Uhuru Kenya, Suluhu Tanzania?

msani

JF-Expert Member
Jun 13, 2011
1,801
1,191
UHURU KENYA SULUHU TANZANIA?

Hii ni kauli ya Mh. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliokuwa Kenya kwenye ziara. Watanzania tumepewa ‘Uhuru’ wa kujivinjari Kenya bila visa wala kibali cha kazi, ni kauli iliyopokelewa kwa shangwe na ni kauli ilitoka papo kwa hapo na kwa lugha nyepesi ilimtega Mh Rais Samia lakini alisimama imara akijua kuna mambo tunahitaji ‘Suluhu’ huku kwetu. Kwa lugha nyingine Mh. Rais ‘alicheza kama Pele’.

Inaumiza akili kusikia kuna makampuni ya Kenya 530 yaliyowekeza Tanzania na kwamba ni makampuni takribani 30 tu ya Tanzania ambayo yamewekeza Kenya. Mgeni akisikia taarifa hii basi hawezi kuacha kuifananisha na wachezaji wa Mpira wa miguu nchini Uingereza ambao wengi wapo Uingereza ambao hawaoni haja ya kwenda nchi zingine kwa sababu wanapata kila kitu ndani ya nchi yao, lakini akisikia kauli ya mheshimiwa Rais Suluhu Hassan juu ya ‘Suluhu’ ya kibiashara basi mawazo yatamtuma kwamba Tanzania huenda ni Mzazi aliyewadumaza watoto wake na sasa hawawezi hata kutoka nje na kudemka na wengine.

Hili linatuamsha kujua matatizo yapo wapi hasa?

Narudi kuangalia mfugaji wa kuku ambaye biashara yake ni kuuza kuku na mayai. Ratiba yake ni kuhakikisha anawahudumia Kuku ilia pate mayai, na wanenepe auze ndipo apate hela. Hauwezi kuwanyima chakula Kuku kama unatarajia mayai kutoka kwao. Hapa wakurya wana msemo wanasema ‘WIN WIN SITUATION’ yaani kila mmoja afaidike na mwenzake. Mpe chakula akupe mayai na bila hayo kufanyika basi katengeneze mayai yao maabara.

Labda niweke jambo moja ambalo huenda tunalijua sote kuhusu biashara na wafanyabiashara.

Biashara nyingi kubwa duniani zinaendeshwa kwa pesa aina mbili:

1. Mtaji wako binafsi ambapo hapa unaamua kiasi cha pesa unachoenda kuwekeza. Iwapo Mtaji wa uwekezaji ni TZS 100, Je una kiasi gani mkononi? Ni asilimia ngapi ya hiyo TZS 100? Kama ni 100% basi umejitosheleza lakini kama ni pungufu basi unahitaji kwenda kwenye taasisi za kifedha ili kupata pungufu yake katika mtaji wa uwekezaji.

2. Ukiisha wekeza basi utahitaji fedha za kuendeshea shughuli hizo za kila siku. Hapa unaweza kuwa ni kwenye baadhi ya mauzo au hata kwenye taasisi za kifedha.

Wawekezaji wachache sana ambao hutumia fedha zao za mfukoni(Ni Lugha tu lakini unaweza kusema fedha zako popote zilipo) kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Sababu zao ni nyingi na moja wapo ni kupunguza uwekzekano wa hasara. Hapa ni wazo la kugawana hasara kwa sababu taasisi ya fedha anakuwa sehemu ya mwekezaji(Kwa nadharia nyepesi)

Kwahiyo msingi mkubwa hapa kwenye maeneo haya tunaona kwamba tunahitaji Taasisi za kifedha(Mabenki ya kibiashara) kwa sababu mwekezaji haji na pesa rundo kwenye kisandarusi kwa ajili ya kuja kuwekeza Tanzania. Ataleta baadhi ya mtaji na zingine anatarajia kuzikuta huku huku Tanzania. Kwahiyo uimara wa Benki zetu ni suala la msingi kabisa kwa uwekezaji Tanzania.

