Vigogo Zanzibar wajipanga
na Mwandishi Wetu
VIGOGO wanaojiandaa kurithi nafasi ya Urais wa Zanzibar mwaka 2010, wameanza kupigana vikumbo kuchukua fomu za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Mjini Magharibi.
Vigogo hao kwa muda mrefu wamekuwa katika harakati za kujiimarisha kisiasa na wamefanikiwa kujipenyeza katika mikoa mbali mbali ya Unguja na Pemba na kujijengea ngome.
Hata hivyo hadi sasa ngome pekee inayopewa nafasi kubwa ya kutoa mgombea huyo ni ile ambayo iko chini ya himaya ya Rais mstaafu, Dk. Salmin Amour, ambayo ndiyo inayoonekana kuwa na nguvu zaidi kisiasa kwa upande wa Zanzibar.
Kuanzia wiki iliyopita, vigogo hao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika ofisi za CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Amani Mjini Unguja, kuchukua fomu huku wengine wakisafirisha wapambe na wengine kuingia kwa kutegeana.
Wanasiasa wakongwe waliojitokeza hadi sasa kuchukua fomu ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna.
Hata hivyo, kundi la vijana ambalo linaonekana kuchukua fomu hizo kwa umakini mkubwa haliko nyuma, lakini idadi kubwa wamo vijana ambao katika uchaguzi uliopita walianguka na kufanikiwa kuingia NEC kulingana na uteuzi wa nafasi zao.
Katika kundi la vijana waliojitokeza hadi sasa ni Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye amekuwa akitajwa sana kuwa ni miongoni mwa watu walio katika pilika pilika za maandalizi ya kurithi nafasi ya Rais Karume.
Hata hivyo, Shamsi mwenyewe hadi sasa hajatoa msimamo wowote juu ya nia hiyo, licha ya baadhi ya viongozi na wananchi kutoka Mkoa wa Kusini Unguja alikozaliwa, kusema kwamba hii ni zamu yao kushika urais.
Hata hivyo, duru za kisiasa zinasema kwamba mtazamo huo huenda usipewe nafasi katika chama, kwa vile hadi sasa kuna makundi yanadai ni zamu ya Pemba na tayari yameanza kujipanga kupitia kundi la wasomi, ambao wanadaiwa kuungwa mkono na CCM Tanzania Bara.
Kundi hilo linadai kwamba kupata Rais wa Zanzibar kutoka Pemba, ndio utakuwa mwanzo wa kuiteka kambi ya CUF Pemba, ambayo inaonekana kuiumiza kichwa CCM Zanzibar.
Vijana wengine waliochukua fomu hizo hadi sasa ni Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, ambaye aliibuka katika siasa za CCM mwaka 2000.
Mansour ambaye ni shemeji ya Rais Amani Abeid Karume, pia amekuwa akitajwa kuwa ni miongoni mwa viongozi vijana wanaokubalika kuchukua nafasi za juu, hasa kwa vile anatoka katika mifupa ya wanamapinduzi wa mwaka 1964.
Baba yake Waziri Mansour, Yussuf Himid, ni miongoni mwa watu mashuhuri walioshiriki katika mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyoung'oa utawala wa kisultani.
Pia waliochukua fomu hizo hadi jana ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar, Machano Othman Said, ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM.
Mjadala mkubwa hadi sasa upo kwa vigogo wawili, Dk. Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mohammed Seif Khatib.
Baadhi ya wajumbe wa NEC wanasema Dk. Bilal chama kinamkubali Zanzibar na Bara, lakini kikwazo kikubwa alikuwa Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Rais Benjamin Mkapa, lakini sasa atakuwa msikilizaji tu katika vikao vya maamuzi ya chama.
Katika kinyang'anyiro hicho pia wanatajwa Dk. Hussein Mwinyi, ambaye ni Mbunge wa Kwahani, Unguja, baada ya kuhama Jimbo la Mkuranga, hatua ambayo inaonekana ni maandalizi ya kuchukua nafasi ya juu Zanzibar.
Hata hivyo, hivi karibuni, Rais Karume alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Zanzibar kuwa ni mapema kufanya harakati za kugombea urais wakati muda wake ukiwa bado.
Rais Karume aliingia madarakani mwaka 2000, baada ya kuwaangusha washindani wake katika vikao vya chama ambao waliongoza katika kura za maoni Zanzibar.
Na katika mwaka 2005, alipata nafasi ya kuwania kiti hicho, baada ya mpinzani wake, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kulazimishwa kujitoa katika usiku wa kuamkia kupiga kura mjini Dodoma.
Uamuzi huo uliotolewa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa, unadaiwa ulilenga kujenga umoja ndani ya chama hicho visiwani.
source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/5/29/habari4.php
hata mie nnaona wakati wa wapemba kupewa nafasi na nnaamini itaisaidia sana CCM kushinda Pemba na kuondoa Dhana kuwa CCm ni chama cha wabara na wa unguja.
pia CUF wkimsimamisha JUma Duni itaondosha ile dhana kuwa CUF ni Chama cha wapemba tu. nnaomba wazanzibari tubadilike