Uhusiano baina ya Chama cha Kikomunisti cha China na vyama mbalimbali vya kisiasa vya Afrika waendelea kupaa juu zaidi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
W020220223789154344639.jpg


Uhusiano na ushirikiano kati ya vyama vya siasa vya China na Afrika ulianza kitambo sana yaani kabla ya nchi nyingi za Afrika kujipatia uhuru wake. Uhusiano huu umekuwa ukiendelezwa siku hadi siku yaani tangu China ilipokuwa Jamhuri mwaka 1949 wakati wa utawala wa Mwenyekiti Mao Zedong hadi utawala wa katibu mkuu na rais Xi Jinping. Katika vipindi vyote hivyo tumeshuhudia chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kikibeba jukumu lake muhimu la kuiongoza nchi pamoja na kuimarisha diplomasia ya vyama katika nchi za nje.

Katika miaka hii 10 tangu Xi Jinping achaguliwe kuwa katibu mkuu wa chama cha CPC, chama hicho kimekuwa ndio muhimili mkuu wa kuhakikisha mahusiano mazuri na vyama vingine duniani hasa vya Afrika, kwani ndani ya kipindi hiki vyama vya kisiasa vya China na nchi za Afrika vimekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kujenga ama kuupaisha juu zaidi ushirikiano uliopo baina ya vyama hivi, chini ya msingi wa kanuni ya uhuru, usawa, kuheshimiana na kutoingiliana kwenye mambo ya ndani.

Chama cha kikomunisti cha China pia kimefanikiwa kuanzisha ushirikiano na mawasiliano na vyama zaidi ya 110 vya kisiasa vya Afrika katika nchi 51 za Afrika. Katika miaka kumi iliyopita vyama vya kisiasa vya Afrika na chama cha CPC vimeshiriki kikamilifu kwenye mazungumzo ya vyama vya kisiasa ya ngazi ya juu duniani pamoja na makongamano juu ya kuunganisha watu kwenye ushirikiano wa kimataifa wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, ambapo vyama vya kisiasa 69 kutoka nchi 42 za Afrika vikiwa pamoja na CPC vilitoa taarifa wakitaka vyama vya siasa kote duniani kuungana pamoja kwenye mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Julai Mosi mwaka 2021, Chama cha Kikomunisti cha China kilisherehekea maadhimisho ya kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Sherehe hii haikuwa kwa wananchi wa China pekee, bali hata vyama mbalimbali vya kisiasa vya Afrika pia viliungana na China kuadhimisha siku hii, ikikumbukwa kwamba CPC na vyama hivi ni makomredi wa zamani walioungana pamoja katika juhudi zao za kupigania uhuru na kuzikomboa nchi za Afrika kutoka kwenye makucha ya wakoloni wa nchi za magharibi.

Katika sherehe hizi kubwa kufanyika nchini China, vyama vya kisiasa na mashirika ya kisiasa ya Afrika yakiwemo ya nchi zaidi ya 80 pamoja na viongozi wa vyama vya kisiasa, walituma salamu za pongezi kwa njia ya telegram ama barua.

Wakuu wa nchi au serikali kutoka nchi nane za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Zimbabwe, Msumbiji, Jamhuri ya Congo, Namibia, Sudan Kusini, Morocco na Mauritius walishiriki kwenye mkutano wa kilele wa CPC na Mkutano wa Vyama vya Kisasa Duniani kupitia njia ya video.

Vyama hivi vya kisiasa sio kwamba vinashirikiana kwenye masuala ya kisiasa tu, la hasha, bali pia vimejikita zaidi kwenye kuinua uchumi wa pande zote mbili. Mathalan katika miaka ya nyuma, mkakati mkuu wa China wa maingiliano na vyama tawala vya Afrika, ulikuwa ndio chachu ya mageuzi ya kiuchumi nchini China kuanzia mwaka 1978.

Mabadiliko haya ya kimsingi ya kisera baadaye yalionesha kwamba kukiwa na uongozi imara na unaojitolea wa chama, basi uchumi wa nchi unaweza kukua zaidi na kwamba mageuzi ya jamii nzima yanakuwa ni matarajio yanayotimizika. Hivi sasa mageuzi ya China yanavutia viongozi wengi barani Afrika wawe wa chama ama serikali na kuichukulia China kama ni mfano wa kuleta mageuzi kwenye nchi za Afrika kupitia vyama vyao vtawala vya kisiasa na hata vya upinzani pia.

Serikali za Afrika na vyama tawala, vikiwa vimekatishwa tamaa na msukosuko wa uchumi, sasa vinakumbatia vipengele muhimu vya mtindo wa uchumi wa China na chama chake cha CPC kikiwa kama mshirika wao, wakitaka kuiga mafanikio ya kiuchumi katika nchi na jamii zao za Afrika.

Leo, karibu kila chama cha kisiasa katika mataifa 54 ya Afrika, kina uhusiano wa kikazi na CPC au kinatamani kuwa nacho. Uhusiano huo unaimarika huku China ikidumisha uungaji mkono kwa Afrika katika kila upande. Kuimarika kwa mahusiano haya ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia vyama vya siasa, ni ujumbe tosha kwa wasomi wa Afrika na watu wa kawaida, kwamba China ipo kwa ajili ya kuwasadia kwa hali na mali masahiba zao Afrika.
 
Back
Top Bottom