Mwekezaji akitaka kuja anaangalia au kufanya tathmini kwamba ni benki ipi itampatia hela. Akikosa Benki na uwekezaji umekufa. Mfano mzuri ni Kampuni ya TOTAL kwenye Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania (Mkoani Tanga). Taasisi za kifedha zilizokuwa zimejiandaa kutoa fedha zilikuwa zimetishia kujitoa. Hivi ndivyo biashara hufanyika duniani.

Nimeandika kwa urefu ili kuonesha ni namna gani Benki zetu haziwezi kuwahudumia wawekezaji, na hapa naongelea Kenya, au itabidi Kampuni ya Kenya irudi kwao Kenya ikakope hela ije Tanzania?

Serikali ni kama mfugaji wa kuku, inapaswa kulisha ili ipate mayai inayokusudia.

Mabenki yetu mengi hapa sio Kamba wanazo hela sehemu wamehifadhi ambazo ni za kwao ili wawakopeshe wawekezaji , HAPANA. Wanatarajia sisi ambao tuna 200 zetu tuziweke huko watutunzie, halafu wawapatie wengine wafanyie biashara na wakati wanafanya biashara hiyo watafanya marejesho na sisi tukihitaji 200 zetu tukienda tutazikuta. Kuna wakati wanahitaji Zaidi ya hizo 200 lakini nani wa kwenda kuziweka huko ndani?

Serikali ndio inakusanya mapato mengi sana ndani ya nchi hii kupitia kodi ambazo wanaozitoa ni hao wawekezaji (Kuku). Wawekezaji hao ni pamoja na hizo benki zilizopo nchini. Kwahiyo benki hizi zinahitaji fedha nyingi sana ziwekwe kwao ili waweze kusukuma mbele biashara nchini na kuvutia wawekezaji wengi Zaidi na hapo mfugaji(serikali) itakusanya kodi (mayai) kubwa zaidi.

Miaka ya karibuni serikali iliondoa utaratibu wa kuweka fedha zake kwenye Benki za Kibiashara na kufungua akaunti moja ya kuhifadhi hizo fedha kupitia benki kuu. Hapa tulimzuia Kuku kula na tulijitafutia utapiamlo sisi wenyewe bila kujijua. Halmashauri,taasisi,wizara n.k ziliweka fedha kwenye benki zetu na wawekezaji walikuwa na uwezo wa kupata fedha nyingi za mikopo na biashara kukua.

Lakini kwa sasa mwekezaji akihitaji TZS 30 bilioni aisee atasota kwa sababu lazima ziungane benki nyingi ziweze kupata hiyo hela. Hii inaua biashara ndani ya nchi yetu. Hakuna mwekezaji atavutiwa kuwekeza kwenye nchi ambayo benki zake haziwezi kumkopesha hata TZS 50 Bilioni kwa haraka.

Mheshimiwa Samia Suluhu, nadhani hapa ndipo tunahitaji ‘Suluhu’ kwa sababu hizi taasisi za kifedha sio maadui zetu bali ni kuku ambao tukiwafuga na kuwalisha vizuri basi tutapata mayai ya kutosha.

Kwasababu mimi sio miongoni mwa utakaokutana nao kwenye ‘Suluhu’ nimeona niandike Makala hii kuelezea kwa undani ninachofahamu, kwamba turejeshe ule utaratibu wetu wa kuweka fedha za serikali kwenye mabenki ya kibiashara ili kusukumua shughuli za biashara na uwekezaji ndani ya nchi yetu.
 
Kwa ufupi ni kwamba ma benki ya Tanzania ni wakomoaji hazisaidie mtanzania kufanya biashara ila ni kumfirisi.

Serikali ya Tz haina urafiki na private sector ina ziona kama mshidani wake, haiko tayari kumsaidia kushindana na mfanya biashara wa nje.

Watumishi na viongozi wa serikali. ie wana siasa waTz nima tajiri kuliko wafanya biashara wa nchini na hao wana siasa hawana ujuzi wa biashara ya ushindani.

Kenya itaendelea kututawala katika biashara paka tufanya total economic overhaul.
 
Back
Top Bottom