Mmanda atetea wingi wa Wachagga TRA
Written by Charles Mullinda
Friday, 21 July 2006
*Asema walipata elimu mapema
HATIMAYE Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa tamko dhidi ya madai ya kuwapo ukabila katika mamlaka hiyo.
Imesema madai hayo si ya kweli ingawa kuna idadi kubwa ya Wachaga wanaoshikilia nafasi nyeti katika taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa walipa kodi wa TRA, Evod Mmanda jana aliiambia Tanzania Daima ofisini kwake kuwa, wingi wa Wachaga katika taasisi hiyo unatokana na watu wa kabila hilo kuelimika mapema zaidi kuliko makabila mengine.
"Hakuna suala la ukabila TRA, haya mambo yanazushwa tu na watu kwa sababu mbalimbali, zikiwamo za chuki binafsi na wengine ni hulka yao kuzua mambo.
Kweli TRA ina watumishi wengi katika nafasi nyeti ambao ni Wachaga, lakini hili ni suala la historia, huwezi kulikwepa, kumbuka Wachanga ni kabila ambalo watu wake walipata elimu ya juu mapema kabla ya watu wa makabila mengine.
Na hapa sio TRA tu, angalia madaktari wengi hasa wa zamani kidogo ambao sasa ni mabingwa, wengi ni Wachaga, na kwa Tanzania nafasi za kazi hazitolewi kwa ukabila bali sifa za muhusika na uwezo alionao katika kuifanya kazi hiyo," alisema Mmanda.
Alisema Wachaga wengi wanapenda masomo ya biashara na ni wafanyabiashara kwa asili, hivyo sio ajabu kuwa wengi katika taasisi za fedha kwa sababu wamesoma na kubobea katika masomo hayo.
Hata hivyo, Mmanda alisema mambo yanabadilika kwa sababu historia ya Wachaga kupenda elimu sasa haipo na hata vijana wanaoajiriwa katika sekta ya fedha nchini wengi sio Wachaga.
Alisema Wachaga wanaolalamikiwa ni wale waliosoma zamani na mchango wao ni mkubwa katika mafanikio ya TRA.
"Sisemi haya kwa sababu mimi ni Mchaga, hapana, bali hata wewe fuatilia ukweli, tunao Wachaga TRA, lakini wote ‘wanafiti' katika nafasi zao, na hawa ni wale waliosoma zamani, leo vijana wa Kichaga wameishia biashara ya kuuza ndizi, wasomi ni wachache na makabila mengine ambayo yanazingatia elimu sasa yanaibuka," alisema Mmanda.
Aliwataka wanaoibua hoja hiyo kuiangalia vizuri historia ya elimu hapa nchini, inayoonyesha jinsi Mkoa wa Kilimanjaro ulivyokuwa na shule nyingi za sekondari katika miaka ya 1960 tofauti na mikoa mingine.
Alisema pamoja na kuwa na shule nyingi, jamii ya Kichaga ya wakati huo ilitilia mkazo maalumu suala la elimu kwa vijana ambao sasa ndio maofisa katika nafasi mbalimbali.
Alisema iwapo wingi wa watu wa kabila moja ndani ya taasisi yoyote nchini utachukuliwa kama kukithiri kwa ukabila katika taasisi hiyo, ya kwanza kutuhumiwa kuhusu hilo ni jeshi ambalo lina watu wengi wa Musoma.