa na mbao zilizowekwa ukindu akimwita mteja anampunguzia hadi kufikia Sh4,800, hivyo lazima atanunua.

Halfan alieleza; “pakiti moja ya rangi ya ukindu ya Sh2,000 unaweka mbao 2,000 ukiwa na pakiti mbili unaweka mbao 4,000, huku kwa upande wa dawa ya kuzuia wadudu Tanalith C dumu la lita 20 unaweka mbao zisizozidi 4,000.”

Mfanyabiashara mwingine wa Manzese, Andrew Sichawa alisema mbao zinatakiwa zipelekwe kiwandani, ili ziwekwe dawa ya Tanalith C ambayo inaingia hadi ndani.

Alisema dawa hiyo hairuhusiwi kuchanganya kwenye maji kwa kutumia mikono kwa kuwa inababua ngozi na muandaaji anapaswa kuvaa barakoa anapoichanganya, ili kuzuia kuvuta sumu kwa kupitia pua na mdomo.

“Hii dawa kwa ajili ya kuzuia mbao zisishambuliwe na wadudu inatakiwa ichanganywe kwenye viwanda maalumu, huwezi ukachukua dawa ya Tanalith C, unaiweka kwenye pipa la maji kisha unaloweka mbao na kuzitoa, lazima ikuletee madhara,” alisema Sichawa.

Alitolea mfano eneo la Manzese kulikotengenezwa mapipa ya kuwekea maji yaliyochanganywa na rangi ya ukindu; “Wauza mbao huzichukua na kuzitumbukiza kwenye maji hayo na wateja hufika kwa wingi kuzinunua.”

Mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo eneo la Mwenge, Manase Isaya alidai kuna tatizo la wao kuuziwa mbao ambazo miti yake haikukomaa hasa zitokanazo na mti wa Saplasi ambazo pia hutumika kutengenezea kenchi.

Alisema miongoni mwa mbao hizo ndizo zinazolowekwa kwenye maji ya ukindu ili zisitambulike.

“Unajua mti wa saplasi mpaka uvunwe unatakiwa ufikishe miaka 18, lakini wakulima wengi siku hizi wanazivuna zikiwa na miaka mtano au sita, jambo linalochangia kuliwa haraka na wadudu,” alisema Isaya.

Wenye viwanda nao wanena
Mmoja wa wamiliki wa kiwanda kilichopo Mwenge aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliliambia Mwananchi idadi ya wauza mbao wanaopeleka bidhaa hiyo kiwandani kwake kwa ajili ya kuwekewa dawa inapungua kila kukicha.

“Hii biashara imeshaingiliwa, siku hizi wanaloweka mbao kwenye maji ya rangi ya mkeka, ikitoka pale kama huna uelewa, utadhani imetiwa dawa lakini siyo.

“Tamaa yao inawaingiza wateja wao kwenye hasara kubwa. “Mfano mbao tunazoweka dawa, tunachaji moja Sh600 hadi Sh1,000 kulingana na urefu na unene, lakini ile ya rangi analipia Sh300 hadi 400,” alisema.

Alisema kwa eneo la Mwenge viwanda kama chake vipo vitatu, Buguruni viwili na Manzese kimoja.
Alisema mbao yenye dawa inayotoka kiwandani, inadumu kwa muda mrefu na si rahisi kushambuliwa na wadudu.

Waathirika nao wanena
Mmoja wa walioathirika na mbao hizo, mkazi wa Chanika, Konga John alieleza kuwa Machi mwaka 2022 alinunua mbao zaidi ya 100 eneo la Buguruni na alifanikiwa kupaua lakini mwanzoni mwa mwaka huu aliamua kuongeza ukubwa chumba cha sebule kutokana kilichokuwepo kilikuwa kidogo.

Konga alieleza alikubaliana na fundi huyo aliyemweleza mbao watakazotumia zikiwemo zilizopauliwa na alielezwa aongeze mbao 2 kwa 4 nane na 2 kwa 2 saba, lakini kilichojitokeza baada ya kutoa bati alikuta mbao zote zimeliwa na wadudu.

Alieleza baada ya fundi kuondoa bati alimweleza mbao zilizokuwepo kwenye chumba hicho zote zimeliwa na wadudu, hivyo anatakiwa anunue zaidi ya mbao alizoambiwa awali.

“Yaani hapa nilipo nimechanganyikiwa nimenunua mbao zinaonekana zina dawa lakini kinachonishangaza mbao zimeliwa na wadudu na kila mbao ya 2 kwa 4 nimenunua Sh7,500 na 2 kwa 2 nilinunua Sh3,500 pale Buguruni.

Konga alisema ndani ya mwaka mmoja zilikuwa tayari zimeoza na ndipo alipobaini kuwa alibambikiwa hakuuziwa zilizokuwa na dawa.

“Basi fundi aliniambia ninunue tu mbao nyingine nikajikuta naingia gharama zaidi,” alisema.

Naye mkazi mwingine wa Zingiziwa, Isaya Robert alisema ana nyumba ya vyumba vitatu ambayo ameezeka bati mwaka 2021, lakini mwaka jana alibaini kuwa baadhi ya mbao zimeliwa na wadudu ndipo alichukua jukumu la kumtafuta mtu apake mafuta machafu kwenye mbao zote, ili kuzuia kuendelea kuliwa na wadudu.

“Utakuta mtu amenunua mbao zinazoonyesha zimewekwa dawa, lakini kabla ya hazijapigiliwa juu wanaweka mafuta machafu ili kuiweka mbao kuwa imara zaidi akihofia kupata hasara kama wengine ilivyowatokea,” alisema.

Mafundi wanena
Mmoja wa mafundi wanaoezeka kenchi kutoka Buguruni, Daud Malya amesema amekutana na changamoto ya wateja wake wanne ambao kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ameezeka bati katika nyumba zao ambazo mbao za kenchi zimeoza kutokana na kushambuliwa na wadudu.

Amesema hivi karibuni kati ya wateja hao alimpa kazi ya kuongeza ukubwa wa vyumba viwili vya nyumba iliyopo eneo la Gongolamboto wakati anatoa mabati alishuhudia mbao kumi za kenchi zimeshambuliwa na wadudu hao.

“Huo ni upande wa nyumba viwili na nilivyoangalia kwenye vyumba vingine kwa haraka niliona mbao kama sita zimeoza kutokana na kushambuliwa na wadudu, kwa kweli tutegemee ndani ya miaka mitano kutakuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi,”amesema Malya.

Fundi mwingine, Rashid Ngonyani aliyepaua chumba cha sebule cha Konga alieleza kuwa alivyoikagua nyumba hiyo mbao nyingi zimeliwa na wadudu hao, hivyo alitoa ushauri atafute mafuta machafu ili apake kwenye mbao zisiendelee kushambuliwa.

Credit: Mwananchi
 
Hili nalitambua, nilijaribu sehemu ndogo kupaka nitest but baada ya miezi miwili bado hola. Sijui tanzania hii kama kuna dawa wanauza ili kupaka. Maana kila ninazoziona kwenye mtandao zote ni za nje
Kuna dawa ya kupuliza, nitaulizia jina lake. Unachangaya na maji unaweza kwenye ile bomba ya kupulizia....haimalizi tatizo ila angalau italipunguza.
 
Back
Top Bottom