Serikali ya Uingereza imeifikisha Tanzania katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), ikitaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa kina kufuatia kile ilichokiita "ukatili wa kushtua" uliotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, ikiwemo tuhuma za mauaji ya kinyume cha sheria na miili ya wahanga kufichwa.
Hoja hiyo imewasilishwa na Balozi wa Haki za Binadamu wa Uingereza, Eleanor Sanders, wakati wa mdahalo mkuu wa 61 wa Baraza hilo jijini Geneva, Uswizi Machi 2, 2026. Uingereza imetumia jukwaa hilo la kidiplomasia kuishinikiza Tanzania kutoa majibu juu ya mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyoripotiwa nchini humo.
Katika tamko hilo, Balozi Sanders ameweka wazi kuwa Uingereza ina taarifa na ushahidi wa matukio ya kusikitisha yaliyojiri kufuatia mchakato wa uchaguzi, jambo ambalo limeutia doa utawala wa sheria na demokrasia nchini.
Pia soma
PostGE2025 - Rais Samia aunda Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi 2025
"Lazima kuwepo na uchunguzi huru, wa wazi na jumuishi wa matukio haya ili kuhakikisha uwajibikaji na kwamba uhuru wa msingi na haki za kikatiba za Watanzania wote zinalindwa," amesisitiza Balozi Sanders.
Hatua hii ya Uingereza ‘kuishitaki’ Tanzania mbele ya Baraza la Haki za Binadamu wakati ambao Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoundwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ikiendelea kukutana na kufanya mahojiano na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa sasa, wastaafu, na wadau mbalimbali ili kukusanya taarifa na ushauri wa kitaalamu juu ya kile kilichotokea.
Mbali na kuisaka haki nchini Tanzania, Uingereza imetumia fursa hiyo kukemea ukiukwaji wa haki maeneo mengine ikiwemo Gaza na Ukingo wa Magharibi ikiitaka Israel kuruhusu misaada na kusitisha ujenzi wa makazi; China, ikitaka kuachiliwa kwa watu waliowekwa kizuizini kiholela Xinjiang na kukomeshwa kwa kazi za suluba; na Ukraine, ikiendelea kuunga mkono mamlaka ya nchi hiyo dhidi ya uvamizi wa Urusi.