SoC02 Ukeketaji wa wanawake Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

guddi

New Member
Sep 5, 2021
3
2
Hodi! Hodi! Hodi! nilibisha mara tatu pasipo na jibu. Mlango ulikuwa wazi na kimya kilitawala nilijongea ndani taratibu nikijua huenda bado wamelala. Au wamehama? nilijiuliza kimoyomoyo, nilikaribishwa na utandu wa buibui, wadudu waliojitengenezea nyumba zao sakafuni na panya waliokimbia huku na kule. Vumbi lililotanda kwenye viti na vyombo lilidhihirisha ya kwamba hakuna aliyeishi pale kwa muda mrefu.

Kwa takribani muda wa dakika kumi niliwaza vingi pasipo na jawabu nikikumbuka fika katika barua ile ya mwisho alinielekeza alipoishi na alipoenda kuandika barua hiyo. Nilitoka na kwenda hadi alipokuwa anaandika barua.

Habari dada, alikua nje akiosha vyombo na mtoto mgongoni, aliponiangalia alitabasamu na kunikumbatia. Alikua Siwema rafiki yangu aliebahatika kujua kusoma na kuandika kwa sababu pacha wake wa kiume alimsaidia kwa siri bila wazazi wao kujua.

Pacha wake alipelekwa shule wakati Swema anaandaliwa kuolewa.

okay

Kabla sijapumzika nilimuuliza, “Sikujua yupo wapi?” Mamaa!! Siwema alipiga kelele kwa uchungu na kuanza kulia nikama nilimtonesha kidonda kibichi. Siwema alisema, Sikujua hatupo nae tena, alisema wakati umetoroka nyumbani tulipelekwa jando na kukeketwa.

Maumivu yalikuwa makali sana lakini kwa Sikujua alilalamika kidonda hakiponi haraka. Zilipita wiki tatu tuliozeshwa kwa wanaume tofauti. Sikujua alibahatika kujifungua watoto mapacha akiwa na miaka 15. Mwaka uliofuata alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume.

Mkunga alimshauri apumzike mwaka unaofuata asibebe mimba, mmmmhhh! Siwema alivuta pumzi nzito na kuendelea kusema, Sikujua alikuja kwangu akiwa na alama za kupigwa sababu ikiwa ni kukataa kubeba ujauzito.

Mateso aliopata Sikujua na vitisho vya kuachwa na jukumu la watoto ilimlazimu abebe ujauzito tena. Bahati mbaya wakati wa kujifungua alipoteza damu nyingi na kwa vile alikua amedhoofika sana alifariki. Mumewe Sikujua alioa mke mwingine baadae na watoto wa Sikujua walipelekwa kuishi na bibi yao.

UKEKETAJI NI NINI
Kilio changu ni Ukeketaji wa wanawake ambayo huusisha uondoaji wa sehemu au sehemu yote ya siri ya nje ya mwanamke au kuweka jeraha lingine kwa viungo vya uzazi vya mwanamke kwa sababu zisizo za kimatibabu (News.UN.org2022).

Mbali na sheria iliopitishwa na serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1998 kuwa ukeketaji ni kosa la jinai. Mila potofu zenye madhara bado zinaendelea na mwanamke mmoja kati ya kumi amekeketwa, asilimia 35 wamekeketwa kabla ya umri wa mwaka mmoja.

Ukeketaji umeenea Zaidi mikoa ya Manyara 58%, Dodoma 47% na Arusha 41%.(News.UN.org2020).

Sababu za ukeketaji za kiutamaduni na kijamii, ya kwamba ukeketaji ni moja ya mila zinazofanywa na watu wa jamii hiyo na hupaswa kufanyika vizazi hadi vizazi. jamii hizo hutumia ukeketaji kama njia ya kumuandaa msichana kuingia ukubwani na tayari kwa kuolewa. Watu wasifanya ukeketaji katika jamii hizo wamekuwa wakitengwa na wenzao na kukosa ushirikiano.

MADHARA YA UKEKETAJI
Ukeketaji hauna faida za kiafya bali una madhara ya muda mrefu na mfupi.Baadhi ya madhara ya muda mfupi ni pamoja na maumivu makali, homa kali, maambukizi ya magonjwa kama vile UKIMWI, matatizo ya uponaji wa jeraha, mshituko na kutokwa na damu nyingi ambayo inaweza kupelekea hadi kifo.

Madhara ya muda mrefu ni maumivu makali ya muda mrefu, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kupungua kwa raha ya kujamiiana, kuongezeka kwa hatari ya kujifungua kwa njia ya upasuaji bila kusahau madhara mbali mbali ya kisaikolojia.

JITIHADA ZA TAIFA
Pamoja na hayo yote serikali ya Tanzania imeitikia wito kwa kuweka mpango wa kukomesha ukeketaji dhidi ya wanawake na watoto ( NPA-VAWC) 2017/2018-2021/2022. Pia serikali ya Tanzania imeiweka sera hii katika sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030.

NINI KIWEKEWE MKAZO
Elimu ni mkombozi wa wengi pia ni mwanga utoao watu gizani. Elimu ikitiliwa mkazo kwa sehemu zenye mila potofu kama ukeketaji itaweza kufumbua macho na masikio ya watu kuona madhara ya ukeketaji, kueleza kwa nini ukeketaji unapaswa kuachwa.

Kuwainua wanajamii wao wanaoonyesha kuwa na nia na vipaji endelevu ili wawe mfano bora kuliko kuwapelekea watu wasio wajua, kuwatumia wao kwa wao inaweza kuleta hamasa ya kuwa wao pia wanaweza kubadilika na kufanya vingi vikubwa zaidi mbali na kushikilia mila potofu. Elimu hizi zitolewe kwaanzia mashuleni. Pia kuhakikisha wasichana kwenda shuleni sawa na wavulana kupunguza jamii yenye watu wasio na elimu.

Sheria ingekuwa na nguvu zaidi ikianzia ngazi ya chini kabisa kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa kijiji hadi kufikia ngaz ya juu. Hii husaidia kuwajibisha watu kwa urahisi.

Mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi waituikie witio na kuunga mkono serikali kuweka jitihada za utokomezaji wa ukeketaji wa wasichana. Kutokomeza jambo hili itakuwa faida na msaada mkubwa kwa serikali kutotumia fedha nyingi kutibu madhara yasabishwayo na ukeketaji na badala yake kuwekeza fedha hizo kwa kukuza uchumi wa sehemu hizo.

Tuwalinde na kuwapenda Watanzania wenzetu!
 
Back
Top Bottom