SoC03 Ukosefu wa vyoo wezeshi: Kizuizi kwa elimu ya wanafunzi wenye ulemavu

Stories of Change - 2023 Competition

mjandwasafi

Member
Jun 6, 2023
10
19
Uwepo wa vyoo bora ni muhimu sana katika shule ili kuhakikisha mazingira salama na afya kwa Wanafunzi ili kuwezesha suala la ufundishaji na ujifunzaji. Hata hivyo katika shule jumuishi changamoto hujitokeza linapokuja suala la vyoo kwa Wanafunzi wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu. Suala hili linaweza kuwa na athari kubwa sana kwa afya, ustawi, na upatikanaji wa elimu kwa kundi hili la wanafunzi.

"Wanafunzi hao ni kati ya wengine maelfu nchini ambao kila siku wanalazimika kupanga foleni, kwa ajili ya kupata huduma hiyo katika vyoo ambavyo siyo tu havina matundu yanayokidhi haja ya idadi ya wanafunzi, pia havina huduma kama vile maji na mifumo ya majitaka." (Mwananchi, machi 16, 2021).

inbound3254632144096593973.jpg

Picha: Mwalimu akionyesha mfano wa choo unavyoonekana katika moja ya shule za msingi nchini.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Hapa tutaangazia jinsi ukosefu wa vyoo bora shuleni unavyokuwa kikwazo kwa Wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalumu.

Moja ya athari kubwa ya ukosefu wa vyoo bora shuleni kwa Wanafunzi wenye ulemavu ni kuathirika afya zao. Kama tujuavyo afya ni mtaji, pasipokuwa na afya bora hakuna kitu kinachoweza kuendelea na kufanikiwa, hivyo hili ni jambo la kipaumbele katika maisha ya mwanadamu yeyote yule. Wanafunzi wenye ulemavu mara nyingi huitaji miundombinu muhimu na salama ambayo hukidhi mahitaji yao. Lakini hii ni tofauti kwani namna ambayo hutumika kusafisha vyoo hivyo vya shule jumuishi mara nyingi si salama kabisa hasa katika shule za msingi, ni hatari kwa afya za wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalumu kwani huweza kuibua magonjwa kama vile kuhara, kuumwa matumbo na wakati mwingine hupelekea hata kifo.

Vilevile, husababisha athari za kisaikolojia kwa Wanafunzi wenye ulemavu. Wanafunzi hawa wanapokabiliwa na mazingira hayo huona kama wanabaguliwa na kutengwa. Hali hii huwafanya kujiona ni wadhaifu na huwa wanyonge, jambo hili ni hatari mno kwao kwani huathiri afya ya akili na saikolojia ya Wanafunzi hao kwa ujumla.

Pia, huathiri suala la upatikanaji wa elimu. Wanafunzi hawa mara nyingi wanakabiliwa na changamoto hii kwani vyoo hivyo havizingatii mahitaji yao. Jambo hili huwafanya wasiwe huru wawapo katika mazingira ya Shule hususani shule jumuishi na hivyo hupelekea wengine kukatisha masomo kutokana na adha wanayo kumbana nayo wakati wa matumizi ya vyoo hivyo.

" Mwanafunzi mmoja kati ya wanne wenye ulemavu alifanikiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2022, wakati wengine walishindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali" (Mwananchi, machi 26, 2022).
Binafsi, nionavyo mimi miongoni mwa sababu mbalimbali ambazo hazikutajwa hapo ni pamoja na kutokuwa na miundombinu rafiki ya vyoo shuleni kwa Wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalumu.

inbound1004628120518083448.jpg

Picha: mwenendo wa elimu kwa watu wenye ulemavu.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kwa kuwa uwajibikaji ni suala la kila mmoja kuhakikisha wanafunzi hawa wanapata kilichobora kabisa wawapo shuleni hatua hizi zinaweza kuwa msaada katika kukabiliana na changamoto hii.

Kwanza, Ushirikishwaji wa wadau mbalimbali. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Asasi za kiraia, mashirika ya kidini kama vile Karita, wataalamu wa masuala ya ujenzi hususani wahandisi wa ujenzi na wananchi kwa ujumla. Ushirikiano huu utawezeaha upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine ewepo na ukarabati wa miundombinu hiyo muhimu.

inbound3591408973621234654.jpg

Picha: Choo cha kisasa na bora kwa Wanafunzi wenye ulemavu.
Chanzo: www. bmgblog.co.tz

Utungaji wa sera wezeshi. Sera zinazotungwa kama njia ya kuhakikisha kundi hili linapata elimu kama wanafunzi wengine ni lazima zifuatwe kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kitaifa na ile ya kimataifa Kwa kuzingatia haki za watu wenye ulemavu.

Hivyo basi, Sisi kama wananchi tunalojukumu la kuhakikisha Wanafunzi hawa wenye ulemavu na mahitaji maalumu wanapata elimu bora, kwa kuwapa ushirikiano kupitia kushiriki katika kufanikisha uwepo wa vyoo rafiki kwao na matumizi sahihi ya vyoo hivyo, sera mbalimbali zinazoandaliwa kulisaidia, kulisimamia na kulitetea kundi hili zisiwe sera dhahania bali zitekelezwe kwa vitendo kwa kuwasaidia na kuwahudumia walengwa na zisiwe tu kwenye maandiko na vitabu.

Kama ambavyo tumekuwa tukiyapa kipaumbele mambo mengine yanayohusu maendeleo yetu binafsi na jamii kwa ujumla, ni wakati sasa kugeuzia shingo upande wa watoto wetu, ndugu zetu wenye ulemavu na mahitaji maalumu ili waweze kupata msaada wa vyoo rafiki shuleni. Kwa kufanya hivyo tutawasaidia Wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalumu katika kupata taaluma bora katika mazingira rafiki na wezeshi kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.
 
Matundu ya shimo ya kawaida yanashindikana, itakuwa choo spesho kwa walemavu? Hii nchi bado sana!
 
Back
Top Bottom